Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Injili ya tunu msingi za maisha ya Kikristo, mfano bora wa kuigwa! Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Injili ya tunu msingi za maisha ya Kikristo, mfano bora wa kuigwa! 

Sikukuu ya Familia Takatifu ya Nazareti: Tunu za Injili ya Familia!

Mama Kanisa anaiweka Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu kuwa ni kielelezo na mfano bora wa kuigwa na familia za Kikristo. Familia Takatifu ni shule ya tunu msingi za Kiinjili, changamoto na mwaliko kwa familia za Kikristo kujenga familia zinazokita mizizi yake katika Injili ya uhai, upendo na mshikamano wa kidugu. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya imani na msamaha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu katika kipindi hiki cha Oktava ya Noeli, Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Sherehe ya Fumbo la Umwilisho. Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na mkombozi wa ulimwengu aliamua kuzaliwa, kukua na kuishi katika familia, ili kutaka taasisi hii ambayo ni msingi wa kila jamii. Yesu katika kimya kikuu, aliishi ndani ya Familia Takatifu ya Nazareti. Maandiko Matakatifu yanaelezea kidogo sana kuhusu maisha ya Familia Takatifu, lakini tunaweza kupata kwa undani kabisa maisha na utume wa Kristo Yesu. Mama Kanisa anaiweka Familia Takatifu kuwa ni kielelezo na mfano bora wa kuigwa na familia za Kikristo. Familia Takatifu ni shule ya tunu msingi za Kiinjili, changamoto na mwaliko kwa familia za Kikristo kujenga familia zinazokita mizizi yake katika Injili ya uhai, upendo na mshikamano wa kidugu. Sikukuu hii inapata chimbuko lake tangu katika uongozi wa Baba Mtakatifu Leo XIII aliyekuwa na maono ya kinabii kuhusu familia. Papa Benedikto XV, kunako mwaka 1921 akaiweka kwenye Kalenda ya Liturujia ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe na Baraka za Noeli kwa Mwaka 2020 maarufu kama “Urbi et Orbi” anasema kwamba, Kristo Yesu alizaliwa katika hori ya kulishia wanyama, lakini akazungushiwa upendo uliokuwa unabubujika kutoka kwa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu. Kwa Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu amebariki, ametakasa na kuweka wakfu upendo wa kifamilia. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwakumbuka na kuwaombea wale wote ambao kutokana na sababu mbalimbali hawataweza kuungana na familia zao; wale ambao wamelazimika kubaki wakiwa wamejifungia majumbani mwao kwa sababu mbalimbali lakini hasa zaidi kutokana na ongezeko kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa watu wote hawa, Sherehe za Noeli ni muda muafaka wa kutambua na kugundua kwamba, familia ni chemchemi ya Injili ya uhai na imani; mahali pa upendo wenye ukarimu; mahali pa majadiliano katika ukweli na uwazi; msamaha, mshikamano wa kidugu na furaha shirikishi; familia ni chemchemi ya amani kwa ajili ya binadamu wote!

Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, huku akiadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Yosefu. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” uliozinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2020 na unatarajiwa kufungwa tarehe 8 Desemba 2021 anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu kuwa ni “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika unyenyekevu Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa haki, akajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa.

Liturujia ya Neno la Mungu, Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu kwa namna ya pekee kabisa inatilia mkazo umuhimu wa upendo, utii, unyenyekevu na msamaha katika maisha ya ndoa na familia. Familia Takatifu ilijitahidi kumwilisha imani katika uhalisia wa maisha yake, hatua kwa hatua. Ikakoleza upendo wake katika hali na mazingira ya kawaida, licha kwanza, walikuwa wamekirimiwa neema kutoka mbinguni. Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa anataka kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Waamini watambue dhambi, vikwazo vya maisha ya ndoa na familia; machungu yake, tayari kujikita katika mchakato wa toba, wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho wa kweli; mwanzo mpya wa maisha ya ndoa na familia.

Baba Mtakatifu anaichambua familia “kama karanga” huku akiwa na jicho la huruma na upendo wa Mungu, ili kuwatangazia wanandoa Injili ya furaha. Wosia huu hauna nafasi ya kumbeza mtu awaye yote bali unajenga jukwaa la upendo, ukarimu, toba, msamaha na upatanisho, tayari kuandika na kushuhudia Furaha ya upendo ndani ya familia. Anakazia kwa namna ya pekee: utakatifu wa maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, watu wote wanahitaji kuonja na kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Wakristo wanapaswa kushuhudia uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia; kwa kuwajibika na kuonesha ukarimu, neema na baraka zinazobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wanandoa wakristo wawe wanyenyekevu wanaoshuhudia uhalisia wa maisha pasi na unafiki, ili kweli vijana wa kizazi kipya waweze kuvutika kujenga msingi wa maisha bora ya ndoa na familia. Wakristo wafahamu pia kwamba, ndoa si lelemama! Ina utakatifu, uzuri na wema wake, lakini pia ndoa ni sawa na dawa ya mchunguti, inachangamoto na karaha zake zinazopaswa kufafanuliwa ili watu waweze na mwelekeo mpana zaidi wa maisha ya ndoa na familia, changamoto ya wongofu wa kichungaji.

Wanafamilia wanahimizwa kutafuta na kutekeleza mapenzi ya Mungu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana; huku kila mtu akijitahidi kutekeleza dhamana na majukumu yake ndani ya familia, ili hatimaye, kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa kibinadamu. Familia imekabidhiwa dhamana na wajibu wa kuendeleza kazi ya uumbaji inayowashirikisha wanandoa upendo na maisha ya Kimungu. Ni katika muktadha huu, familia inapaswa kuwa ni “tabernakulo ya Injili ya uhai” dhidi ya utamaduni wa kifo. Huuu ndio ushuhuda wenye mvuto na mashiko, unaopaswa kutolewa na wanandoa wenyewe, kwani haya ni maisha yanayowataka watu kuthubutu. Hii inatokana na ukweli kwamba, familia ni chemchemi ya utakatifu wa maisha. Upendo ndani ya familia unapaswa kupyaishwa siku kwa siku ili kuboresha maisha ya ndoa na familia. Huu ni upendo kwa Mungu na jirani. Huu si upendo wa mtu kujisikia, bali ni ule upendo wa dhati kabisa yaani “Agape” kama anavyosimulia Mtakatifu Paulo katika utenzi wa upendo. Rej. 1 Kor. 13: 1-13. Hiki ni kielelezo cha upendo unaogeuka kuwa zawadi na sadaka, msingi bora wa familia.

Ndoa ni safari inayowawezesha wanandoa kusaidiana, kutakatifuzana na kutanguzana katika maisha, wakati wa raha na machungu; wakati wa furaha, kicheko na shangwe ya mafanikio ya maisha! Jambo la msingi ni kujenga dhamiri nyofu miongoni mwa watu; kwa kujikita katika malezi, elimu na katekesi makini na endelevu, kuhusu maisha ya ndoa na familia, tayari kumjengea mtu uwezo wa kuwajibika na kudumu katika maamuzi yake. Utengano na talaka ni magumu na machungu yasiyovumilika katika maisha ya ndoa! Mchakato wa uhuru na ukomavu ni muhimu sana katika udumifu wa maisha ya ndoa na familia. Dhamiri nyofu inaweza kuanza kutambua nyakati za shida na magumu ya maisha tayari kuzifanyia kazi kwa kutafuta ufumbuzi wa kudumu, na ukomavu wa maisha ya Kikristo mchakato unaotekelezwa kwa kumwambata Kristo Yesu.

Msamaha ni msingi wa amani, utulivu wa ndani, uhai na maisha mapya. Pasi na msamaha wa kweli, familia zitageuka kuwa ni uwanja wa fujo. Msamaha unauhisha moyo, unasafisha na kutakasa akili na hivyo kuuweka moyo huru. Ni changamoto ya kuponya madonda ya ndani, tayari kuanza upya kwa ari na moyo mkuu. Msamaha ni chemchemi ya furaha, upendo, ukarimu na unyenyekevu na kwamba, msamaha ni matunda ya neema ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Wanafamilia wajifunze kusamehe na kusahau. Itakumbukwa kwamba, Kanisa tangu mwanzo limekuwa likitoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa familia, kwa kutambua kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana.

Huu ndio mwelekeo wa pekee uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto inayofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Lakini, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto pevu kama zilivyoainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa.

Familia Takatifu
26 December 2020, 15:44