Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 5 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Dhana ya mateso na mahangaiko katika maisha ya mwanadamu! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 5 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Dhana ya mateso na mahangaiko katika maisha ya mwanadamu! 

Tafakari Jumapili 5 Mwaka B: Fumbo la Mateso Katika Maisha!

Maradhi mbali mbali yanayo msumbua mwanadamu iwe wema kwa wabaya, labda pengine mwanadamu anaweza kushawishika kuwa ni laana nikiri kwa kweli kufikiri namna hiyo ni sawa na kukufuru. Mungu ni upendo ulio kamili na wala hana sababu ya kumlaani mwanadamu. Mungu ametuumba kwa kuwa anatupenda. Mungu anatuangalia kwa wema na huruma yake ya Kimungu.

Na Padre Gaston Mkude, - Roma

Amani na Salama! Fumbo la mateso katika maisha ya mwanadamu linabaki kuwa ni swali linaloumiza na hasa tunapojaribu kujiuliza kwa nini Mungu aliye Baba yetu mwema na mwenye upendo bado anaruhusu mateso katika maisha ya mwanadamu, na hasa kwa wale wanaojitanabaisha kuwa ni marafiki zake Mungu. Kuna mateso au uovu unasababishwa na mwanadamu, ukatili na ubinafsi wa mwanadamu dhidi ya mwanadamu mwingine, lakini juu ya yote swali linabaki hasa pale tunajiuliza je kwa nini Mungu anaruhusu mateso katika maisha yetu mathalani magonjwa na hata majanga mbali mbali? Leo dunia nzima inalia na kutabika na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, (COVID-19), tunamlilia Mungu na hata kumuuliza kwa nini ameruhusu na hili litutese na kutuweka katika mazingira hatarishi, leo duniani kote mwanadamu anataabika na kuishi kwa hofu kubwa dhidi ya janga hilo, na pia tunasali na kumlilia kwa kuwa tuna hakika na wema na upendo wake kwetu. Maradhi, majanga mbali mbali na hata kifo, bado vinabaki kutupatia maswali magumu yasiyokuwa na majibu wala majawabu rahisi.

Maradhi mbali mbali yanayomkuta na kumsumbua mwanadamu iwe wema kwa wabaya, labda pengine mwanadamu anaweza kushawishika kuwa ni laana au adhabu kutoka kwa Mungu, nikiri kwa kweli kufikiri namna hiyo ni sawa na kukufuru. Mungu ni upendo ulio kamili na wala hakuna hata nafasi moja ya kufikiri Mungu anayeadhibu na kulaani mwanadamu, Mungu ametuumba kwa kuwa anatupenda na hata tunapokuwa mbali naye kwa uovu na ukaidi wetu bado Mungu anatuangalia kwa wema na huruma yake ya Kimungu. Katika somo la Injili ya leo, tunaona Yesu anafika nyumbani kwa Simoni Petro na kumkuta mama mkwe wa Simoni akiwa kitandani hawezi homa. Yesu leo hatoi katekesi kwa nini maradhi au mateso katika maisha ya mwanadamu. Yesu hatuambii kwa nini mateso katika maisha yetu, kwa maradhi mfano huu wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, (COVID-19). Yesu anasikia mahangahiko yake kuwa alikuwa kitandani hawezi homa, na hapo anamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono na hapo homa ikamwacha.

Kumbe, Yesu anaguswa na mahangahiko ya kila mmoja wetu. Itoshe kumshirikisha tukiongozwa na imani thabiti na ya kweli. Mitume kama anavyotuonesha leo Mwinjili Marko walitambua kuwa hawakuwa na la kufanya, lakini moja walikuwa na hakika nalo ni lile la kumshirikisha Yesu kwa imani, wakitambua wema na upendo na huruma yake ya Kimungu kwa kila mmoja wetu. Na ndio mwaliko ambao nasi tunaalikwa kuwa nao kila mara tunapopitia magumu na nyakati za mateso na mahangahiko, ni kumkimbilia na kumwambia hali zetu na hasa uduni na unyonge wetu. Ndio hatua muhimu na ya lazima ili tuweze tena kurejea katika hali inayokuwa njema na bora zaidi. Mateso yetu si tu ya kimwili bali hata ya kiroho, mara nyingi tunasongwa si tu na maradhi ya kimwili bali na hata yale ya kiroho. Kila mara hatuna budi kutambua ni kwa kumkimbilia Yesu na kumshirikisha kwa imani.

Ni hapo Yesu anamkaribia, anamwinua kwa kumshika mkono. Ndio daima hakika ya kila mmoja anayemkimbilia na kumshirikisha hali zetu. Daima Yesu anamkaribia kila mmoja wetu anayekimbilia wema na huruma yake. Ni Yesu anakuja kwetu hasa kwa njia ya Neno lake na katika masakramenti yake. Anakuja ili atuguse iwe ni maradhi yetu ya kimwili na hata yale ya kiroho. Yesu hatukimbii, hasimami mbali na kutuangalia kwa mshangao bali anamkaribia kila mmoja anayekimbilia upendo na huruma yake ya Kimungu. Akamwinua kwa kumshika mkono, ndio kusema nguvu yake ya Kimungu ikapata kumponya yule aliyekuwa hawezi homa. Kumshika mkono na kumwinua ni kumtoa katika hali duni na kumrejeshea tena uhai, ni sawa na kumfufua aliyekuwa hana tena uhai. Na ndio hali zetu za ndani kila mara tunapokuwa mbali na Mungu, tunakuwa sawa na wafu, tunahitaji tena nguvu ya Mungu mwenyewe kututoa katika uduni na udogo wetu.

Ni Yesu anayekuja kila mara katika maisha yetu kwa msaada wa masakramenti yake ili sisi tuweze kujaliwa tena uzima ndani mwetu. Ni baada ya kupokea uponyaji wa kweli, tunaona mama huyu anasimama na kuanza kuwatumikia. Ndio kusema kila mmoja anayekuwa na uzima wa Kimungu ndani mwake anatambua wajibu wake, na hasa wajibu wa kila mbatizwa ndio ule wa kutumikia na sio kutumikiwa, ni mwaliko wa kutambua kuwa tu wagonjwa kila mara tunaposhindwa kuwatumikia wengine kwa upendo na sadaka. Kutumikia ndio ishara ya kuwa katika mahusiano mema na Mungu na jirani, ndio mwaliko kwa kila mmoja wetu kuwatumikia wengine, kuwa wadogo katika maisha yetu, kuwatanguliza wengine kabla ya sisi wenyewe, ni kuepuka ubinafsi na umimi katika maisha ya kumfuasa Kristo. Kila Dominika tunakusanyika na kuadhimisha Sadaka ile ya Kristo pale msalabani, ndio kusema ni fursa ya kutafakari ulazima na umuhimu wa sadaka na mateso kwa wokovu wetu. Ni nafasi ya kujihoji na kuangalia maisha yetu kama bado tupo chini ya msalaba wake Kristo Msulubiwa. Ni pale msalabani tunaonja upendo na huruma ya Mungu, ni katika mateso yake sisi tunakombolewa, ni katika kifo chake sisi tunapokea uzima wa Kimungu, ndio wokovu wetu.

Sehemu ya pili ya Somo la Injili, tunasikia si tu alimponya mama mkwe wa Simoni bali hata na wengine waliokuwa hawawezi na wenye pepo. Yesu anaponya kila aina ya magonjwa, na hata kuwatoa pepo wachafu wanaomuingia na kuharibu maisha yetu. Ilikuwa ni siku ya Sabato na ndio maana tunaona wayahudi hawakufika mapema kuwaleta wagonjwa bali saa ile jua lilipokwisha kuchwa. Wanatambua uwezo wa Kimungu wa Yesu wa kuponya, wa kurejesha tena hali inayokuwa njema na bora zaidi.  Mwinjili Marko anatuonesha kuwa Yesu hakuwaruhusu pepo kunena, hakuwaruhusu kuendelea kuharibu maisha ya wale watu, na ndio hata nasi tunamkimbilia ili daima maisha yetu yaongozwe na Neno lake, yaani Injili yake. Pamoja na kuwaponya lakini Yesu anatuonesha kuwa utume wake ni zaidi ya kuponya maradhi na magonjwa na pepo, utume wake ni kuhubiri Injili, Habari Njema ya Wokovu, Habari ya Furaha na Matumaini kwa kila mmoja anayekutana nayo. Ujio wake ni ili kuujenga ufalme wa Mungu katika maisha yetu wanadamu wote. Ni kubadili namna zetu za kutenda na hata kufikiri, ni kuanza kuipokea na kuongozwa na mantiki mpya, ya kuwa watumishi kwa wengine, ya kuwapa nafasi ya kwanza wengine kabla yetu, ya kuepuka ubinafsi katika maisha yetu.

Kipindi hiki kigumu chenye changamoto nyingi katika historia ya maisha ya mwanadamu, hatuna budi kutambua hata mara moja Mungu hawezi kutuacha kwa kila mmoja anayemlilia na kumkimbilia kwa imani. Ni Mungu anayetuangalia kwa huruma na upendo usiokuwa na kipimo. Ni Mungu anayetaka kusafiri nasi katika maisha yetu ya hapa duniani na hatimaye tuweze kuunganika naye baada ya maisha ya hapa ulimwenguni. Sehemu ya mwisho ya Injili ya leo, tunakutana na Yesu akiwa katika sala. Hata kati ya Wayahudi kulikuwa na aina kuu mbili za sala, yaani zile za jumuiya nzima na zile za mtu mmoja mmoja, sala binafsi. Tumesikia siku ya Sabato, Yesu aliungana na wengine katika Sinagogi, na siku iliyofuata kungali alfajiri anatoka na kujitenga ili asali na kuomba mahali pasipokuwa na watu. Yesu anatuonesha umuhimu na ulazima kwa kila mmoja wetu kutenga wasaa wa kubaki na Mungu katika sala, kusali ni kitendo cha kimahusiano zaidi kati ya wawili wanaopendana, ni kuunganika na Mungu kwa kuingia naye katika mazungumzo ya kirafiki kabisa. Ni kukaa miguuni mwake, ni kujikabidhi wazima wazima na kuingia katika ulimwengu wa mahusiano ya ndani kabisa na Muumba wetu. Ni katika sala humo tunachota nguvu na hata maana ya mateso na mahangahiko katika maisha yetu.

Sala sio kukimbia uhalisia wa mateso, bali ni kisima cha kuchota nguvu ya kubeba msalaba, Yesu kabla ya saa ile ya kuikusanya roho yake alisali pale bustanini Getsemani, ndio kusema ni kwa njia ya sala pekee hapo tunapata nguvu ya kiroho kuweka kubeba msalaba katika maisha yetu. Hivyo hata miujiza inafanyika sio ili kututoa katika mateso lakini haswa ni kama kidole cha kutuonesha ulimwengu mpya, mahusiano mapya na Mungu wetu. Watu wote wanakutafuta. Hii ilikuwa ni kauli ya mitume wake Yesu, lakini wanamtafuta kwa malengo yasiyokuwa sahihi. Ni hapo Yesu anawageukia na kuanza kuwaonyesha kuwa misheni ya kwanza sio hiyo ya kutenda miujiza bali ya kuhubiri Habari Njema, ya kuujenga ufalme wa Mungu hapa duniani, ya kumfanya mwanadamu hata kama anapitia magumu na shida mbali mbali, daima hana budi kuishi na kuongozwa na Neno la Mungu.

Watu wale walimtafuta sio kwa sababu walimtambua kuwa ni Bwana na Masiha wao bali kwao waliishia kumuona kama mtenda miujiza, hivyo Yesu anatualika leo kutambua mahusiano yetu na Mungu hayana budi kuongozwa sio na mantiki ya ulimwengu huu bali ile ya mbinguni. Twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako. Watu wale walitaka kumtumia Yesu, walitaka kumbinafsisha Yesu, na hii ndio mantiki ya kidunia, kutumia wengine, kuwabinafsisha kwa ajili ya masilahi yangu na yako. Yesu Kristo ni Bwana wa wote, ni Habari Njema kwa dunia nzima, amekuja sio kwa ajili ya watu fulani tu bali kwa ajili ya dunia nzima. Kamwe tusiingie katika kishawishi cha kumtafuta ili baki nasi tu, anatualika nasi tutoke katika mantiki na sababu zisizokuwa sahihi ili tuweze kuongozwa na mantiki ile ya Injili. Nawatakia tafakuri na Dominika njema.

05 February 2021, 15:19