Tafakari Jumapili 3 Kipindi cha Majilio: Furahini Katika Bwana!
Na Padre Gaston George Mkude, -Roma.
Amani na Salama! Katika somo la Injili ya Dominika ya leo kama ile iliyopita tunaona Yohane Mbatizaji kama mmoja wa wahusika wakuu. Mwinjili Marko katika Injili ya Dominika iliyopita alituonesha Yohane Mbatizaji kama mtangulizi, kama mmoja aliyetumwa kuandaa njia kwa ajili ya ujio wake Masiha, ni kwa njia yake anawaandaa pia watu kubadili maisha yao kwa kupokea ubatizo wa maji ili wawe tayari kumpokea Masiha. Na leo Mwinjili Yohane anatuonesha pia Yohane Mbatizaji kama mtangulizi, kama mmoja anayekuja ili kutoa ushuhuda, kama sauti. Mwinjili Yohane katika utangulizi wa Injili yake, anamtambulisha Yohane Mbatizaji kama shuhuda, anayekuja kutoa ushuhuda wa Neno wa Mungu anayefanyika mwili na kukaa kati kati yetu. Bado Yohane Mbatizaji kama sauti au kama kidole kinachotuonesha na kututambulisha Kristo, Masiha wa Mungu anayekuja na kukaa kati yetu. Yohane mbatizaji anakuja ili kuishuhudia ile nuru ya kweli, nuru itokayo kwa Mungu mwenyewe.
Katika masomo ya Dominika ya leo tunakutana na sauti za watu au makundi matano. Sauti zote hizi zikiwa na nia moja ya kutuonesha na kutulekeza ulipo Ufalme wa Mungu, alipo Mungu, ilipo nuru na mwanga wa kweli, ilipo furaha ya kweli. Ni sauti ya Nabii Isaya katika somo la kwanza, anajitambulisha kujawa na Roho wa Bwana kwa kumpaka mafuta ili akahubiri Habari Njema, akahubiri Injili, Habari ya Furaha na matumaini kwa watu wake waliokuwa bado uhamishoni Babeli. Nabii Isaya ni mjumbe wa Habari ya Jubileo kuu, anayekuja kutangaza mwaka wa kuachiwa huru watumwa, wadeni kusamehewa madeni yao, na kuutangaza mwaka wa amani. Kwa wayahudi wakiwa katika nchi yao ya ahadi, kila baada ya miaka hamsini, walifanya jubileo, ndio mwaka wa furaha na shangwe kubwa, ni mwaka uliokubalika machoni pa Bwana.
Mwaka wa Jubilei, ni Mwaka wa huruma ya Mungu kwa watu wake, ni mwaka ambapo walipokea tangazo la furaha na matumaini, wafungwa kuwa huru, matumaini mapya kwa maskini na waliokata tamaa na waliosetwa na jamii. Na jubileo kuu ilikuwa ni mwaka ule waliporejea tena katika mji ule mtakatifu wa Yerusalemu. Maneno haya tunayoyasikia kutoka kwa Nabii Isaya, baada ya karne tano baadaye yanasikika tena katika sinagogi pale Kapernaumu, ni maneno yanayotimia katika nafsi yake Yesu Kristo: “Andiko hili mlilosikia limetimia leo” (Luka 4:16-21). Ndio kusema unabii wa Isaya unatimia kwa ujio wake Yesu wa Nazareti, ni kwa njia ya Yesu kama Masiha na Kristo wa Bwana, watu wote wanapata uhuru, amani na furaha ya kweli. Ni kwa njia yake Mwenyezi Mungu anatuzushia nuru yake ya kweli. Hata hivyo haikuwa rahisi kuitambua au kumtambua Yesu wa Nazareti kama Kristo wa Bwana, si tu kwa watu wa nyakati zake bali hata katika siku zetu leo hii.
Mwinjili Yohane anatuonesha kuwa ujio wa Yesu Kristo ulimwengu, ni sawa na nuru kutuzukia sisi tuliokuwa tukitembea bado gizani. “Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu. Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda” (Yohane 1:4-5). Na ndio tunaona katika somo la Injili ya leo, Yohane Mbatizaji anatambulishwa kama mmoja aliyetumwa ili kuja kuishuhudia hiyo nuru. Katika aya mbili tu, neno ‘’ushuhuda’’ linatajwa mara tatu. “Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohane. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Na huu ndio ushuhuda wake Yohane.” Ilikuwa ni mnano mwishoni mwa karne ile ya kwanza, wakati Yohane Mwinjili alipoandika Injili hii, ilhali walikuwepo bado wafuasi wake Yohane Mbatizaji, nao waliona kuwa walipaswa kubaki kuwa wafuasi waamini wa Yohane Mbatizaji na kuacha kuwa wafuasi wa Yesu Kristo. Ni katika muktadha huo, Mwinjili Yohane anaona umuhimu na ulazima wa kuwaonesha kazi ya Yohane Mbatizaji kama mtangulizi ilikuwa ni kwa shuhuda wa nuru itokayo kwa Mungu, kuwa kidole au sauti inayomtambulisha Masiha na kumaliza kazi yake na kupungua ili watu waweze kukutana na Neno na Nuru ya kweli, yaani Yesu Kristo.
Mwinjili anatuonesha leo, kuwa Yohane Mbatizaji hakuwa ile Nuru wala hakuwa Neno la Mungu bali ni sauti tu inayobeba ujumbe, na ili ujumbe au neno litufikie ile sauti haina budi kupotea na kuishia. “Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote” (Yohane 1:8-9). Ni kipindi hiki cha majilio tunaona Yohane Mbatizaji anatumika kutuonesha mwanga wa kweli. Ni kwa kupitia Yohane Mbatizaji, Mama Kanisa anapenda kumtumia ili atuoneshe kila mmoja wetu mwanga wa kweli kwa ulimwengu, yaani Yesu Kristo. Ni kwa kupitia yeye, sisi sote tunapata msaada wa kumtambua na kumwendea aliye kweli nuru na mwanga wa ulimwengu mzima. “Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu. Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uhai” (Yohane 8:12). Ni kwa njia ya Kristo pekee tunapata kujua kweli na maana ya maisha yetu, kweli ambazo zinatupeleka kwenye maisha ya kweli na sio katika kupotea kunakotokana na uongo wa yule muovu.
Mashaka juu ya utambulisho wa Yohane Mbatizaji yalikuwepo pia hata kati ya viongozi wa dini, na ndio wakawatuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize hasa kuhusu yeye na pia yale aliyokuwa akiyafanya. Wakuu wa dini ya Kiyahudi walianza kujawa na mashaka na wasiwasi kwa kuona watu wengi wakisikiliza mahubiri yake na kutoka mijini na kwenda kule jangwani na kupokea ubatizo wa maji, na kubadili njia na maisha yao. Na ndio tunaona leo wanamuuliza mara tatu, u nani basi wewe? Ilienea na kusambaa kati ya watu kuwa Yohane Mbatizaji ndiye Masiya, wapo waliomuona kama mmojawapo wa manabii na hata wengine kudhani kuwa ni Eliya. Ni hapo tunaona Yohane Mbatizaji anawajibu na kukiri mbele yao, kuwa siyo yeye Kristo wa Bwana, wala Eliya au nabii mkubwa. Yohane anajitambulisha kama “Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya.”
Yohane Mbatizaji anatambua kuwa yeye ni mtangulizi tu, sio yeye anayepaswa kukaziwa macho, yeye ni kidole kinachotuonesha kule uliko mwanga na nuru ya kweli, kule aliko Kristo wa Mungu. Yeye ni sauti tu, sauti inabeba ujumbe, hivyo ni chombo tu cha kutufikishia ujumbe, ujumbe wenyewe tunakutana nao katika maneno. Ndio kusema tayari katika utangulizi wa Injili ya Yohane tunaona ni Yesu Kristo mwenyewe aliye Neno wa Mungu, anayekuja na kujimwilisha kati kati yetu, anayetaka kufanya makazi yake pamoja nasi, katika maisha yetu. Yohane Mbatizaji kama sauti, kama chombo, kama kidole, kazi yake ni kutufikisha na kutukutanisha na Kristo. “Ni lazima yeye azidi kuwa maarufu, na mimi nipungue” (Yohane 3:30). Ni fundisho hata nasi kwetu, wahubiri wa Injili, kama Yohane Mbatizaji, utume na misheni yetu sio kujihubiri na kujitangaza sisi wenyewe, bali kuwaonesha na kuwapeleka wengine kukutana na Yesu Kristo. Ni kwa njia ya mahubiri ya maneno na mifano mema ya maisha yetu wengine wapata kukutana na Yesu Kristo.
Leo wapo wanaojitenga na Kanisa, kwa kisingizio kuwa wanakwazwa na watumishi wa Neno la Mungu, kila mhubiri kazi yake ni ile ya Yohane Mbatizaji, ya kukubali kupungua, ya kutojihubiri na kujiweka mwenyewe katika nafasi isiyokuwa yangu au yako. Ni kuwasaidia wengine bila kuwazuia iwe kwa maneno yetu au kwa mifano mibaya ya maisha yetu na hivyo wengine kukutana na Yesu Kristo. Yohane Mbatizaji alihubiri kwa maneno na hata kwa maisha yake na hivyo kuwafanya wengi na hata nasi leo kumtambua Kristo wa Mungu. Ili kumtambua Yesu Kristo – nuru na mwanga wa kweli, ni muhimu uwepo wa mashuhuda, kama Yohane Mbatizaji. “Tena, watamwaminije kama hawajapata kusikia habari zake? Na watasikiaje habari zake kama hakuna mhubiri? Hivyo basi, imani inatokana na kuusikia ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo” (Waroma 10:14-17). Hivyo, imani inatokana na mahubiri iwe kwa maneno au kwa mifano mema ya maisha yetu sisi tulio wafuasi wake Yesu Kristo. Kila mmoja wetu, hata Yohane Mbatizaji pia alipitia safari ya kiimani katika kumtambua Yesu wa Nazareti kama ndiye Kristo wa Mungu. Yohane 1:29-34.
Hata Yohane Mbatizaji kuna nyakati akawa na mashaka na kutuma wanafunzi wake kwa Yesu ili kumuuliza. “Basi, Yohane akawatuma wanafunzi wake, wamwulize: Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngojee mwingine? Yesu akawajibu, nendeni mkamwambie Yohane mambo mnayoyasikia na kuyaona” (Mathayo 11:2-6). Safari hii ya imani ni ya kila mwanafunzi wake Yesu Kristo, pale tunapokutana na Kristo kwa mara ya kwanza, yaani siku ya Ubatizo wetu na kuendelea kukua na kukomaa katika imani, hata kuweza kuwa mashahidi na mashuhuda wa kweli za Injili si tu kwa maneno yetu bali hasa kwa maisha yetu. “Niliamini, ndio maana nilinena. Nasi pia, tukiwa na moyo huohuo wa imani, tunaamini, na kwa sababu hiyo twanena” (2 Wakorintho 4:13). Sehemu ya tatu ya Injili ya leo, ni maonyo kutoka kwa Yohane Mbatizaji si tu kwa watu wa nyakati zile bali hata kwetu leo. Aya 26-28: “Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye nami sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake.” Wanawaisraeli walimsubiri na kumngojea Masiha kwa miaka mingi sana, lakini hata pale alipokuja hawakumtambua. Ni kama macho yao yalikuwa yamefumbwa na kitambaa kizito kiasi cha kushindwa kumuona na kumtambua Yesu wa Nazareti, kama Kristo na Masiha wa Mungu. Ni upofu uliotokana na picha za Mungu walizoziumba na kuzitengeneza na kujiaminisha wao wenyewe.
Ni kutokana na kushindwa kubadili vichwa na kuongozwa na mantiki ya Mungu mwenyewe kwa kushupalia mantiki zao wenyewe. Ni upofu unaoweza kutusumbua hata nasi leo, hasa pale tunaposhindwa kukubali kubadili vichwa, kukubali kuongozwa sio na mantiki zetu za kibinadamu bali zile za Mungu mwenyewe. Israeli kama taifa teule, waliishi na kujiona ni wao tu wateule wa Mungu na ndio taifa takatifu kwani Mungu yu kati yao, na hivyo waliwadharau watu wa mataifa mengine kwani waliwaona ni wapagani na hivyo pia najisi. Hivyo, kwao ujio wa Masiha ni kwa ajili yao tu, hawakumtarajia Masiha anayekuja kwa ajili ya wokovu wa watu wote. Ilikuwa ni kinyume na matarajio yao, Masiha anayekuja na kuwakosoa na kuwasahihisha, na hata kuwakaripia. Yohane Mbatizaji alifaulu kuwabadili wale tu waliokubali kuwa ni wadhambi na kuupokea ubatizo wa maji, ili kwao waweze kumpokea Masiha. Ni hata nasi katika kipindi cha majilio, ni kipindi cha kubadili maisha yetu, ni kipindi cha neema kuacha njia zetu za zamani na kuanza kuishi maisha mapya, maisha kadiri ya Neno la Mungu, huku tukimpenda Mungu na jirani.
Ni kwa kufanya toba ya kweli, kwa kukubali kwenda jangwani, ili kubadili maisha yetu, ili kuanza mwanzo mpya, hapo nasi tutapona upofu wetu na kumtambua Yesu Kristo kama nuru na mwanga wa kweli anayetutoa katika giza, ndio katika uovu. Kipindi cha majilio ni kipindi cha kuandaa njia ya Bwana, ni kuandaa mioyo na roho zetu kwa kufanya kitubio na toba ya kweli. “Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake.” (aya 27) Mara nyingi tunaelewa msemo huu wa Yohane Mbatizaji kama ishara ya unyenyekevu. Ndio lakini kwa kweli ni msemo ambao ulieleweka vema na wasikilizaji wake Yohane Mwinjili na hata Mbatizaji wa nyakati zile. “Kuilegeza gidamu ya kiatu”, ilikuwa ni kitendo cha kisheria, kinachoruhusu mmoja kuoa mwanamke aliyekuwa wa mchumba wa mtu mwingine awali. Kumbukumbu la Sheria 25:5-10. Hivyo kusema, “mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake.”, maana yake ni yeye hana uwezo wa kuchukua mchumba wa Kristo. Ni kwa njia ya Yesu Kristo, aliye Masiha, Mungu pamoja nasi, anayekuja ili kuweka agano la mapendo ya daima pamoja na ulimwengu mzima, ni Yesu Kristo aliye mume wa kweli wa mchumba wake, yaani Kanisa. Ndio kusema Yohane anakiri na kutuonesha nafasi yake kama mtangulizi, kama shuhuda, kama kidole, kazi yake ni kutuonesha Bwana harusi wa kweli na wa daima, yaani Yesu Kristo. “Nanyi wenyewe mwaweza kushuhudia kuwa nilisema: Mimi siye Kristo, lakini nimetumwa ili nimtangulie!
Bibi harusi ni wake bwana harusi, lakini rafiki yake bwana harusi, anayesimama na kusikiliza, hufurahi sana anapomsikia bwana harusi akisema. Ndivyo furaha yangu ilivyokamilishwa. Ni lazima yeye azidi kuwa maarufu, na mimi nipungue” (Yohane 3:28-30). Majilio, ni kipindi ambapo bi harusi (Ulimwengu mzima na Kanisa), anajiandaa kumpokea Bwana harusi, yaani, Yesu Kristo. Yohane Mbatizaji ndiye rafiki wa bwana harusi anayefanikisha biharusi kukutana na bwana harusi katika mkutano huo wa upendo. Hivyo nasi hatuna budi kusali na kumuomba Mungu neema zake za kumtambua Yesu Kristo katika Neno lake na masakramenti yake, huko ambako anatuita ili tuweze kukutana na mapendo yake yasiyo na masharti, huko kwenye nuru na mwanga wa kweli ili kutuweka huru na kututoa katika maisha ya giza. Niwatakie Dominika na tafakari njema na maandalizi mema ya Noeli, sherehe za umwilisho wake Bwana wetu Yesu anayekuja na kukaa kati yetu.