Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Kwanza ya Kwaresima: Majaribu!
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na salama! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi Cha Kwaresima kwa Mwaka 2021 unaonogeshwa na kauli mbiu: “Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu:” Mt. 20:18: Kwaresima ni Kipindi cha Kupyaisha Imani, Matumaini na Mapendo. Ni hapo tunaona Yesu anawafunulia siri kuu ya misheni na ujio wake ulimwenguni. Kwaresma ni kipindi cha neema, ni “Kairos”, wakati wa kutafakari fumbo la ukombozi wetu kwa mapana na marefu yake, lakini hasa kuutafakari upendo wa Mungu kwetu wanadamu. Kwaresima ni kipindi cha toba, kufanya mageuzi na mapinduzi ya kweli katika maisha yetu, ndani mwangu na mwako, kila mmoja wetu anaalikwa katika Kwaresima ya mwaka huu kupyaisha tena Imani yetu, kwa kuchota maji ya uzima yenye matumaini nah apo kuonja upendo wa Mungu kwetu wanadamu.
Safari ya Kwaresima ya siku arobaini, ambayo inakolezwa na kusindikizwa kwa mfungo, sala na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mathayo 6:1-18. Ni kwa kufunga, hapo tunajikatalia na kujifukarisha kwa ajili yaw engine wanaokuwa wahitaji zaidi yetu. Kwa matendo ya huruma tunawageukia na kuwakaribia na kuwagusa wenye uhitaji mkubwa zaidi yetu, na ni katika sala tunaingia katika mazungumzo ya kimdahalo na Baba yetu wa mbinguni, anayetuwezesha kuwa na Imani ya kweli, matumaini hai na upendo unaojidhihirisha katika matendo. Baba Mtakatifu anatuambia, Imani inatutaka kuukumbatia ukweli na kuwa mashahidi wa kweli zile tunazoziamiani, mbele ya Mung una mbele ya kaka na dada zetu. Baba Mtakatifu anakumbusha kuwa kisima cha mwanzo za kweli za Imani yetu ni Neno la Mungu. Ni kwa njia ya Neno lake, Imani yetu inapata kuenea kutoka kizazi kimoja mpaka kingine na kwa njia ya Kanisa. Ukweli huo sio kwa ajili ya watu wachache wenye karama na kipawa Fulani bali ni Yesu Kristo Mwenyewe anayekuja na kutaka kufanya makazi yake katika maisha ya kila mmoja wetu.
Matumaini kama maji ya uzima, yanatuwezesha kuendelea na safari hii ya Kwaresima ya siku arobaini. Yohane 4:10. Mwanamke msamaria pale kisimani mwanzoni hakuelewa kuwa anayeomba maji ndiye maji ya uzima, yaani ujio wa Roho Mtakatifu kama anavyotushikia na kutupa tena matumaini ndani mwetu kwa wale wote waliopoteza matumaini katika maadhimisho ya Pasaka. Sote tu mashahidi kuwa tunasafiri katika kipindi kigumu cha historia ya mwanadamu, kote ulimwengu tunapopambana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, gonjwa na janja baya linalosababishwa na kirusi cha korona, ni wakati tunaalikwa basi kumwangalia Yesu msulubiwa na kumkimbilia yeye ili tusipoteze matumaini ya kweli ndani mwetu. Tunaalikwa kuwa wajumbe wa matumaini iwe katika nafsi zetu wenyewe, familia zetu na katika ulimwengu mzima. Waamini na hasa marafiki zake Kristo mfufuka tunapaswa kuwa wajumbe na mashahidi wa matumaini, matumaini yale tunayoyachota sisi wenyewe kwa nafasi ya kwanza kwa Kristo Mfufuka.
Upendo, tunaopaswa kujifunza kutoka kwa Kristo Mwenyewe, kwa kumwangalia kwa huruma mwingine, ndio ishara ya Imani na matumaini yetu ya kweli. Upendo unafurahi pale ninapoona mwingine anakua. Na ndio maana upendo wa kweli, unaniacha nateseka kila mara ninapoona mwingine; yu mpweke, mgonjwa, bila makazi, anadharaulika, akiwa na uhitaji na kadhalika na kadhalika. Upendo ni kufungua mioyo yetu anasema Baba Mtakatifu na kutoka ndani mwetu, katika ubinafsi na umimi wetu na kujifungamanisha na kushirikiana na mwingine. Upendo unaweza kupyaisha ulimwengu wetu wa leo, ambapo Baba Mtakatifu katika “Fratelli Tutti”, yaani “Sisi sote ni ndugu” (tafsiri yangu), anatualika wanadamu wote kukumbuka na kuzingatia kuwa sisi sote ni ndugu bila kujali rangi, imani, taifa, kabila, jinsia, au tofauti yeyote ile. (FT 183). Kila mmoja kwa hiyo anaalikwa kusafiri Kwaresma akiwa na moyo ulio wazi, moyo wa upendo kwa wengine, sio upendo wa maneno bali upendo wa kujisadaka kwa ajili ya wengine anayekuwa katika uhitaji.
Neno la Mungu hasa Injili, katika Dominika ya Kwanza ya Kwaresima katika mizunguko yote mitatu, yaani mwaka A, B na C ya Kiliturjia ni juu ya majaribu ya Yesu Kristo jangwani. Simulizi hilo kadiri ya Mwinjili Marko tulilosikia leo ni fupi sana, kwani ni aya mbili tu (1: 12-13) na hivyo kupelekea wahubiri wengi kupata ugumu kuelezea sehemu hii ya Maandiko Matakatifu na mwishowe wanajikuta wanaanza kuelezea kadiri za Wainjili Mathayo na Luka. Ni vema kubaki waaminifu kujaribu kuingia na kutafakari kadiri ya Mwinjili Marko na humo kuchota utajiri mkubwa uliojificha katika aya hizi chache mintarafu majaribu ya Yesu Kristo huko jangwani. Mwinjili Marko anatueleza kuwa Yesu Kristo aliongozwa jangwani na Roho wa Mungu ili ajaribiwe. Yafaa kuwa makini kuwa Mwenyezi Mungu kamwe hatuweki majaribuni na ndio maana tunasali atuokoe kutoka majaribuni.
Katika Maandiko Matakatifu pia tunakutana na nyakati ambapo Mwenyezi Mungu anaruhusu watu wema na sio waovu kuingia katika majaribu. Yoshua Bin Sira 2:5. Kuna majaribu katika maisha ya mwanadamu ambayo anapitia ni na shabaha yake si kumwingiza mwanadamu kutenda dhambi au kuenenda kinyume na Muumba wake, bali kumsaidia mwanadamu kukomaa na kuimarika katika imani yake kwa Mungu. Na ndio maana tunasoma kutoka Waraka kwa Waebrania kuwa hata Yesu Kristo alijaribiwa kama sisi isipokuwa hakuwa na dhambi. (Waebrania 4:15) Mwinjili Marko anaonesha kuwa Yesu Kristo alijaribiwa jangwani. Hivyo yafaa kutafakari kwa nini jangwani? Yesu Kristo kama alivyokuwa Yohane Mbatizaji na manabii waliotangulia kabla yake walijitenga na kukaa jangwani, sehemu ya upweke ili kutafakari na kusali. Ni katika jangwa, sehemu ya upweke mmoja anapata nafasi ya kuongea na Muumba wake, ni kutoka katika ulimwengu wa kawaida na kuingia katika ulimwengu wa mahusiano ya karibu zaidi na Mungu. Hivyo ilikuwa ni kawaida kabisa kwa wale wenye utume maalumu kwenda jangwani ili kuongea na Mungu na kusikiliza sauti ya Mungu.
“The holiness of silence” (Utakatifu wa ukimya), katika nyakati zetu hizi ni kidu adimu sana, na hata nyakati za kujitenga na kubaki wenyewe mara nyingi tunazikosa maana tumezungukwa na kila aina ya makelele, iwe yake ya sauti au hata ya kimitandao na kisaikolojia. Kipindi cha kwaresma ni mwaliko wa kusaka nafasi na wasaa wa kusali, yaani kuongea na kumsikiliza Mwenyezi Mungu. Si tu kuongea, narudia bali pia tuwe na ukimya wa ndani ili kumsikiliza Mwenyezi Mungu. Sala ni mazungumzo ya pande mbili, ni mdahalo kama anavyotukumbusha Baba Mtakatifu katika ujumbe wake wa Kwaresima. Hebu tufikirie pale mmoja anapokwenda kwa rafiki yake na tangu anafika mpaka mwisho anazungumza yeye tu, bila kumpa rafiki naye nafasi ya kuzungumza. Sala ni mazungumzo ya kirafiki, hivyo hatuna budi pia kumpa Mwenyezi Mungu nafasi ya kuzungumza nasi. Na ndio kuwa jangwani kwenye manufaa. Na ndio kupyaisha kwetu imani kunatokana na kusoma, yaani kusikiliza Neno la Mungu.
Mwinjili Marko anatueleza kuwa Yesu Kristo alibaki jangwani akijaribiwa kwa muda wa siku arobaini. Muda huu wa siku arobaini maana yake nini katika Biblia? Yeye alikuwa sawa na sisi isipokuwa na dhambi. Je, Yesu Kristo alijaribiwa kwa siku arobaini tu? Kama alikuwa sawa na sisi, ndio kusema maisha yake yote hapa duniani alipitia katika majaribu kama ilivyo kwangu na kwako. Hata wale walio watakatifu wakubwa kabisa, maisha yao ya siku kwa siku bado yanabaki na majaribu na vishawishi vya kila aina, ila kwa neema za Mungu wanavishinda. Yesu Kristo kama mtu kweli basi naye katika maisha yake ya hapa duniani alijaribiwa kila siku, na sio kwa siku arobaini tu. Arobaini ni namba yenye kuonesha kuwa siku zote mpaka akiwa pale msalabani alibaki katika majaribu ya kuenenda kinyume na mapenzi ya Baba yake aliyemtuma. Kwaresma kama safari ya siku arobaini inaakisi ukweli ya kuwa maisha yetu yote tunabaki katika jangwa la majaribu na vishawishi vya kila aina.
Wapendwa Kwaresima ni kipindi kimetengwa na Mama Kanisa kwa siku arobaini ila ni mwaliko wa wongovu kwa maisha yetu ya siku zote hapa duniani. Hivyo siku arobaini ni lugha ya kiishara kumaanisha kuwa Yesu Kristo naye alijaribiwa siku zote za maisha yake. Na hata pale kabla ya mateso yake alisali ili kikombe kile cha mateso aepukane nacho na kuwaalika wanafunzi wake kukesha na kusali pamoja naye. Na hata pale juu msalabani alisali maana alihisi kubaki peke yake bila msaada wa Mungu Baba. Ni mwaliko pia kukumbuka kuwa majaribu katika maisha yetu hatuwezi kuyashinda kwa nguvu zetu za kibinadamu bila neema na msaada wa Kimungu. Neno shetani linatokana na neno la Kiebrania ‘’satan’’ ambalo sio jina la mtu fulani ila ni jina jumlishi likimaanisha, anayekwenda kinyume, na ndio adui au mzushi au msingiziaji, anayenena uongo, asiye na kweli ndani mwake. Nyakati za Yesu lilimaaisha pia pepo wabaya, adui wa mwanadamu na anayeharibu mipango ya Mungu. Katika Injili ya leo linatumika kumaanisha mambo yote maovu yanayokwenda kinyume na mpango wa Mungu, ambayo Yesu Kristo alipambana nayo kwa siku arobaini, yaani muda wote wa maisha yake hapa duniani.
Shetani ni nani leo? Ni chuki, kinyongo na kisasi, ubinafsi, tamaa ya mali, tamaa ya madaraka na kutawala kwa nguvu na hila mifano hapa tunayo mingi tu hasa tukiangalia katika chaguzi zetu za kisiasa katika taifa letu zinazozaa siasa za chuki na uhasama na uadui, tamaa mbali mbali za mwili, na mengine mengi tunayoweza kufikiria katika maisha yetu. Haya ndio baadhi ya mambo ambayo mimi na wewe tunaalikwa kumwomba Mungu ili kwa neema na msaada wake tukiongozwa na Roho wa Mungu anayefanya kazi katika Neno la Mungu na masakramenti ili tuweze kuepukana nayo, Kwaresma ni kipindi cha mapambano ya kiroho kuelekea kuwa watu wapya katika Kristo. (Waefeso 4:13) Mwinjili Marko pia anatuelezea uwepo wa wanyama wa porini na malaika. Kuhusu wanyama wakali wa porini baadhi ya wataalamu wa Maandiko wanarejea kuwa Mwinjili Marko alikuwa anajaribu kuelezea ile hali ya paradiso iliyokuwepo mwanzoni mwa ulimwengu kabla ya dhambi kuingia ulimwenguni, mwanadamu wa kwanza kabla ya dhambi aliishi kwa amani na wanyama wote. (Mwanzo 2:19-20) Yesu Kristo amekuja kuleta ulimwengu mpya, ulimwengu ule wa amani na urafiki kabla ya dhambi kuingia.
Mwinjili Marko, pia zaidi ya kuelezea kuwa Yesu Kristo ameleta amani ulimwenguni, wanyama wa mwituni anajaribu kutumia lugha ya picha kuelezea nguvu onevu na kandamizi za ulimwengu huu. (Danieli 7). Kutoka Kitabu cha Nabii Daniele lugha ya picha ya wanyama wa mwituni inatumika pia kuonesha juu ya watawala kandamizi, simba akionesha utawala wa damu wa Babiloni. Badala ya kuwatumikia watu na kutenda haki, watawala hawa wamekuwa chanzo cha uonevu na kukosa haki hasa kwa wanyonge. Wanyama wa porini ambao alikuwa nao Yesu katika jangwa la majaribu ndio pia watawala wa ulimwengu wa leo, ndio watawala wa kisiasa, wa kiuchumi, na hata wa kidini (Masadukayo, Sanhedrini, makuhani wakuu), viongozi wa kiroho(waandishi) waliokuwa wanasali sala ndefu na usiku waliingia katika nyumba za wajane (Marko 12:40), wale waliokuwa wanamhubiri Mungu mwenye haki ila anawachukia wadhambi (mafarisayo).
Yesu Kristo alipambana kila mara na watawala wa namna hii ili kumweka mwanadamu huru na kuwafundisha sura ya kweli ya Mungu Baba, kuwa ni Baba wa wote bila upendeleo na Mungu mwenye huruma na rehema. Hata Malaika pia yafaa kuelewa kuwa Marko hapa hamaanishi malaika kama viumbe wa kiroho tu. Neno Malaika kama linavyotumika na Mwinjili Marko, halimaanishi tu viumbe wale wa kiroho bali kila kiumbe anayetumika kama mjumbe wa Mungu katika kutimiza mapenzi na mipango ya Mungu hapa duniani. Musa aliwaongoza Wanawaisraeli kule jangwani aliitwa pia Malaika (Kutoka 23:20,23), Yohane Mbatizaji pia anatambulishwa na mwinjili Marko kama Malaika (Marko 1:2). Malaika hapa ni wale wote wanaokubali na kutumika katika kutimiza mapenzi ya Mungu hapa duniani. Ni kipindi cha kwaresma tunaalikwa na kukumbushwa wajibu wetu wa kuwa wajumbe au malaika wa Mungu kwa maisha ya sala, sadaka na mfungo. Kila mmoja wetu anatualika Baba Mtakatifu kuwa Kwaresima kiwe ni kipindi cha neema kwa kupyaisha tena imani, matumani hai na mapendo.
Ni Malaika anayejitoa sadaka kupatanisha watu wa ndoa waliofarakana na kugombana na hata kutengana, ndiye anayeonesha wengine kuenenda katika njia ya Bwana, ni njia ya utatu na utakatifu. Yafaa tuwe macho kwani twaweza kuwa shetani, kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu hata kwa ndani mwetu tukiwa na nia njema, maana siku hizi wengi utasikia huyu anafanya kwa nia njema, haitoshi nia njema kutenda wema, hivyo lazima kuenenda katika Njia ya Yesu Kristo mwenyewe. Mfano mzuri ni Simon Petro ambaye anakalipiwa na Yesu Kristo na kuitwa shetani na arudi nyuma kwa kuwa alikuwa kinyume na mpango wa Mungu. Kwa haraka haraka Simon Petro alipenda kuona Bwana na Mwalimu wetu hapitii katika njia ile ya mateso na kifo, ni nia njema kibinadamu ila ni kinyume na mpango wa Mungu. Hivyo haitoshi nia njema peke yake. (Marko 8:33). Tusikubali kuingia katika kishawishi cha siku hizi utasikia acha kiongozi afanye jambo fulani kwa kigezo kuwa anafanya kwa nia njema, ni vyema kuwa makini na vishawishi vya namna hii, maana utasikia hata pale haki za kibanadamu zinapokiukwa bado wengi wetu tunashangilia kisa tu tunataka maendeleo, hakuna maendeleo ya kweli kama utu wa mtu unakanyagwa na kukiukwa, yafaa tukemee na kulaani tabia zinazoibuka katika jamii zetu.
Sehemu ya pili ya Injili ya leo tunaona Yesu Kristo habaki kule jangwani kama alivyofanya Yohane Mbatizaji bali anaenda Galilaya. Haendi kwanza Yerusalemu kwenye mji ule mkuu iwe kidini na hata kisiasa bali anakwenda pembezoni katika mji uliodharaulika, mji wa watu nusu wapagani. Ni katika Galilaya anawaita wanafunzi wake wale wa kwanza waliokuwa wavuvi katika ziwa Galilaya, na huko anawaita hata watoza ushuru na kula na kuambatana nao. Ni ujio wake unaleta matumaini mapya kwa watu wale waliokuwa watengwa kwa kigezo cha kuwa watu waliodharaulika na wadhambi. Ufalme wa Mungu umefika. Sio ufalme wa kimabavu wa kisiasa au kiuchumi na hivyo kukosa kueleweka na baadhi ya wasikilizaji wake bali ni ufalme wa upendo, haki na amani. Ni ufalme wa urafiki na Mungu. Kuamini katika Injili, Injili sio kwa maana ya kitabu bali Habari njema ya Mungu kukaa katikati yetu. Ni Mungu anayefanyika mwanadamu kwa kuwa anatupenda upeo.
Kipindi cha Kwaresima ni καιρος (kairos), wakati muafaka wa kutopoteza muda, ni wakati muafaka wa kuanza maisha mapya, maisha ya urafiki na ukaribu na Mungu. Ni kipindi cha kujiweka karibu na Mungu ili kwa msaada wake wa daima tuweze kumshinda yule mwovu, yaani shetani na kuenenda daima katika njia ya Yesu Kristo. Nawatakia tafakari njema ya upendo wa Mungu katika kairos hii ya Kwaresima. Dominika njema.
In cordes Mariae,