Tafakari Jumapili Ya Pili ya Noeli: Yesu Ni Mwanga wa Mataifa
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Liturujia ya Dominika ya 2 ya Noeli, masomo ya Misa bado yanatualika kulitafakari Fumbo la Noeli, yaani, fumbo la Umwilisho wa Neno wa Mungu. Somo la Injili la Dominika hii ni lile tulilolisikia katika Misa ya mchana ya siku ya Noeli, ni somo la Utangulizi wa Injili ya Yohane. Kama ilivyo kwa Wainjili wengine, katika utangulizi hapo inabeba ujumbe wa msingi unaobebwa na Injili nzima. Ni mahali muhimu kabisa ili kuweza kuielewa Injili husika kwani hata baadhi ya mada kuu huanza kutambulishwa ama kwa kugusiwa moja moja katika utangulizi. Hivyo, kuuelewa vema utangulizi unasaidia sana kupata ujumbe wa Injili husika. Mwinjili Yohana tofauti na Wainjili wengine, Utangulizi wa Injili yake ni wimbo wenye ujumbe mzito wa Kitaalimungu. Ni hapo katika wimbo wa utangulizi tunaona aina ya uandishi wa Yohane, kwani tayari ujumbe wa Injili yake unatupa picha kamili ya Injili nzima. Ni Injili inayotualika tangu mwanzoni kuisoma sio tu kama masimulizi bali zaidi sana kama ujumbe wa Kitaalimungu. Yesu anatambulishwa kama mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, asili ya uhai wote, mwanga wa ulimwengu, aliyejaa neema na kweli yote, Mwana pekee wa Baba anayekuja kuufunua utukufu wa Mungu.
Katika sehemu ya kwanza ya wimbo huu wa utangulizi wa Injili yake, aya 1-5, Yohane anatumia lugha ya Vitabu vile vya Hekima. Hekima inazungumziwa kuwepo milele yote kabla ya kuumbwa kwa dunia. “Mwenyezi Mungu aliniumba mwanzoni mwa kazi yake, zama za zama kabla ya kuwako kitu chochote. Nilifanywa mwanzoni mwa nyakati, nilikuwako kabla ya dunia kuanza. Nilizaliwa kabla ya vilindi vya bahari, kabla ya chemchemi zibubujikazo maji. Kabla ya milima haijaumbwa, na vilima kusimamishwa mahali pake, mimi nilikuwako tayari. Kabla Mungu hajaumba dunia na mashamba yake, wala chembe za kwanza za mavumbi ya dunia. Nilikuwapo wakati alipoziweka mbingu, wakati alipopiga duara juu ya bahari; wakati alipoimarisha mawingi mbinguni, alipozifanya imara chemchemi za bahari; wakati alipoiwekea bahari mpaka wake, maji yake yasije yakavunja amri yake; wakati alipoweka misingi ya dunia.” Mithali 8:22-29. Hekima inachukua tena nafasi ya nafsi hata Kitabu cha Sira 24:3-8 na 22. Hekima inajinafsisha katika Torati, katika Sheria na kutwaa makao yake katika Israeli.
Mwinjili Yohane anajua vema Maandiko na hasa Agano la Kale na ndio anatumia rejelea hizi katika kumtambulisha huyu Mtoto aliyezaliwa, ni Neno wa Mungu, ni Hekima ya Mungu ya milele yote, ni Mungu katika umilele wake. Huyu Mtoto ni Hekima ya Mungu inayokuja na kutwaa makazi yake kati yetu, katika maisha yetu, katika nafsi na maisha ya kila mmoja wetu na kwa namna ya pekee ili nasi tuweze kuongozwa katika hekima hiyo ya Kimungu. Ni Neno wa Mungu wenyewe anayekuja na kukaa kati yetu, tofauti na Sheria ile ya Musa, sasa ni Mungu mwenyewe anayetwaa mwili na kuwa sawa na sisi isipokuwa hakuwa na dhambi. Tofauti na hekima iliyochukua nafsi katika Kitabu cha Sira 24:9, Neno wa Mungu, sio kwamba liliumbwa bali ni Mungu wa milele yote anayetwaa mwili na kukaa kati yetu. Mwinjili Yohane anatuonesha leo kuwa Mtoto aliyezaliwa ni Mungu anayetwaa mwili wetu na kukaa kati kati yetu, ni yeye aliye mtoaji wa uzima wote tangu milele.
Ujio wake, na ndio fumbo la Umwilisho, unaigawa historia ya mwanadamu katika sehemu kuu mbili. Kabla ya ujio wake, ndio wakati ambapo mwanadamu alitembea gizani, na baada ya ujio wake, ambao wale wote waliompokea walianza kutembea katika nuru na kweli. Ni Neno linalokuja ili kuiondoa lile giza la uovu ndani ya mwanadamu, linakuja kutupa uzima wa kweli kwa kila mmoja anayekubali kuongozwa naye, kwa kuupokea mwanga na kutembea katika nuru ya kweli. Kuanzia aya ile ya 6-8, Mwinjili Yohane anamtambulisha mhusika wa pili naye ni Yohane Mbatizaji, lakini huyu tofauti na Neno wa Mungu, hakuwa Mungu na wala sio wa milele, bali amekuja ili kuishuhudia ile nuru. Yohane Mbatizaji hakuwa ile nuru bali kazi yake inatajwa mara tatu, nayo ndio ile ya kuishuhudia nuru ya kweli, ya kuwa mtangulizi ili kuwatambulisha watu kuilekea ile nuru, ni kidole kinachotuonesha na kutualika kuifuata ile nuru ya kweli na ya milele.
Aya ya 9-13, inajaribu kutuonesha sasa ile nuru ya kweli inayokuja ulimwenguni, yaani, Mtoto Yesu aliyezaliwa kwetu. “Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua.” Mwinjili Yohane anamtofautisha Yesu, kuwa ndiye nuru ya kweli inayokuja ulimwenguni. Kwa kuwa sisi sote tunatamani kutembea katika nuru, katika iliyo kweli, basi leo tunaalikwa ni kwa kumpokea Yesu, Neno wa Mungu, ni kwa kulishika Neno lake hapo tunakuwa na hakika ya kutembea katika nuru na kweli. Lakini pia Mwinjili Yohane anatuonesha kuwa pamoja na ujio wa nuru ya kweli, lakini bado si wote wamempokea. “Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale walioaminio jina lake; waliozaliwa sio kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.”
Noeli ni sherehe ya mwanga, ya Neno wa Mungu aliye nuru ya kweli anayekuja ili kila anayempokea aenende na kutembea katika nuru, lakini kinyume chake ni kushupaa na kubaki katika giza, katika maovu na dhambi, Noeli ni sherehe ya kutualika sisi tutembee katika huru kwa kuachana na utumwa wa yule mwovu na hila zake. “Nilitafuta kwao wote mahali pa kupumzika, nikatafuta ni eneo la nani ambako ningeishi. Hapo huyo Muumba wa vitu vyote akanipa amri; huyo aliyeniumba akanipangia mahali pa maskani yangu. Aliniambia, fanya makao yako kwa Yakobo, pokea sehemu yako kutoka kwa Israeli.” Sira 24:7-8. Lakini hata watu wake yaani, taifa lile la Israeli halikuwa tayari kumpokea. Hawakuweza kumtambua Mungu katika mtoto huyu mchang, mtoto fukara na maskini aliyezaliwa na wazazi wa hali duni kabisa, na tena katika hori la kulishia wanyama badala ya majumba ya kifalme.
Ni mshangao kwani Yesu anakataliwa sio tu na watu wa kawaida bali hata na wale wenye uelewa mkubwa wa Maandiko Matakatifu. Hata Yesu pia alibaki na mshangao mkubwa juu ya kutokuamini kwao. “Alishangaa sana kwa sababu ya kutoamini kwao.” Marko 6:6 Nuru inayokuja kutoka juu haitulazimishi kuipokea, na badala yake inatuacha huru kabisa kuipokea au la. Haitumii mabavu wala maguvu, na ndio daima Mungu anavyokuja kwetu haji kwa kutulazimisha kwa kutupora uhuru na utashi wetu, bali anatualika ili tuweze kuiona nuru na kuipokea katika maisha yetu. Kumpokea au kuamini hakutokani na akili za kibinadamu na badala yake ni kumpokea kwa mapendo mazima katika maisha yetu. Imani ni zawadi kutoka kwa Mungu, ni Mungu anayejitoa zawadi kwa mwanadamu, hivyo ni kwa kutumia utashi na uhuru wetu kuipokea zawadi ile au la.
Wale wanaompokea wanafanyika kuwa watoto wa Mungu. Ndio kuzaliwa mara ya pili ambako Yesu anazungumzia kwa Nikodemo. Yohane 3:3. Ni kuzaliwa kiroho kunakotokana sio na mwili bali na Roho Mtakatifu. “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” Kwa kweli hapo ndio haswa ujumbe mzima wa Noeli umebebwa, wa fumbo zima la Umwilisho wake Mwana pekee wa Mungu, wa kuutwaa mwili na kukaa kati yetu. Na ndio ukweli wa Imani tunaoukiri katika siku hizi takatifu za Noeli, ndio kanuni ya Imani ya Nisea tunayoisali kila Dominika, kila mara tunakiri na kusema tunasadiki kuwa Yesu ni mtu kweli na Mungu kweli.
Ni katika fumbo hili la umwilisho hapo tunauona utukufu na ukuu wa Mungu, ndio hasa upendo wa kustaajabisha wa Noeli, kwani Noeli ni sherehe ya mshangao. Ni mshangao tunaobaki na kugubikwa nao kila mara tunapofika katika pango ili kumsujudia Mtoto Yesu, ni Mungu anayekaa pangoni, anayekubali kutwaa hali duni kabisa, ni Mungu anayetaka kufanana nasi isipokuwa dhambi. Ni sherehe ya mshangao mkubwa! “Mwili” katika Maandiko ndio kusema hali yetu duni, ya kuweza kuteseka na kutaabika. Ni hapo kwa kweli tunabaki na mshango mkubwa, Neno wa Mungu, aliye wa milele yote, anayetoa uzima wote, lakini anakubali kujivua hadhi yake na kuutwaa mwili wetu unaoharibika. Nabii Isaya anaonesha wazi hali yetu ya kuwa katika mwili pale anapoimba na kusema; “Sikiliza! Kuna sauti inasema, tangaza! Nami nikauliza, nitangaze nini? Naye: Tangaza: binadamu wote ni kama majani; uthabiti wao ni kama ua la shambani. Majani hunyauka na ua hufifia, Mwenyezi Mungu avumishapo upepo juu yake. Hakika mwanadamu ni kama majani. Majani hunyauka na kufifia, lakini Neno la Mungu wetu ladumu milele.” Isaya 40:6-8.
Ni mwaliko ambao kwa namna ya pekee katika janga la maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, tunaalikwa tena kutafakari unyonge na uduni wetu, ni mwaliko wa kuona kuwa maisha yetu hayana maana nje ya Neno la Mungu. Ni mwaliko wa kumkimbilia Mwenyezi Mungu siku zote za maisha yetu. Neno anafanyika mwili, ndio kusema anakuwa sawa na sisi katika kila hali isipokuwa dhambi. Neno anatwaa hali yetu duni na dhaifu ya kuweza kuteseka na kuwa na mipaka isipokuwa hakuwa na dhambi. Ni upendo wa kutaka kufanaan nasi, unayempenda unataka kushiriki hali yake iwe ni furaha au huzuni, unataka kumhakikishia kuwa upo pamoja naye, ni upendo wa Mungu huu unaotuacha na mshangao katika sherehe hizi za Noeli, za Mungu kuwa sawa nasi katika hali zetu duni na dhaifu. “Nasi tukauona utukufu wake.” Ndio kusema katika hali ya kawaida sio rahisi kumuona Mungu wala utukufu wake, ila ni hakika leo kwa kila mmoja anayempokea huyu Neno wa Mungu, anayetwaa mwili na kukaa kwetu.
Pangoni tunaalikwa kuiona ishara, ndio kuuona utukufu wa Mungu, kukutana na kumwona Mungu katika Mtoto Yesu aliyezaliwa kwetu. Ni pale pangoni tunaalikwa kubaki na mshangao. Ni vema katika sherehe hizi kila mmoja wetu akachukua wasaa wa kufika pangoni na kuutafakri upendo na utukufu wa Mungu katika fumbo zima la umwilisho. “Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.” Tunaona na kuusikia tena ushuhuda wa Yohane Mbatizaji si tu kwa watu wa nyakati zile bali hata kwetu leo. Yohane Mbatizaji alipaza sauti yake ili kuishuhudia kweli hii ya imani, ni tangazo la imani, linalotutaka nasi leo kulikiri sio tu kwa vinywa na maneno bali hasa kwa maisha yetu, kwa kuonesha kuwa kweli sisi ni watoto wa Mungu na tumefanyika kuwa kwa njia yake Yesu Kristo, ndio kuishi maisha ya nuru na kweli, maisha ya kufanana na Mungu katika utakatifu. Yesu Kristo anakubali kutwaa mwili na kukaa kwetu ili nasi tuweze kufanyika wana wa Mungu.
“Kwa kuwa katika ukamilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torat ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.” Ndio Mwinjili Yohane anahitimisha kwa kutuonesha kuwa zawadi ya Noeli haina mfano wala ulinganisho wake, ni Mungu mwenyewe anayejitoa zawadi na ndio maana Noeli ni sherehe inayotuacha sote na mshangao mkubwa. Ni Mungu anayekuja na kukaa kati yetu, sio tena sheria yake bali ni Yeye mwenyewe. Ni sasa tunaweza kumwona Mungu kwa namna ya pekee na katika ukamilifu wake kwa njia ya Mtoto Yesu. Na hata leo kama alivyopenda kusema Mwenyeheri Carlo Acutis, kuwa sisi leo tuna bahati kuliko hata wale walioishi Palestina katika enzi zake Yesu wa Kihistoria, nyakati zile ili kukutana naye ilibidi wasafiri ila sisi leo ni katika Neno lake, ni katika masakramenti yake na katika Kanisa lake anazidi kujimwilisha na kubaki kati yetu. Noeli ni fumbo la Umwilisho, ni fumbo linalotuacha na mshango mkubwa hasa tunapoutafakari upendo na huruma ya Mungu kwetu. Nawatakia nyote Dominika njema ya kulitafakari fumbo la Umwilisho. Na kila mmoja namtakia mwaka mpya wenye kila neema juu ya neema zitokazo kwake Mtoto Yesu.