Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili Pili ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Yohane Mbatizaji anamtambulisha Kristo Yesu kuwa ni Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za dunia! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili Pili ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Yohane Mbatizaji anamtambulisha Kristo Yesu kuwa ni Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za dunia! 

Neno la Mungu Jumapili 2 Mwaka B: Mwanakondoo wa Mungu

Baada ya Kristo Yesu kupokea Ubatizo wa toba uliotolewa na Yohane Mbatizaji, baadaye anamtambulisha kuwa Kristo Yesu ndiye Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu. Utambulisho huu unatoa nafasi kwa wanafunzi wa Yohane Mbatizaji kuanza kumfuasa Kristo Yesu, ili waweze si tu kushinda naye siku ile, bali kuwa ni Mitume wake ili kutangaza Injili ya Kristo!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na salama! Sehemu ya Injili ya leo inaonesha jinsi walivyoitwa baadhi ya mitume wa Yesu Kristo, ila tofauti na Injili ndugu ambazo zinatueleza kuwa mitume wale waliitwa katika mazingira ya maeneo ya ziwa Galilaya. Mwinjili Yohane kinyume na Injili zile ndugu, anataja kuwa ni katika kingo za mto Yordani, mahali alipobatizwa Yesu Kristo na Yohane Mbatizaji. Siku iliyofuata maanake ni siku baada ya ubatizo wake Yesu Kristo na hivi Yohane Mbatizaji aliendelea kubaki katika kingo za mto Yordani. Yohane Mbatizaji anamtambulisha Yesu kama Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za duniani. Ni vema katika tafakari yetu la leo tukaelewa jinsi mwinjili Yohane anavyotumia lugha ya picha kutupatia ujumbe mkubwa na hasa juu ya utambulisho wa Yesu Kristo. Mwinjili Yohane anatualika leo kutafakari kwa kina utambulisho huo, na hasa kwa kuangalia na kuzingatia lugha ya picha inayotumika. Wakati Yohane Mbatizaji alibaki katika kingo za mto Yordani, tunaona Yesu tayari ameanza kutembea, na hivi ni kusema ameanza utume wake mara baada ya Ubatizo ule wa toba uliotolewa na Yohane Mbatizaji. Yohane Mbatizaji sasa amemaliza kazi yake na sasa ni Yesu ndiye anayetembea na kutimiza utume wake. Na hivi Yohane Mbatizaji anawatambulisha wafuasi wake kwa Yesu Kristo na kuwaacha waanze kumfuasa Yesu Kristo na siyo yeye tena. Yesu anapaswa kuongezeka na yeye Yohane Mbatizaji kupungua. Rej. Yoh. 3:29-30

Yohane Mbatizaji alimkazia macho Yesu, kwa lugha ya Kigiriki neno linalotumika ni έμβλεψας (emblepsas – èmblepein) ambalo sio tu kuangalia kwa kawaida bali kuangalia ndani kabisa, kumwangalia mtu kiundani ili kuijua nafsi. Na ndio mwaliko anaotupa pia Yohane Mbatizaji wa kumwangalia Yesu Kristo sio kwa juu juu au kinjenje bali kuingia na kumwangalia kwa ndani kabisa, ni kuingia ndani mwake na kukutana naye katika uhalisia wake. Ni kumfahamu haswa huyu tunayemfuata na kujua ni nani kwangu na kwako. Yohane Mbatizaji, baada ya kumwangalia Yesu Kristo kiundani anamtambua kama Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za dunia. Kwa nini Yohane Mbatizaji anatumia picha ya mwanakondoo kumtambulisha Yesu Kristo. Yohane Mbatizaji hatumii majina mengine ambayo yangeweza kueleweka kirahisi kwa wasikilizaji wake, angeliweza kutumia majina kama ya mchungaji, mfalme, hakimu na kadhalika. Lakini anaona bado hakuna jina la kumfaa na kumtambulisha vema yeye aliyemtambua kwa kumwangalia ndani kabisa, bali ni kwa jina la Mwanakondoo.

Yohane Mbatizaji alijua vema Maandiko na ndio maana anatumia kumtambulisha Yesu kama Mwanakondoo wa Mungu. Yohane Mbatizaji anamtambulisha Yesu Kristo kama mwanakondoo akirejea kama mwanakondoo wa Pasaka ambaye damu yake ilipakwa katika miimo ya milango na hivi kuwaokoa wanawaisraeli. Na ndio damu yake Yesu Kristo itamwagika kwa ajili ya kutukomboa wanadamu wote. Yoh 19:14. Pia Yohane Mbatizaji anamtambulisha Yesu Kristo kama mwanakondoo akirejea unabii wa Isaya juu ya mtumishi wa Mungu anayeteseka (Anawim of Yahweh), anatepelekwa machinjioni kama mwanakondoo. Rej. Isaya 53:7,12. Yesu Kristo ndiye mwanakondoo anayekuja duniani kuondoa dhambi za ulimwengu kwa maana ya kuanzisha ufalme wa Mungu kati yetu, maisha ya mwanga na uwana wa Mungu. Ni mwokozi wa ulimwengu anayebeba dhambi zetu pale juu msalabani ili kutufanya kuwa wana wa Mungu. Pia Yohane Mbatizaji anarejea mwanakondoo yule ambaye Abrahamu alimtolea Mungu sadaka. Wakati wakiwa njiani mwanaye Isaka anamuuliza Abrahamu, moto tunao na kuni tunazo ila yu wapi mwanakondoo wa kutolea sadaka.

Na hivyo Abrahamu anamjibu Isaka kuwa Mungu atawajalia mwanakondoo. Mwanzo 22:7-8 Kama alivyo Isaka mwana pekee mpendwa na ndivyo alivyo Yesu Kristo, ni mwana pekee aliyependwa na Mungu Baba. Ndiye Mwanakondoo anayetolewa na Mungu mwenyewe ili damu yake itolewe sadaka pale juu msalabani kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. TAZAMENI MWANAKONDOO ndio mwaliko mkuu wa Dominika ya leo, kumwangalia Yesu Yesu Kristo kiundani na kumtambua kama mwanakondoo anayekuja kututoa katika utumwa wa dhambi. Kama ambavyo Isaka alikubali kutolewa sadaka kadiri ya masimulizi ya Midrashi na ndivyo pia Yesu Kristo alitupenda upeo mpaka anakubali mapenzi ya Baba yake ili afe kama mwanakondoo asiye na hatia kwa ajili ya mimi na wewe tulio wadhambi. Ni UPENDO wa namna gani huu! Ujio wake ni HABARI NJEMA kwa ulimwengu mzima. Yesu Kristo ni Habari Njema kwako na kwangu! Na ndio wanafunzi wake Yohana Mbatizaji hawakutilia shaka fursa hii adimu na adhimu na kutaka kumfuasa Yesu Kristo.  Na kinachoshangaza walianza kumfuasa bila hata ya kuitwa au kualikwa na ndio Yesu anawauliza wanatafuta nini.  

Ni katika swali hili tunakutana na maneno ya kwanza kabisa ya Yesu Kristo katika Injili ya Yohana.Ni swali pia kwangu na kwako kutoka kwa Yesu Kristo kama wafuasi wake.Ni swali la msingi na maana ili baadaye tusijejikuta tunamfuasa kwa sababu zisizo sahihi. Je, kwangu na kwako Yesu Kristo ni mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za duniani? Je, namfuasa Yesu Kristo kwa vile natarajia kupata mema ya dunia hii, au kutaka muujiza fulani katika maisha yangu, je naelewa vema juu ya huyu ninayemfuasa kuwa ni mwanakondoo ananialika nami kuishi kama mwanakondoo kwa maana ya kutimiza mapenzi ya Mungu? Pia cha kushangaza kutoka kwa wale wafuasi wawili badala ya kujibu swali la Yesu Kristo nao wanauliza swali lingine? Unakaa wapi? Yesu Kristo hakuwa na nyumba wala mahali pakulaza kichwa chake, hivyo swali lao maana yake ni nini haswa? Unakaa wapi au kwa kigiriki, (που μενεις) (pu meneis), maanake walitaka kuunganika kabisa naye, kuwa naye daima, kubaki naye popote na katika hali yeyote, ni kufunga ndoa na Yesu Kristo.

Hivyo swali lao halikumaanisha mahali bali kutaka nafasi katika maisha na nafsi yake Yesu Kristo. Ni mfano wa swali alilomuuliza Mungu mwanadamu yule wa kwanza baada ya kuanguka, upo wapi akimaanisha kwa nini umetoka katika urafiki na ukaribu nami, kwa nini umeenenda kinyume na maagizo yangu? Hivyo unakaa wapi ni kutaka urafiki na ukaribu na huyu mwanakondoo wa Mungu. Ni kutaka kuunganika kabisa na Yesu Kristo katika maisha ya kila mfuasi. Daima tunapotaka urafiki na Yesu Kristo katika maisha yetu jibu lake ni chanya kwako na kwangu. Ni mwaliko wa kutoka tulipo au kuachana na hali zetu za awali na kukaa naye na pia kumwangalia yeye anayetuita. Mwaliko wa Kikristo ni huo wa kwenda ili tubaki na Yesu Kristo tukimtazama (Ecce Agnus Dei).  Kama vile unapokutana na mtu unayempenda yatosha kumwangalia tu na kutabasamu kwa furaha na ndio mwaliko wetu kumtazama mwanakondoo wa Mungu! Wafuasi wale walifanya maamuzi baada ya mwaliko wa kwenda na kuona. Νa wakabaki naye mpaka saa 10 kwa maana ya siku nzima maana siku iliisha saa 10 jioni na saa 11 ulianza usiku, hivyo walibaki naye siku nzima kwa maana walibaki naye kwa maisha yao yote na walitembea daima katika nuru kwa maana maisha mapya.

Walimtazama Yesu Kristo na kumtambua kama Mwalimu na Masiha. Hivyo ni mwaliko pia wa kubaki daima na Yesu Kristo. Leo tunaalikwa nasi kujiuliza kama tunabaki na Yesu katika hali zote za maisha yetu, ni katika kubaki naye hapo tunakuwa kweli wafuasi wake, tunakuwa kweli rafiki wa kweli wa Yesu. Ile hamu na shauku ya kukutana na Masiha, daima haiwezi kumwacha mtu mfuasi wa Yesu Kristo salama, kutumia lugha ya siku hizi, hivi wanajawa na furaha na shauku ya kuwashirikisha na wengine. Andrea anakwenda kumshirikisha ndugu yake Simoni kuwa wamemwona Masiha. Na sasa tofauti na pale mwanzoni ambapo ilikuwa Yohane Mbatizaji aliyemtazama Yesu Kristo mpaka ndani (εμβλεψας) na kumtambulisha kama Mwanakondoo wa Mungu, sasa ni Yesu anayemtazama Simoni Bar Yona na kumuona kwa ndani na kumpa jina jipya linaloonesha utume wake mpya. Simoni sasa ataitwa Petro kumaanisha jiwe hai kama ishara ya kuimarisha Kanisa la Kristo katika imani, kama Kiongozi na Papa wa kwanza katika historia ya Kanisa.

Mwinjili Yohane kati ya wale wafuasi wawili waliomfuasa kwanza Yesu Kristo anatutajia jina moja tu la Andrea; Yafaa kuheshimu kwa nini mwinjili hamtaji huyo mfuasi mwingine, kwa kweli jina la huyo mwingine ni wewe na mimi, yafaa tuweke jina lako na langu kawa mfuasi yule mwingine ambaye inatosha kukutana na Yesu Kristo na kumfuasa na kubaki naye tukimtazama. Ni kwa kumtazama Yesu Kristo na kubaki naye daima ndio mwaliko wa kila mkristo. Na ndiyo maneno haya tunayotumia katika Liturjia ya Ekaristi: “Ecce Agnus Dei, ecce qui tollit peccata mundi. Beati qui ad cenam Agni vocat sunt” Neno: ‘’Tazameni…tazameni anayeondoa dhambi…heri yao walioalikwa kwenye kalamu ya mwanakondoo’’ Hakika Yesu Kristo ndiye mwanakondoo wetu, ni Yesu kweli katika Ekaristi Takatifu, hivyo tunaalikwa kumtazama huyu mwanakondoo na kufurahi, yatosha kumtazama unayempenda na kufurahi! Je, mimi na wewe tunapomtazama Yesu wa Ekaristi, tunakuwa na hiyo furaha ya kweli, je tunamuona Yesu Kristo kweli katika Ekaristi Takatifu? 

Ni lazima kutazamana kwa jicho kama la Yohane Mbatizaji na jicho la Yesu Kristo kama tulivyosikia katika Injili ya leo. Jicho la imani ndio pekee linaloweza kutusaidia na kutuongoza katika kumtambua Yesu katika maumbo yale duni ya mkate na divai katika Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu. Wapendwa tumwombe Mungu atujalie nasi jicho la imani ili tumtazame Yesu Kristo katika Ekaristi Takatifu na Neno lake na kumtambua kuwa ndiye Mwanakondoo na Masiya wetu. Dominika njema.

15 January 2021, 10:31