Tafakari Jumapili 6 Mwaka B: Yesu Ni Ufunuo wa Huruma na Upendo
Na Padre Gaston Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Ni najisi, ni najisi! Hicho ndio kilikuwa kilio cha kila mwenye ukoma katika taifa lile la Wanawaisraeli kama tulivyosikia katika somo letu la kwanza kutoka Kitabu kile cha Makuhani, ndicho Kitabu cha Walawi. Mwenye ukoma alipaswa kuvaa mavazi yalioraruliwa, kichwa wazi na kufunika mdomo wake wa juu na kupiga kelele akijiita na kujitambulisha kuwa yu najisi. Mwenye ukoma si tu alitengwa iwe na familia na jamaa zake, jamii nzima na hasa jamii ya dini ya Kiyahudi, hakupaswa hata kutembea karibu na ukuta wa mji mtakatifu wa Yerusalemu. Mwenye ukoma alihesabika kuwa sawa na maiti inayotembea, na hivyo kuponywa ukoma kulifananishwa sawa na kufufuka kutoka wafu. Mwenye ukoma hakupaswa kukaa jirani wala karibu na wengine, alipaswa kuishi mapangoni na mbali na watu wengine. Unajisi wake ulihesabika ni kutokana na dhambi kubwa aliyoifanya, hivyo ukoma ulihesabika kuwa ni balaa na laana kubwa. Ni laana iliyotokana na madhambi aidha ya muhusika au ya kurithi. Kwa Wayahudi katika Agano la Kale, maradhi au magonjwa zaidi ya huo wa ukoma yalihesabika kuwa ni adhabu na laana kutoka kwa Mungu. Rejea Ayubu 18:13.
Mkoma alihesabika kuwa ni mdhambi mkubwa na alistahili kutengwa na jumuiya ya kijamii, kidini na hata yeye mwenyewe kukataliwa na ajihesabu na kujitambua kuwa ni najisi. Kutokana na hali hiyo basi Kitabu cha Walawi kimetenga sura mbili zinazotueleza nini kifanyike na makuhani pale mmoja anapoonekana kuwa ni mwenye ukoma. Walawi 13-14. Na Yesu katika Injili ya leo anaonekana kufahamu vema na vizuri kabisa sheria zile kutoka Kitabu cha Walawi. Na ndio baada ya kumponya kwa kumtakasa anamwalika aende akajioneshe kwa makuhani, ilikuwa ni makuhani wenye wajibu wa kumtangaza mmoja kuwa ni najisi na vile vile kumrejesha tena katika jumuiya baada ya kupona au kutakasika kwake. Yesu Kristo pamoja na kujua sheria na taratibu zile, tunaona leo anatualika si tu watu wa nyakati zake bali hata zetu kubadili vichwa na mitazamo yetu mintarafu ndugu, kaka na dada zetu wanaokuwa katika hali duni, hali ya kutengwa na kusetwa na jamii, iwe kifamilia, kikanisa na hata kijamii.
Yesu anatulika leo kuwa na mtazamo na hulka yake ya kuwahurumia wengine na hasa wanaokuwa katika hali duni zaidi yetu. Kuwaangalia wengine sio kwa jicho la kuwahukumu na kuwatenga bali kuwakaribia na kuwaonjesha upendo na huruma ya Kimungu. Leo dunia nzima inapotembea katika kipindi kigumu cha janga hili la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, wengi wetu tunafahamu masharti magumu ya kuwatenga wale wote wanaopatwa na kirusi cha korona, na hata kati yetu tunaalikwa na wataalamu kutokukubali kukaa sehemu zenye misongamano, kutokusalimiana kwa kugusana mikono, kutokukaa karibu na mwingine hata mtu wa nyumba moja, wa Kanisa au jumuiya moja, kifupi kila mmoja kuwa mbali na mwingine, ndio kusema kumwona mwingine ni hatari kwa maisha na uhai wako. Pamoja na kusema jilinde na pia mlinde mwingine, lakini tafsiri yake rahisi kuwa kila mmoja ni hatari kwa mwingine. Ni mtazamo kama ule uliokuwepo enzi na nyakati za Yesu kwa wale waliokuwa na ugonjwa wa ukoma.
Ukoma unaambukiza hivyo ni vema kuwa macho, kukaa mbali na mwenye ukoma, Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ni sawa na ukoma unaambukiza na hivyo wanatuhimiza kukaa mbali baina yetu na zaidi sana wale ambao tunahisi wana dalili za ugonjwa huo. Ni rahisi kumtenga mwenye ugonjwa, lakini hali inakuwa nguvu pale mgonjwa ninapokuwa ni mimi au wewe, kuonja na kupitia uzoefu huo wa kutengwa, wa kukimbiwa hata na wale unaodhani ni watu wako wa karibu. Sehemu ya kwanza ya Injili ya leo, inaweka wazi jinsi mtu yule mwenye ukoma alivyokuwa anakwenda kinyume na sheria, kwa kumsogelea Yesu na kupiga magoti mbele yake na kutoa kilio chake cha kuomba atakaswe, haombi kuponywa kwa nafasi ya kwanza, kwani anatambua ukoma wake unatokana na yeye kuwa najisi, kuwa mdhambi. Kutakasika ni sawa na kuweza naye kurudi katika jamii yake iwe ile ya maisha ya kawaida, lakini kama myahudi ile ya kuweza kurejea katika maadhimisho yake ya kidini iwe katika Sinagogi au Hekaluni. “Ukitaka, waweza kunitakasa”, ndio sala ya mkoma yule, ya kuomba kupatanishwa na Mungu na jamii yake, ya kurejeshewa tena urafiki na ukaribu na Mungu na wengine, ndio kupokea uhai tena kwani mkoma alihesabika kama maiti inayotembea, ni sawa na mtu mfu.
Tunaona Yesu anaguswa na hali yake na hata Mwinjili anatuambia; “Naye akamuhurumia, akanyoosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika.” Hivyo hata matendo ya Yesu tunayoyasikia, yalikuwa kinyume na sheria, kwani hakupaswa kumsogelea sembuse kumgusa. Yesu si tu anamsogelea na ingetosha hata kumponya bila kumgusa lakini anamsogelea na zaidi sana anamgusa. Kumgusa, ndio kitendo cha Mungu, huruma na upendo wake kwa kila mmoja anayekimbilia msaada na rehema zake. Yesu leo anatuonesha sura halisi ya Mungu, upendo na huruma yake kwetu na hasa tunapokuwa katika hali duni kabisa mintarafu mahusiano yetu tenge naye na hata na wengine. Yesu hatuoneshi kuwa Mungu aliye Mtakatifu kabisa kuwa yu mbali na watu wake na hasa wale wanaomlilia na kumkimbilia wakilia. Mungu anatusogelea na kutugusa ili nasi tuweze kutakasika. Mungu hakai mbali nasi kwa kuwa sisi ni wadhambi. Upendo wake na huruma yake daima unatufuta na kutusogelea. Hakika hata pale tunapodhani ni sisi tulifanya jitihada na bidii za kumtafuta Mungu, hapo tunapaswa kutambua daima ni Yeye anayechukua hatua ya kwanza kunitafuta mimi na wewe. Kila mmoja wetu anapendwa sawa na Mungu, kwa kuwa sisi sote tumeumbwa sio kwa nasibu bali ni matunda na matokeo ya upendo ule ule wa Kimungu.
Yesu tangu mwanzoni mwa utume na misheni yake, anakubali kupokea ubatizo wa maji wa Yohane Mbatizaji, ndio kusema anajiunga na jamii yetu wanadamu, anatusogelea na kujitambua kuwa sawa nasi isipokuwa hakuwa na dhambi, anataka kusafiri na historia ya mwanadamu. Ni Mungu anayekaa na kubaki pamoja nasi daima hata nyakati zile tunapojitenga na kujiweka mbali naye kwa madhambi na maisha yetu yanayokwenda kinyume na Neno na Maagizo yake. Upendo na huruma yake ni wa milele! Yesu daima alibaki kuwa karibu na watu walioonekana na kuhesabika kuwa ni wadhambi, hakujitenga kamwe na wadhambi, lakini si kwamba yeye aliambukizwa hali zao bali alibaki na kutembea nao ili waweze kutembea katika nuru. Mwanga hata kama ni mdogo kiasi gani daima unaonekana katika giza nene na zito. Unapofungua mlango wa chumba chenye mwanga sio kwamba giza lililopo nje linaingia ndani bali ni mwanga ndio utakaoangaza nje.
Katika tafakuri yetu ya leo, labda pia tunajiuliza, kwa nini Yesu aliamua kuchukua hatua kinyume na sheria. Mwanzoni kabisa Mwinjili Luka anatuambia, “Naye akamhurumia”. Mwinjili Marko anataka kutuonesha kuwa udhaifu wa Mungu ni katika upendo na huruma yake. Ni maneno ambayo wainjili wengine Mathayo na Luka hawayaweki katika muujiza ule, lakini Mwinjili Marko anatuonesha wazi wazi kuwa Yesu ni Mwenye Huruma, kwa kila mmoja anayekuwa katika hali duni na ya kutengwa na kukataliwa. Huruma na Upendo ni sifa za Kimungu, kinyume chake tunakosa kuielewa sura halisi ya Mungu. Hata nasi katika maisha yetu tunaalikwa daima kuongozwa kabla ya sheria nyingine yeyote na upendo na huruma. Upendo na huruma ndio sheria mama na ndio zinapaswa daima kuongoza maisha ya kila rafiki na mfuasi wake Yesu Kristo. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Mwaka wa Jubileo ya Huruma ya Mungu alituandikia kitabu chenye kichwa cha habari, “Jina lingine la Mungu ni Mwenyehuruma”, ni nia na lengo la Baba Mtakatifu kutualika kuwa sura halisi ya Mungu inaonekana katika huruma na upendo wake kwetu, tena kwetu tulio duni na wadhambi, ni mwaliko wa kubadili vichwa na mitazamo yetu kumhusu Mungu.
“Akamtakaza kwa nguvu, akamwondoa mara, akamwambia, angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajioneshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao”. Ni maneno yanyotuacha si tu na maswali bali pia mshangao si tu kwa wasikilizaji wa nyakati za Yesu bali hata kwetu leo. Maagizo haya mawili tunaweza kusema yanapingana, kwani anamuagiza asimwambie mtu na hapo hapo anamwamuru akajioneshe kwa kuhani. Ni wazi ili arejee katika jamii yake, iwe ya kifamilia na ile ya kidini na kijamii lazima kuhani athibitishe kuwa amepona, na hapo kwa hakika watu wangelijua tu. Hata hivyo Mwinjili Marko anatuonesha kuwa aliyeponywa hakutii maagizo ya Yesu, hata kama hatusikii kama alienda kwa makuhani bali anatuonesha kuwa alisambaza habari zile njema na za furaha za kutakasika na uponyaji alioupokea. Ni wazi na hakika ni kitendo cha kukosa shukrani kukosa kukiri ni nani amekutendea makuu katika maisha. Ni wazi asingeweza kupokeleka katika jamii yaka bila kwanza kujionesha kwa makuhani, lakini Mwinjili Marko anatoa taarifa za aliyeponywa kuanza kutangaza neno lile.
Katika Agano la Kale tunakutana na matukio mawili tu ya watu waliopokea uponyaji wa ukoma wao. Miriamu dada yake na Musa, Hesabu 12:4-6 na Naamani, 2Wafalme 5. Leo Yesu hamponyi huyu mwenye ukoma kwa njia zile za Miriamu na Naamani bali kwa nguvu ya Neno lake, kwa nguvu za Kimungu. “Nataka, takasika!”. Mwinjili Marko katika Injili yake mara kadhaa atarudia makatazo ya Yesu kwa watu mbali mbali kutoka na kuanza kumtangaza kuwa ni Masiha, kuwa ni Mungu (Siri ya Kimasiha). Ndio kusema njia sahihi ya kumtambua Yesu kuwa ni Kristo, kuwa ni Masiya na Bwana na Mkombozi wetu sio katika miujiza au matendo makuu anayoyafanya bali katika upendo na huruma wake pale msalabani, ni hasa katika saa ya Yesu tunaalikwa kumtambua kuwa kweli ni Mungu na Bwana wetu, ni saa ile ya upendo na huruma yake upeo kwetu wanadamu wote, ndio saa ambapo sote kila mmoja wetu tunapokea huruma na ukombozi wetu. Ndio kusema sio miujiza inayoimarisha imani zetu, bali ni imani inayokubali matendo makuu ya Mungu kwetu, hivyo ni imani inapaswa kuwa msingi wa safari yetu na si miujiza.
Hata hivyo Yesu anataka kuwa safari ya kumtambua kuwa Yeye ni Masiha wa Bwana ianze na makuhani wale, waanze wao kubadili vichwa na mitazamo yao iliyokuwa inakinzana na sura halisi ya Mungu. Pamoja na ukweli kuwa Injili iliandikwa baada ya kifo na ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo, Mwinjili Marko anatuonesha ugumu wa makuhani na wakuu wa dini ya Kiyahudi katika kumwamini Yesu kuwa ni Kristo, na ndio tunaona aliyeng’amua na kujawa na shauku ya kumtangaza Yesu kuwa ni Masiha hawakuwa makuhani wala wakuu wa dini, ambao ni wao walimkamata na kumshitaki na kumtesa na hatimaye kumuua pale msalabani. Ni huyu aliyekuwa mkoma, ni huyu aliyekutana na kuonja huruma na upendo wa Yesu Kristo anatoka na kueneza habari zile njema, habari za furaha. Mwinjili Marko anamalizia kwa kutuonesha kuwa Yesu hakuishia tu katika kumhurumia na kumponya yule mkoma bali akakubali kuishi hali ile aliyekuwa nao awali mkoma. Sasa ni Yesu aliyeishi jangwani na kujitenga, na aliyeponywa akawa mjini akichangamana na wengine.
Baba Mtakatifu Francisko katika kupambana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na hasa mwaka huu wa Mtakatifu Yosefu, anatualika kuwaangalia mara nyingi mashujaa wengi ambao hatuwasikii katika vyombo vyetu vya Habari au Mitandao ya kijamii lakini ni wao kama Mtakatifu Yosefu wamehatarisha na hata kuyatoa maisha yao kwa ajili ya wengine. Yesu anabaki jangwani, anabaki katika wakati mgumu na hatarishi kwa kuwa aliona la kwanza ni kumuonjesha upendo na huruma yake yule mkoma, Mtakatifu Yosefu ambaye hatumsikii hata mara akiongea katika Maandiko, lakini tunaona ni mtu wa vitendo, aliongea kwa matendo yake ya upendo na huruma. Na ndio wahudumu wengi popote duniani hata wengine wamepoteza maisha yao ya wapendwa wao kwa kuwahudumia wagonjwa wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, waliokubali wao kutengwa na familia zao hata kwa miezi kwa kuwahudumia wengine, na bado wanaendelea kuuvaa uduni kwa ajili ya wengine wanaokuwa katika uhitaji.
Wapo matabibu, wapo wauguzi, wapo wahudumu mbali mbali katika nafasi mbali mbali, wapo hata watawa na mapadre wengi wanaokubali kuweka rehani maisha yao ili kuwahudumia wanaokuwa katika uhitaji na hasa nyakati hizi. Ni nafasi nzuri katika Dominika hii kuwaombea hawa wote ambao hatusikii mara nyingi habari zao bali ni mashahidi wa upendo na huruma ya Mungu kwa watu wake, ili kwa maombezi ya Mtakatifu Yosefu wajaliwe nao ujasiri kama wa Baba yetu Mtakatifu Yosefu. Mwinjili Marko anatuonesha kuwa watu wote wakamwendea bado hata alipokuwa amejitenga jangwani, ndio kusema nasi hatuna budi kuwa na nafasi hasa kwa watu wale wanaokuwa katika hali duni na wahitaji, ndio maskini iwe wa kimwili na hata kiroho. Tuzidi kumwomba Mungu atujalie neema nasi kama mtu mmoja mmoja lakini kama Kanisa kuwa tayari kuwapokea wale wanaokuwa wa mwisho, wanatengwa na kusetwa, wanaokataliwa na jamii zetu kutokana na hali zao mbali mbali. Kanisa daima lidumu kuakisi sura ya Mungu anayetupenda na kutuhurumia. Leo kuna wakoma wa aina mbali mbali, ndio wale wote wanaokuwa katika uhitaji mbali mbali, wanaojikuta wametengwa kutokana na hali zao mbali mbali. Nawatakia Dominika na tafakari njema.