Kristo Yesu Ni: Neno wa Mungu, Nuru, Njia, Ukweli Na Uzima!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Jumapili ya Pili Baada ya Sherehe ya Noeli, Mwaka B wa Kanisa. Katika historia ya wokovu, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo amejifunua kwa njia ya Sheria, kielelezo cha utambulisho, dira na mwongozo wa watu wa Mungu. Mwenyezi Mungu amejifunua kwa njia ya Manabii wake watakatifu, waliotumwa kutangaza na kushuhudia uwepo wake endelevu katika hija ya maisha ya waja wake. Hatimaye, Mwenyezi Mungu katika nyakati hizi amejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, Uso wa huruma na upendo wa Baba wa milele. Huyu ndiye Neno aliyekuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huu ni muhtasari wa Injili kama ilivyoandikwa na Yohane, kama tunavyousoma katika Dibaji au Utangulizi wa Injili yake. Hii ni sehemu ya Habari Njema ya Wokovu inayowaambata na kuwakumbatia watu wa nyakati zote. Ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Huyu ndiye Nuru halisi inayomtia nuru kila mtu na wala hakuna mtu awaye yote anayeweza kuikwepa nuru hii. Ndiye Kristo Yesu, aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli.
Hivi ndivyo Mama Kanisa anakiri na kuungama katika imani yake. Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima. Mtakatifu Augustino Askofu na Mwalimu wa Kanisa anasema, Kristo Yesu ni ukweli uliofanyika njia inayowapeleka watu mbinguni kwa Baba yake wa milele. Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, alizaliwa bila kuumbwa, mwenye umungu mmoja na Baba; ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu! Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba amejaa neema na kweli. Yesu mwenyewe anajitambulisha kwa kusema, “Mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi” Yn. 14:6. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu amekuwa njia, ukweli na uzima. Hii ni KIRI ya Imani inayoshuhudia kwamba, Kristo Yesu ni njia ya wokovu wa binadamu wote: “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu waliopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo” Mdo. 4:12.Huu ni utambuzi na utume wa Wakristo wote wa kutangazwa na kushuhudiwa si tu kwa maneno, bali kwa vitendo kama kielelezo cha imani tendaji.
Mtakatifu Paulo, Mtume katika Waraka wake kwa Waefeso, katika Somo la Pili, anasema, alipopata habari za imani yao katika Bwana Yesu na pendo lao kwa ajili ya watakatifu wote, haachi kutoa shukrani kwa ajili yao, akiwakumbuka katika sala zake, ili Mungu wa Bwana wetu Yesu, Baba wa utukufu, awakirimie roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua Yeye. Rej. Efe.1: 16-17. Kristo Yesu, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu ameupatanisha ulimwengu wote na Mwenyezi Mungu. Huyu ndiye Neno wa Mungu “ambaye hapo mwanzo alikuwako kwa Mungu naye Neno alikuwa Mungu” Yn. 1:1. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, wanawahimiza waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa njia ya maisha yao yanayokita mizizi yake katika heshima na upendo kwa njia ya majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, tayari kutamadunisha mila na desturi njema, daima waamini wakijitahidi kusoma alama za nyakati. Rej. AG. Namba 11.
Somo la Kwanza, linadokeza Hekima ambayo ilimwilishwa katika Sheria, ikawa dira na mwongozo wa kuwaonesha njia Waisraeli katika safari ya wokovu. Manabii wakaitangaza na kuishuhudia Sheria hii kama ufunuo wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Katika muktadha huu, Yohane Mbatizaji anamshuhudia Kristo Yesu kwa kusema “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo”. Yn. 1:17. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ni Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kumpokea Kristo Yesu, Nuru ya ulimwengu, Ukweli na Uzima chachu ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo yenye mvuto na mashiko. Waamini wajitahidi kukutana na Kristo Yesu katika: Neno na Sakramenti za Kanisa; kati ya maskini na wanyonge wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa kidugu unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Neno wa Baba wa milele, Nuru ya uzima ambaye amekuwa: Njia, Ukweli na Uzima.