Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 4 ya Kipindi cha Majilio: Utenzi wa Bikira Maria: Magnificat! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 4 ya Kipindi cha Majilio: Utenzi wa Bikira Maria: Magnificat! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 4 Majilio: Utenzi wa Bikira Maria

Utenzi wa Bikira Maria, ni mtazamo mpya kuhusu Mwenyezi Mungu na ulimwengu. Ni shule ya uinjilishaji, toba na wongofu wa ndani. Utenzi wa “Magnificat” unatoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu, ambaye ni: Bwana na Mkuu: ni mwingi wa huruma na mapendo; ni mtakatifu na enzi zote ni zake na kwamba, huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Hekalu la kweli! Hata nasi leo, nawaalika katika kulitafakari hekalu la kweli na la milele; hekalu ambalo halijajengwa kwa kutumia mawe, mapambo au mikono. Ilikuwa ni hamu na shauku ya Mfalme Daudi kumjengea Mungu hekalu katika mji ule wa Yerusalemu katika mlima Sayuni. Usiku ule, neno la Bwana likamfikia nabii Nathani; “Tena Bwana anakuambia ya kwamba Bwana atakujengea nyumba. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele”. Ilhali Mfalme Daudi alitaka kumjengea Mungu nyumba, tunaona ni Mungu mwenyewe atakayemjengea nyumba ya milele Daudi, nyumba isiyojengwa kwa mikono wala mawe, wala mapambo. Ni nyumba inayojengwa kwa kutumia mawe hai, yaani watu. Badala ya Hekalu la mawe, Mwenyezi Mungu anachagua kuifanya nyumba ya milele, ndio ile ya kuwaleta watu wake pamoja katika Yeye, kwa kuungana na Mungu mwenyewe.

Ni somo la kwanza la Dominika ya leo, kutoka Kitabu cha Pili cha Samweli, kinatusaidia pia kulielewa vema somo letu la Injili kutoka kwa Mwinjili Luka. Ni somo linalojulikana na tumetoka kulisikia katika Sherehe za Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili (Imakulata). Unabii ule wa Nathani pia tunaona ukitimia katika somo la Injili ya Kupashwa Habari Mama yetu Bikira Maria kuwa Mama wa Mungu. Katika Liturujia ya Kiambrosiani, Dominika ya Nne ya Kipindi cha Majilio inajulikana pia kama Sherehe ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, hivyo wanasherehekea Sherehe ya Mama Bikira Maria, na pia inajulikana kama Dominika ya “Ndio ya Maria” (Fiat) Ni katika somo la Injili ya leo, Yesu Kristo anatambulika kama wa ukoo wa Daudi: “Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho”.  Na pia kadiri ya Mwinjili Luka, Bikira Maria anatambulishwa kama Binti Sayuni, au Sayuni mpya, katika mlima ambapo hekalu la Bwana lilijengwa.

Ni kwa njia ya Bikira Maria, Mungu amefanyika mwanadamu kwa kutwaa mwili na kukaa kati yetu, kwanza katika tumbo la Mama Bikira Maria na pili kwa kumzaa Mwana wa Mungu. Ilikuwa katika mlima Sayuni, yaani katika hekalu, Wayahudi waliuona uwepo wa Mungu, na hivyo utukufu wa Mungu pia. Hivyo kwa kumwilika kwake Yesu Kristo katika tumbo la Maria, Maria anakuwa pia Sayuni mpya. Uwepo wa Mungu haupo tena katika hekalu lile lililojengwa kwa kutumia mawe na miti ya mierezi, bali katika hekalu la Mwili wake Yesu Kristo, yaani, Neno aliyefanyika mwili na kukaa kati kati yetu, ndiye Mungu pamoja nasi. Ndiye Mungu anayedumu na kusafiri pamoja nasi katika Mwili fumbo wale, yaani Kanisa. Ni katika Neno lake na Sakramenti yake, Mungu anaendelea kuwepo kati kati yetu. Ni Mungu aliyetwaa mwili na kukaa kati yetu.

Mwenyeheri Carlo Acutis, angali bado kijana mdogo alimwona na kumtambua Mama yetu Bikira Maria kama Tabernakulo ya kwanza. Ni kwa njia yake Mungu anakuja na kufanya makazi yake ya milele kati kati yetu. Mungu anayedumu na kuendelea kutembea na Kanisa lake, yaani Mwili fumbo wake siku zote za maisha yetu hapa duniani. Ni Mungu asiyebanwa tena na mipaka ya kijiografia wala ya muda, bali anayekuwepo daima na popote pamoja nasi, Mungu tunayekutana naye katika Mwili wake bado, ndio Yesu wa Ekaristi Takatifu, Mungu na Mtu kweli katika maumbo yale ya mkate na divai, katika tabernakulo za makanisa yetu. Mwenyeheri Carlo alipenda kusema kuwa sisi leo tuna bahati kuliko wale walioishi nyakati zake Yesu Kristo wa historia. Ndio kusema nyakati za Yesu wa historia, ili kukutana na Yesu walipaswa kusafiri umbali mrefu ili kukutana naye, lakini sisi leo, tuna bahati iliyoje, kwani Yesu yupo kweli katika makanisa yetu, katika tabernakulo katika maumbo ya mkate na divai. Ndiye Yesu wa Ekaristi Takatifu!

Niwaalike sasa turejee katika somo lenyewe la Injili moja moja ili kwa pamoja kupata ujumbe kusudiwa. Katika Maandiko Matakatifu daima kila mara anapozaliwa mtoto asiye wa kawaida pia tunakutana na mazingira yasiyokuwa ya kawaida kwa hao watoto. Isaka anatungwa mimba wakati mama yake Sara akiwa mzee wa miaka 90 na baba yake Abrahamu akiwa na miaka mia na ishirini (Mwanzo 17:17). Samsoni (Gideoni 13:3) na Samueli (1 Samueli 1:5), mama zao wote wawili awali walikuwa tasa; Yohane Mbatizaji, wazazi wake si tu wote walikuwa wazee bali pia mama yake alikuwa tasa. Na hata kuzaliwa kwake Yesu Kristo ni katika muktadha huo huo usiokuwa wa kawaida kwani Maria alikuwa bado ni bikira (parthénos). Maandiko yanaonesha wazi kuwa watoto wa aina hii sio tu matunda ya kuzaliwa kikawaida kwa kufuata sheria za maumbile bali yanatuonesha kuwa ni matendo makuu ya Mungu kwetu wanadamu, ni zawadi kutoka mbinguni. Ukombozi, matumaini waletayo watoto hawa ulimwenguni ni zawadi kutoka kwa Mungu Mwenyewe. Ni matendo makuu ya Mungu kati ya watu wake.

Somo la Injili ya leo, yawezekana tukakosa kupambanua tangu mwanzo kuwa muhusika mkuu sio malaika kutoka mbinguni wala Mama yetu Bikira Maria, bali ni Yesu Kristo Mwenyewe. Ni somo linalopaswa kutusaidia sisi leo kuelewa Yesu Kristo, au mtoto anayezaliwa ni mtoto wa namna gani. Ni wazi tunaalikwa kwenda ndani zaidi ili kuweza kupata lengo la Mwinjili Luka katika somo la Injili ya leo. Na ndio tunaona Mwinjili Luka anatuonesha kuwa huyu mwana wa Maria, pia ni Mwana wa Mungu, ni Muumbaji na pia Bwana wa historia ya mwanadamu, ni Mkombozi wetu, ni Mungu pamoja nasi. Ni kutokana na ukweli huo wa kiteolojia, Mtakatifu Ambrosi alimtambua Maria kama hekalu la Mungu. Na ndio tunaona katika picha nyingi zinazomuonesha Bikira Maria akinyoosha kidole chake kumwelekea Yesu, ni Mama anayetutangulia kumtambua Kristo kama Mwana wa Mungu na kutualika sote katika imani hiyo.

Yerusalemu, si tu kwa kila Myahudi ulikuwa ni mji mtakatifu, mji ambamo kwamo lilijengwa Hekalu la Mungu bali ndio mji kwamo alitarajiwa Masiha na Mkombozi wa Taifa lile teule. Ni mshangao wa kwanza tunaona Malaika anatumwa katika kijiji kidogo cha Nazareti, katika mkoa wa Galilaya. Ni kijiji kidogo hivi hakitajwi hata mara moja katika Agano la Kale. Ni kijiji walipoishi watu wa kawaida sana na hata waliokuwa wamechangamana na wapagani. “Naye Nathanaeli akamwuliza Filipo, Je, kitu chema chaweza kutoka Nazareti?” Yohane 1:46. Na mshangao mwingine, Mungu hamtumi mjumbe wake kwa mtu mwenye nguvu na shujaa bali kwa “parthénos” (παρθενον), yaani, bikira kwa Kigiriki. Na mwinjili analitaja jina hilo mara mbili la “parthénos” na bikira huyo anatajwa pia kwa jina kuwa ni “Mariamu”.

Mwanamwali Bikira, au kama nilivyosema “parthénos”, yafaa tujiulize kwa nini Mwinjili Luka anatumia neno Mwanamwali bikira na kulitaja mara mbili katika somo la Injili ya leo? Yawezekana tukaishia kuona ni lengo la Mwinjili kutaka kutuonesha kuwa Mariamu alikuwa bado binti mdogo na mwanamwali bikira. Katika tamaduni za Kiyahudi, ubikira ulikuwa ni kitu cha thamani kabla ya ndoa na si baada ya ndoa. Hivyo binti kubaki maisha yake kama bikira haikuwa kitu chenye sifa njema wala cha kujivunia, hivyo kubaki bikira ilikuwa ni ishara ya kukosa thamani au lugha ya kileo tunaweza kusema kukosa mvuto na ushawishi wa kumvuta mwanaume wa kuoa huyo binti anayebaki bikira. Mwanamke asiye na watoto alifananishwa sawa na mti ulionyauka kwa kukosa kuzaa matunda, hivyo kubaki bikira, kubaki bila mume haikuwa kitu cha thamani wala kujivunia wala kuona fahari kwacho. Mji wa Yerusalemu pale ulipovamiwa na hata kuharibiwa na kubaki bila matumaini ulitambulika kama “Binti Sayuni au kwa maneno yangu Bikira Sayuni”. Yeremia 31:4 na 14:13. Sayuni ukiwa katika mahangaiko unatambulika kama bikira kwani maisha yalisitishwa kwake, hakukuwa tena na ustawi wala kuzaliana katika mji ule.

Hivyo, Maria sio tu bikira kwa maana ya kibaiolojia, bali pia kwa maana ya Kibiblia. Maria alitambua kuwa yeye ni bikira kwa maana ya kuwa maskini na mdogo na mnyonge asiyeweza kitu chochote isipokuwa kwa msaada wake Mungu, yaani kwa neema za Mungu zitokazo juu. Katika tukio la kupashwa Habari Maria kuwa Mama wa Mungu, tunasherehekea hasa makuu ya Mungu, Yeye aliyetenda makuu na Jina lake ni Takatifu kama anavyoimba Maria katika wimbo ule wa sifa wa “Magnificat”. Tunaliona hili katika salamu ya malaika kwa Maria. Malaika anatumwa kwa huyu aliye bikira, aliye fukara na mnyonge, aliye katika hali duni, lakini salamu ya malaika kwa “parthénos”, inabadili kila kitu. Malaika anafika kwa Mariamu na kumwamkia; “Kaire, kekaritoméne”, ni maneno ya Kigiriki yenye maana ya furahi(kaire), Bwana yu pamoja nawe(kekaritoméne). Huyu ambaye machoni mwa mwanadamu ni bikira, yaani, “parthénos”, anaalikwa na Mungu mwenyewe kufurahi kwani yupo pamoja naye, huyu ambaye anaonekana ni duni na dhaifu machoni kwa mwanadamu, ni mmoja ambaye Mungu yupo pamoja naye, yumo na anakaa na anatenda ndani katika maisha yake. Huyu aliyejaliwa “karin”, yaani, neema.

Tunaona Injili ya Luka, ni Injili pia ya maskini, ambao kwao Mungu anawarejeshea tena furaha na matumani, na ndio tunaona tangu mwanzoni kabisa mwa Injili yake, tunaona Mungu anawachagua walio wa mwisho, walio wanyonge na duni, wale ambao wamedharauliwa machoni pa watu. Kwa kuweza kuwajalia uzao, matumbo ya nchi ile bikira ya Sayuni na katika tumbo la mwanamwali bikira, ndio kusema Mungu anaonesha ukuu na uwezo wake wa kuuhisha pale ambapo hapakuwa na matumaini tena ya uhai wala maisha. Na ndio Mungu kwa njia ya nabii Isaya anatuonesha uwezo wake wa kubadili mioyo inayokuwa migumu kwa kuinyeshea maji ya Roho wake (Isaya 32:15). Maneno yale ya malaika kwa Mariamu, kwa kweli pamoja tunasoma katika Injili yetu ya Kiswahili kuwa ni “Salamu, uliyepewa neema”, kwa Kigiriki ni “Χαιρε, κεχαριτωμενη,” (Kaire, kekaritomene), kwa tafsiri nzuri inapaswa kuwa; “Furahi, Bwana yu pamoja nawe”. Kuwa na Bwana ni sawa na kusema kujawa na neema. Ni salamu hii tayari ilishatumiwa na Nabii Sefania, ilitumika wakati wa anguko la kimaadili la Mwanamwali Bikira Sayuni.

Mwanzoni, Nabii Sefania anatumia lugha kali na yenye kutisha na kuogopwa na Binti Sayuni akisema: “Ole wake mji wa Yerusalemu, mji mchafu, najisi na dhalimu” (Sefania 3:1) na baadaye anatumia lugha laini na yenye matumaini tena kwa mji ule wa Binti Sayuni akisema: “Imba kwa sauti, ewe Sayuni, paza sauti ee Israeli. Furahi na kushangilia kwa moyo wote, ewe Yerusalemu! ... Nitakuondolea maafa yako, nawe huhitaji kuona aibu kwa ajili yako” (Sefania 3:14-18). Ni baada ya mji ule kubadili njia zake kwa kufanya toba ya kweli, ni hapo Nabii Sefania anawaalika tena kuinua macho yao juu na kuuona upendo na huruma ya Mungu kwa watu wake, uwepo wake kati yao tena. Ni leo tunaona Mwinjili Luka katika salamu ya malaika kwa Maria; Maria anaalikwa kufurahi kwani ni kwa njia yake Mungu anawajia watu wake, Mungu anakuwa kwa nafasi ya kwanza pamoja naye mwanamwali bikira, aliye mnyonge na kuonekana mdogo machoni pa watu.

Katika Biblia, kila mara Mungu anapomuita mtu fulani anamuita kwa jina lake, lakini leo tunaona kwa Mariamu, haanzi kutaja jina lake bali wasifu wake, ni huyu aliye “Parthénos” na pia “Kekaritomene”, yaani, mwanamwali bikira na Bwana yu pamoja naye. Mungu anamtambulisha kwa majina mengine kwa nafasi ya kwanza kabla ya jina lake la kawaida, ndio kusema ni mmoja anayeitwa na Mungu kushiriki katika mpango wa Mungu mwenyewe. Ibrahimu ataitwa Abrahamu kwa kuwa atakuwa baba wa mataifa yote. Mwanzo 17:5 na 15 na hata mkewe pia anabadilishwa jina. Ni kwa njia ya huyu mwanamwali Bikira, ambaye pia Bwana yu pamoja naye, Mwenyezi Mungu anakwenda kutenda makuu, anakwenda kutwaa mwili na kukaa katikati yetu, ni kwa njia yake Mkombozi anazaliwa duniani kwa ajili ya wokovu wetu. Ni kwa njia ya huyu mwanamwali bikira, mdogo na mnyonge, Mwenyezi Mungu anakwenda kutenda makuu, anakwenda kuufunua upendo na huruma yake kwetu sisi wanadamu. Rejelea Magnificat (Utenzi wa sifa wa Maria; Luka 1:46-55)

Hata maneno anayotumia malaika tunakutana nayo kutoka kinywani kwa Nabii Nathani (2 Samueli 7:12-17). Unabii unatimia katika nafsi ya huyu mtoto wa Mwanamwali bikira Mariamu. Ni Yesu aliye masiha na Kristo anayekuja ili kutawala watu wake milele (Isaya 7:14, Matayo 1:22-23 na Luka 1:35). Mtoto atakayezaliwa si tu wa uzao au ukoo wa Daudi bali anazaliwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, na hivyo ni Mwana wa Mungu aliye juu. Na ndio tunaona Mwanamwali Bikira Mariamu anatambulika pia kwa Kiebrania kama “gebira”, Mama wa Bwana, Mama wa Mungu. Na jina lake mtoto huyu ataitwa “Yesu”. Ni jila la Kiebrania lenye mzizi wake katika jina la Kiebrania, “Yeshua”, lenye maana ya mkombozi (Mathayo 1:21). “Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye ndiye atakayewaokoa watu wake katika dhambi zao.” Mwanamwali bikira ni “gebira”, Neno la Kiebrania likiwa na maana ya, Mama wa mfalme, kama anvyotuonesha pia Mwinjili Luka. “na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake.”

“Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa aliye juu” Ni majina yanayoonesha kuwa huyu anayezaliwa ni Mungu. Mwana wa Mariamu, pia ni Mwana wa Mungu, huyu mtoto pia ni Muumbaji, ni Mungu. Kuwa Mwana maana yake ni kuwa na mfanano ulio kamili, ni kuwa sawa kabisa na baba. Na hata mwanamwali bikira alipouliza litawezekanaje neno lile; “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.” Katika Agano la kale tunaona kivuli na hata wingu ni ishara za uwepo wa Mungu. Mungu aliwatangulia katika muundo wa wingu wakati wa tukio la safari ile ya kutoka nchi ya utumwa kuelekea nchi ya ahadi. Kutoka 13:21, na hata wingu likafunika kambi yote wakati Musa alipoingia hemani kukutana na Mungu (Kutoka 40:34-35) na hata mlimani wingu likaufunika mlima (Kutoka 19:16). Ndio kusema Mwinjili Luka anatoa fundisho la kiimani tangu mwanzo kuwa huyu mtoto anayezaliwa ni mtu kweli na Mungu kweli, kama tunavyokiri kila Dominika wakati wa sala ile ya Nasadiki ya Nisea.

“Hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu”, ni maneno kutoka kwa mjumbe wa Mungu, na ndio maneno yale yale pia Mungu anayotamka kwa Abrahamu kabla ya kuzaliwa kwake Isaka (Mwanzo 18:14). Ni maneno yenye faraja kwa kila mmoja anayejisikia mnyonge na duni, ni mwaliko wa kumtegemea na kumkimbilia Mungu kila mara tunapotambua udogo na unyonge wetu katika kukubali mapenzi yake katika maisha yetu. Ni kwa uwezo wa Mungu, hata Elizabeti aliyekuwa tasa sasa ni mwezi wa sita, Mwenyezi Mungu ametenda makuu katika maisha yake. Ni mwaliko kwetu sote katika uweza na hasa wema na huruma ya Mungu kwa mwanadamu aliye mnyonge na dhaifu. “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.” Ndilo jibu au ndiyo ya mwanamwali bikira kwa wito na mpango wa Mungu katika maisha yake. Ni “fiat” ya Maria katika kukubali sio mapenzi yake, bali mapenzi ya Mungu kwanza katika maisha yake. Mwanamwali bikira anaitika kwa kusema “genoito”, ni kitenzi kwa lugha ya Kigiriki, kikiwa na maana ya shauku yenye furaha kubwa kuona mpango na mapenzi ya Mungu yanatimia katika maisha yake. Ni furaha kuona Mungu anatenda katika maisha yake, ni furaha ya kumpa Mungu nafasi ya kwanza katika maisha yake.

Maria anayesalimiwa pale mwanzoni kwa maneno ya “Kaire”, yaani “furahi”, pia anaitikia wito na mwito wa Mungu kwa furaha, ndio kusema kila mmoja anayekubali mpango wa Mungu katika maisha yake, anajazwa pia furaha ile ya kweli, kwani Mungu daima anabaki na kila mmoja anayeruhusu Yeye atawale na aongoze maisha yake. Majilio na Noeli ni kipindi ambapo tunaalikwa kufungua maisha yetu na kumkaribisha Yesu Kristo ajimwilishe, afanye hema na makazi yake katika maisha yetu, na ni hapo tunakuwa na hakika ya kujawa na furaha ya kweli itokanayo na uwepo wa Mungu katika maisha na nafsi zetu, yaani Emanueli, Mungu pamoja nasi. Nawatakia maandalizi na pia maadhimisho mema na yenye furaha na kila neema ya Umwilisho wake Bwana wetu Yesu Kristo. Mtoto Yesu anataka kuzaliwa katika nafsi na maisha yetu na iwe sala yetu ikapate kutimia kwa kumruhusu azaliwe ili atujalie furaha ya kweli maishani. Heri ya Noeli na Dominika njema.

15 December 2020, 12:01