Sikukuu Ubatizo wa Bwana: Sakramenti ya Ubatizo!
Na Padre William, Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Dominika inayofuatia sherehe ya Epifania, yaani Tokeo la Bwana, Kanisa huadhimisha sherehe ya Ubatizo wa Bwana. Sherehe hii ya Ubatizo wa Bwana ndilo adhimisho linahitimisha kipindi cha Noeli na kuashiria kuanza kwa kipindi cha kawaida cha liturjia katika Mwaka wa Kanisa. Kwa adhimisho hili ni kama vile tunahama sasa kutoka kuadhimisha kuzaliwa na utoto wa Yesu kuanza saa kuadhimisha utume ambao Yesu ameufanya. Ubatizo wa Yesu unakuwa ni kiashirio kwamba wakati wake umefika, wakati wa kuanza kuutekeleza utume wake. Karibu ndugu msikilizaji na msomjaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu kwa sherehe hii ya Ubatizo wa Bwana. Masomo ya Misa kwa ufupi: Somo la Kwanza (Is 55:1-11). Katika somo hili la kwanza, Nabii Isaya anatoa mwaliko wa kuupokea wokovu. Isaya anatoa mwaliko huu kwa wana wa Israeli waliokuwa utumwani Babeli na wokovu anaowatangazia ni kuwa hali yao ya utumwa itaisha na watarudishwa katika nchi yao. Anatumia lugha ya picha kuuelezea wokovu huo ambao kimsingi ni Mungu mwenyewe ndiye anayeutoa.
Na lugha anayotumia ni ile lugha ya wachuuzi au ya wafanya biashara katika masoko au minada tuliyoizoea. Anasema “kila aonaye kiu aje anywe, kila asiye na fedha na aje. Njooni mnunue divai na maziwa bila fedha na bila thamani kwani haifai kutoa fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula”. Kwa lugha hiyo, Isaya anaonesha kuwa mwaliko anaoutoa ni mwaliko unaohitaji mwitikio wa haraka. Ni bure kwa maana kwamba hauna gharama na hivyo haumpi mzigo wowote yule anayealikwa. Tunaona kwamba huu ni mwaliko wa wokovu kwa sababu maneno “kula na kunywa” au wakati mwingine inapotamkwa “karamu” ni maneo ambayo kibiblia yanaashiria wokovu na furaha ya kukutana na Mungu na kushibishwa mema yake. Na wale walio na “njaa na kiu” ndio wale wahitaji wa wokovu huo. Isaya anapowaonywa kuwa “kwa nini kutoa fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula” anawaonya wasihangaikie mambo yasiyo ya maana kwao, wasiweke tumaini lao katika yale yasiyoweza kuwasaidia na wasiwasikilize wale ambao mwisho wa siku watawahadaa.
Waisraeli wakiwa huko utumwani Babeli, waliibuka pia manabii wa uongo. Wengine waliwakatisha tamaa kwamba hawatakaa warudi makwao na wengine kuwajaza hofu na kuwatangatangisha kiimani. Onyo analolitoa Isaya ni kwa watu hawa waliojaa hofu na wanaotangatanga kiimani kuwa wokovu wa Mungu upo na ni wa uhakika. Ahadi zake ni za kweli na Neno lake ni lazima litimie. Isaya anawaalika watulie katika imani yao, waendelee kumtumainia Mungu na waupokee mwaliko wake wa wokovu. Somo la Pili (1Yoh 5:1-9): Somo hili linatoka katika Waraka wa Mtume Yohane kwa watu wote. Mwanzoni kabisa mwa waraka huu, Yohane anaeleza kuwa ameuandika ili kuwahubiria watu habari za Neno la Uzima kwa lengo la kuwapa uhakika wa kuupata uzima wa milele. Katika somo la leo anaeleza sasa kuwa hilo Neno la Uzima analohubiri ni Yesu Kristo ambaye amezaliwa na Mungu. Ndiye aliyekuja ulimwenguni katika maji na damu, yaani kwa kuutwaa ubinadamu halisi. Kuwa na imani kwake ni kuushinda ulimwengu na kuushinda ulimwengu ndio kuupata uzima wa milele.
Anachokiandika mtume Yohane sio kitu kipya. Tayari wakristo walikifahamu na kukiamini tangu mwanzo. Upekee wa fundisho hili la Yohane unakuja tukiangalia mazingira ambapo Yohane aliandika waraka wake huu. Kilikuwa ni kipindi ambacho yalikuwa yanaanza malumbano ya kiimani kumhusu Kristo hasa kuhusu ubinadamu wake. Baadhi ya makhalifa wa Mitume walianza kuelemewa na malumbano hayo kiasi cha kuanza kupindisha mafundisho ya imani. Waraka huu wa Yohana ulikuja katika kipindi hicho ukikiri na kuihifadhi imani halisi kuhusu umungu na ubinadamu wa Kristo na kusisitiza kuwa ni imani hii ndiyo itakayoushinda ulimwengu, yaani ndiyo itakayoshinda changamoto mbalimbali ambazo ulimwengu unazileta kwao wanaomwamini Kristo. Kwa maneno mengine, somo hili linaonesha jitihada za kulinda imani kwa Kristo, jitihada ambazo zimewekwa tangu mwanzo wa Kanisa na ni jitihada ambazo zinapaswa kuendelezwa kizazi hata kizazi kwa sababu changamoto za kiimani hazikomi bali hubadilisha sura kutoka enzi moja hadi nyingine.
Injili (Mk 1:7-11): Somo la Injili ya dominika hii ya ubatizo wa Bwana linaelezea tukio lenyewe la ubatizo kama lilivoandikwa na Marko. Huenda tofauti kidogo na wainjili wengine, mwinjili Marko anapoelezea tukio la ubatizo wa Yesu, anajikita zaidi kuelezea yale yanayotokea baada ya Yesu kubatizwa. Matokeo yenyewe ni kuwa mbingu zinafunguka, Roho kama njiwa anashuka juu yake na sauti inasikika “wewe ni mwanangu mpendwa wangu nimependezwa nawe”. Matukio yote haya yanaashiria kuwa kile kipindi cha kimasiha ambacho kilitabiriwa tangu kale na manabii, sasa kimefika. Kufunguka kwa mbingu kunaashiria kurudi kwa mahusiano ya moja kwa moja kati ya Mungu na mwanadamu, Tutakumbuka kuwa Mungu alipowafukuza Adamu na Eva bustanini Eden, tukio hilo lilimaanisha kufungwa kwa mahusiano ya moja kwa moja kati ya Mungu na mwanadamu na ndio kufungwa kwa mbingu.
Roho wa Bwana kushuka na kukaa juu ya Yesu kunatafsiriwa kuwa ndio kitendo cha Yesu mwenyewe kuwekwa wakfu na kupakwa mafuta kwa Roho Mtakatifu. Ni hapa ndipo Yesu anatambulishwa kama Kristo, yaani mpakwa mafuta wa Bwana. Mafuta aliyopakwa ndio ujazo wa Roho Mtakatifu mwenyewe. Sauti iliyosikika ni sauti ya Mungu mwenyewe, naye akamtangaza Kristo kuwa “ndiwe mwanangu”. Maneno haya “wewe ndiwe mwanangu mimi leo nimekuzaa” ni maneno ya Zaburi 2:7 ambapo yalitumika kwa mfalme Daudi. Leo maneno haya yanapata ukamilifu wake katika kuonesha kuwa mwana wa Mungu aliyekuwa anatajwa tangu enzi za mfalme Daudi ni Kristo. Pamoja na hilo, sauti inaongeza maneno “mpendwa wangu, nimependezwa nawe”. Kwa wayahudi, sifa hiyo ya mwana mpendwa waliihusianisha mara moja na Isaka mwana wa Abrahamu ambaye Mungu alipotaka atolewe sadaka alimwambia Abrahamu amchukue mwanae ampendaye (Mwa 22:2). Kumbe kusikika maneno hayo kwa Yesu kuliashiria tangu mwanzo sadaka ambayo Yeye mwenyewe angejitoa kwa ajili ya wanadamu na sadaka ambayo Mungu Baba angependezwa nayo.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tukio la Ubatizo wa Yesu tunaloliadhimisha dominika hii ni tukio linalomtambulisha Yesu kama Mwana wa Mungu. Kwa mara nyingine tena, Mungu anamfunua na kumtambulisha Yesu kuwa mwanae na tena mwanae mpendwa. Ni kwa sababu hii adhimisho la Ubatizo wa Bwana limeitwa pia Epifania ya pili. Na kama anavyotufundisha Papa Francisko, ni mwendelezo wa ufunuo ule ule wa Noeli, yaani Neno wa Mungu kutwaa mwili kuwa mwanadamu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni katika ufunuo huu tunauelewa vizuri zaidi ule mwaliko wa nabii Isaya tuliousikia katika somo la kwanza. Tunamwona Yesu kuwa ndiye ile “bidhaa” adimu na ya thamani lakini inayotolewa bure kwa wote wanaoipokea; wote walio na njaa na kiu yake.
Ubatizo wa Bwana ni tukio linalotukumbusha na kututafakarisha pia kuhusu ubatizo wetu sisi wenyewe. Mwinjili Marko amesisitiza mambo yale yaliyotokea baada ya ubatizo wa Yesu: mbingu kufunguka, Roho kushuka kwa mfano wa njiwa na sauti kusikika kuwa “wewe ni mwanangu mpendwa ninayependezwa nawe”. Hayo yaliyotokea kwa Yesu ndio yaliyotokea hata kwetu sisi baada ya ubatizo na ndiyo yanayoendelea kutokea kwa wote wanaobatizwa. Mbingu imefunguliwa wazi kwa ajili yetu kuingia, Roho Mtakatifu ameshuka akatutia alama isiyofutika milele, akakaa kwetu na kufanya miili yetu kuwa hekalu lake na Mungu mwenyewe ametufanya kuwa watoto wake wapendwa. Ni mambo makubwa sana yametendeka katika ubatizo wetu. Leo ni siku basi ya kumshukuru Mungu kwa zawadi hii kubwa na kumwomba ili neema za ubatizo tulioupokea ziendelee kufanyika upya ndani yetu. Ni siku pia basi ya kukiri upya imani tuliyoipokea katika ubatizo na kujiweka upya zaidi kuziishi ahadi zetu za ubatizo. Yesu Kristo mwana wa Mungu aliyefanyika mwili kwa ajili ya wokovu wetu na awe dira na chaguo letu la kudumu katika maisha.