Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 5 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Maana ya magonjwa na mateso katika maisha ya Kristo! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 5 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Maana ya magonjwa na mateso katika maisha ya Kristo! 

Tafakari Jumapili 5 Mwaka B: Mateso Katika Maisha ya Kikristo!

Yesu Kristo ni faraja na tumaini letu kwani ameutwaa udhaifu wetu na kuyachukua magonjwa yetu; anatuponya kiroho kwa kutusamehe dhambi zetu ili tuwe na uzima wa kimwili. Hivyo tukiyapokea magonjwa na mateso kwa imani; nguvu, hekima na upendo wa Mungu vinadhihirika ndani mwetu. kwa kuwa tukiwa katika udhaifu tunaongeza juhudi za kusali na kuombea wengine

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 5 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya domenika hii yanatupa nafasi ya kutafakari juu ya uwepo wa Mateso na magonjwa katika maisha ya mwanadamu. Japo mateso na magonjwa ni matunda ya dhambi; lakini si kila mgonjwa ni mdhambi. Ndiyo maana Mitume walipomwuliza Yesu, ni nani aliyetenda dhambi hata mtu huyu akawa kipofu (Yn 9:1ff), Yesu akajibu: “Jambo hili halikutukia kwa sababu ya dhambi zake yeye wala za wazazi wake. Alizaliwa kipofu ili nguvu za Mungu ionekane ikifanya kazi ndani yake. Yesu Kristo ni faraja na tumaini letu kwani ameutwaa udhaifu wetu na kuyachukua magonjwa yetu; anatuponya kiroho kwa kutusamehe dhambi zetu ili tuwe na uzima wa kimwili, kwani roho ndiyo itiayo uzima. Hivyo tukiyapokea magonjwa na mateso kwa imani; nguvu, hekima na upendo wa Mungu vinadhihirika ndani mwetu kwani ni kwayo tunakuwa karibu na Mungu kwa kuwa tukiwa katika udhaifu tunaongeza juhudi za kusali na kuomba wengine watuombee na tunakuwa karibu na ndugu zetu kwani mmoja akiugua, tunakusanyika kumhudumia na kumfariji, na hivyo tunakuwa karibu zaidi na Kristo.

Katika somo la kwanza la Kitabu cha Ayubu; Ayubu mtu mwema, mchamungu na mwaminifu, tajiri wa mifugo, aliheshimiwa na wengi kwa wingi wa neema na baraka za Mungu, kwa ujasiri mkuu anayakubali na kuyapokea mateso na mahangaiko yake kama sehemu ya maisha akisema; nami nimepewa miezi ya ubatili iwe fungu langu. Hii ni baada ya kupoteza mali zake zote, kufiwa na watoto wake, na yeye kupata ugonjwa mbaya wa ngozi ulioambatana na madonda na maumivu makali. Katika hali hii machoni pa watu alionekana kuwa ametenda dhambi na kumwasi Mungu hata na mke wake na rafiki zake watatu Elifazi Mtemani, Bildadi Mshuhi na Sofari Mnaamathi. Ayubu alijitetea kuwa hajafanya uovu ambao ungemstahilisha hiyo adhabu na ya kwamba yeye anamwamini Mungu aliye mkuu na wa ajabu hivi kiasi kwamba hatuwezi kuelewa njia na mipango yake. Akiwa katika mateso makali hayo, Ayubu alikiri kwamba anampenda Mungu na Mungu anampenda. Hivyo aliendelea kusimama katika uaminifu na uadilifu wake mpaka mwisho bila kutishwa na yale yote yaliyompata wala maneno ya rafiki zake, akashinda na Mungu akambariki maradufu.

Kitabu hiki cha Ayubu kinatufundisha kumtumainia Mungu wakati wote na katika hali zote. Majaribu, mateso na mambo mabaya yanayompata mcha Mungu si lazima yawe matokeo ya dhambi au mabaya aliyotenda. Wakati mwingine Shetani huushambulia uadilifu wa mtu ili amkufuru Mungu, ila kwa kuwa Mungu yu pamoja na wale wamchao, huwaokoa na mabaya yote. Shetani alimshtaki Ayubu kwamba hamchi Mungu bure bali ni kwa sababu Yeye Mungu alikuwa amemzunguka pande zote. Naye Mungu alimpa shetani ruhusa amjaribu Ayubu ili kumthibitishia uelekevu na uadilifu wake. Kwa hiyo kazi ya majaribu yale ambayo Mungu anayaruhusu ni: Kututhibitisha katika imani, kuonyesha uweza na uaminifu wa Mungu, kudhihirisha kushindwa kwa Shetani kwa baraka zinazoandamana na ushindi baada ya majaribu. Mateso yanatufanya tutambue uwepo na umuhimu wa kuwa karibu na Mungu kwani tunaposhindwa kuyatatua ndipo tunapokata rufaa kwake yeye mwenye uwezo wa yote.

Mateso yetu na ya wengine yanatukumbusha kuishi maisha ya fadhila mbalimbali za kikristo kama vile kuwa na huruma kwa wanaoteseka, ukarimu na majitoleo kwa wahitaji, ujasiri katika shida, mashaka na taabu, nguvu palipo na udhaifu, upendo palipo na chuki, faraja palipo na huzuni. Mateso yetu na ya wengine yanatupa nguvu ya kutenda mema zaidi na kumtegemea Mungu zaidi. Katika somo la pili la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho tunapata wasifu wa dini ya kweli na wa mhubiri wa kweli yeye mwenyewe Paulo akiwa mfano hai na wa kweli akieleza ni kwanini alikubali kuwa mhubiri. Yeye ni mhubiri si kwa sababu ya uhiari wake bali ni sehemu ya wito wake kwa Mungu. Ni wajibu anaopaswa kuutekeleza. Hawezi kujivuna wala kuhubiri anachotaka. Tena anatambua kuwa kama asipohubiri atapata taabu ndiyo maana anasema; Ole wangu nisipoihubiri Injili. Kipimo cha Paulo kwa maendeleo ya kuhubiri kwake ni kuangalia idadi ya wanaoupokea na kuuishi ujumbe ule uletao wokovu. Mtindo wake wa kuhubiri ni kuwa yote kwa ajili ya wote; Kwa wayahudi anakuwa myahudi na kwa watu wa mataifa anakuwa kama wao ili nao wapte kumjua Kristo.

Mtume Paulo anatukumbusha nasi wajibu wetu wa kuihubiri Injili kwa watu wa mazingira yote. Hili ni jukumu la kila mkristo kwani kwa ubatizo, sote tumeshirikishwa ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo, hivyo tuna wajibu wa kuitangaza injili, kwa maneno na matendo yetu. Mtume Paulo anatuasa tusijisifu wala kujivuna kwa lolote bali tumpe Mungu sifa. Na yote tunayofanya yatoke moyoni si kwa kulazimishwa na hapo ndipo tutapa neema. Sala zetu, mahangaiko yetu, mateso yetu na mema yote tunayoyafanya yana matokeo yake katika fumbo la mwili wa Kristo na daima hutoa matunda mema kwa njia ambazo hatuwezi kuzielewa. Hili ndilo fumbo lililomfanya Mtume Paulo asema ghafla; “sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiza katika mwili wangu yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake yaani kanisa.

Katika Injili ilivyoandikwa na Marko tunakutana na Yesu akihubiri juu ya Ufalme wa Mungu huku akiponya wagonjwa na kuwatakasa wote waliomjia. Sala kwake ni muhimu ili kuongea na Mungu Baba, ampate uwezo wa kung’amua mapenzi yake na kuyatekeleza. Yesu kuwaponya wagonjwa ni kielelezo cha huruma yake kwa wagonjwa. Anatekeleza kile walichoagua manabii juu yake kwamba: “Yeye mwenyewe ameondoa udhaifu wetu, anayachukua magonjwa yetu (Isa 53:4, Mt 8:17), ndiyo maana Mtakatifu Yohane Paulo II akiwa Jimbo kuu la Mwanza Tanzania katika Kanisa Kuu la Epifania 03/09/1990 akiwapa faraja wagonjwa alisema; “Yesu bado yu karibu sana na wagonjwa! Yuko karibu na kila mmoja katika mateso. Yuko karibu nawe wakati ukiwa mpweke na unapoogopa na unapohisi kuwa hakuna yeyote anayeuelewa uchungu wako. Yuko karibu zaidi na wale wanaokufa na wenye magonjwa yasiyotibika. Yesu yuko pamoja nanyi kwa kuwa yeye aliye Mungu alipata mateso. Kwenye Bustani ya Gethsemane alihuzunika na kusononeka wakati akiikabili sadaka kuu (Mt. 25:38-39). Mikono na ubavu wake bado vina alama za mateso na kifo chake.

Hivyo msiogope kumruhusu Yesu kuyatumia magonjwa yenu kama neema maalum, ya kuwasogeza zaidi kwake. Kupitia udhaifu wenu, atawasaidia kukua katika hekima, busara na ufahamu wa kiroho. Zaidi ya yote kuweni na imani kwamba kwa muungano wenu na Kristo, mateso yenu yatazaa matunda mema ya kiroho kwa faida ya Kanisa na ulimwengu.” Maneno haya ya Mtakatifu Papa Yohane Paulo II yanatukumbusha kuwa kwa ubatizo tuliunganishwa na Yesu katika Fumbo la kifo chake na kufufuka kwake kwa ajili ya maisha mapya (Rum. 6:5), na tuliletwa ulimwenguni kwa ushuhuda na ushindi wake dhidi ya dhambi na kifo. Hivyo Yesu anatutaka tuimarishe muungano wetu katika imani na kuzidi kufanana naye (Rum 8:29), katika magonjwa yetu anatutaka kuonyesha katika miili yetu nguvu ya ushindi wa neema yake. Kristo ameutwaa udhaifu wetu na kuyachukua magonjwa yetu. Hivyo, tumtegemee katika shida zetu maana yeye ni kimbilio letu. Tunaalikwa pia kuendeleza kazi hiyo ya kuutwaa udhaifu wa watu, kuwasaidia wanaoteseka.

Familia ya Kikristo lazima ioneshe upendo kwa ndugu zetu wagonjwa. Kristo alijihusisha na wagonjwa kama ishara ya uwepo wa Masiha na mwazo wa ufalme wa Mungu uliojengwa katika misingi ya furaha, amani na upendo. Kujihusisha kwetu na wagonjwa na kuwashughulikia kidugu ni ishara ya imani yetu kwa Kristo kwa ulimwengu usiomwamini Kristo bado. Tunaalikwa kuwajali wagonjwa pasipo kuwabagua juu ya nafasi yao au hali yao katika jamii. Tuwasaidie kwa hali na mali. Tukiwatembelea, kuwafariji, kuwapa mahitaji muhimu ya kimwili na ya kiroho kama kusali nao, kuwasaidia waweze kupokea sakramenti ya Kitubio, Ekaristi Takatifu na Mpako wa Wagonjwa na kuwaandaa kupokea mapenzi ya Mungu katika hali iliyo njema. Tuombe basi neema na baraka za Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu ili tuyapokee mateso na mahangaiko yetu na ya wengine pasipo kunung’unika ili yaweze kutukomaza kiimani na kutuweka karibu zaidi na Mungu na hivyo tuweze kustahilishwa kuingia katika ufalme wake mbinguni.

Jumapili ya 5
05 February 2021, 15:43