2020.12.13 Tafakari ya Dominika ya III ya Majilio 2020.12.13 Tafakari ya Dominika ya III ya Majilio 

Neno la Mungu Dominika ya III ya majilio mwaka B:Furahini Bwana yu karibu!

Tunaishi na watu maskini,walemavu,wagonjwa na wenye shida mbalimbali.Tunapaswa kuwa sauti ya faraja na matumaini kwao ili kwa kupitia sauti yetu na matendo yetu wapate kumtambua Kristo aliye faraja na furaha ya kweli.Tutambue kuwa Mungu ana mpango na kila mmoja wetu,lakini ataweza kutimiza mpango wake tu kama tukimruhusu aingie katika maisha yetu,afanye maskani yake ndani ya roho zetu na kuyatawala na kuyaongoza maisha yetu.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa radio Vatikani, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya tatu ya majilio mwaka B wa Kanisa. Tupo katika sehemu ya pili ya kipindi cha majilio. Sehemu ya kwanza ya kipindi cha majilio huanza kwa dominika ya kwanza na kuishia domenika ya pili ya majilio ambapo masomo yalitualika zaidi kujiandaa kwa ujio wa Kristo siku ya mwisho. Masomo haya yalisisitiza kuwa Kristo atakuja siku ya mwisho kuwahukumu wazima na wafu. Yeye atakuja kama mfalme kutawala na hapo hapo kama hakimu mwenye haki anayemhukumu kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Atakuja siku tusioidhania kama vile mwivi ajavyo kuvunja na kuiba siku usioidhania, ndivyo Kristo atakavyokuja siku ya mwisho pale anapomtuma mjumbe wake kutuita, hii ndiyo siku ya kifo cha kila mmoja wetu.

Sehemu hii ya pili ya kipindi cha majilio inaanza na dominika ya tatu hadi ya nne ambapo masomo yake yanasisitiza kuwa Bwana yu karibu kuja. Na hivyo yanatuandaa zaidi kusherekea kwa furaha na amani tele mioyoni mwetu sikukuu ya noeli yaani kuzaliwa upya kwake Bwana wetu Yesu Kristo katika maisha yetu. Ndiyo maana wimbo wa mwanzo unatualika tufurahi ukisema; Furahini katika Bwana siku zote; tena nasema furahini. Bwana yu karibu. Mwaliko huu wa furaha unaipa domenika hii jina la Gaudete kwa kilatini ikimaanisha domenika ya furaha. Na masomo yote ya domenika hii yanatualika kufurahi.

Somo la kwanza linatueleza jinsi Nabii Isaya alivyotumwa na Mungu kuwapelekea Waisraeli habari njema ya kukombolewa kwao kutoka utumwani na taabu zake zote. Hivyo anasisitiza juu ya furaha wanayopaswa kuwa nayo wana wa Israeli. Lakini ujumbe wa Nabii Isaya ni utabiri wa kuja kwake Masiha Bwana wetu Yesu Kristo akisema: Roho ya Bwana Mungu yu juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta, niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufungukiwa kwao. Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu.

Ujumbe huu wa furaha, ni kama tangazo la mwaka wa jubile, mwaka wa ukombozi na neema. Kila msimu wa Majilio ni wakati wa ukombozi, utakaso na wongofu unaofumbatwa katika kulisikiliza neno la Mungu, ambalo ni neno la amani, neno la msamaha na neno la furaha. Furaha hii Nabii Isaya anaielezea kwa msisitizo mkubwa akisema: Nitafurahi sana katika Bwana, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bwana arusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu. Maana kama nchi itoavyo machipuko yake, na kama bustani ioteshavyo vitu vilivyopandwa ndani yake; ndivyo Bwana Mungu atakavyootesha haki na sifa mbele ya mataifa yote.

Hii furaha itokayo kwa Mungu na kuzaliwa ndani mwetu ni furaha kamili. Na hii furaha sio kitu kingine isipokuwa kujisikia huru na kuishi katika uhuru wa watoto wa Mungu. Furaha hii ni kama vazi tunalovikwa na Mungu mwenyewe. Ndiyo neema ya utakaso inayotupa uzuri wa ajabu ambayo ndiyo sura ya Mungu ndani mwetu. Ni furaha ambayo Bikira Maria anaishangilia ndani kabisa mwa mtima wa moyo wake kama wimbo wa katikati unavyosema; Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, na roho yangu imemfurahi Mungu, Mwokozi wangu; kwa kuwa ameutazama unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, toka sasa vizazi vyote wataniita mbarikiwa. Bikira Maria anazidi kufurahi na hivyo anakuwa na ujasiri wa kumsifu Mungu akisema; Nafsi yangu itashangilia katika Mungu mwokozi wangu.

Mtume Paulo katika somo la pili la waraka wake wa pili kwa Wathesalonike naye anasisitiza juu ya furaha akisema: Furahini siku zote, tena nasema furahi; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. Il furaha hii iwe ya kweli kuna masharti yake ambayo Paulo anayasisitiza akisema; Msimzimishe Roho; msitweze unabii; jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna. Tukiyazingatia haya mambo Paulo anasema; Mungu wa amani mwenyewe atawatakasa kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe muwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Kumbe furaha hii inahitaji utakaso moyoni na kuishi katika neema, ili nafsi zetu, roho zetu mioyo yetu na miili yetu ibaki bila lawama wakati wa kuja kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Hii ndiyo Noeli tunayoisubiri, ambapo tukijiandaa vyema, Kristo kweli atazaliwa ndani mwetu nasi tutakuwa na furaha ya kweli. Utimilifu wa furaha yetu unaonekana katika kuyafanya mapenzi ya Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Mwinjili Yohane katika Injili anaonyesha furaha ya Yohane Mbatizaji katika kutimiza mapenzi ya Mungu kwa kutangaza kuja kwake Masiya, Mwana wa Mungu, mwanga wa kweli wa ulimwengu. Yeye alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, inayowaangazia watu wote walio katika giza la dhambi na mauti wapate kuuona utukufu wa Mungu. Ni katika kuipokea Nuru hii ambaye ndiye Bwana wetu Yesu Kristo ndipo tunapokuwa na furaha ndani mwetu. Uaminifu wa Yohane Mbatizaji katika kutimiza mapenzi ya Mungu uliwavutia watu kutoka pande zote wakaja kubatizwa mtoni Yordani. Hii iliwafanya Wayahudi washangae na wakatuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemuili wamwulize, Wewe u nani? Wasemaje juu yako? Kwanini wabatiza? Yohane alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Yeye si Kristo, wala si Eliya wala si nabii yule waliomsubiri bali ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana yanyosheni mapito ili nuru ya kweli ipate kuingia ndani mwenu na kuwaangazia.

Maneno ya Yohane Mbatizaji kuwa: Yule ajaye nyuma yangu, mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake, ni maneno mazito sana na yenye maana kubwa mno katika historia ya wokovu wetu. Tukisoma kitabu cha Ruthu 4:1-11 tunapata maana ya kulegeza gidamu ya kiatu chake. Ilikuwa hivi; mwanamke aliyefiwa na mume wake akabaki mjane, kaka ya mume wake au ndugu wa karibu alipaswa kumchukua yeye pamoja na mali zake ili amtunze. Kama akimkataa alipaswa kufungua gidamu ya viatu vyake na kumkabidhi ndugu anayefuata kama ushahidi ili kudhibitisha na kuhalalisha kuwa hana hadhi ya kupokea huo urithi. Katika historia ya wokovu uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu unaelezwa kama uhusiano wa mume na mke. Kristo anakuja kurejesha uhusiano huu ulipotea kwa njia ya dhambi kama kumuoa mwanamke aliyeachwa na mume wake. Yohane kusema kuwa yeye hastahili kufungua gidamu ya viatu vya Yesu ni kuonyesha na kukiri kuwa mwenye mastahili ya kurudisha uhusiano huu ni Yesu mwana Mungu Masiha aliyetiwa mafutwa kama alivyotangaza nabii Isaya.

Yohane Mbatizaji anafurahia kuwa sauti tu ya kumshuhudia Kristo aliye nuru ya kweli, furaha ya kweli, amani ya kweli. Kumbe furaha ya kweli ya Mkristo imo katika kuinua sauti yake kama Yohane mbatizaji ili kumtangaza na kumleta Kristo kwa wengine. Hii ni kumpa Mungu nafasi yake ya kwanza kabisa. Kumbe tukitaka kuwa na furaha ya kweli ni kumpa Mungu nafasi yake, kumtumikia Mungu na sio vitu au watu. Tukifanya hivyo Bwana anakuwa karibu nasi ambaye ndiyo sababu ya Paulo kutuambia; furahini siku zote, tena nasema furahini, Bwana yu karibu. Ndiye Emanueli tunayemsubiri, Mungu pamoja nasi anayekuja kutufariji katika taabu zetu zote, lakini kwanza sisi wenyewe tunapswa kuwa faraja kwa wengine, kwani furaha inaingia mioyoni mwetu kwa kuwahudumia wengine.

Tunaishi na watu maskini, walemavu, wagonjwa na wenye shida mbalimbali. Tunapaswa kuwa sauti ya faraja na matumaini kwao ili kwa kupitia sauti yetu na matendo yetu wapate kumtambua Kristo aliye faraja na furaha ya kweli. Tutambue kuwa Mungu ana mpango na kila mmoja wetu, lakini ataweza kutimiza mpango wake tu kama tukimruhusu aingie katika maisha yetu, afanye maskani yake ndani ya roho zetu na kuyatawala na kuyaongoza maisha yetu. Tukifanya hivi masiha atakapozaliwa atazaliwa ndani ya mioyo yetu na kukaa humo akitimiza mpango wa Mungu katika maisha yetu.

TAFAKARI DOMINIKA III YA MAJILIO
11 December 2020, 17:26