Tafakari ya Neno la Mungu Kesha la Noeli: Yesu Mwanga wa Mataifa
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, katika misa ya mkesha wa kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni sherehe ya umwilisho, Neno wa Mungu kutwaa mwili, Emmanueli, Mungu pamoja nasi. Kuzaliwa kwake Yesu Kristo, kunatuwezesha kumfahamu Mungu Baba na kuuonja upendo wake kwetu sisi wanadamu hata akamtoa mwanae wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele (Yn 3:16). Katika adhimisho la sherehe ya Noeli mama Kanisa ameweka Misa tatu; Misa ya usiku, Misa ya alfajiri na Misa ya mchana. Kila Misa ina sala na masomo yake. Tafakari hii ni ya masomo kwa ajili ya Misa ya usiku. Misa hii ya usiku katika wimbo wa mwanzo tunaimba; Bwana aliniambia, ndiwe mwanangu, mimi leo nimekuzaa (Zab.2:7). Tunaalikwa kufurahi katika Bwana, kwa sababu Mwokozi wetu amezaliwa duniani, amani ya kweli imetushukia toka mbinguni.
Katika usiku mtakatifu wa kuzaliwa Yesu Kristo, tunaalikwa kufurahi kwa kuwa nuru imetushukia duniani na giza kuondolewa. Tukumbuke kuwa giza, usiku au usingizi katika lugha ya kibiblia, linawakilisha hali ya dhambi, hali ya kutokuwepo kwa neema ya Mungu; hali ya kufa. Na mtu aliye katika hali ya dhambi basi yumo gizani; haoni. Kwa upande mwingine nuru inawakilisha hali ya neema. Ili kutuonyesha kuwa Yesu Kristo ndiye nuru halisi ambayo giza haliwezi kuishinda, maadhimisho ya kuzaliwa na kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristo huanza usiku ikiwa ni ishara wazi ya kutuonyesha ile nuru ya kweli yaani Bwana wetu Yesu Kristo kama maneno ya sala ya mwanzo yanasema; Ee Mungu, uliyefanya usiku huu mtakatifu kung¢ara kwa nuru ya mwanga wa kweli, tunakuomba sisi tuliofahamu mafumbo ya mwanga huo hapa duniani, utuwezeshe pia kuzipata furaha zake mbinguni. Kumbe Kristo anapozaliwa anakuja kuondoa giza na kuleta mwanga. Kuondoa dhambi na kutuletea neema ya utakaso.
Nabii Isaya katika somo la kwanza anatabiri ujio wa “Siku ya Bwana”, siku ambayo Mungu atawakomboa wale waliopelekwa utumwani. Mungu atawaletea ufalme wa amani atakaoshika mtoto wa ukoo wa kifalme. Uaguzi huo umetimia katika Yesu aliyetukomboa kutoka utumwa wa shetani. Isaya anatangaza kuja kwa Nuru ya kweli akisema; Watu wale waliokuwa katika giza, Wameiona Nuru kuu (Isa.9:2). Jeshi la Assyria lilipowashambulia waisraeli, liliteketeza makazi yao, wakawaua walioonesha upinzani, wapo waliochukuliwa mateka, wengine kujeruhiwa wakawa walemavu wa viungo mbalimbali kama vipofu, viwete na viziwi na wengine kubahatika kujificha ndani ya mahandaki. Hali hii ni kama “uvuli wa mauti”. Mungu kwa kinywa cha Nabii Isaya anawatangazia watu wake amani na kuwapa matumaini mapya kwamba Nuru inakuja, wale waliokwenda katika giza wataona nuru na wale wanaokaa katika uvuli wa mauti nuru hiyo itawaangaza. Nuru hii ni Masiha. Anawaalika wafurahi kama mkulima afurahiavyo mavuno yake ya kwanza, kama mwindaji afurahiavyo mawindo. Furaha hii italetwa na Mtoto atakayezaliwa. Mtoto huyo ni mtoto wa kiume, ana uweza wa kifalme mabegani mwake.
Jina lake ni mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, mfalme wa amani, na ufalme wake hautakuwa na mwisho. Matukio yanayoambatana na ujio wake ni kwamba; wote wanapata Uhuru. Ni mwisho wa vita chuki na ugomvi. Atasimika Ufalme wa Amani, Upendo na Haki. Nuru anayoitanga Nabii Isaya ni Kristo mwenyewe, aliyekuwepo kwa Mungu tangu mwanzo, naye ni Mungu. Yeye ni mwanga kwa watu. Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza haliwezi kuushinda. Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote wanaompokea (Yoh.1:1-5,9). Yesu Kristo ndio mwanga unaotung’aria katika usiku wa Krismasi ili tusitembee tena gizani; kama Kristo mwenyewe anavyotuambia “Mimi ndimi nuru wa ulimwengu, yeye anifuataye mimi hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima wa milele” (Yoh.8:12). Kristo ni mfalme wa amani kama Nabii Isaya anavyosema; “naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa Amani” (Isa.7:6). Mtume Paulo katika somo la pili la waraka wake kwa kwa Tito anatusihi kuwa; tukitaka kuishi kitakatifu, yatupasa kukataa ubaya na tamaa za kidunia kwa kuifuata neema ya Mungu iliyofunuliwa kwetu katika fumbo la umwilisho la Mungu kujifanya mtu akisema; “Maana neema ya Mungu mwokozi wetu inayowaokoa wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa (uchaji) katika ulimwengu huu wa sasa” (Tito 2:11, 12).
Katika Injili ilivyoandikwa na Luka tunapata simulizi la kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Habari hizi hazikutolewa kwa wafalme au wasomi na watu mashuhuri, bali kwa wachungaji; watu wasio na nafasi katika jamii, wapagani, hawakuruhusiwa kusali Hekaluni, ushahidi wao haukukubalika mahakamani, walionekana kuwa ni wadhambi, wapagani, watu duni na wadanganyifu, lakini ndio wanaoambiwa; “Msiogope, leo katika mji wa Daudi, amezaliwa kwa ajili yenu, Mwokozi ndiye Kristo Bwana”. Ishara wanazopewa wachungaji ni za kawaida kabisa: Mtoto mchanga, aliyevikwa nguo za kitoto, akiwa amelazwa katika hori la kulishia wanyama. Hii inatuonyesha kutimia kwa utabiri wa Nabii Isaya katika somo la kwanza kuwa; Kristo amekuja kwa ajili ya wanyonge kama; walemavu, viwete, viziwi, taaira, vipofu, yatima na wajane, amekuja kuangamiza dhambi inayosababisha mateso na mahangaiko kwa wanyonge. Hawa ndio waliomngojea masiha, wakampokea, wakafurahi na kumtukuza ili katika yeye waonje Upendo, wapate furaha, amani ambayo ni matunda ya haki. Hawa ndio waliohitaji uponyaji na neno la uzima. Hawa ndio wale Kristo anaambatana nao katika hali zao unyonge ili awarudishie hadhi na utu wao kwa kuwajalia uhai na uzima, akiwaponya udhaifu wa kiroho na kimwili.
Mazingira duni aliyozaliwa mtoto Yesu, ni mazingira ya hali ya binadamu mnyonge anayeteseka na kuteswa sio tu na ibilisi kwa dhambi na kifo bali pia na binadamu mwenzake. Yesu kutwaa mwili na kuingia katika hali hii ya binadamu, siyo ili sisi tuendelee kubaki katika umasikini, ujinga, maradhi, dhambi, ukandamizo wa shetani na kifo, bali ili atuokoe katika mazingira hayo na aturudishie hadhi yetu tuliyoipoteza; hali ya umungu. Ubinadamu waficha umungu wake; mazingira haya yanaficha umungu wake, nguo za kitoto zafifisha umungu wake; mateso na kifo cha aibu vyaficha umungu wake. Bila imani hatuwezi kutambua umungu wake. Hata katika maumbo ya mkate na divai hata ubinadamu wake unatoweka. Ndio ulimwengu na ubinadamu unaoficha utukufu wa Mungu. Kristo amekuja kuondoa vizuizi vyote hivyo, ili mwanadamu abaki anang’ara kwa utukufu wake wa kimungu. Nguo za kitoto ni masaibu yanayomzingira binadamu na kumfanya duni. Ndiyo maana katika ufufuko Yesu ameachana na masaibu haya: Nguo za kitoto na sanda; zikazongwazongwa, zikaachwa mbali na mfufuka mtukufu! Huyu ni neno wa Mungu aliyetwaa mwili ili toka kwake tujaliwe neema juu ya neema tupate kuondokana na yote yanayofifisha hadhi na heshima ya binadamu.
Katika usiku mtakatifu wa sherehe ya Noeli tunaalikwa kuogopa giza na kuishi katika nuru ya kweli. Nuru hii ituangaze tuzione dhambi tulizozizoea na kutufanya tutembee gizani, tuiruhusu ipenye mioyoni mwetu ili giza lisitutawale tena. Tuiruhusu Neema ya Mungu mwokozi wetu iliyofunuliwa leo, itufundishe kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa (uchaji) katika ulimwengu huu wa sasa.” Hapo kweli Kristo atakuwa amezaliwa mioyoni mwetu na katika maisha yetu, furaha yetu itakuwa na maana, kusherehekea kwetu kutakuwa kwa maana. Sisi tunaosherehekea kuzaliwa kwake Kristo tunawajibu wa kuyamulika na kuyaweka hadharani maneno na matendo yote yanayodhalilisha hadhi ya utu wa mtu hasa yale matendo yanayowatia wengine kilema kwa kuwapiga, kuwatesa kimwili, kiakili na kisaikolojia, pia kumnyima mtu uhuru wa kiroho. Ni mwaliko wa kupambana na matendo yote yanayovunja heshima ya mwanadamu kama; kufungwa bila hukumu, utumwa mamboleo, ukahaba, uuzaji wa wanawake na watoto, hali nyonge za kazi za kuwatumikisha wengine kama vyombo vya kuleta faida tu.
Basi tujiombee sisi wenyewe; tuziombee tawala mbalimbali duniani ziondoe sheria zinazotetea mambo ya giza na kila aina ya uovu. Tuzingatie maadili ya utu na kutetea haki na amani. Tushikilie mafundisho ya Kanisa yatupatie mwelekeo wa Maisha kama anavyotushauri Mtume Paulo akisema; “Basi, tutupilie mbali mambo yote ya giza, tukajitwalie silaha za mwanga. Na tuishi kwa adabu kama inavyostahili wakati wa mchana, na wala sio kwa ulafi na ulevi, uchafu na uasherati, ugonvi na wivu. Bwana Yesu Kristo awe vazi lenu” (Rum.13:12-13). Kwa namna hiyo Krismasi itakuwa na maana na tutakuwa na haki ya kuimba; Leo amezaliwa kwa ajili yetu Mwokozi, ndiye Kristo Bwana na sala baada ya komunyo tunayosali; Ee Bwana Mungu wetu, sisi tunafurahi kufanya sikukuu ya kuzaliwa kwake Mkombozi wetu. Tunakuomba utujalie kuishi vema, tupate kustahili kufika kwake; itafika mbele za Mungu na kupata kibali machoni pake.