Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio: Mambo msingi: Kukesha, kusali na kufunga kama njia ya kuratibu vilema vya maisha tayari kumpokea Masiha anayezaliwa katika maisha. Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio: Mambo msingi: Kukesha, kusali na kufunga kama njia ya kuratibu vilema vya maisha tayari kumpokea Masiha anayezaliwa katika maisha. 

Tafakari Jumapili 1 ya Majilio: Kesha, Funga na Sala!

Kipindi cha Majilio ni wakati muafaka kwa waamini kutafakari kuhusu Fumbo la Umwilisho pamoja na Ujio wa pili wa Yesu, atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Ni muda kwa waamini kujikita zaidi katika maisha ya kukesha, kufunga, kusali, kujinyima pamoja na kumwilisha yote haya katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Na Padre Gaston George Mkude, -Roma.

Amani na Salama! Dominika ya kwanza ya Majilio, ndio Dominika ya kwanza ya Mwaka wa Kiliturjia wa Kanisa. Mwaka wa Kiliturjia wa Kanisa umegawanyika katika vipindi mbali mbali, na nia na shabaha yake ni katusaidia kutafakari fumbo la Kristo. “Lakini, shukrani kwa Mungu anayetuongoza daima katika msafara wa ushindi wa Kristo. Yeye hutufanya tuueneze ukweli wa Kristo kama harufu nzuri, kila mahali” 2 Wakorintho 2:14. Hivyo Mama Kanisa kwa kusukumwa na ukweli wa utume huo wa kusambaza harufu nzuri ya wema wa Mungu kwetu, amepanga sherehe mbali mbali zinazimuhusu Kristo, ili kwa msaada wa hizo tuweze kumtafakari ili tuweze kumjua na kumpenda zaidi na zaidi. Pamoja na kwamba, leo tunaona mwaka wa Kanisa unaanza, Dominika ya kwanza ya majilio, Dominika nne zinazotangulia sherehe ya Umwilisho, na ndio Noeli, mambo hayakuwa hivyo katika Kanisa lile la mwanzo. Waamini wale wa Kanisa la mwanzo, daima walikutana siku ya kwanza ya juma, waliyoiita pia “Siku ya jua”, walikusanyika pamoja katika siku hiyo ya kwanza ya juma, kusikiliza Neno la Mungu, kuumega mkate, yaani kuadhimisha Ekaristia na hata kwa kweli walikuwa wanakula mlo wa kawaida wa pamoja.

Na baada ya maadhimisho hayo kila mmoja alirejea nyumbani kwake. Hivyo, walikusanyika kila siku ile waliyooita ya jua na kuadhimisha kwa pamoja, na hapo waliagana na kukutana tena siku nyingine ya jua. Ni tayari katika karne ya pili, jumuiya nyingi wakaanza kuona uhitaji wa kutenga siku pia ili kuadhimisha Sherehe ya Pasaka. Hata hivyo wakaona tena siku moja tu kuadhimisha fumbo la mateso, kifo na ufufuko wake Kristo, haikutosha, na hapo wakaongeza iwe ni kipindi cha majuma saba, ndio siku hamsini za Pasaka na kuhitimishwa na Sherehe za Pentekoste. Hivyo, sherehe ya Noeli, ndio ya Umwilisho wa Kristo, ilianza kuwepo baadaye sana mnamo katika karne ya nne. Ilikuwa ni mwaka 354 BK, walipoanza kuadhimisha sherehe ya Noeli, Disemba 25. Ni moja ya siku katika kipindi cha majira ya baridi huko Roma, ambapo ilikaribia na ile siku walipoanza kuliona tena jua kwa muda mrefu, kipindi ambapo pole pole mchana unaanza tena kuwa mrefu kuliko usiku. Na kwa kweli Warumi, walikuwa wanasherehe zao nyingi za kipagani, kuhusu mungu jua.

Waamini wale wa Mwanzo, kwa kumtambua Yesu Kristo kama jua la kweli na haki, ndiyo nuru ya kweli iliyoshuka kutoka mbinguni, wakaona umuhimu wa kubadili maana zile za kipagani na kuanza kusherehekea sikukuu kumuhusu Yesu Kristo. “Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma. Atatuchomozea mwanga kutoka juu, na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo, aongoze hatua zetu katika njia ya amani.” Luka 1:78-79. “Huo ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote.” Yohane 1:9 Ilikuwa kuanzia mwaka 600 BK, waamini wale wa kwanza, wakaona umuhimu wa kutenga majuma kadhaa ya matayarisho pia kabla ya kuadhimisha Sherehe za Noeli. Na ndio hapo wakaona mwaka wa Kanisa hauna budi kuanza na Dominika ya kwanza ya Majilio, Dominika inayoangukia mwishoni mwa mwezi Novemba au mwanzoni wa Disemba. Majilio, ni neno linalotokana na neno “Ujio”, na hata katika mazingira ya kipagani walitumia neno hilo kumaanisha ujio wa miungu yao, anayekuja ili kuwabariki, au pia ujio wa mtu fulani muhimu kama vile mtawala na wafalme.  Na ndio utaona wakristo wale wa mwanzo, nao wanatumia neno hilo la ujio wakimaanisha ujio wa Kristo katika maisha yao.

“Hivyo akawaambia, kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa kifalme aliyefanya safari kwenda nchi ya mbali ili apokee madaraka ya ufalme, halafu arudi. Basi, kabla ya kuondoka, aliwaita watumishi wake kumi, akawapa kiasi cha fedha kila mmoja na kuwaambia: Fanyeni nazo biashara mpaka nitakaporudi.” Luka 19:12-13. Kutoka mfano huo, tunaposoma tena zaidi Maandiko tunakutana na maneno mengine ya Yesu; “Sitawaacha nyinyi yatima; nitakuja tena kwenu.” Yohane 14:18. Hata waamini wa Kanisa la mwanzo daima walisali kwa imani; “MARANATHA – BWANA NJOO!” 1Wakorintho 16:22 Na hata Kitabu cha Ufunuo pia kinahitimishwa kwa maneno au sala hiyo ya ujio wa Yesu Kristo. “Njoo Bwana Yesu!” Ufunuo 22:20. Ni kawaida kujiandaa kwa ujio wa mtu muhimu, na ndio basi Kanisa linatenga majuma haya manne ili kimoja wetu apate nafasi ya kujiandaa kwa ujio wake Masiha. Somo la Injili ya leo, linaweka mkazo mkubwa katika wazo zima la “Kesheni”, ndilo neno linalotumika mara nyingi katika sehemu ya Injili ya Dominika ya kwanza ya Majilio.

“Angalieni, kesheni”, “…naye amemwamuru bawabu akeshe”, “Kesheni basi”, “…nawaambia wote, kesheni”. Ndio kusema neno kuu leo au wazo kuu katika somo la Injili ni “Kukesha”. Na Yesu analirudiarudia mara nyingi, ndio mtindo wa marabi hasa pale walipotaka kufundisha jambo zito na ili kuwasaidia wanafunzi wao kuweka maanani na kulizangatia fundisho, walifundisha kwa kurudiarudia ili kutilia mkazo na msisitizo. Yesu leo anarudiarudia ili kuweka msisitizo juu ya umuhimu na hasa ulazima wa kukesha. Mwanzoni tunashindwa kupata ujumbe wa kukesha, kwani matukio yanayojiri katika sehemu ya Injili ya leo ni ngumu kupata muunganiko wake. Ni Yesu kwa nafasi ya kwanza anaongea moja kwa moja kwa wanafunzi na wasikilizaji wake, na ghafla tunaona anaongea nao kwa mfano, na mwisho anarudia kuongea nao moja kwa moja. Mwanzoni, wito wa kukesha, Yesu anautoa kwa wote; “Yesu aliwaambia wafuasi wake: Angalieni, kesheni, kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo” Na mara tunaona anaanza kuongea na bawabu, ndio mlinda au mlinzi wa mlangoni. “…naye amemwamuru bawabu akeshe”, Na tena anaona wito huo sio tu kwa bawabu peke yake, kwa mlinda mlango, bali pia kwa wote tunaalikwa kukesha.

Ni katika somo hili, tunaona Yesu akiwaalika kwa nafasi ya kwanza sisi sote kukesha na pili anapowageukia pia mitume, wale wenye wajibu maalumu katika Kanisa, kama walinda mlango, wenye wajibu wa kuwaongoza wengine, ndio wao wanaopaswa kubaki mlangoni ili kuhakikisha usalama wa kundi zima zizini, na ndio leo Baba Mtakatifu, na Maaskofu wanaokuwa na wajibu ule ule wa Mitume, na wasaidizi wao, yaani makasisi na mashemasi, hawa ni walinda mlango, ni bawabu, wanaoalikwa nao kwa namna ya pekee kukesha. Lakini Injili ya leo tunaona Yesu anapanua mwaliko wake kwa sisi wengine wote, kwa jumuiya nzima ya wanakanisa, tunaalikwa sote kuwa macho na kukesha. Kwa nini kukesha? Kwa nini kila mara msisitizo ni ujio wa saa ya usiku? Kwa nini bwana mwenye nyumba anakuja siku ile tusiyodhania, na kwa nini asije saa ya mchana, saa ambayo sisi sote tunakuwa macho na hivyo tayari kumpokea na kumlaki? Na labda anakuja kutoka wapi? Haya na maswali mengi, ni msaada kwetu katika kupata ujumbe kusudiwa wa somo la Injili ya leo juu ya kukesha na ujio wake mwenye nyumba.

“Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi; asije akawasili ghafula akawakuta mmelala”. Kwa kweli yafaa tangu mwanzoni kama tulivyoona hapo juu, Yesu hata baada ya kupaa mbinguni, bado yupo pamoja nasi, yupo kati kati yetu sio tena kwa namna ile kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake, bali anabaki kuwepo katika namna nyingine, katika mtindo mwingine, hivyo ujio wake kati yetu, hauwezi kuwa na maana kana kwamba sasa hayupo kati yetu, hayupo pamoja na Kanisa lake. Mhusika mkuu wa mfano anaoutumika leo, ni Yesu Kristo mwenyewe. Lakini tunajiuliza mara moja, Je, Yesu amekwenda wapi, je, kweli hayupo kwa sasa pamoja na Kanisa lake? Kwa hakika tunaona Yesu hajaondoka na kuliacha au kulitekeleza Kanisa lake, ila anadumu kuwepo katikati yetu katika mtindo mwingine, katika namna nyingine. Leo, Yesu yupo karibu nasi sote kuliko hata alipokuwa akitembea katika mitaa ile ya nchi ya Palestina.

Mwenyeheri Carlo Acutis, daima alitambua kuwa sisi tunaoishi leo kuwa wenye bahati kuliko wazee wetu walioishi nyakati za Yesu akiwa duniani katika mwili wa nyama, Mwenyeheri Carlo Acutis, alikuwa anapenda kusema na kufananisha kuwa walioishi nyakati za Yesu ili kumuona Yesu, walipaswa kutembea na kumuona au kumshika na kumgusa pale alipokuwepo kwani alikuwa bado anabanwa na mahali na muda, lakini sisi leo itoshe tu kukutana naye katika Neno lake, katika masakramenti na kwa namna ya pekee, katika Yesu wa Ekaristi Takatifu. Leo kila Kanisa lenye Yesu wa Ekaristi Takatifu ni Yerusalemu ndogo, ni mbinguni kwa hakika, ni hapo tunakutana na Yesu mzima, Mungu kweli na mtu kweli katika maumbo yale ya mkate na divai. Imani yetu inajengeka katika fumbo la “Umwilisho”, kama vile hakuna wokovu bila umwilisho, basi hata na uhai wa Kanisa bado unategemea katika uwepo wake Kristo katika Sakramenti ya altare na katika Injili yake, yaani Neno lake linalodumu na kukaa katikati yetu. Yesu Kristo, katika mwili wa ufufuko, ni mwili usiotawala tena wala kuwa chini ya mipaka ya kimahalia na muda, ni Yeye anayebaki kila mahali na hasa akitaka kuweka makao yake katika nafsi na maisha yak ila muumini. “Nami nipo pamoja nanyi siku zote; naam, mpaka mwisho wa nyakati.” Mathayo 28:20

Na kwa vile Yesu leo anabaki katikati yetu sio katika mwili wa nyama bali ule wa ufufuko, hatuna budi nasi kumuona sio kwa jicho la nyama, bali lile la imani. Ni kwa jicho la imani, tunamwona Yesu mzima katika maumbo yale duni ya mkate na divai, tunamuona kati ya ndugu zetu maskini na wahitaji na waaokuwa wanyonge, tunamuona katika masakramenti na pia katika Injili yake, katika Habari Njema. Tuzidi kumuomba Mungu, imani thabiti na ya kweli ili tuweze daima kutambua uwepo wake katikati yetu.  “Lakini kumbukeni jambo hili: kama mwenye nyumba angejua siku mwizi atakapofika, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe. Kwa hiyo, nanyi pia muwe tayari, kwa maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia.” Matayo 24:43-44. Na hata wala wanawali kumi; “Kwa kuwa bwana arusi alikawia kuja, wale wasichana wote walisinzia, wakalala. Usiku wa manane kukawa na kelele: Haya, haya! Bwana arusi anakuja, nendeni kumlaki.” Mathayo 25:5-6

Wazo la kukesha ni wazo linalojirudiarudia tena kwa msisitizo mkubwa katika Injili, sio wazo tunalolisikia mara moja tu, kama tulivyoona hapo juu kila mara wazo hili na umuhimu wa kukesha ukijirudia tena kwa msisitizo mkubwa. Usiku katika Maandiko, ndio muda wa giza kubwa, ndio wakati wa kuishi kinyume na mapenzi ya Mungu, kinyume na Neno lake. Kukesha hapa, haina maana ya kutokulala usingizi wa kawaida, bali tunahimizwa kutokubali kusinzia katika kuacha kutenda yale anayotuagiza Yesu Kristo katika Injili yake. Ni sawa na kuwa usingizini pale tunapokwenda kinyume na Injili ya Yesu Kristo kwa kukubali kuongozwa na mantiki na mitindo ya ulimwengu, kwa kukubali kuwa mbali na Mungu ni sawa na kutembea katika giza nene, ni kubaki usingizini kwa kukubali kuenenda katika matendo ya giza. Katika matendo yanayokuwa kinyume na mapenzi yake, kinyume na Neno lake. Anayekesha ni yule daima anayekubali kuishi heri za mlimani na amri ile kuu ya mapendo kwa Mungu na kwa jirani, ni mmoja anayekubali kuongozwa na mantiki ya Injili n asio ile ya ulimwengu huu. Ni mmoja anayekubali daima Mungu mwenyewe awe mtawala na kiongozi wa maisha yake. Kila mmoja wetu tunaalikwa kutembea kama wana wa mwanga, kwa kuongozwa na Yesu Kristo Mwenyewe katika maisha yetu.

Ili tuweze kudumu katika kukesha, kuna silaha za kutusaidia kubaki katika kukesha, na siri ya kwanza ni sala. Kusali ni kuingia katika mahusiano na Mungu, sio mahusiano ya ujasiriamali, hatusali ili tujaliwa vitu fulani fulani kutoka kwa Mungu, hapana, kusali ni kujenga mahusiano mazuri na Mungu kwa nafasi ya kwanza, kusali ni kuongea na Mungu kwa nafasi ya kwanza, ni mazungumzo ya Baba yetu Mwema na Mwenyehuruma kwetu na ndio maana katika mazungumzo hayo tunaweza kumpelekea shida na mahangaiko yetu, tunaweza kumsifu hali kadhalika kuomba huruma yake. Kusali ni kitendo cha kumpenda Mungu, katika sala zetu hapo tunaonesha kwa nafasi ya kwanza mapendo yetu kwa Mungu na ndio maana kila anayesali kweli basi atampenda Mungu na jirani. Haitoshi kusema tunampenda Mungu kama hatumpendi jirani, na sala zetu zinabaki kama za mafarisayo, chukizo mbele ya Mungu kwani hazijajenga katika upendo kwa Mungu na baadaye kwa jirani, kwa mwingine anayekuwa muhitaji na mnyonge katika maisha yetu.

Maisha yetu hayana budi kila mara kumuakisi Kristo, iwe ni maneno yetu, matendo yetu, mawazo yetu, kueneza harufu nzuri ya uwepo wake katika ulimwengu wetu, iwe katika familia zetu, jumuiya zetu, mahali pa kazi, maparokiani na popote pale. Maisha ya kukesha ni maisha ya kuwa mwanga wa kweli na chumvi katika ulimwengu wetu wa leo. Leo uinjilishaji wa kweli na ambao unagusa wengi, sio kusimama majukwani na kuhubiri bali kuhubiri kwa maisha yetu, kuhubiri kwa matendo yetu ya siku kwa siku, kuwa kweli nuru kwa wengine ili waweze kukutana kweli na Yesu Kristo. Kila muumini anapaswa kuwa mbebaji wa Yesu Kristo, hivyo kila mara ninapokutana na wengine na hasa wale wanaokuwa mbali na Kristo waweze kukutana naye kupitia sisi tulio marafiki na wafuasi wake Kristo.

Mwenyeheri Carlo Acutis, atuombee ili nasi tuweze kuwa na imani iliyo komaa na thabiti kama yake, ya kuutambua uwepo wa Yesu Kristo mzima katika Ekaristi Takatifu, kuwa na hamu ya kukutana na Yesu anayedumu katika makanisa yetu na pia katika Injili yake Takatifu, tupende kulisoma Neno lake na kuliruhusu kubadili maisha yetu. Dominika na tafakari njema.

14 December 2020, 14:58