Tafuta

Jumapili ya Neno la Mungu: Umuhimu wa Neno la Mungu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Jumapili ya Neno la Mungu: Umuhimu wa Neno la Mungu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. 

Dominika ya Neno la Mungu: Neno la Mungu Katika Liturujia ya Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko Lengo la Dominika ya Neno la Mungu ni: Kulisoma, kuliadhimisha, kulitafakari na kulimwilisha katika maisha ya kikristo, ikiwa ni pamoja na kusisitiza juu ya uhusiano uliopo kati ya Liturujia ya Neno na Liturujia ya Ekaristi Takatifu katika sadaka ya Misa. Waamini wajenge utamaduni wa kuliishi Neno la Mungu ambalo ni chakula cha kiroho na taa ya maisha yetu.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 3 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Domenika hii imepewa jina la “Domenika ya Neno la Mungu” na Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake binafsi “Motu Proprio” iliyopewa jina la “Aperiut illis” maana yake: “Aliwafunulia akili zao” ya 30/09/2019, katika kumbukumbu ya miaka 1600 baada ya kifo cha Mtakatifu Yeronimo Jalimu na Gwiji wa Maandiko Matakatifu. Lengo la Baba Mtakatifu Francisko kuiweka domenika hii kuwa ya Neno la Mungu ni kuliadhimisha, kulitafakari na kulieneza Neno la Mungu zaidi katika maisha ya kikristo, ikiwa ni pamoja na kusisitiza juu ya uhusiano uliopo kati ya Liturujia ya Neno na Liturujia ya Ekaristi Takatifu katika sadaka ya Misa Takatifu, kuwakumbusha waamini umuhimu na thamani ya Neno la Mungu katika maisha yao na hivyo kuwahimiza na kuwajengea utamaduni wa kulisoma, kulitafakari na kuliishi Neno la Mungu ambalo ni chakula chetu cha kiroho na taa ya maisha yetu.

Maneno ya mwanzo kabisa ya “Aperiut illis” yanasema; “Aliwafunulia akili zao ili waweze kuyaelewa Maandiko na kumtambua Yeye” (Luka 24:45).  Bwana wetu Yesu Kristo mfufuka, kabla ya kupaa kwake mbinguni aliwatokea wanafunzi wa Emaus waliokuwa wameshikwa na hofu na kukata tamaa, akawafunulia maana ya fumbo la Pasaka: yaani mateso, kifo na ufufuko wake ili kwalo awajalie watu wote wongofu na msamaha wa dhambi. Kabla ya kuwafumbua macho yao ili wamtambue kwa kuumega mkate (Sehemu ya pili ya Misa Takatifu, Liturujia ya Ekaristi Takatifu, ndiyo Sadaka ya Kristo Msalabani inayotolewa katika hali isiyo ya Damu Altareni), kwanza aliwafafanulia, akiwafunulia na kuwaeleza habari zake jinsi zilivyoandika katika Maandiko Matakatifu tangu Agano la Kale akianzia na Musa na Manabii wote, (Sehemu ya kwanza ya Misa Takatifu, Liturujia ya Neno). Hapa tunaona uhusiano uliopo kati ya Liturujia ya Neno na Liturujia ya Ekaristi Takatifu katika adhimisho la Misa Takatifu. Kumbe tunapoadhimisha Domenika hii ya Neno la Mungu tunatafakari kwa kina zaidi Fumbo la Ukombozi wetu ambapo bila kuyafahamu Maandiko Matakatifu, haiwezekani kulielewa. Lakini tunapolisoma Neno la Mungu mioyo yetu na inawaka na hivyo tunaweza kumtambua vyema Kristo Mkombozi wetu katika kuumega Mkate, Ekaristi Takatifu, Mwili wa Kristo ulio chakula chetu cha kiroho.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kuwa; “Utambulisho wetu Wakristo unafumbatwa kwa namna ya pekee katika uhusiano wa dhati kati ya Bwana Yesu Mfufuka, jumuiya ya waamini na Maandiko Matakatifu. Bila ya Bwana Yesu anayetuangaza (kwa njia ya Roho Mtakatifu zawadi alitujalia baada ya kupaa kwake mbinguni), haiwezekani kabisa kuelewa kwa kina Maandiko Matakatifu; lakini pia ni kweli kinyume chake: yaani, bila ya Maandiko Matakatifu haiwezekani kuelewa matukio ya utume wake Yesu na wa Kanisa lake ulimwenguni.” Ndiyo maana Mt. Yeronimo aliweza kuandika: “KutojuaMaandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo.” Masomo ya domenika hii ya tatu ya mwaka B wa kiliturjia kipindi cha kawaida yanatualika kumrudia Mungu. Injili inatuambia; “Tubuni na kuiamini Injili.” Katika somo la kwanza tunakutana na ujumbe wa Nabii Yona kwa waninawi ukisema; Siku 40 zimebaki, kiama inakuja, tubuni. Muda uliobaki si mwingi, jitayarisheni, wakati umetimia, ufalme wa Mungu umekaribia. Ni mwaliko wa Neno la Mungu unaotutaka tubadili mwenendo mbaya wa maisha yetu na tumgeukie Mungu wetu. Ili kumgeukia Mungu kunahitaji kuacha njia za shetani, kuacha dhambi, kuacha mazoea mabaya. Katika kufanikisha haya moyo wa sadaka unahitajika, moyo wa kudhubutu kuacha, ndio maana neno “acha” limetajwa mara tatu katika masomo ya leo.

Katika somo la kwanza la Kitabu cha Nabii Yona tunasoma: “Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.” Katika Injili tunasoma: “Mara wakaziacha nyavu zao wakamfuata.” “Wakamwacha baba yao na watu wa mshahara wakamfuata.” Tunaalikwa kuacha yote yasiyompendeza Mungu. Mungu alimwambia Yona aache kumtoroka na aende Ninawi Kuhubiri habari ya Kutubu na kumuungama kwa waninawi. Nao walipoziacha njia zao mbaya Mungu akaachana mpango wake wa kutaka kuwaadhibu. Yesu naye anawaalika Wagalilaya kuachana na maisha ya dhambi; “wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.” Si hivyo, Simoni, Andrea, Yakobo na Yohane nao wanaziacha nyavu na vyombo vyao, wazazi na watu wa mashahara, wamfuata Yesu. Katika Somo la pili Mtume Paulo anawaambia Wakorintho waachane na mambo ya Ulimwengu huu, kwani huu ulimwengu unapita.

Masomo haya yanatufundisha kuwa na Moyo wa sadaka. Kuacha kunaendana na moyo wa sadaka. Ili kuwa wakristo wa kweli ni lazima kuachana na mienendo ya zamani isiyoendana na imani ya kikristo. Watu wa Ninawi waliacha njia zao mbaya. Na Kristu anasema “tubuni na kuiamini njili.” Lazima kuacha na dhambi na kukiendea kitubio. Lazima kuachana na tamaduni na mila zisizoendana na ukristo wetu na ahadi zetu za ubatizo. Kumbe maisha mwanadamu ni safari ya kuacha. Na mwisho wa safari hii tunapokufa, tunauacha ulimwengu na kuingia mbinguni, ili kuingia mbinguni lazima kuicha dunia, na roho itauacha mwili na mwili utaiacha roho. Tusipojifunza kuacha tutalazimika kuacha kifo kitakapotujia. Tuangalie basi ni vitu gani vinavyotufanya tusiwe na uhusiano mzuri na Mungu au na wenzetu na tuseme inatosha sasa na kuamua kuviacha. Tunapaswa kujitafakari na kujiuliza; Je, ni kitu gani unakipenda sana lakini kinakupoteza? Achana nacho. Je, ni mtu gani unampenda sana lakini anakuharibia maisha yako, wito wako, ndoa yako? Achana naye. Je, hasira ndiyo inakufanya ukosane na wengine? Achana nayo.

Je, ukabila ndio unakufanya uwadharau wengine? Achana nao. Je, wivu ndio unakufanya uwachukie wengine? Achana nao. Je, uko kwenye urafiki mbaya unaokuharibia maisha yako? Achana nao. Je, uongo na kusengenya wengine ndio unakufanya watu wakuchukie? Achana nao. Je, dharau na kiburi ndio vinaleta shida katika familia yako? Achana navyo. Je, nyumba ndogo ndio imemaliza pesa zako na kukuvunjia ndoa? Achana nao. Je, pombe ndio inakufanya usahau watoto wako, kazi na familia? Achana nayo. Lakini kuachana na kitu ulicho kizoea au unachokipenda si kazi rahisi; kunahitahi moyo wa sadaka. Hii itawezekana tukijijengea moyo wa kulipenda, kulisoma na kulitafakari Neno la Mungu lenye hazina na utajiri wa mambo yote mazuri ya Mungu kama anavyotuambia Mtakatifu Efrem: “Nani anaweza kufahamu, ee Bwana, utajiri wote wa mojawapo ya maneno yako? Ni zaidi sana wingi wa tunayokosa kushika, kuliko tunaloweza kulifahamu. Sisi ndio watu wenye kiu, tunaokinywea chemchemi ya kikombe che Neno lako. Neno lako linatujalia maana nyingi mbalimbali, kama ilivyo mingi mitazamo ya wenye kulisoma na kulitafakari. Bwana alitilia neno lake uzuri wa rangi mbalimbali, kusudi wale wanaolichunguza waweze kugundua ndani yake kile wanachokipendelea. Alificha hazina zote katika neno lake, kusudi kila mmoja wetu apate utajiri wake ndani ya lile analolitazama.”  Niwatakie tafakari njema ya Neno la Mungu ambalo ni taa ya maisha yetu ili tujifunze kwalo kuacha yaliyo mabaya na kyatenda yaliyo mema kwa ajili ya ufalme wa mbinguni.

Jumapili Neno la Mungu
21 January 2021, 16:25