Tafakari ya Neno la Mungu Sherehe ya Epifania, Tokeo la Bwana: Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anajifunua kwa watu wa Mataifa kwa njia ya Kristo Yesu. Tafakari ya Neno la Mungu Sherehe ya Epifania, Tokeo la Bwana: Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anajifunua kwa watu wa Mataifa kwa njia ya Kristo Yesu. 

Sherehe ya Epifania: Ufunuo wa Mungu kwa Watu wa Mataifa!

Epifania ni sherehe inavyoonesha watu wa Mataifa walivyomtambua Yesu Kristo kama Mfalme, Kuhani na Mkombozi, kwa njia ya Mamajusi, wataalamu wa nyota waliotafuta ukweli wa mambo kupitia elimu ya nyota. Hawa walipoiona nyota ya pekee angani, walikumbuka utabiri wa Manabii Mika na Danieli usemao kwamba; Masiha atakapozaliwa itatokea nyota ya pekee mashariki.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, katika sherehe ya tokeo la Bwana, yaani Epifania. Neno Epifania asili yake ni lugha ya Kigiriki, likimaanisha kutokea, kujionesha au kujifunua. Epifania ni sherehe ya Mungu kujifunua kwa watu wa mataifa yote kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo kama tunavyosali katika sala ya mwanzo; Ee Mungu, uliyewafumbulia mataifa siku ya leo Mwanao wa pekee wakiongozwa na nyota, utujalie kwa wema sisi tuliokwisha kukutambua kwa imani, tuongozwe mpaka tuuone uso wako mtukufu. Kumbe Epifania ni sherehe inayotuonesha jinsi watu wa Mataifa walivyomtambua na kumkiri Kristo kama Mfalme, Kuhani na Mkombozi, kwa njia ya Mamajusi, wataalamu wa elimu ya nyota waliotafuta ukweli wa mambo kupitia elimu ya nyota. Hawa walipoiona nyota ya pekee angani, walikumbuka utabiri wa Manabii Mika na Danieli usemao kwamba; Masiha atakapozaliwa itatokea nyota ya pekee mashariki.

Katika somo la kwanza Nabii Isaya anatabiri kujifunua kwa Mungu kwa mataifa yote kupitia taifa lake teule la Israeli akisema kwamba; utukufu wa Bwana utakuja na kuiangaza Yerusalemu wakati huo kutakuwa na giza katika mataifa mengine ili watu waione hii nuru na kuja kuishujudia. Mataifa, wafalme na watu toka pande zote za dunia watakuja na kukusanyika ili waangazwe na hii nuru nao watamsujudia Bwana kama wimbo wa katikati unavyoimba; Mataifa yote ya ulimwengu watakusujudia ee Bwana. Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake kwa Waefeso anadhibitisha utabiri wa Nabii Isaya kuwa; ahadi ya kuletewa mkombozi Yesu Kristo, haikuwa kwa ajili ya Waisraeli tu, bali ni kwa ajili ya mataifa yote. Paulo anasema kwamba yeye alifunuliwa na kujulishwa siri kwamba; mataifa ni warithi pamoja na waefeso urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja wa ahadi yake Mungu iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.

Injili ilivyoandikwa na Mathayo inasimulia njinsi mamajusi walivyomtambua, wakamsujudia na kumtolea zawadi mtoto Yesu kama Mfalme wa mataifa yote. Mamajusi hawa ni mashahidi na wawakilishi wa watu wa mataifa kwa kumtambua na kumkiri Kristo. Licha ya kuwa Biblia haitaji majina yao wala nchi walikotoka, lakini wataalamu wa historia ya Maandiko Matakatifu wanasema kuwa majina ya Mamajusi hawa yalikuwa ni; Melkiori akitokea Uturuki, Baltazari akitokea Mongolia na Gaspari akitokea Ethiopia; kila mmoja peke yake akitokea katika nchi yake, walikutana njiani wakaamua kwa nia moja kuifuata ile nyota ili kumtafuta Masiha. Hatari, uchovu na urefu wa njia havikuwakatisha tamaa, mpaka wakafike alikokuwa mtoto Yesu. Bila shaka walitarajia kumkuta mtoto mfalme katika mji mkuu ndani ya nyumba ya kifalme ndiyo maana walipofika Yerusalemu walienda Ikulu ya Herode na kumuuliza, “yuko wapi yeye aliyezaliwa Mfalme wa Wayahudi, Kwa maana tuliiona nyota yake Mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Lakini kinyume chake wanamkuta Bethlehemu mji mdogo; tena si ndani ya nyumba ya kifalme.

Baada ya kumwona na kumtambua mwana wa Mungu wakapiga magoti wakamsujudia, wakafugua mikoba yao wakampa zawadi zao: dhahabu ikiwa ni ishara ya ufalme wa Kristo, ubani alama ya ukuhani wa Yesu na Umungu wake, na manemane ambayo ni mafuta ya kupaka maiti, kwa ajili ya maziko, ilikuwa ni ishara kuwa Yesu atajitoa sadaka, kuteswa na kufa kwa ajili ya dhambi zetu ili tupate kukombolewa. Kumbe, tunu au zawadi ambazo Mamajusi walizomtolea mtoto Yesu ni kama ushuhuda wake katika kumkomboa mwanadamu ndiyo maana katika sala ya kuombea dhabihu katika sherehe hii tunasali; Ee Bwana, tunakuomba utazame kwa wema dhabihu za Kanisa lako. Siyo dhahabu, ubani na manemane vinavyotolewa sasa, ila yule ambaye kwa dhabihu hizi tunamtangaza, tunamtoa sadaka na kumpokea, yaani Yesu Kristo.

Baada ya kutimiza haya yote Roho wa Mungu aliwaonya mamajusi wasimrudie Herode, kwani nia yake ni kumwangamiza mtoto Yesu maana habari za kuzaliwa zilimfadhaisha yeye pamoja na Yerusalemu yote. Naye alipoona hawajamrudia alitoa amri ya kuwaua watoto wote wakiume waliozaliwa kipindi cha Yesu, kwa lengo la kumuua mtoto Yesu ndiyo maana tarehe 28/12 kanisa linaadhimisha sikukuu ya watoto mashahidi, hawa ndiyo waliouwawa na Herode. Katika masomo ya siku hiyo utabiri wa nabii Yeremia unaosema, “Bwana asema hivi sauti imesikika Rama, kilio na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, asikubali kufarijiwa kwa kuwa hawako” ulitimia (Yer 31:15-16). Tumtafute Kristo kama Mamajusi walivyofanya. Mamajusi ni ishara kwa kila mtu anayemtafuta Mungu kwa moyo wote. Maisha yote ya mkristo ni safari ya kumtafuta Mungu. Safari hiyo ni ndefu ipitayo katika jangwa lenye hatari nyingi, hatupaswi kuwa na hofu sababu tunaye Kristo nyote yetu, daima yupo nasi, tujikabidhi kwake.

Tunapokutana na Kristo katika Neno lake, na katika Ekaristi Takatifu, ni lazima tuongoke, turudi nyumbani kwa njia nyingine kama Mamajusi yaani tuwe watu wapya tukiwa tumeuvua utu wa zamani wa dhambi na kuuvaa utu mpya wa neema. Ni kwa njia hiyo tutaweza kumpa Yesu kile chetu kilicho bora kama vile wale mamajusi walivyompa zawadi bora kabisa za dhahabu, uvumba na manemane. Maisha yetu yote ni hija kama ya Mamajusi, tukiongozwa na imani kuelekea Bethlehemu ya Mbinguni Kristo aliko. Hivyo, maisha yetu ni safari ya kwenda mbinguni ili kumwona Kristo uso kwa uso kama Yohane anavyotwambia “Lakini tunajua kwamba, wakati Kristo atakapotokea, tutafanana naye kwani tuamwona vile alivyo” 1Yoh.3:2.

Tuige pia mfano wa Mtakatifu Yosefu ambaye alikuwa mtu wa haki, mpole na mkimya, wala hasikiki akilalamika wa kunung’unika bali katika upole wake na ukimya wake anasikiliza sauti ya Malaika na kutekeleza kile alichoambiwa tangu siku ya kwanza alipoambiwa asiogope kumchukua Bikira Maria kama mke wake, alipoambia amchukue mtoto na mama akimbilie Misri na alipoambiwa amchukue na kurudi tena Yerusalemu na njiani anaagizwa asiende Yerusalemu bali Nazareti. Tuombe neema na baraka zake ili nasi tuweze kuisikia na kuifuata sauti ya Mungu ili ituangaze katika nuru ya kweli kama tunavyosali katika sala baada ya komunio tukisema; Ee Bwana, tunaomba ututangulie daima na popote kwa nuru yako ya mbinguni; na hili fumbo ulilolitaka kutushirikisha, tulitambue waziwazi na kulikubali kwa upendo.

04 January 2021, 07:38