Sikukuu ya Familia Takatifu Yesu, Maria na Yosefu: Upendo
Na Padre Paschal Ighondo, -Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, katika Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Katika Liturujia ya sherehe hii maneno ya wimbo wa mwanzo yanaeleza wazi wahusika wakuu wa familia takatifu ukisema; Wachungaji wakaenda kwa haraka wakamkuta Maria na Yosefu, na yule mtoto mchanga amelala horini. Katika sala ya mwanzo tunaomba neema ya kuiga mfano bora wa hii familia tukisema; Ee Mungu, umependa kutuonyesha mifano bora ya Familia takatifu. Utujulie kwa wema tuweze kufuata mifano ya hiyo Familia takatifu katika fadhila za nyumbani na kuungana kwa mapendo. Kumbe upendo ni kiini cha familia ambao kwao furaha inapatika ndiyo maana Papa Francisko katika barua yake ya kichungaji juu ya maisha ya familia, maneno yake ya mwanzo kabisa ni “Amoris Letitia” furaha ya upendo. Kwamba katika magumu yote; upendo unaleta furaha.
Kiini na mwanzo wa sherehe hii. Mnamo mwaka 1921 Baba Mtakatifu Benedicto XV, aliiweka rasmi sikukuu hii iadhimishwe jumapili katika oktava ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, au tarehe 30 Desemba. Katika sherehe ya Kristo Mfalme mwaka 1981, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II aliandika barua ya kitume “Familiaris consortio” ikieleza wajibu wa familia ya Kikristo kwa Kanisa na ulimwengu, anasema kuwa; familia ni kanisa la nyumbani. Familia ni shule ya sala, shule ya upendo, shule ya amani na mshikamano. Familia ni makao ya furaha na kitalu cha uhai. Katika hitimisho la barua hii Baba Mtakatifu Yohane Paulo II aliziweka familia zote chini ya ulinzi na usimamizi wa Yesu, Maria na Yosefu. Kumbe kiini na lengo kuu la Kanisa kuadhimisha sikukuu hii ya familia Takatifu, ni kuziombea familia zote zikue na kuishi kwa mshikamano zikimpendeza Mungu, zikidumu katika pendo lake, ziweze kujaa amani tele na baraka zake mwenyezi Mungu ziwe ndani mwao milele yote.
Familia ni nini? Familia ni muungano wa Mume na mke, unaofungamishwa na upendo na tunda litokanalo na Upendo wao ni watoto ambao ni zawadi toka kwa Mungu na ndiyo inayowafanya waitwe wazazi; Baba na mama. Familia ni mpango wa Mungu. Tangu mwanzo aliwaumba mume na mke, Adamu na Eva akawashirikisha uwezo wake wa uumbaji ili tunu ya uhai iendelee kuwepo duniani. Kumbe familia ni wito wa kuishi pamoja kwa wanandoa, kuendeleza kazi ya uumbaji na kuwezesha mwendelezo wa tunu ya uhai kwa kuzaa watoto, kuwalea na kuwaridhisha tunu zilizo njema. Kanisa linajali familia kwani ndiyo ni kitovu cha uumbaji, shule ya kutambua mapenzi ya Mungu. Katika familia Injili inapaswa kusomwa na kutafakariwa, liturujia inapata msingi kwa njia ya sala, nyimbo na sakramenti.
Katika somo la kwanza Yoshua Bin Sira anawausia watoto namna wanavyopaswa kuishi na wazazi wao, kwamba wanapaswa kuwa na heshima ya kina na upendo kwa wazazi wao, hususani wanapozeeka. Yoshua Bin Sira anasema; watoto wanaowaheshimu wazazi wao watapata baraka tele duniani, na sala zao zitasikilizwa na kamwe hawatajuta katika maisha yao hata siku moja. Mungu lazima atawalipa kwa heshima na upendo wao kwa wazazi wao, atawajalia watoto wa uzao wao wenyewe, atawapa maisha marefu yenye fanaka hapa duniani, atawasamehe dhambi zao na mwisho kwa ukarimu wao atawapokea katika ufalme wake mbinguni. Hivi ndivyo wanavyopaswa kuwa watoto katika familia za kikristo. Lakini haya yote yanategemea msingi wa malezi bora ya kiimani na kimaadili toka kwa wazazi; Baba na Mama ambao wanapaswa kukaa pamoja kwa upendo ili toka kwao watoto wajifunze tunu bora na njema.
Mtume Paulo katika somo la pili la waraka wake kwa Wakolosai, anatupa miongozo ya familia ya Kikristo kwa nyakati zote ambayo ni fadhila Kristo hasa upendo na uvumilivu. Kila mmoja katika familia atampendeza Mungu kwa kutimiza wajibu wake. Lakini tukumbuke kuwa Paulo anaongea juu ya familia za aina mbili, yaani familia asili ya baba, mama na watoto na familia ya kiimani, ndiyo Jumuiya ya Kikristo. Paulo anatambua fika kwamba mstakabili wa familia ya kiimani yaani jumuiya ya Kikristo hutegemea sana vile zilivyo familia asili ya baba, mama na watoto. Umoja na mshikamano katika jumuiya ya kikristo vitakuwepo kama tukijivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, moyo wa kuchukuliana na kusameheana kama Mungu anavyotusamehe sisi huku tukiepuka ubinafsi na tujivike upendo ambao ndio kifungo cha ukamilifu wote. Haya yote yanapaswa kufundishwa katika familia kwani; familia ni msingi wa mafundisho yote ya kiimani na kimaadili.
Fundisho la kwanza katika familia linasimikwa katika sala. Familia ni shule ya sala. Upendo wa kifamilia na mshikamano hutokomea mara tu familia inapoacha kukutana kwa sala na kutokusoma neno la Mungu. Ndiyo maana Paulo amesema: “Neno la Kristo likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi na nyimbo, na tenzi za rohoni, huku mkimwimbia Mungu kwa Neema mioyoni mwenu” Kol 3:16. Familia ya kikristo inapaswa kukusanyika pamoja ili kulisoma neno la Mungu na kulitafakari ili kushirikishana utajiri na tunu zilizomo katika neno la Mungu na hivyo sala yao kupata msisimko utokanao na mwangaza wa Roho wa Mungu na hivyo furaha ya upendo itadumu kati ya wanafamilia.
Injili ilivyoandikwa na Luka inaeleza jinsi wazazi wa Yesu walivyoshika Torati na desturi za kidini za taifa lao ambazo kwazo walimridhisha mtoto wao Yesu naye akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake. Yosefu na Maria walimtolea Yesu Hekaluni. Hili ni tendo la utakaso, Ibada na Majitoleo. Katika hili wanamkuta Simeoni Hekaluni, akitoa unabii wake juu ya Yesu na Maria ya kwamba Mtoto Yesu atakuwa, nuru ya mataifa, wokovu kwa wengi, anguko la wasiomwamini. Maria atateseka kwa sababu ya mwanae kwani utabiri unasema, “upanga utapenya Moyoni mwake, na humo yatafunuliwa mawazo mengi.” Maria anayaweka haya moyoni mwake. Katika familia baba anapaswa kuwa ni nguzo inayohakikisha ulinzi, ustawi, mahitaji na maendeleo ya kweli ya familia yanapatikana. Kwa upendo, Baba anapaswa kufanya kazi kwa bidii, huku akimcha Mungu, kuwapa watoto wake malezi bora kwa kuwawekea na kuwapa mipaka katika maisha yao ili waweze kujengeka katika utu wema, wakimpenda Mungu na jirani.
Katika familia Mama ni jiwe la msingi katika kulea watoto, kulinda tunu za familia yaani utu, kazi, upendo, umoja, nidhamu na amani. Mama mwema wa familia siku zote atamheshimu mume na kuwapenda watoto wake, atamcha Mungu na kupigania ustawi na mafanikio ya familia yake kiroho, kimaadili na kiuchumi. Huyu ni mke mwema. Ataepuka majungu, starehe feki, usaliti na uvivu. Watoto ni zawadi toka kwa Mungu katika Familia, ni vyema basi kumtukuza Mungu kwa kuwalea vyema katika maadili mema ya jamii, kumwogopa Mungu na siku zote kuwaridhisha tunu za kiutamaduni na kidini. Watoto pia wanapaswa kuwaheshimu wazazi wao ambao ni wawakilishi wa Mungu duniani ili waishi vyema kama Yesu na wakue katika kimo na hekima. Kwa bahati mbaya sana malezi ya watoto nyakati hizi yamekuwa ya mayaya na shule tu. Kazi zimekuwa chanzo cha kuwanyima watoto haki zao za msingi na kuonja upendo wa wazazi; Baba na Mama. Haki za watoto zinakanyagwa bila shida. Wazazi wanapoamua kupeana talaka sababu ya ubinafsi na umimi uliokidhiri, hawaangalii kabisa hatima ya watoto.
Kwa sababu ya kulinda hadhi na uzuri wa mwanamke; watoto wananyimwa haki ya uhai; wanauwawa wangali tumboni mwa mama zao, na wakiruhusiwa kuzaliwa, wananyang’anywa haki ya chakula chao; maziwa ya mama. Hivyo jamii yetu ya kisasa inakuwa na wazaaji zaidi ya wazazi, na hivyo kusababisha watoto yatima wengi, mbaya zaidi kuwa na watoto yatima wa wazazi walio hai, maana wazazi hawana mda nao mayaya na walezi tunaowaita shule wamechukua nafasi zao. Dhana ya kuwa familia ni shule ya Upendo, uinjilishaji, utu, tabia, imani na kitovu cha miito mitakatifu ya ndoa, utawa na ukuhani inazidi kufifishwa na kuuwawa kikatili. Wazazi tuwajibike. Tuwapende na kuwajali watoto wetu. Urithi kwa watoto wetu ni malezi na elimu bora ya kimwili na kiroho. Tusizinajisi ndoa na familia zetu. Tuzilinde tunu za ndoa ya Kikristo; Upendo, uaminifu, uvumilivu, uwazi, uwajibikaji, kusameheana na maisha ya sala. Tukumbuke kuwa ndoa imeasisiwa na Mungu. Ni agano lisilotenguliwa ambapo wanandoa wanajitoa na kupokeana na kwa njia ya sakramenti ya ndoa wanajitakatifuza na kutembea pamoja kuelekea ukamilifu wa maisha ya utakatifu. Tutambue kuwa familia bora ya Kikristo ni lazima iwe na Kristo kama mhimili wake akimsaidia kila mmoja kutimiza wajibu wake vyema; mke kumtii mme wake, mme kumpenda mke wake, watoto watawatii wazazi wao na wazazi nao hawatawachokoza watoto wao, nao hawatakata tamaa.