Tafuta

Maadhimisho ya Juma Kuu: Jumapili ya Matawi: Mwaliko kwa waamini kusoma na kutafakari simulizi la mateso na kifo cha Kristo Yesu, chemchemi ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Maadhimisho ya Juma Kuu: Jumapili ya Matawi: Mwaliko kwa waamini kusoma na kutafakari simulizi la mateso na kifo cha Kristo Yesu, chemchemi ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. 

Maadhimisho ya Juma Kuu: Jumapili ya Matawi: Mateso!

Mwinjili Marko ndiye aliyeandika wa kwanza simulizi hizi, na lengo na shabaha yake ni kuwaimarisha waamini wale wa jumuiya za wakristo za mwanzo ambao bado walikuwa wanapitia mateso na magumu mengi katika kuishi imani yao, jumuiya ambayo haikuweza kutumia hata ishara ya Msalaba waziwazi. Kristo Yesu anabaki mtulivu na mkiya, wakati wa kuhukumiwa na kuteswa kwake

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na salama! Simulizi la Mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo, pamoja na kuwa ni refu, naomba niwaalike japo kutenga muda na kulisoma lote kama sala na huku tukiingia katika kutafakari upendo wa Mungu kwako na kwangu. Ni simulizi lililojaa na kusheheni katekesi nzuri kabisa kama mwongozo kwa maisha yetu ya kiimani. Ni katika tafakari yetu ya leo, kwa pamoja tunaweza kuona nini maana ya mateso na hasa kifo katika maisha yetu. Mateso na kifo ni vitu vya kutisha na kuogofya kwetu wanadamu, hata Yesu aliogopa kama mtu kweli pale saa ile ya mateso na kifo chake ilipowadia. Ni faraja na basi Yesu anatuonesha leo wapi, mimi na wewe tunaweza kupata nguvu ya kupokea saa ya mateso na kifo katika maisha yetu, ni kwa kumlilia na kumkimbilia Mungu pekee. Kwa bahati wainjili wote wanne wameandika juu ya simulizi la mateso na kifo chake Yesu wa Nazareti. Kila mmoja anaandika kwa mtindo na namna yake kutegemea nini lengo na nia yake na hasa upande wa katekesi aliyolenga ifike kwa jumuiya ile aliyoilenga. Hivyo nasi leo tubaki japo kutafakari simulizi la mateso na kifo chake Bwana wetu Yesu Kristo, kama ilivyoandikwa na Mwinjili Marko. Ndio simulizi la kwanza kabisa kuandikwa kabla ya Wainjili wengine.

Mwinjili Marko anasimulia juu ya mateso na kifo katika namna yake na hapo tutajaribu japo kifupi kuangalia mafundisho makuu au tabia za pekee anazopenda kutuonesha Mwinjili Marko. Mwinjili Marko ndiye aliyeandika wa kwanza simulizi hizi, na lengo na shabaha yake ni kuwaimarisha waamini wale wa jumuiya za wakristo za mwanzo ambao bado walikuwa wanapitia mateso na magumu mengi katika kuishi imani yao, jumuiya ambayo haikuweza kutumia hata ishara ya Msalaba waziwazi. Yesu Kristo anabaki mtulivu na mnyamavu, asiyesema kitu wala kujitetea katika wakati ule wa kukamatwa kwake na kuhukumiwa na kuteswa. Wakati Mwinjili Luka anatuonesha Yesu anayesema neno baada ya busu la Yuda Iskarioti, rejea Luka 22:48, na hata kwa Simoni Petro pale alipotoa upanga wake na kumkata sikio mtumishi wa kuhani mkuu, rejea Matayo 26:52. Mwinjili Marko anatuonesha Yesu anayebaki kimya na mpole na mtulivu katika matukio haya ya kutisha na kusikitisha.

Ni yote ili Maandiko yapate kutimia. Rejea Marko 14:49. Mwinjili Marko anamwonesha Yesu aliye mpole na anayekabili mateso na kifo chake kwa utulivu na unyenyekevu mkuu ili kuwaonesha waamini wale wa jumuiya za kwanza za kikristo kubaki na hali hiyo hiyo hata katika nyakati za mateso. Tunaona Mtume Petro anajaribu kumtetea kwa upanga, kwa kweli ni kuwaza na kufikiri kama wana wa ulimwengu huu. Mwanafunzi wa Yesu hatendi kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu, bali daima kadiri ya mpango na mapenzi yake Mungu. Ni mwaliko wa kukabili mateso ikiwa ni katika kutimiza mapenzi ya Mungu hasa tunapojitoa sadaka kwa ajili ya mwingine au wengine. Ni upendo wa Kimungu wa kujitoa bila kujibakiza wala kujitetea, ni katika kuangamiza nafsi zetu ndipo tunapoziokoa. Anayetumia njia ya vurugu na mabavu daima anakuwa mbali na Mwalimu wetu yaani Yesu Kristo, aliyebaki mtulivu na mkimya katika wakati huu mgumu wa maisha yake hapa duniani. Mwinjili Marko anatuonesha tena kuwa wanafunzi wake baada ya kuona Mwalimu wao amebaki kimya bila kujitetea wao wanaamua kukimbia.

Mwinjili Marko anamtaja kijana mmoja aliyebaki kumfuata kwa mbali. Labda tunabaki na kicheko tunapofika katika simulizi la kijana huyu. Mapokeo yanamwona kijana huyu kuwa ndiye Marko mwenyewe. Kijana anayeacha shuka lake na kukimbia akiwa uchi bila shuka. Kijana katika kigiriki ni νιανισκο (nianisko) na shuka ni σινδονα (sindona); Hivyo mwandishi katika simulizi ili anajaribu kutueleza mambo mawili. La kwanza, kijana huyu ni ishara ya Yesu Kristo mwenyewe, ambaye katika tukio hili yeye anabaki mzima kwa maana anafufuka na kuwaachia adui zake ile sanda tu (sindone), shuka lile aliloliacha yule kijana. Na hivyo adui hawafaulu kumwangamiza yeye ila wanabaki na shuka tupu. Na pili, ni fundisho katika kumfuasa Yesu Kristo ni mwaliko kuacha yote nyuma na kubaki sisi wenyewe, ndio picha ya uchi kuonesha kutojishikamanisha na malimwengu au vitu vya ulimwengu, ni kuukimbia ulimwengu ili kuokoa nafsi zetu. Ni kwa njia ya kuacha malimwengu tunaweza kuokoa nafsi na maisha yetu, yaani, kuupata ukombozi wa kweli. Wakati Wainjili wengine wanajaribu kuonesha kuwa jinsi Yesu alivyokuwa anakabiliwa na mateso, akajikuta anabaki na watu wachache karibu naye, hasa wanafunzi wake na baadhi ya wanawake. Ila Mwinjili Marko anatuonesha kuwa alibaki mwenyewe katika wakati huu mgumu wa mateso.

Mwinjili Marko haoneshi uwepo wa mtu yeyote karibu na Yesu anayeteswa. Ni baada ya kifo chake ndio anatuonesha uwepo wa wanawake waliosimama kwa mbali. Marko 15:40-41. Mwinjili Marko anatuonesha kuwa alibaki mpweke na hivyo Yesu hata akalia kwa Mungu Baba. “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha?” Rejea Marko 15:34. Wakati wa kifo chake pale msalabani, Yesu anajisikia kuwa peke yake bila nguvu zile za Kimungu, anabaki mtu kweli anayeteseka na kuuwa kwa ukosefu wa haki, iwe kwa upande wa kidini, na hata ule wa kisiasa. Ni mwaliko kwetu kuwa kuna nyakati katika kutetea haki na ukweli tutajikuta tumebaki wenyewe, tumeachwa na wote hata ndugu na jamaa na marafiki, hivyo hatuna budi kusali pamoja na Yesu kumuomba Mungu atusaidie. Ni fundisho kuwa hata Yesu aliteseka na kushawishika kuona yupo peke yake katika saa ile ya kutimiza mapenzi ya Mungu Baba. Ni kishawishi cha kibinadamu kuona tupo peke yetu katika mateso na hasa saa ile ya umauti.

Mwinjili Marko tofauti na wainjili wengine anatuonesha pia upande wa Yesu kama mtu kweli na hasa katika nyakati hizi ngumu za mateso na kifo chake. Yesu akiwa bustanini Getsemani, alijawa na uoga na hofu kubwa. Rejea Marko 14:33. Kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu mtu hodari na shujaa anakikabiri kifo au mateso bila uoga au hofu yeyote. Ni kama vile mwanafalsafa wa Kigiriki Sokrate aliyekikabiri kifo kwa ushujaa mkubwa. Mwinjili Marko anatuonesha Yesu Kristo aliye mtu kweli na sio mtu wa kipekee katika mateso, ni kama mimi na wewe. Kama mtu kweli alikiogopa kifo! Kinyume chake Marko Mwinjili katika simulizi zima anatuonesha Yesu aliyebaki kimya, iwe kwa viongozi wa kidini walipomuhoji kama yeye ni masiha na hata kwa Pilato aliyemuhoji kama yeye ni mfalme wa wayahudi. Anajibu kwa maneno mafupi sana; “Ni mimi”, Marko 14:62; 15:2. UKIMYA wake sio ule wa unyonge au kukosa ujasiri, bali ni ule wa nguvu ya ndani ya nafsi, ule wa kutojitetea katika dhulma dhidi ya haki na kweli, dhidi ya hila na uongo na fitina za kila aina. Ni ukimya unaowaalika watesi wake kujitafakari na hivyo kuenenda kadiri ya haki  na kweli.

Kadiri ya Mwinjili Marko, simulizi la mateso na kifo chake Yesu wa Nazareti linahitimishwa na kukiri kwa imani, ni jemadari wa kirumi, mtu mpagani ndiye anayenena wazi wazi chini ya Msalaba wake Yesu Kristo, anamtambua kuwa huyu ni Mwana wa Mungu, huyu ni Kristo. Ni kinyume maana huyu sasa ni mfu ila bado jemadari haoni kushindwa kwa huyu mtu bali anakufa kama mwenye uwezo na nguvu, kama Mwana wa Mungu. Ni katika kubaki chini ya msalaba nasi tunaalikwa kuona ukuu na nguvu za Yesu, Sio katika kutenda miujiza na kutoa pepo ila katika saa ile ya wokovu, saa ile ya upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Kifo cha ushindi ni kifo cha upendo, ni kifo cha ukombozi, ni kifo cha maisha mapya kwangu na kwako. Ni saa hii Yesu anakubali kutambulishwa kama MWANA WA MUNGU, Mwanzoni daima aliwazuia kumtambulisha kama Masiha na Kristo ila katika saa ya kifo chake sasa anatambuliwa na mpagani kuwa hakika huyu ni Mwana wa Mungu!

Tunasoma kuwa jemadari alimtambua sio kwa tetemeko la ardhi au kwa ishara ya giza juu ya sura ya nchi bali katika kifo chake. Kifo cha Yesu pale msalabani hakina budi kutusaidia nasi kuweza kukiri upendo wa Mungu katika maisha yetu. Na ndio mwaliko wa Juma kuu tunalolianza leo kubaki chini ya msalaba wake Yesu Kristo na kutafakari upendo wa Mungu kwetu wanadamu, ni mwaliko wa kumpenda Mungu kama ambavyo Jemadari yule wa Kirumi alivyoweza kumkiri Yesu kuwa ni Kristo, kuwa ni Mwana wa Mungu. Kupasuka kwa pazia la hekalu ni ishara ya mwanzo mpya, yaani sasa sote tunaweza kumfikia Mungu na si tu Kuhani mkuu peke yake aliyeweza kuingia pale patakatifu pa patakatifu. Mungu hayupo tena mbali na watu wake, hivyo sote tunaanza mahusiano mapya na Mungu Mwenyezi hata tukiwa na dhambi kubwa kiasi gani, sote tunapata fursa ya kumkaribia Mungu na kupata huruma na upendo wake wa Kimungu na ndio msamaha wa dhambi zetu.

Baada ya kifo cha Yesu pale juu msalabani, mwinjili Marko anamleta katika simulizi mtu aliyeheshimika na asiye kuwa na uoga, ni Yusufu wa Arimateya, anayefika kwa Pilato ili kupata kibali cha kumzika Yesu kwa heshima. Ni Marko mwinjili pekee anayetuonesha kuwa kitendo chake ni cha kishujaa na kinapaswa kuigwa nasi wafuasi wa Yesu Kristo. Marko 15:43 Ni katika nyakati kama hizi ambapo wote wanamkimbia na kumkana na kumuasi Yesu, Yusufu wa Arimateya anafika kwa Pilato na kujitambulisha kama rafiki wa kweli. Rafiki wa kweli utamjua katika shida na dhiki! Yesu pale juu Msalabani anamwita Baba yake wa mbinguni Abbà, neno linalotumika na watoto wadogo wanapojifunza kuita Baba. Ni ile imani anayokuwa nayo mtoto mdogo kwa baba yake ndio anayo Yesu hata saa ile ya mateso pale msalabani, ni imani kamilifu pasi na mashaka yeyote. Ni mwaliko kwetu pia kubaki na imani kwa Mungu Baba yetu hata katika nyakati ngumu kiasi gani, yeye ni Abbà, hivyo tuna hakika ya upendo na uwepo wake katika nyakati za majaribu katika maisha. Yeye ni mwaminifu hawezi kutuacha kamwe.

Wapenda Watanzania wenzangu na watu wote wenye mapenzi mema, tunajua tunapitia katika wakati mgumu kabisa wa kuondokewa na mpendwa rais wetu Mheshimiwa sana Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, tuna huzuni na simanzi kubwa, lakini zaidi sana tuna maswali kwa nini sasa, kwa nini Mungu hakumwepusha na kifo? Maswali ya haki kabisa iwe kwa familia yake na watu wake wa karibu lakini hata kwetu ambao ni raia wa Tanzania kwa nafasi mbali mbali, lakini faraja yetu kubwa leo itoke pale tunalitafakri fumbo la ukombozi wetu, yaani mateso, kifo na ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Ni kwa kukubali nasi kuwa chini ya msalaba wake Yesu, na hapo kuutafakari kwa mshangao upendo wa Mungu kwa mwanadamu, ndipo hakika tunaweza kujichotoe nguvu na kuona thamani ya mateso na kifo kwani ni kutupelekea nasi kushiriki katika utukufu wa ufufuko. Nawatakia nyote tafakari njema ya Juma Kuu, ni juma la kutafakari hasa Upendo wa Mungu kwetu wanadamu. Dominika njema!

24 March 2021, 11:55