Tafakari Jumapili 6 Mwaka B: Utu, Mshikamano na Upendo wa Kweli!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayapatia ufafanuzi na tafakari masomo ya dominika ya 6 ya mwaka B wa Kanisa. Ufafanuzi wa Masomo ya Misa kwa ufupi. Somo la Kwanza (Wal 13:1-2, 45-46): Katika somo la kwanza, tunakutana na mojawapo ya miongozo ya Torati ya Musa kuhusu ugonjwa wa ukoma. Miongozo hii inaangukia katika ile miongozo mipana zaidi ya Torati iliyohusu unajisi na usafi. Kwa kifupi kabisa, unajisi ni uchafu. Huu haukuwa uchafu wa aina nyingine yoyote bali ulikuwa ni uchafu wa kiibada, yaani ile hali inayomfanya mtu, mnyama au kitu kupoteza sifa ya kumkaribia Mwenyezi Mungu katika moyo wa ibada. Aliyekuwa najisi au kitu kilichokuwa najisi kilipaswa kutakaswa kwanza ndipo kistahili kumjongea Mwenyezi Mungu katika ibada.
Tunachokiona katika somo hili la kwanza, ambalo linatoka katika kitabu cha Mambo ya Walawi, ni mwongozo kuhusu mtu aliyekuwa na ukoma. Kwanza, mgonjwa mwenyewe alipoona hizo dalili zinazoelezwa alipaswa kwenda kujisalimisha kwa Kuhani. Kuhani yeye alipaswa kubainisha kama dalili hizo ni ukoma au la. Alibainisha si kama daktari bali kama mhudumu wa matakatifu. Na ni yeye aliyepaswa kutamka kama mhusika atapaswa kuendelea kujiunga na wenzake katika ibada au la. Na endapo sasa kuhani alithibitisha uwepo wa ukoma, mgonjwa alitengwa na jamii. Alipaswa kuvaa nguo zilizoraruriwa, hakupaswa kufunika kichwa chake na hakupaswa kuwasogelea watu.
Ni nini basi ilikuwa ni mantiki ya kuwa na taratibu kali namna hii? Kwanza kabisa, ukoma ulihusishwa na dhambi. Aliyepata ukoma alionekana ni mtu aliyeadhibiwa na Mungu kwa sababu ya dhambi zake. Ndiyo maana hakuruhusiwa kushiriki tena ibada hadi hapo atakapopona. Kupona kwake ukoma kulimaanisha kutakaswa pia kwa ndani. Na hap dhambi zake zilionekana zimeondolewa. Sababu ya kumtenga asikutane na watu ilikuwa ni kuilinda jumuiya. Kuilinda jumuiya isiambukizwe na hivi na yenyewe kupoteza sifa ya kushiriki katika ibada. Sasa jumuiya au taifa zima la Israeli lilikuwa ni taifa ambalo uwepo na ustawi wake ulitegemea mahusiano yao na Mungu. Kushindwa kushiriki ibada kwa jumuiya au taifa zima kwa sababu ya unajisi kulimaanisha kuangamia kabisa kwa taifa zima.
Somo la Pili (1Kor 10:31-11:1): Somo la pili linaanza na maneno ya Mtume Paulo akisema “Basi mlapo au mnywapo au mtendapo jambo lolote, fanyeni yote kwa sifa na utukufu wa Mungu”. Hapo awali, Mtume Paulo amewaandikia wakorinto kuhusu tatizo walilokuwa nalo kuhusu vyakula. Wakristo wa Korinto walikuwa ni wa makabila tofauti. Walikuwapo wayahudi na walikuwapo pia wayunani. Wayahudi wao wakifuata tamaduni zao walizozirithi toka katika Torati ya Musa, kuna vyakula walikuwa hawali kwa sababu waliviona ni najisi. Wayunani wao hawakuwa na mila hizo, wao walikula kila kitu. Hili lilileta tatizo kati yao. Wote ni wakristo: hawa wanakula hiki na hawa wanasema hicho ni najisi. Hawa wanakwazika kuwaona wengine wanakula chakula najisi na wao wanakwazika kwa nini wasile!
Msimamo wa Mtume Paulo kuhusu suala hilo ulikuwa wazi. Katika aya ya 25 anasema “kuleni kila kitu kiuzwacho sokoni…. Maana dunia ni mali ya Bwana na vyote viijazavyo (Rej. 1Kor 10:25-26). Lakini pamoja na hayo, Mtume Paulo huyo huyo katika somo la leo anatoa angalisho. Na angalisho analolitoa ni kuwa katika kujenga jumuiya, wasifanye mambo kwa kukwazana. Wasifanye mambo bila kuangalia kama wanakwaza dhamiri za wenzao au la. Kwa maneno mengine Mtume Paulo anawakumbusha kujenga fadhila ya kuchukuliana katika jumuiya. Wasiache kujenga umoja wa jumuiya kwa kuendekeza utofauti wa dhamiri kuhusu nini kinafaa kuliwa na nini hakifai. Wafanye yote kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Anayeamua kufuata dhamiri yake na kutokula aina fulani ya chakula aendelee; si kwa ajili ya kumhukumu au kumkwaza mwingine bali afanye hivyo kwa ajili ya kumpa Mungu sifa na utukufu. Hali kadhalika anayeamua kufuata dhamiri na kula vyote bila utofauti afanye hivyo si kwa lengo la kumkwaza mwingine bali kwa ajili ya kumpa Mungu sifa na utukufu.
Injili (Mk 1:40-45): Kutoka katika somo la kwanza ambalo limetupatia iliyokuwa miongozo ya Torati ya Musa kuhusu ugonjwa wa ukoma, Injili ya leo inamwonesha Yesu akimponya mgonjwa wa ukoma. Hapa picha inakuwa ni tofauti kabisa. Mwenye ukoma hakuruhusiwa kumkaribia mtu yeyote, hapa anamkaribia Yesu, anampigia magoti na anaomba kuponywa. Kwa upande wa Yesu hali pia ni tofauti na ilivyoagiza Torati ya Musa. Mtu mzima hakuruhusiwa nayeye kumkaribia mwenye ukoma, Yesu lakini anamsogelea na hata anamgusa! Anamwambia “nataka, takasika” naye muda ule ule akatakasika kutoka ukoma aliokuwa nao. Akamtuma aende kujionesha kwa makuhani ili aruhusiwe tena kuungana na jumuiya, aishi maisha ya kawaida. Hiki alichokifanya Yesu ni muujiza wa uponyaji. Muujiza huu lakini ulikuwa na lengo lingine kubwa zaidi lililokuwa limejificha. Na lengo hilo lilikuwa ni kumrudisha mgonjwa wa ukoma katika jumuiya iliyokuwa imemtenga. Mgonjwa huyu wa ukoma anawakilisha kilio na kiu ya wagonjwa wengine wa ukoma kuunganishwa na jumuiya na familia zao. Kwa bahati mbaya hakukuwa na hata mmoja wa kuwaonea huruma isipokuwa Yesu. Mgonjwa huyu inawezekana alishasikia habari za Yesu ndio maana akapata ujasiri wa kumkaribia.
Hapa linabaki swali. Je, Torati ya Musa iliyoamuru wagonjwa wa ukoma watendewe hivyo ilikuwa na makosa? Torati haikuwa na makosa. Lengo la mwongozo wa Torati lilikuwa ni kulinda utakatifu wa ibada na kuilinda jumuiya nzima, si katika masuala ya usafi wa kiafya bali katika usafi wa kiibada. Hiyo yote ilikuwa ni kuhakikisha kwamba watu wanamtolea Mwenyezi Mungu ibada wakiwa wametakasika. Kristo sasa, amekuja kutuonesha kuwa utakaso unaohitajika mbele ya Mungu sio ule wa nje bali ni ule utakaso wa ndani. Zaidi ya hapo hata pale utakaso wa ndani unapokosekana kwa sababu ya dhambi na makosa ya kibinadamu, anatuonesha kuwa wakosefu waangaliwe kwa macho ya huruma na kwa huruma hiyo wasaidiwe kuufikia utakaso wanaoukosa na wanaouhitaji. Mwinjili Marko katika Injili hii ya leo ameonesha pia msisitizo wa huruma. Ametuonesha kuwa kitu cha kwanza alichokifanya Yesu baada tu ya kusikia ombi la mwenye ukoma ni huruma, “naye akamhurumia”. Ni dhahiri kabisa kuwa unapomwangalia mtu kwa jicho la huruma ni rahisi zaidi kuyaelewa mahangaiko yake na kumuongoza kupata misaada anayohitaji kulingana na hali yake.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika hii ya 6 ya mwaka B wa Kanisa yanazungumza nasi kuhusu uundaji wa jumuiya. Yanatualika kuunda Jumuiya zinazounganisha sio kugawa, zinazokusanya sio kutawanya na zinazotanguliza huruma wala si hukumu. Huu ni mwaliko wa kuunda jamii ambayo ustawi wa mtu na manufaa ya mtu vinapewa kipaumbele katika harakati zote za maisha ya kijamii. Kama tulivyoona katika ufafanuzi wa masomo, mwongozo wa Torati ya Musa ulipokewa katika msisitizo wa kuilinda jumuiya dhidi ya unajisi. Msisitizo huo ulipewa uzito mkubwa kiasi kwamba jumuiya haikujishugulisha hata kidogo kumsaidia mwenye ukoma. Na mbaya zaidi kilio chake hakikuweza kusikika kwa sababu tayari mfumo wa maisha uliokuwepo haukumpa nafasi wala sauti.
Jumuiya na mfumo wake wa maisha ulijiona salama kwa kuwatenga wakoma ikasahau kuwa ili jumuiya iwe jumuiya, ni lazima uwepo muunganiko wa mtu mmoja mmoja. Na kwa vyovyote vile kumweka pembeni mtu mmoja mmoja hakuwezi kuijenga jumuiya. Hiki ndicho Yesu anachokuja kukirekebisha katika Injili. Mwaliko huu wa masomo ya leo unatutaka sasa na sisi tuziangalie jumuiya zetu: familia, Kanisa na jamii kwa ujumla. Mifumo ya maisha pamoja na harakati mbalimbali za ustawi na maendeleo visimwache yeyote kando. Baba Mtakatifu Francisko katika mafundisho yake kuhusu jamii ametuasa mara kadha wa kadha kuwa kiini cha ustawi na maendeleo ya kweli ya jamii ni mtu. Ustawi na maendeleo yanayojengwa juu ya mifumo na kumwacha mtu pembeni ni ya nadharia na yakinzana na hadhi na heshima ya utu wenyewe. Mungu na atujalie neema na atuangazie kujenga jamii inayounganisha, inayokusanya na kujali hasa wale walio dhaifu na wahitaji kati yetu.