Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima: Maana ya Jangwa katika maisha ya Mkristo! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima: Maana ya Jangwa katika maisha ya Mkristo! 

Tafakari Jumapili 1 Kwaresima: Jangwa Katika Maisha ya Kikristo!

Kwa kuzingatia historia ya Waisraeli waliosafiri jangwani kwa miaka 40 kuelekea nchi ya ahadi, jangwa lilikuwa ni mahala pa kujaribiwa uamifu, kutakaswa na kuonja wema, upendo na huruma ya Mungu. Wakiwa jangwani Mungu aliwaonyesha upendo wake mkuu kwa kuwalinda, kuwaongoza na kuwapatia chakula. Yesu anaenda jangwani mara tu baada ya Ubatizo na huko anajaribiwa!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Tupo katika kipindi cha Kwaresima tulichokianza Jumatano ya Majivu na leo tunayapatia ufafanuzi na tafakari masomo ya dominika ya kwanza ya Kwaresima. Ufafanuzi wa Masomo ya Misa kwa ufupi: Somo la Kwanza (Mwa 9:8-15). Somo la kwanza linaelezea Agano ambalo Mungu aliliweka na Nuhu baada ya lile gharika kuu. Agano, kwa maneno rahisi ni mkataba au makubaliano yanayofunga pande mbili zinazouweka. Katika Biblia tunaona mara nyingi Mungu anawega Agano na watu wake. Ameweka na Abraham, Isaka na Yakobo, ameweka na taifa zima la Israeli mlimani Sinai na hatimaye kwa njia ya Kristo ameweka Agano Jipya na la milele. Mara zote hizo ambazo Mungu amejishusha akaweka Agano na watu, anaweka si kwa faida yake bali anaweka kwa faida ya watu. Agano analoliweka na Nuhu ni kuwa hataangamiza tena ulimwengu kwa gharika kama alivyofanya wakati wa Nuhu.

Wakati huo wa Nuhu, Mungu aliiangamiza dunia kwa sababu ya dhambi. Dhambi hiyo inaelezwa awali katika sura ya 6 kuwa waana wa wanadamu walijitwalia wake kutoka katika waana wa Mungu. Maana yake ni kuwa mwanadamu hakuridhika kubaki katika nafasi yake ya kuwa mwanadamu. Akavuka mipaka na kujichukulia umungu. Mungu akakasirika akaamua kuiangamiza dunia kwa gharika. Hata hivyo kwa njia ya Nuhu akawaokoa wachache katika safina. Katika Agano ambalo analiweka sasa, Mungu anatandaza upinde wa mvua. Hii ni ishara ya amani. Mungu mwenyewe anatangaza amani na mwanadamu. Kama wanajeshi walio vitani wanapoamua kuweka silaha chini na kuacha mapigano, Mungu naye anautandaza upinde wake ambao hauwi tena upinde wa vita bali upinde wa amani. Kwaresima tuliyoianza, inaakisi kipindi hicho cha amani kati ya Mungu na mwanadamu, amani ambayo Mungu mwenyewe anamtangazia mwanadamu; anatutangazia sote.

Somo la Pili (1Pet 3:18-22): Kwaresima ni kipindi cha kutafakari mateso na kifo cha Kristo. Somo la pili, kutoka waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa watu wote, linatoa muhtasari huo wa mateso na kifo cha Kristo ambavyo tangu mwanzo ndio vimebeba kiini cha mafundisho yote ya Kikristo. Tunaweza kubainisha mambo matatu kutoka katika somo hili. La kwanza ni kuwa Kristo aliteswa kwa ajili ya wenye dhambi, la pili – kisha kufa, Kristo alishuka kuzimu kuzihubiria wokovu roho zilizokaa kifungoni na tatu, safina ya Nuhu iliyookoa watu na gharika ni mfano wa ubatizo. Tuchukue tu hilo la kwanza, kwamba Kristo aliteseka kwa ajili ya wadhambi. Kuteseka kwa ajili ya wadhambi, kiasi fulani ni tungo tata. Inaweza kumaanisha kuteseka kwa niaba ya wadhambi, lakini pia kunaweza kumaanisha kuteseka kwa manufaa ya wadhambi.

Mafundisho ya Kanisa yamesisitiza zaidi tafsiri ya pili, kuwa mateso ya Kristo ni kwa manufaa ya wadhambi. Na manufaa hayo ni wokovu. Ni hapa ulipo pia msingi wa kuelewa fumbo la mateso ya mwanadamu kwa jicho la imani ya Kikristo. Mateso ambayo ni lazima katika njia ya maisha ya mwanadamu yanapopokelewa katika imani hii hayaangaliwi tu katika upande wake unaoumiza bali katika kile yanachoweza kumfaidia mwanadamu. Ni kwa jinsi hii na katika imani hii, katika kipindi hiki cha Kwaresima tunaamua kwa hiyari kujitesa sio tu kuyaenzi mateso ya Kristo bali pia kwa ajili ya wokovu wetu wenyewe na wokovu wa wengine.

Injili (Mk 1:12-15): Somo la Injili ya dominika hii inaturudisha mwanzoni mwa Injili ya Marko. Ni baada ya Yesu kubatizwa na Roho kutua kama njiwa juu yake. Roho huyo huyo aliyetua juu ya Yesu, katika somo la leo, anamtoa Yesu na kumpeleka jangwani. Huko anakaa siku 40 akijaribiwa na Shetani. Hizi ni alama zenye maana kubwa sana katika utume wa Yesu. Jangwa, katika Biblia, ni mahala ambapo mtu anajitambua “ni nani” mbele ya watu na mbele ya Mungu. Kwa kuzingatia historia ya Waisraeli waliosafiri jangwani kwa miaka 40 kuelekea nchi ya ahadi, jangwa lilikuwa ni mahala pa kujaribiwa uamifu, mahala pa kutakaswa na mahala pia pa kuonja wema, upendo na huruma ya Mungu. Wakiwa jangwani Mungu aliwaonesha upendo wake mkuu kwa kuwalinda, kuwaongoza na kuwapatia chakula.

Yesu anaenda jangwani mara tu baada ya ubatizo na mara tu baada ya kutangazwa na Mungu mwenyewe kuwa ndiye mwanae mpendwa. Kwenda kwake jangwani kunakuwa ni kuipitia tena historia hiyo ya babu zake waisraeli; kupitia majaribu kama wao na kudhihirisha kuwa Yeye ni kweli mwana wa Mungu kwa kuyashinda majaribu hayo. Ni kwa sababu hiyo anakaa siku 40, namba ambayo inaakisi maana ile ile ya jangwa. Kama Musa alikaa siku 40 mlimani Sinai akipokea amri 10 (Kutoka 34:28), Kama Eliya alifunga siku 40 kabla ya kwenda mlima Horebu kumdhihirisha Mungu wa kweli (1Wafalme 19:8) na kama Waisraeli walivyokaa jangwani miaka 40. Mwinjili Marko anaendelea kutuonesha kuwa ni baada ya siku hizo 40 jangwani Yesu akaanza kuhubiri. Na mahubiri yake ya kwanza yakawa ni kualika toba: “wakati umetimia na ufalme wa Mungu umekaribia, tubuni na kuiamini Injili”. Ni vizuri kuona kuwa Injili hii inatuonesha yale ambayo sisi nasi tunayapitia katika kipindi cha Kwaresima. Tunaishika Kwaresima kwa siku 40 ambazo zinakuwa ni kipindi ambacho kiroho tunakwenda jangwani kwa lengo lile lile la kufanya toba na kuiamini Injili kama ulivyo ujumbe wa Kristo.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tumeanza kipindi cha Kwaresima. Masomo ya dominika hii ya kwanza ya Kwaresima, tayari yametupatia dondoo zinazotuingiza katika roho ya kipindi hiki cha neema. Ni kipindi cha sala, ni kipindi cha mfungo, ni kipindi cha toba na mageuzi ya kiroho na ni kipindi cha kuzidisha matendo ya huruma kwa wenzetu. Katika kipindi kama hiki cha Kwaresima, Baba Mtakatifu hutoa ujumbe wake kwa lengo la kuwasaidia waamini kuuishi kikamilifu mwaliko wa Kwaresima. Kwa mwaka huu ujumbe wake huo, pamoja na mambo mengine, unatualika tuipokee Kwaresima kama kipindi cha kuhuisha imani, matumaini na mapendo.

Imani, Matumaini na Mapendo ni fadhila za kimungu. Ni Mungu anayemjalia mwanadamu ili kumuwezesha kutenda kama mtoto wake na kustahili uzima wa milele (Rej. KKK n. 1812-1813). Upo hata hivyo, uwezekano wa mwanadamu kuzififisha fadhila hizi zisionekane katika maisha yake au yeye mwenyewe asizione katika maisha yake. Kumbe mwaliko anaotupatia Baba Mtakatifu ni wa maana sana. Anatualika tuihuishe imani ili tuweze kuupokea ukweli na kuushuhudia mbele ya Mungu na mbele ya wenzetu. Anatualika tuyahuishe matumaini ili tuweze kupata nguvu ya kusonga mbele katika maisha. Katika nyakati hizi ngumu tulizomo, nyakati ambazo inaweza kuwa vigumu kuongea kuhusu matumaini, Kwaresima inatualika kurudi kwa Mungu na kuona katika msamaha wake nguvu mpya ya kusonga mbele. Mwisho, Baba Mtakatifu anatualika tuhuishe mapendo yetu kwa kuonesha kujali na kuguswa kwa huruma na wengine kama alivofanya Kristo. Na hivi basi Kwaresima ya mwaka huu iwe ni Kwaresima ya kukuza: imani, matumaini na mapendo.

Liturujia Kwaresima
19 February 2021, 08:25