Tafakari ya Neno la Mungu, Noeli Misa ya Alfajiri: Furahini katika Bwana! Kwa ajili yenu amezaliwa Mshauri wa ajabu, Mungu, Mfalme wa amani na Baba wa Milele. Tafakari ya Neno la Mungu, Noeli Misa ya Alfajiri: Furahini katika Bwana! Kwa ajili yenu amezaliwa Mshauri wa ajabu, Mungu, Mfalme wa amani na Baba wa Milele. 

Tafakari ya Neno la Mungu Noeli: Misa ya Alfajiri: Mfalme wa Amani

Maana kwa ajili yetu Bwana atazaliwa; naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu, Mungu, Mfalme wa amani, Baba wa milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. (Isa. 9,2.6; Lk.1:33). Ee Mungu Mwenyezi, sisi tumemulikwa na mwanga mpya wa Neno wako aliyejifanya mwanadamu. Tunakuomba utujalie tuonyeshe kwa matendo yetu ile imani inayong’aa akilini mwetu. Noeli Njema!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Katika adhimisho la Sherehe ya Noeli Mama Kanisa ameweka Misa tatu; Misa ya usiku, Misa ya alfajiri na Misa ya mchana. Kila misa ina sala na masomo yake. Tafakari hii ni ya masomo kwa ajili ya Misa ya alfajiri. Katika wimbo wa mwanzo tunaimba; Nuru itatuangazia leo, maana kwa ajili yetu Bwana atazaliwa; naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu, Mungu, Mfalme wa amani, Baba wa milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. (Isa. 9,2.6; Lk.1:33) Katika sala ya mwanzo tunasali; Ee Mungu Mwenyezi, sisi tumemulikwa na mwanga mpya wa Neno wako aliyejifanya mwanadamu. Tunakuomba utujalie tuonyeshe kwa matendo yetu ile imani inayong’aa akilini mwetu. Katika somo la kwanza la kitabu cha nabii Isaya, Mungu anaualika mji wa Yerusalemu ufurahi kwa furaha kubwa. Kwa kuwa mji wa Yerusalemu ulijengwa juu ya mlima Sayuni, maandiko matakatifu yanauita mji huu Binti Sayuni kama kiitikio cha wimbo wa Komunio kinavyosema; Furahi sana, ee binti Sayuni; piga kelele, ee binti Yersalemu; tazama, Mfalme wako anakuja; ni mtakatifu na mwokozi wa dunia.

Yerusalemu inafananisha na mwanamke, lakini sio kama mji wenyewe bali watu walioishi ndani mwake yaani wana wa Israeli ambao mahusiano yao na Mungu yalielezwa kama mahusiano kati ya Mume na Mke. Mungu anaialika Yerusalemu ifurahi kwa sababu mbili; Kwanza kwa sababu mwokozi wake anakaribia kufika akisema; angalia mwokozi wako anakuja (Is 62:11). Mungu mwenyewe anakaribia kuja kuwaokoa na kuwaongoza, watoto wa Yerusalemu kutoka uhamishoni na kuwarudisha nyumbani kwao. Katika kuwaleta nyumbani, Mungu atawatakasa dhambi zao na kuwapa jina jipya, nao wataitwa “watu waliookolewa”, “watu watakatifu”. Yerusalemu iliposhambuliwa na maadui zake kwa sababu ya dhambi za kumuasi Mungu na kupelekwa uhamishoni au utumwani, aliitwa “aliyeachwa”, maana alikuwa kama mwanamke aliyeachwa na mumewe. Lakini kutoka sasa na kuendelea mji wa Yerusalemu utaitwa “Yule ambaye mumewe anamtamani”, mpendwa wa Mungu.

Sababu ya pili ya kufurahi ni upendo wa pekee ambao Mungu atauonesha mji wa Yerusalemu; kama Bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu atakavyokufurahia wewe. Kama mwanamwali anavyofurahi anapotafakari juu ya upendo wa Bwana wake. Anajisikia salama; bwana wake atamlinda na hatari zote (Is 62:5). Kumbe, kwa kinywa cha Nabii Isaya, Mungu alitangaza matukio mawili; kuja kwake kuwaweka huru watu wa Israelli kutoka uhamishoni na kuwaleta nyumbani kwao “Yerusalemu Mpya” na ujio wake katika nafsi ya Masiha aliyejifanya mwanadamu kuwaokoa wanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi. Hivyo tunaposoma somo hili katika sherehe hii ya Noeli tunakumbushwa kuwa kwa ubatizo wetu tulifanywa watu wapya, taifa jipya la Israeli, Yerusalemu mpya yaani Kanisa, jamii mpya ya watu wake Mungu kwa njia ya Yesu Kristo, Emmanueli, Mungu pamoja nasi. Na hivi tunaalikwa kufurahi kwa moyo wote kwa kuwa sasa sisi ni watu waliookolewa, watu wapya.

Mtume Paulo akimwandikia Tito, kijana mdogo ambaye yeye mwenyewe Paulo alimteua kuongoza Kanisa katika kisiwa cha Krete anaeleza hali yetu ilivyokuwa yakutisha kabla ya kumpokea Kristo akisema; Kumbuka kuwa kuna wakati, sisi pia tulikuwa wajinga, wasio watii, tuliopotewa na kutawaliwa na vionjo na aina zote za tamaa tulipoishi katika uovu na utashi potovu tukichukiana na kujichukia wenyewe (Tito 3:3). Sisi sote kabla ya kumpokea Kristo na kubatizwa tulikuwa wajinga, wajinga wa upendo wa Mungu kwetu na wa njia ya kufika kwake. Tulikuwa tumepotea maana dhambi zetu zilituweka mbali na Mungu. Hatukuwa watii maana namna yetu ya kuishi ilikuwa kinyume na mapenzi ya Mungu. Tulikuwa watumwa wa shetani tuliofungwa na minyororo ya dhambi zetu. Tulichukiana kwa sababu ya ubinafsi wetu, tuliwatumia jirani zetu kama vyombo ili kufikia matakwa yetu.

Lakini baada ya kumpokea Kristo, Emmanueli, Mungu pamoja nasi, hali yetu imebadilika; Tumetakaswa dhambi zetu na kupewa maisha mapya, tunaitwa sasa watoto wa Mungu na wa Kanisa. Tumekuwa warithi wa uzima wa milele. Tumekuwa na furaha hapa duniani, furaha ambayo itakamilika tutakapofika mbinguni. Ndiyo maana Kanisa linatualika nyakati zote kufurahi hasa tunaposherehekea Sherehe ya Fumbo la Umwilisho, Mungu kuchukua mwili wa kibinadamu, Noeli, kuzaliwa kwake Kristo, Emmanueli, Mungu pamoja nasi, kama anavyotuambia nabii Isaya; furahi kwa maana mwokozi wako amekuja (Is 62:1. Kumbe Umwilisho wa Mungu ni ishara ya upendo na huruma yake kwetu sisi wanadamu (Tito 3:5), kwa maana hakuna chochote kabisa tulichofanya ili kutustahilisha mastahili ya mkombozi kuzaliwa.

Ni upendo wa Mungu tu, upendo uliokuwa bila kipimo uliomleta duniani Yesu Kristo, Emmanueli, Mungu pamoja nasi. Na ukweli unaendelea kujidhihirisha katika maisha yetu; chochote anachofanya Mungu ni matokeo ya huruma yake. Ni kwa kuzaliwa kwake Kristo, ukarimu na upendo wa Mungu umefunuliwa kwetu yaani neema ya Mungu imefunuliwa kwetu (Tito 3:4). Kama ilivyo katika maisha ya kawaida mtoto anapozaliwa tunaagalia amefanana na nani katika familia kwa tabia na sura yake, ndivyo ilivyo kwa mtoto Yesu; kwake tunatambua wema na upendo wa Mungu unaoakisiwa na kuonekana katika yeye kama waraka kwa waebrania unavyosema kuwa; Yesu ni chapa halisi ya sura ya Mungu (Wabr. 1:3). Kumbe Yesu ni sura halisi ya Mungu Baba. Anafunua upendo wa Mungu Baba kwa mwanadamu kwa namna ya pekee, upendo aliouonesha katika fumbo la ukombozi; mateso kifo na ufufuko wake.

Katika Injili wachungaji, watu waliodharauliwa walipopokea habari za kuzaliwa kwa mkombozi waliamini wakaenda kwa haraka Bethlehemu nao walipomwona mtoto aliyezaliwa walimsifu Mungu kwa upendo wake wa kumtuma mwokozi, wakawatangazia wengine kile walichofunuliwa. Nasi tunaposherehekea sherehe hii tunaalikwa kuutambua upendo wa Mungu usio na mipaka, kumsifu kwa huruma yake na kuwatangazia wengine huruma na upendo wa Mungu ambao bado hawajauonja. Bikira Maria aliyaweka maneno yote, akiyafikiri moyoni mwake aliyoyasikia kutoka kwa wachungaji nasi pia tufungue mioyo yetu, Nuru hii ituangaze, tuwe na amani ya kweli ndani mwetu tuishi kwa furaha ya kidugu. Kama tunavyosali katika sala baada ya komunio katika Misa ya Alfajiri tukisema; Ee Bwana, sisi tunaoadhimisha kwa ibada na furaha kuzaliwa kwake Mwanao, tunakuomba utujalie tutambue kwa imani kubwa siri ya fumbo hili kulipenda kwa moyo wote; basi Noeli hii itujaze furaha ya kweli na kutuimarisha katika imani yetu.

24 December 2020, 16:47