Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima: Ubatizo ni kielelezo cha Agano Jipya la Milele kwa kufa na kufufuka na Kristo yesu! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima: Ubatizo ni kielelezo cha Agano Jipya la Milele kwa kufa na kufufuka na Kristo yesu! 

Tafakari Jumapili Ya Kwanza ya Kwaresima: Ubatizo: Agano Jipya!

Kiini cha ujumbe wa masomo ya Dominika hii umejikita katika dhana ya Agano jipya na la milele, utimilifu wa ahadi ya Mungu kwa jamii ya wanadamu ya tangu Agano la Kale. Agano alilofanya Mungu na Nuru baada ya gharika kuu ambalo utimilifu wake ni Agano jipya na la milele alilofanya Mungu na jamii ya mwanadamu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo kwa wafu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya kwanza ya Kwaresima mwaka B wa Kanisa. Ni siku ya 5 ya kipindi cha Kwaresima kinachodumu kwa siku arobaini za majiundo ya kiroho kwa kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kufanya matendo ya huruma ili kujenga muunganiko na Mungu wetu mtakatifu katika kuwatumikia ndugu zetu waliodhaifu na wahitaji. Ni kipindi cha kumwilisha ndani mwetu Amri Kuu ya mapendo. Kilele cha kipindi hiki ni adhimisho la Fumbo la ukombozi wetu yaani Pasaka: mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kipindi hiki tulikianza siku ya Jumatano ya Majivu tulipopakwa majivu katika paji la uso. Kwa tendo hili takatifu la kiroho tulijikubali kuwa sisi ni jumuiya ya wakosaji tunaohitaji kufanya toba ya kweli na kutakaswa kwa huruma na upendo wa Mungu. Kiini cha ujumbe wa masomo ya Dominika hii umejikita katika dhana ya Agano jipya na la milele alilofanya Mungu na jamii ya wanadamu kwa njia ya mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Agano hili jipya ni utimilifu wa ahadi ya Mungu kwa jamii ya wanadamu ya tangu Agano la Kale kama somo la kwanza kutoka kitabu cha mwanzo linavyosimulia Agano alilofanya Mungu na Nuru baada ya gharika kuu ambalo utimilifu wake ni Agano jipya na la milele alilofanya Mungu na jamii ya mwanadamu kwa njia ya Yesu Kristo.

Somo la pili la Waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa Watu Wote linatukumbusha kuwa sisi nasi tunafaidi matunda ya Agano hili jipya na la milele kwa njia ya Sakramenti ya ubatizo. Kama vile maji ya gharika yalivyowaangamiza wadhambi na dhambi zao, ndiyo maji ya ubatizo yanavyomwangamiza shetani na mitego yake na kutufanya washindi dhidi ya dhambi na mauti. Mwinjili Marko katika Injili ya dominika hii naye anaeleza juu ya ushindi wa Yesu dhidi ya majaribu ya shetani alipojaribiwa akiwa jangwani mara baada ya Ubatizo wake. Ushindi huu nasi tunaushiriki kwani kwa ubatizo tumejazwa nguvu ya Roho Mtakatifu ya kupambana na ibili. Ndiyo maana Mtume Paulo anatuambia; “Tulipobatiza tuliungana na kifo chake Kristo, tukazikwa pamoja naye, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka wafu, sisi pia tuweze kuishi maisha mapya” (Rum.6:4). Kabla na mwanzoni, Mungu alifanya maagano mbalimbali kama maandalizi ya hili Agano jipya na milele. Tuyatafakari basi haya maagano ili yatuwezeshe kujitafiti jinsi tunavyoliishi Agano hili Jipya na la milele katika maisha yetu na tupate nguvu ya kulihuisha katika kipindi hiki kitakatifu cha Kwaresima.

Tuanze na Agano lililopo katika somo la kwanza la domenika hii ya kwanza ya kwaresima kutoka kitabu cha mwanzo. Hili ni Agano alilofanya Mungu na Nuhu baada ya gharika kuu (Mwa. 9: 8-15). Mungu aliye Muumba na Mweza wa yote anafanya agano na Nuru akiwakilisha jamii ya Mwanadamu, kiumbe dhaifu. Katika hili agano, Mungu anatoa ahadi ya kutowaangamiza wanadamu tena na viumbe vingine vyote kwa gharika. Lakini Nuhu-mwanadamu, hatoi ahadi yoyote kwasababu hana cha kuahidi kwani yote ni ya Mungu. Sisi wanadamu hatuna chochote chetu isipokuwa tu dhambi zetu. Hapa tunaonja upendo wa Mungu kwa viumbe vyake zaidi sana kwa mwanadamu. Mungu anaamua kujipatanisha na wanadamu. Ni Agano la Upendo lisilokuwa na Masharti. Ni Agano la ukarimu lisilokuwa na mipaka. Ni maandalizi ya wanadamu kumpokea Mwokozi.

Halafu likaja Agano la Mungu na Ibrahimu baba wa Imani (Mw. 15:9-21): Baada ya Agano la Mungu na Nuhu, Mungu alimteua Ibrahimu kuwa Baba wa Taifa kubwa ambalo kwalo Mwokozi atazaliwa na hivyo akafanya naye Agano. Katika Agano hili Mungu anamwahidi Ibrahimu mambo mawili: Uzao na nchi ya ahadi. Historia inasema kuwa wakati wa Ibrahimu, katika kufanya mikabata kati ya pande mbili, mnyama kama ng’ombe au kondoo alichinjwa na kukatwa vipande viwili. Wadau wa mkataba huo walipita katikati ya vipande hivyo viwili, ishara kuwa atakayekosa uaminifu katika mkataba huo atapaswa kukatwa vipande viwili kama mnyama huyu. Lakini katika Agano la Mungu na Ibrahimu ni Mungu peke yake ndiye aliyetembea katikati ya vipande hivyo viwili vya mnyama katika ishara ya moto ambaye Mungu alimwamuru Ibrahimu amchinje. Ibrahimu alipaswa kuwa na Imani isiyoyumba kwa Mungu, ajiachilie kwake. Naye Ibrahimu akawa Baba wa Imani.

Agano baina ya Mungu na watu wa Israeli (Kut. 19:3-24:8): Ahadi ya Mungu ilitimia. Ibrahimu alimzaa Isaka. Isaka akawazaa Esau na Yakobo. Yakobo akazaa watoto 12, ndiyo makabila 12 ya Israeli. Kwa sababu ya njaa, Waisraeli wakaingia utumwani Misri. Musa kwa mkono wa Mungu akawatoa utumwani, wakaaanza safari kuelekea Nchi ya Ahadi, aliyomwahidi Ibrahimu na Uzao wake. Siku kabla ya kuondoka Musa alipaswa kunyunyizia damu ya mwanakondoo katika miimo ya nyumba (Kut.12:1-30). Walipofika Mlima Sinai Mungu akafanya nao Agano. Agano hili siyo kati ya mtu mmoja kama vile lile la Nuhu au lile la Ibrahimu na Mungu, bali na Taifa zima la Israeli. Katika Agano Mungu anaahidi kuwa atakuwa Mungu wao, atawaongoza na kuwalinda kama watakuwa waaminifu katika kuzishika Amri zake 10 alizowapa kupitia Musa. Hata katika Agano hili Mungu pekee ndiye anatoa amri na kuwaahidi nchi yenye maziwa na asali, kwani Israeli hana chochote cha kumpa Mungu, isipokuwa kuwa mwaminifu kwake.

Katika Maagano haya mambo ya msingi yanajitokeza. Kuna mtu anahusika katika kila Agano [Nuhu, Ibrahimu na Musa]. Kuna Ishara ya agano: Upinde kwa Nuhu, moto uliopita katikati ya vipande vya nyama, Damu ya wanyama iliyonyunyizwa kwenye miimo ya milango. Daima Mungu amekuwa mwaminifu kwa maagano yake: Alimpa Ibrahimu mtoto aliyemwahidi ndiye Isaka. Aliwapa ardhi aliyoahidi kwa Ibrahimu na uzao wake nchi ya Palestina, Nchi ya Ahadi. Aliwaongoza na kuwalinda wana wa Iraeli kutoka utumwa wa Misri, kupita Bahari ya Shamu na kuwavusha katika jangwa huku akiwalisha manna, akifanya miujiza mingi kwa manufaa yao.

Lakini tukiacha Nuhu, Ibrahimu na Musa ambao walikuwa waaminifu kwa Mungu kwa maisha yao yote, Taifa la Israeli halikuwa aminifu kwa Mungu kwa nyakati zote. Kila mara walimuasi Mungu naye Mungu aliwaadhibu kwa kuwapeleka utumwani. Ndiyo maana Mungu akaahidi kufanya Agano Jipya na la Milele kwa njia ya mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Agano hili sio agano kati ya Mungu na mtu binafsi au na kundi la watu, bali ni Agano kati ya Mungu na jamii yote ya wanadamu. Agano hili linathibitishwa kwa njia ya Ubatizo. Agano hili ni la milele, ndio kusema kuwa hakuna Agano jingine litakalofanyika tena kwa milele yote. Agano hili limeidhinishwa mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Agano hili linaratibishwa na Yesu Kristo Mwana wa Mungu. Agano Jipya limefanywa kwa Damu siyo ya wanyama bali ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Agano hili Jipya linatufanya kuwa wana wa Mungu na warithi wa uzima wa milele pamoja na Kristo. Mungu amejishusha na kujifanya mwanadmu ili aturudishie hadhi yetu ya kimungu. Agano hili lilitangazwa na Manabii, likaratibishwa na kuadhimishwa na Kristo, jioni kabla ya kifo chake katika Karamu ya Mwisho.

Katika Karamu hiyo alichukua Mkate akaugeuza kuwa Mwili wake na Divai kuwa Damu yake, iliyomwagika kwa ajili ya wengi, kwa maondoleo ya dhambi na wokovu wa wote watakaompokea na kumwamini. Lilitiwa Mhuri kwa Damu yake alipokufa Msalabani. Tunaposhiriki Ekaristi Takatifu, tunaadhimisha Agano na Kristo kwani Ekaristi ni ukumbusho la Agano hili Jipya. Sadaka ya Upendo na Msamaha. Maisha mapya katika Roho Mtakatifu. Tiketi ya kwenda Nchi ya Ahadi –Yerusalemu Mpya yaani Mbinguni. Kwa Ubatizo sisi ni wadau wa Agano hili Jipya, ni wabia kwani tumeshiriki katika kile kiapo. Kwa kifo cha Yesu Msamaha umepatikana kwa wote. Lango la mbingu liko wazi kwa wote wanaopenda kuingia. Katika kipindi hiki cha Kwaresima Mama Kanisa anatukumbusha tena na tena kuzihuisha na kuziishi ahadi na maagano ya Ubatizo wetu kwa kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kufanya matendo ya huruma.

Tunaalikwa kuzishika na kuziishi Amri za Mungu ili kujenga uhusiano mwema na Mungu na jirani zetu. Utimilifu wa amri hizi ni Upendo kwa Mungu na jirani. Maana Maandiko Matakatifu yanatuambia: “Msiwiwe na deni lingine isipokuwa deni la kupendana. Kule kusema usizini, usiibe, usiue, usitamani mwanamke au mwanaume asiye wako, usiseme uongo; haya yote hupata ukamilifu wake katika amri ya mapendo kwani pendo halimfayi jirani neno baya. Ujumbe wa Yesu katika Injili ni; tubuni na kuiamini Injili. Basi tuishi vyema agano tulilofunga na Mungu kwa njia ya ubatizo. Kwa wanandoa tunzeni maagano yenu ya ndoa, mdumishe maisha ya familia, Kanisa la nyumbani, shule ya sala na maadili mema, watawa na mapadre tutunze maagano ya miito yetu mitakatifu. Tuishi kadiri ya miito yetu tukimfuata Kristo aliye Njia Ukweli na Uzima. Na wengine ambao bado hamjachagua aina ya maisha, ishini kiamifu mkitafakari vizuri ili mfanye maamuzi yaliyo mema.

Jumapili 1 Kwaresima
18 February 2021, 16:09