Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 4 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Nguvu ya Injili ya Kristo Yesu inayoganga, kuponya na kuokoa! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 4 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Nguvu ya Injili ya Kristo Yesu inayoganga, kuponya na kuokoa! 

Tafakari Jumapili 4 Mwaka B: Nguvu ya Injili ya Kristo Yesu!

Mwinjili Marko anatuonesha Kristo Yesu akifundisha kwa mamlaka na hata kuwaponya waliokuwa wagonjwa na wenye mapepo, yote ni kuonesha nia ya ujio wa Yesu duniani. Ujio wake ni kwa ajili ya kumwokoa mwanadamu kutoka utumwa wa kiroho na hata kimwili pia, maana mwanadamu ni mwili na roho. Mahibiri yake yaliwashangaza wengi, mwaliko ni toba na wongofu wa ndani!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na salama! Mara baada ya Yesu kuwaita wale wanafunzi wake wanne wa kwanza (Marko 1:16-20), anaweka makazi yake katika mji ule wa ufukweni mwa ziwa Galilaya, yaani Kapernaumu, na huu sasa ndio unakuwa mji wake na kuachana na kijiji chake kidogo cha Nazareti. Yesu anapokelewa na kufanya makazi yake katika nyumba iliyopo ufukweni kabisa na karibu na Sinagogi, ndimo nyumbani mwa Simon Petro. Mwinjili Marko anatuonesha Yesu akifundisha kwa mamlaka na hata kuwaponya waliokuwa wagonjwa na wenye mapepo, yote ni kuonesha nia ya ujio wa Yesu duniani. Ujio wake ni kwa ajili ya kumwokoa mwanadamu kutoka utumwa wa kiroho na hata kimwili pia, maana mwanadamu ni mwili na roho. Siku ya Sabato, kwa desturi Wayahudi wanakusanyika katika masinagogi yao kwa ajili ya kusali na kusikiliza Neno la Mungu. Kwa desturi Rabi ndiye aliyeandaa mikusanyiko ile ya siku ya Sabato. Ingawa mara nyingi Neno la Mungu lilisomwa na hata kufafanuliwa na rabi, lakini pia iliwezekana Myahudi mwanaume mtu mzima pia angeweza kupewa nafasi ya kusoma na kufafanua Neno kwa wote waliokusanyika.

Hivyo wengi waliofanya hivyo walijitahidi kuchagua masomo au sehemu ya Maandiko Matakatifu waliyokuwa wanayakumbuka maelezo ya ufafanuzi wake kutoka kwa mmoja wa walimu wa Kiyahudi. Hivyo anayefafanua ilitosha kurudia mafundisho ya Marabi na kuwashirikisha wengine katika kusanyiko la siku ya Sabato. Yesu kama Wayahudi wengine anaungana leo pamoja na watu wake kwa ajili ya kusali na kusikiliza Neno la Mungu. Kwa kawaida somo la kwanza lilitoka kutoka Vitabu vile vitano vya Sheria na somo la pili lilitoka kutoka kwa mmoja wapo wa manabii. Na aliyesoma somo la pili anapomaliza angeweza kuwashirikisha wengine kwa kuzingatia kama nilivyotangulia kusema hapo juu kukumbuka mafundisho ya Marabi. Yesu kinyume na mazoea na wengine wote tunaona leo Mwinjili Marko anatuonesha kuwa alifundisha kwa mamlaka. “Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi.” Marko 1:21-22. Ndio kusema Yesu hakurudia rudia yale waliyoyajua na kuyasikia kutoka kwa walimu wao wa dini, anakuja ili wabadili vichwa vyao, kuanza kufikiri kwa namna tofauti kabisa na ile ya kimapokeo.

Sio kusema Yesu anapingana na wale waliohubiri kabla yake bali sasa anatualika kuwa na picha sahìhi ya sura ya ufunuo wa Mungu. Dominika iliyopita Yesu Kristo alitualika kutubu na kuamini Injili, ni mwaliko wa kubadili kichwa, kuwa na mtazamo mpya kumhusu Mungu. Ni mwaliko wa kuwa na mahusiano mapya ya upendo kwa Muumba na jirani zetu. Na leo katika somo la kwanza na hata wimbo wa katikati wa leo na somo la Injili, tunaalikwa kuwa wasikilizaji wa Neno la Mungu. Ni katika Neno la Mungu hapo Mungu ananena nasi na kutufundisha njia zake, lakini zaidi sana kama tutakavyoona kwa kuruhusu Neno lake liingie na kusikika ndani mwetu pia hapo tunapokea uponyaji wa kweli katika maisha yetu, uponyaji kutoka nguvu za yule muovu na uovu. Yesu Kristo katika sehemu ya Injili ya leo anaonekana akiwa Kapernaumu, ni mji mdogo pembeni mwa Ziwa Galilaya, ni mji wa Petro na Andrea. Yesu Kristo haendi kuishi katika mji wake wa Nazareti bali tunaona sehemu kubwa ya utume wake anaufanya katika mji huu wa Kaperrnaumu na hapo anaishi katika nyumba au familia ya Simoni Pietro na Andrea nduguye.

Yesu Kristo anabadili mji wake, anabadili nyumba yake, ndio kusema anajiachanisha na mapokeo yote yaliyokuwa kinyume na utume na ujumbe wake, na ndio mwaliko wake katika maisha yetu hasa tunaposikia Injili yake kila Dominika inayotutaka na kutualika kubadili vichwa, kuanza mahusiano sahihi na Mungu na hata na wenzetu. Mwinjili Marko anaelezea juu ya nguvu ya Neno la Yesu Kristo, ni Neno lenye nguvu na kubadili kabisa maisha ya yeyote anayelisikia Neno hilo. Ni katika sinagogi, Yesu Kristo alifika kusali kama Wayahudi wengine wote. Ni baada ya kukutana na kulisikia Neno la Kristo, hapo tunasikia kuwa katika sinagogi alikuwepo mtu mwenye pepo mchafu. Mtu huyu kabla hatusikii habari zake, ndio kusema alibaki kimya na hata kwa utulivu wakati wa Ibada zikiendelea, watu wakisali, wakiimba na hata wakisikiliza Neno, lakini ghafla tu tunasikia mtu yule akapaza sauti, akisema “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu” Kama tulivyoona mtu yule hakuingia baadaye katika Sinagogi bali alikuwepo tangu mwanzoni mwa Ibada ile, lakini ikapika hatua fulani kitu kikamsukuma na kumfanya alipuke kwa kilio cha sauti kuu juu ya maangamizi yake.

Ndani ya mtu yule ndio tunaona kulikuwa na mgawanyiko wa nafsi, uwepo wa nguvu za Kimungu lakini pia uwepo wa yule muovu, ndiye Mwinjili anamtambulisha kama pepo wachafu. Ni ndani mwake si tu kulikuwa uwepo wa muovu bali hata na wema wa Kimungu, ni mtu aliyekosa kuwa mmoja ndani mwake mwenyewe. Ni hali tunazojikuta nazo katika maisha yetu. Tunabaki katika hali ya kuonekana tuna utulivu na amani mpaka pale itakapoingia sauti yenye nguvu za Kimungu, Neno lake Yesu Kristo ili kuangamiza uovu na ubaya ndani mwetu. Ni baada ya kusikia Neno la Yesu Kristo, Mwinjili Marko anatueleza kuwepo pia katika sinagogi mtu mwenye pepo wabaya. Uwepo wa Yesu katika maisha yetu daima unawafukuza pepo wabaya. Huyu mtu mwenye pepo alikuwepo pale tangu mwanzo, ila baada ya kusikia Neno la Yesu Kristo, ndiyo wale pepo wakaanza kumtesa huyo aliyekuwa na mapepo wabaya. Hapa amefika mmoja mwenye nguvu zaidi, ni uwepo wa nguvu kubwa zaidi, ni nguvu ya uwepo wa Yesu Kristo hata pepo wanaanza kupiga kelele na kulalamika. Yesu Kristo amekuja kuvunja nguvu zote za huyu ibilisi na ufalme wake.

Huyu mtu alikuwa na mapepo, kwa maana ya wingi wa nguvu za Ibilisi ndani mwake. Τοισ πνευμασι τοισ ακαθαρτοισ – the spirits unclean.  Ni nguvu za ibilisi zinazomzuia huyu mtu kuishi maisha ya ukaribu na Mungu.  Ni nguvu zinazokwenda kinyume na ubinadamu wetu, ni hulka na tabia zote zinazokwenda kinyume na upendo kwa Mungu na jirani mathalani, ubinafsi, chuki, visasi, na kila aina ya hila na ubaya ndani mwetu. Ni hali hizi basi Yesu amekuja ili kutuponya nazo, ni kwa kulisikia Neno lake na kuliruhusu liongoze maisha yetu tu hapo nasi tunapata uhuru wa wana wa Mungu. Ni kwa kuruhusu Neno lake liwe taa ya kutuongoza hapo tunapokea uponyaji wa kweli, kwani maisha yetu hayatakuwa tena chini ya yule muovu. Hali ya huyu mtu mwenye pepo inaonesha hali ya mtu ambaye bado hajakutana na Yesu Kristo katika maisha yake. Ni mmoja anayekuwa chini ya ufalme wa Ibilisi.  Yesu Kristo anamnyamazisha huyu mwenye pepo.  Kunyamazisha maana yake ni kumzuia kuendelea kuwa na mtazamo wake wa kale, ni kumtaka kuanza kuwa na mtazamo mpya katika maisha yetu.

Mara nyingi katika maisha yetu kwa kutaka kuendelea kutenda kwa namna zetu, kila mara tunasaka na kutoa sababu kadha wa kadha, ila Yesu Kristo anatutaka leo kunyamaza, kwa maana kubadili mtazamo wetu, na kuwa na mtazamo mpya. Mtazamo mpya ni huo anaoutangaza Yesu Kristo juu ya kumpenda Mungu na jirani.Tusiwe na neno wala sababu nyingine katika maisha yetu zaidi ya UPENDO kwa MUNGU na JIRANI. Yesu Kristo anaamuru pepo wabaya kutoka katika maisha yetu na ndio hali zetu za awali kabla ya kukutana na Yesu Kristo anayetutaka kubadili namna zetu. Kubadili kichwa na kuvaa kichwa cha Yesu Kristo mwenyewe. Ndugu zangu mwaliko wa Yesu Kristo katika Dominika hii ni kututaka kuwa wapya, kuwa na mtazamo na maisha mapya. Mtazamo na maisha mapya yatokanayo na NGUVU ya INJILI. Yesu Kristo amekuja ili tuwe na uzima na furaha ya kweli. Ni kwa kulisikiliza na kuliishi Neno lake tutakuwa huru kutoka nguvu za huyu mwovu. Pepo mchafu anataka bado kuendelea kutawala maisha ya huyu mtoto wa Mungu, anataka kuendelea kuwa sauti ya kuongoza maisha na hata fikra zake.

Na ndio tunaona pepo yule akimsihi Yesu amuache kwa amani, aismuondoe katika maisha ya yule mtu. Yesu anapokuja katika maisha yetu basi hapo yule muovu na hali za uovu ndani mwetu hazibaki tena katika utulivu na amani. Uwepo wa Yesu katika maisha yetu na hasa pale tunaporuhusu Neno lake liingie na kuongoza maisha yetu, kwa hakika yule muovu na uovu ndani mwetu vitalia kwa sauti na maumivu makuu, kama Yesu hampi nafasi ya kuongea wala kujieleza na kujitetea yule muovu, basi nasi tusikubali hata mara moja kulinyamazisha Neno la Mungu linapotukaripia na kutualika kubadili njia na maisha yetu. Ni kwa njia hiyo pekee ya kuruhusu Neno la Mungu kuchukua nafasi ya kutawala maisha yetu hapo nasi tunapokea uponyaji wa kweli. Pepo mchafu kama hata ilivyokuwa kwa Mtume Petro anamtambua Yesu kama Mtakatifu wa Mungu. Lakini pamoja na kulitambua na kumtaja bado Yesu alimwamuru anyamaze. “Simon Petro akamjibu, Bwana tutakwenda kwa nani? Wewe unayo maneno ya uhai wa milele. Sisi tunaamini, na tunajua kwamba wewe ndiwe yule Mtakatifu wa Mungu.” Yohane 6:59.

Mwinjili Marko kama ilivyo kwa Mwinjili Yohane, kutambua Yesu kuwa ni Mtakatifu wa Mungu, kuwa ni Mungu sio swala la mara moja au kwa njia ya muujiza bali ni mchakato unaofikia kilele na ukomo wake pale Kalvario. Ni ufahamu tunaoweza kuufikia baada ya safari ya imani pamoja na Yesu mpaka saa ile ya wokovu, ndio saa ya pale Msalabani. Imani ya kweli kwa Kristo haizaliwi kwa njia ya miujiza bali kubaki na Yesu katika saa ngumu ya maisha yetu, kubaki naye tukiwa chini ya msalaba. Na ndio mwaliko wa Mama Kanisa tunapotembea katikati ya janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kubaki chini ya Msalaba wake Yesu tukisali na kulia kwa imani, pamoja na Mama yetu Bikira Maria. Ni kwa kukubali kusamehe na kupenda hapo nafsi zetu zinapokea uponyaji wa ndani katika maisha yetu. Kila mara tukienenda kadiri ya Neno na maagizo yake, na ndio njia ya kumnyamazisha yule muovu na uovu unaokuwepo katika maisha ya kila mmoja wetu. Neno la Mungu tunalolisikia labda wengine kila siku katika Ibada zetu mbali mbali halina budi kubadili maisha yetu, kuyaponya na kuyafanya kuwa bora zaidi.

Ni wito wa Kristo kwa kila mmoja wetu kuruhusu Neno lake kuingia na kubadili maisha yetu. Haitoshi kulisikia na kurejea kuishi ukale, kuishi kadiri ya yule muovu na uovu, kwani hapo tunakuwa sio wakristo wa kweli, sio rafiki zake Kristo. Rafiki na muumini wa kweli ni yule anayekubali kukua, anayekubali kubadilika maisha yake kwa kuwa karibu zaidi na zaidi kwa Mungu na jirani.Nawaalika kama wanavyotutaka sasa viongozi wetu wa Kanisa nchini Tanzania, basi pia tuchukue tahadhari kubwa bila woga au taharuki kujilinda na kujikinga dhidi ya janga la Corona, COVID-19. Kila mmoja wetu kwa nafasi yake hana budi kulinda uhai wake na pia wa jirani yake, yaani wa mwingine. Turudie tena kutekeleza ushauri wa wataalamu ili tusiwe chanzo cha kudhulumu maisha yetu wenyewe na ya wale wanaotuzunguka. Pamoja na hayo hatuna budi kutambua umuhimu na ulazima wa kusali na kumlilia Mwenyezi Mungu ili atuponye na kutukinga na janga hili. Kusali ni kukaa mbele ya Mungu, ni kujadiliana na Mungu, ni kwenda mbele ya mmoja anayetupenda kwa hakika, hivyo tusali kwa imani.

Lakini pia Mwenyezi Mungu ananialika mimi na weye pia kutimiza wajibu wetu kwa kuchukua tahadhari zote muhimu. Kamwe tusipuuzie inapowezekana kufuata ushauri wa wataalmu wetu wa afya. Nawasihi hatuna sababu ya kutaharuki kwani huko ni kuzidi kuingia katika shida zaidi. Kutaharuki na kuogopa ni kuacha kutumia “vema vichwa vyetu” na hata kunaweza kulifanya tatizo liwe kubwa zaidi. Kila mmoja wetu atulie na aone njia sahihi za kujilinda na kuwalinda wengine bila kuwaogofya wala kuwafanya wengine washindwe kuishi. Tusiruhusu woga utawale bali imani yetu kwa Mungu ituongoze na pia kwa kutumia vema mapaji ya akili na utashi aliyotujalia Mungu katika nyakati hizi ngumu na zenye changamoto duniani kote. Nawatakia Dominika na tafakuri njema! Bikira Maria, afya ya wagonjwa, utuombee!

29 January 2021, 11:18