Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya V ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka B wa Kanisa: Msalaba ni kielelezo cha ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa binadamu mdhambi! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya V ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka B wa Kanisa: Msalaba ni kielelezo cha ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa binadamu mdhambi! 

Jumapili V Kipindi cha Kwaresima: Fumbo la Kifo & Utukufu wa Kristo

Msalaba ni ishara ya upendo na huruma ya Mungu. Tunaalikwa kutafakari upendo usioelezeka wa Mungu kwa kila mmoja wetu. Ni upendo uliotundikwa pale juu Msalabani, ni Yesu anayatoa maisha yake ili mimi na wewe tuweze kufanyika marafiki zake. Msalaba ni ishara ya urafiki wa Mungu anayeshuka ili nasi kama walivyosema Mababa wa Kanisa tuweze kushiriki Umungu!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na salama! Kati ya mahujaji waliofika Yerusalemu wakati wa sikukuu ya Pasaka, walikuwepo pia Wagiriki au Wayunani, ambao wanamwomba Filipo na baadaye Filipo anamshirikisha pia Andrea ili waweze kumuona Yesu wa Nazareti. Mwinjili Yohane anawataja hapa hawa watu wa mataifa mengine au wapagani sio kwa bahati mbaya maana anataka kuonesha pia kuwa Mwana wa Adamu amekuja sio tu kwa Taifa pekee la Israeli bali kwa watu wote. Hata wapagani nao wana hamu na shauku ya kumuona Yesu wa Nazareti. Watu wa mataifa mengine waliopenda kujiunga na Dini ya Kiyahudi waliruhusiwa pia kufika Yerusalemu, ili kwa ajili ya kusikiliza Torati na pole pole baadaye waliweza kutahiliwa ili waweze kushiriki hata katika kutoa sadaka hekaluni na kuongozwa na Mungu wa Israeli kama tusomavyo katika  unabii wa Isaya 2:3. Yesu Kristo katika Injili ya Yohane 10:16-17 pia anazungumzia juu ya kondoo wale wengine ambao nao anapaswa kuwaongoza, na ndio hawa sasa wanamkaribia Yesu Kristo ili waweze kuisikia sauti yake na kumfuasa.

Hawa wapagani wanaotajwa na Mwinjili, tayari walishaanza safari yao ya kiroho na kiimani, kabla ya tukio la leo la kutaka kumuona Yesu wa Nazareti. Ni hamu ya mioyo yao kuweza kumjua zaidi Mungu wa Israeli na kuweza kumfuasa vema na ndio maana wanafika pia hekaluni kama ilivyokuwa desturi kwa wayahudi wengine na ndio hapo wanapata hamu ya kumuona Yesu wa Nazareti. Imani ni safari ya upendo, ni kuguswa na kuvutiwa na Yesu Kristo mwenyewe, “It is falling in love with the person of Jesus Christ in the first place.” Wanaenda kwa Filipo ambaye pia Mwinjili anamtambulisha kuwa alikuwa ni mfuasi wa Yesu Kristo na alikuwa mwenyeji wa Betsaida ya Galilaya. Kwa nini anataja na kijiji chake. Filipo anatokea katika mji wa mpakani ambapo pia waliishi si tu Wayahudi bali na wapagani na hata jina Filipo lina asili ya Kigiriki na sio Kiyahudi, ndio kusema pia Filipo alikuwa wazi zaidi kwani alitokea katika mji wenye wakazi wa mataifa mbali mbali. Andrea pia jina lake lina asili ya Kigiriki, hivyo hawa wawili wanatajwa na Mwinjili wanaenda kwa Yesu ili wageni wale waweze kumuona Yesu wa Nazareti.

Hili neno “Kuona” katika Injili ya leo lina maana kubwa kuliko ile tunayoweza kuipata mara moja. Wagiriki hawa wanamuomba Filipo kumuona Yesu, Je, wanataka kumuona Yesu wa Nazareti kama superstar, mtenda miujiza na mwalimu mashuhuri au kuna maana nyingine zaidi. Kuona kwa namna hii wengi waliweza hata wanaweza kufanya kila siku pale tunaposikia mtu mashuhuri na maarufu anafika katika mazingira yetu. Katika Agano Jipya, kitendo cha kuona kinaweza kumaanishwa na maneno mawili ya Kigiriki nayo ni “βλεπω na οραω”, unaweza kutamka kama “blepo” na “orao”. Neno la kwanza blepo likimaanisha kuona kwa kawaida au kwa juu juu au kwa nje nje tu. Ni sawa na kwenda kumshangaa mtu maarufu kama rais wa nchi anayefanya siasa zake majukwaani au mwanamuziki fulani anayefika maeneo yetu kutoa burudani. Ni baada ya kuona mara nyingi hakuna la ziada linatuunganisha na mtu huyo mashuhuri.

Hapa neno lenyewe ni orao (οραω), ndio kuona kwa jicho la ndani hasa au la kiroho ili kuweza kuwa na mahusiano ya kiimani. Kuona huku sio kule kwa kutumia macho ya nyama tu, bali ni kutaka kuona kwa ndani. Ni muono wa kukutana na nafsi ya yule unayemuona, ni muono wa kuipenda nafsi nyingine, ni kuona kwa ndani kabisa na kuanza mahusiano ya upendo. Hiyo ndio ilikuwa shauku na nia ya wageni wale. Yafaa kujiuliza mimi na wewe, Je, tunamtafuta Yesu kumuona kwa juu juu tu kama tufanyavyo kwa watu mashuhuri wa ulimwengu huu au tunataka kumuona kwa jicho la kiroho ili tuanze mahusiano naye? Ni mara ngapi kwetu Yesu Kristo anabaki ni mtenda miujiza tu, au atujalie neema fulani maishani? Je, tuna mahusiano naye kwa kuwa tumetambua nafsi yake na kumpenda. Je, ni rafiki wa dhati na wa moyoni? Hatuna budi kumuona Yesu kwa jicho la ndani ili tuweze kujenga urafiki naye. Imani ni safari ya upendo kwa Mungu mwenyewe, ni kutoka ndani mwetu ili tuweze kukutana naye aliyegusa maisha yetu, hivyo tunataka kuanza safari ya kujenga mahusiano ya karibu na ndani zaidi.

Wagiriki hawakuwa na haja ya muono wa nje ila kukutana na nafsi ya YESU WA NAZARETI ili kukidhi kiu yao ya kiroho. Hivyo nasi hatuna budi kama kweli tunataka kukua katika safari yetu ya imani, lazima kujaribu kukutana na kumtafuta Yesu ili kujenga naye mahusiano ya upendo na ya daima maishani mwetu, ni kutaka kuungana naye katika maisha ya sasa ulimwenguni na yale ya umilele. Andrea alikuwa ni kati ya wafuasi wa Yohana Mbatizaji waliopokea mwaliko kutoka kwa Yesu Kristo: Njooni nanyi mtaona. Rejea Yohane 1:39 Naye alienda na kuona, kwa maana ya οραω(orao), ile ya kuona kwa ndani, hivyo alijenga urafiki na Yesu Kristo na sasa anawasaidia hawa wagiriki kupata fursa ya kumuona Yesu Kristo, kujenga urafiki na Yesu. Mwinjili Yohane hasemi sana kama hawa wagiriki walipata fursa ile adimu ya kumuona Yesu Kristo au la, maana hatuwasikii tena katika simulizi la Injili ya leo.  Ni kama alivyofanya kwa Nikodemo, wanatoweka ghafla katika simulizi. Uwepo wao na hamu yao ya kumuona Yesu Kristo imeandaa mazingira ya mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Yesu Kristo anatoa katekesi kwa yeyote anayetaka kuiona nafsi yake ili kujenga urafiki wa kweli. Rafiki humfichi jambo, na ndio afanyalo Yesu Kristo kwetu katika Injili ya leo, anajiweka wazi kama vile ungefanya pale unapoenda kwa rafiki yako. Rafiki anagusa maisha yako, na taratibu unapata nafasi ya kumfahamu rafiki yako, na jinsi unavyomfahamu na ndivyo pia unakua urafiki wenu, basi nasi katika kipindi cha mfungo wa Kwaresima, kipindi cha neema, ni nafasi ya kukua zaidi na zaidi ya urafiki wetu na Bwana wetu Yesu Kristo, ni kipindi ambacho tunapouangalia na kuutafakari Msalaba hapo tunaonja upendo na huruma yake ya Kimungu kwa kila mmoja wetu. Ni rafiki aliyetoa maisha yake kwa ajili ya wokovu wetu. Yesu Kristo sasa anatumia fursa hii kujifunua na kujionesha au kujiweka wazi, sio tu kwa wale waliomsikiliza miaka zaidi ya 2000 iliyopita bali kwa wasikilizaji wa Neno lake, yaani wewe na mimi leo hii. Yesu Kristo anatoa katekesi juu ya yeye ni nani ili nasi tuweze kumuona Yesu Kristo sio kwa jicho la nyama bali kwa jicho la kiroho (οραω). Tuweze kuifahamu nafsi yake, na hatimaye tuweze kujenga urafiki wa kudumu naye.

Yesu Kristo katika kujifunua nafsi yake anatumia mfano wa kawaida kutoka katika mazingira ya wakulima. Anatumia mfano wa mbegu ya ngano ambayo haina budi kufa ardhini, ili kuweza kuzaa mazao mengi na mazuri. Yesu Kristo kinyume na mantiki ya ulimwengu wetu, maisha ya kweli ni katika kujitoa sadaka ya upendo kwa ajili ya wengine, hivyo naye anatuonesha mfano wa kutoa maisha yake pale juu msalabani kwa ajili ya wokovu wetu. Msalaba ni ishara ya upendo na huruma ya Mungu kwetu wanadamu! Ni kila tunapoutafakari Msalaba tunaalikwa kutafakari upendo usioelezeka wa Mungu kwa kila mmoja wetu. Ni upendo uliotundikwa pale juu Msalabani, ni Yesu anayatoa maisha yake ili mimi na wewe tuweze kufanyika marafiki zake. Msalaba ni ishara ya urafiki wa Mungu anayeshuka ili nasi kama walivyosema Mababa wa Kanisa tuweze kushiriki Umungu! Kwa Wagiriki maisha ya kweli ni yale ya kuwa na heshima na hadhi katika jamii. Kwa Kigiriki watu waliofanikiwa katika maisha wanaitwa αριστοι (Aristoi), na ndio leo hii kuna neno la Kiingereza aristocracy, kumaanisha watu wa hadhi na daraja la juu, watu wenye mafanikio, mathalani watawala kama wanasiasa wetu, wabunge, mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, rais na wengine wengi tunaoweza kusema “wanakula kuku kwa mrija” hata kati ya jamii maskini kabisa kama ya Tanzania.

Leo hii ukitaka utajiri wa haraka na mafanikio makubwa katika mataifa mengi maskini utasikia ni kujiunga au kuwa mwanasiasa. Na pia kundi la pili ni kufungua Makanisa haya yanayojiita ya kiroho, ambapo wahubiri wake wanahubiri “Injili ya utajiri na mafanikio katika maisha”, hakuna nafasi kabisa ya kuutafakari wala kuhubiri juu ya “upendo wa Mungu ulijifunua na kujidhihirisha pale juu Msalabani”, Yesu aliyejitambua pamoja na wadhambi, maskini na watu waliosetwa katika jamii zao. Leo wapendwa tunaalikwa kuutafakari Msalaba wake Bwana wetu Yesu Kristo, ni hapo juu msalabani tunauonja upendo na huruma ya Mungu kwa kila mmoja wetu. Hivyo kwa Wagiriki Yesu Kristo anatoa mafundisho kuwa utukufu wa kweli ni katika kuanguka ardhini na kufa ili kuweza kuzaa matunda. Na ndio saa yake imefika ya kutoa maisha yake kwa ajili ya wanadamu wote. Ni saa ya utukufu wa Mungu, ni saa ya upendo wa Mungu kwa watu wake. Utukufu wake ni katika kujitoa sadaka, ni kinyume na utukufu wa ulimwengu wetu wa leo. Utukufu wake Yesu Kristo, haupo katika kuikoa nafsi yake ila kuitoa kwa upendo kwa ajili ya rafiki zake.

Utukufu wake ni katika kupenda mwanadamu! Udhaifu wa Mungu ni katika kupenda, maana anatupenda bila masharti, bila mastahili yetu kwa kuwa tu wema au watu wenye sifa fulani njema na nzuri katika jamii! Ni upendo wa ajabu na usiopimika wala kuelezeka kwa lugha na vipimo vyetu vya kibinadamu, ni upendo unatoacha na mshangao mkubwa na ubumbuwazi pia! Hivyo, sio lazima kumuona Yesu katika mwili wake ili kuweza kuiona nafsi yake ya Upendo. Kila mmoja wetu anaweza kumuona Yesu Kristo kwa kutafakari upendo wake. Sura yake anayotuonesha inatualika nasi kubadili vichwa vyetu (μετανοια), metanoia ya kweli ni kubadili mtazamo wetu juu yake na juu ya ufuasi wetu. Sura yake ya kweli ni makwazo kwa wayahudi na upumbavu kwa wayunani au wagiriki watu wa falsafa na mawazo ya juu. Yesu Kristo ni yule mwenye sura isiyotamanika machoni pa watu. Rejea Isaya 52:13; 53:3. Kumfuasa Yesu Kristo ni kushiriki nasi katika upendo wake, ni katika kumpenda Mungu na jirani. Ni upendo wa kujisahau sisi wenyewe kwa ajili ya Mungu na jirani, ni upendo wa kujisadaka kama mbegu ya ngano inayokufa ardhini ili kuweza kuzaa matunda mengi na mazuri. Nawatakia Dominika njema tunapotafakari sura yake Yesu Kristo na ufuasi wetu. Na pia maandalizi mema ya kuingia Juma Kuu la Mateso, Kifo na Ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo.

 

20 March 2021, 08:03