Tafakari Jumapili 2 Kwaresima: Imani, Matumaini na Mapendo!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya pili ya Kwaresima mwaka B wa Kilitrujia, siku ya kumi na mbili ya majiundo ya kiroho. Baada ya kosa la wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva la kukaidi maagizo na amri za Mungu (Mw. 3:1-5:32), walipoteza neema ya utakaso, sura ya Mungu ndani mwao (Mw 1:26-27). Walichokipoteza Adamu na Eva, tulipokipoteza nasi kwani ubinadamu wetu ulikuwa tayari kwao. Hata hivyo Mungu kwa upendo wake hakuwaacha wapotee, akamtoa na kumleta mwanaye wa pekee ndiye Mkombozi wetu yesu Kristo aliyeteseka, akafa, akazikwa siku ya tatu akafufuka ili arudishe tena uhusiano wetu na Mungu. Katika Dominika hii ya pili ya kipindi cha Kwaresima, Mungu anamdhihirisha kwetu mlimani Tabor katika wingu akisema; “Huyu ni mwanangu mteule wangu, msikieni yeye”. Ujumbe mkuu wa domenika hii ni kuisikiliza na kuitii sauti ya Mungu. Ndiyo maana katika sala ya mwanzo (Koleta) Padre kwa niaba ya taifa la Mungu anasali akisema; Ee Mungu, umetuamuru tumsikie Mwanao wa pekee. Upende kutulisha neno lako ndani yetu. Nasi tukiisha takata, tufurahi kuuona utukufu wako. Kama ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2021 usemavyo: Ingekuwa heri leo msikie sauti yake msifanye migumu mioyo yenu!
Katika somo la kwanza la kitabu cha Mwanzo Mungu anamjaribu Ibrahimu kwa kumtaka amtoe mwanae wa pekee Isaka aliyemuahidi kuwa taifa kubwa kama sadaka ya kuteketezwa. Ibrahimu akiwa na imani kubwa kwa Mungu, alisikiliza na kuitii sauti, amri na maagizo ya Mungu akaenda kumtoa mwanae sadaka ya kuteketezwa mbele za Mungu. Mungu kwa kuona Imani ya Ibrahimu anampatia kondoo dume iwe mbadala wa sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanae Isaka. Kisha Mungu akamwambia Ibrahimu; katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibariki; kwa sababu umetii sauti yangu. Kitendo cha Mungu kumpatia Ibrahimu kondoo dume kwa ajili ya kutoa sadaka ya kuteketezwa anatuonesha kuwa sadaka za kumwaga damu ya binadamu hazipokei tena. Kwani yeye ni Mungu wa uhai. Katika simulizi hili tunajifunza ukuu wa Imani kwa Mungu ulivyo na nguvu ya ajabu kwa sababu umesimikwa ndani kabisa mwa mtima wa moyo wa mwanadamu. Ibrahimu anatii na kujaribu kumtoa mwanae wa pekee kafara ili kwamba Imani yake kwa Mungu isipotee. Huu ni utabiri wa upendo wa Mungu kwa wanadamu kwani Mungu alimtoa mwanaye mpenzi awe fidia ya dhambi zetu.
Somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi linatukumbusha kuwa Kristo aliyetolewa sadaka na Baba ili atukomboe ndiye anayetuombea, na ndiye atakayetuhukumu siku ya mwisho. Mtume Paulo anatuambia kuwa Mungu akiwa upande wetu hakuna atakayeshindana nasi akatushinda. Kwa njia ya sakramenti ya Ubatizo sisi tumewekwa kuwa upande wa Mungu. Kwa ubatizo Mungu alipendezwa nasi kwa sababu tulikiri kumkataa shetani na fahari zake zote. Injili kama ilivyoandikwa na Marko inasimulia tukio la Yesu kugeuka sura, siku sita baada ya ungamo la Petro kuwa Yesu ni mwana wa Mungu (Mk 8:29) na ni majuma machache tu kabla ya mateso na kifo chake msalabani. Katika simulizi hili la kugeuka sura kwa Yesu kuna mambo ya kuzingatia. Kwanza; Yesu aliwatwaa Petro, na Yakobo na Yohane, wanafunzi wake watatu kati ya 12. Pili, aliwapeleka juu ya mlima mrefu faraghani peke yao, tatu walitokea Eliya pamoja na Musa, wakazungumza na Yesu na walipomaliza wakatoweka. Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu ikisema; Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu, msikieni yeye. Mwisho walipokuwa wakishuka mlimani Yesu aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, kwa sharti mpaka pale atakapofufuka katika wafu.
Kwanini mbele ya wanafunzi watatu? Wanafunzi hawa ndio walioshuhudia kufufuliwa kwa binti Yairo (Mk 5:37), na ndio watakao shuhudia mateso ya Yesu kule Gethsemane (Mk 14:33). Kabla ya tukio la kugeuka sura, Yesu alitoa utabiri juu ya Mateso yatakayompata. Wanafunzi hawakuelewa na walikwazika kiasi kwamba Mtume Petro akasema: Hasha Bwana hayo hayatakupata (Mt. 16:22), naye Yesu akamkemea na kumwambia rudi nyuma yangu shetani wewe, maana unawaza ya kibinadamu n asio ya Mungu. Lengo la Yesu kuwachukua hawa wanafunzi watatu ni kuimarisha ndani yao imani, matumaini, na mapendo kwa kuwaonesha utukufu wake ili wakati wa majaribu ya Bwana wao wasitetereke nao waweze kuwaimarisha na mitume wenzao. Petro akiwa kiongozi mkuu wa kwanza wa Kanisa alipaswa kuwa na imani dhabiti na imara. Ndiyo maana baadaye alikuja kusema; Hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu wa watu tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake bali tulikuwa tumeona wenyewe ukuu wake (2Pt. 1:16ff). Yakobo ni Mtume wa kwanza kuteswa na kufa shahidi kwa ajili ya Kristo, alipaswa kuwa na matumaini makubwa kwa Kristo Bwana wake. Na Yohane aliyeandikiwa kumpokea Bikira Maria, Mama wa Kanisa na mama yetu sote alipaswa kuwa na mapendo makubwa na safi kabisa.
Kumbe, kugeuka sura mbele yao ni kuwafundisha kuwa utukufu unapatikana katika kuvumilia mateso. Ndivyo maana katika utanguliza wa domenika hii Padre anasali akisema; Yeye aliwaambia mapema wafuasi wake kwamba atauawa; na pale katika mlima mtakatifu aliwaonyesha utukufu wake, akaonyesha kwamba kama ilivyoandikwa katika Torati na Manabii, atapata utukufu wa ufufuko kwa kuteswa. Na katika sala ya kuombea dhabihu Padre anasali; Ee Bwana, tunakuomba sadaka hii ifute dhambi zetu na kuwatakasa waamini wako mwili na roho, wapate kuadhimisha sikukuu ya Paska. Na katika sala baada ya komunyo anahitimisha akisali; Ee Bwana, baada ya kupokea mafumbo yako matakatifu, tunataka kukushukuru kwa maana ingawa tuko bado hapa duniani watushirikisha ya mbinguni. Idadi yao watatu ni uthibitisho kuwa walichokiona ni ukweli mtupu na ushuhuda wao ni wa kweli wakizingatia ushahidi wa watu watatu kama kitabu cha kumbukumbu la torati kilivyodai kuwa; Lazima shauri lithibitishwe kwa ushuhuda wa mashahidi wawili au watatu (Kumb. 19:15).
Ndiyo maana Musa na Eliya wakiwakilisha Agano la Kale lililotabiri ujio wa Yesu Kristo; Musa akiwakilisha Torati ama sheria, na Eliya akiwakilsha manabii wakiungana pamoja na Kristo nao wakakidhi idadi paswa ya ushahidi huo wa kutimia kwa Agano la kale katika yeye kwani Agano la Kale ni ufunuo wa Agano jipya alilofanya Mungu nasi kwa njia ya Yesu Kristo nalo Agano hili jipya na milele ni utimilifu wa Agano la kale. Bila ya Agano la kale Yesu Kristo ni fumbo tusiloweza kulitambua. Ndiyo maana ili kuwafanya wanafunzi wa Emausi waelewe maana ya kifo na ufufuko wake aliwafungua akili na mioyo yao akiwafafanulia maandiko akianzia na Musa na manabii wote akawaeleza katika maandiko mambo yote yaliyo mhusu yeye mwenyewe (Lk 24:27). Kwanini wingu kutanda mlima wote na kisha sauti ikatoka? Katika Agano la Kale wingu lilimaanisha uwepo wa Mungu. Kumbe, sauti kutoka katika wingu ni udhibitisho kuwa ni sauti ya Mungu Baba ikimtambulisha Yesu kuwa ni mwana wake mpendwa. Hivi yeyote anayetaka kumpendeza ni lazima afuate nyayo zake (Yesu). Baada ya maneno hayo kumalizika, Yesu alibaki peke yake. Musa na Eliya walitoweka kuthibitisha kuwa wakati wa kuwasiliana na Mungu kwa njia yao umekwisha. Na sasa tunapaswa kuwasiliana na Mungu kwa njia ya mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo.
Ni dominika ya kugeuka sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Nasi tunapaswa kugeuka kiroho kutoka katika hali mbaya ya dhambi, kufanya toba ya kweli, na kuanza maisha ya utakatifu, kuacha matendo maovu na sio kwenda likizo ya dhambi, sio kuahirisha kutenda dhambi ni kubadili kabisa mwenendo, kuwa watu wapya, kuanza maisha mapya ya kumsikiliza mwana wa Mungu na kuishi kadiri ya amri za Mungu. Katika kipindi hiki kila mmoja katika hali yake ajiulize amebadilika katika lipi, tangu kwaresma ianze kama bado tukio la Kristo kugeuka sura lituimarishe tufanye juhudi za makusudi kabisa kumgeukia Mungu kwa kuacha kabisa yale yote yanayotutenga na upendo wake. Tumwombe Mwenyezi Mungu atujalie imani thabiti na moyo wa usikivu kwa maongozi ya Mwanae Bwana wetu Yesu Kristo ili siku ya Pasaka tufufuke pamoja naye.