Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya V ya Kipindi cha Kwaresima: Fumbo la Umwilisho linapata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya V ya Kipindi cha Kwaresima: Fumbo la Umwilisho linapata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu! 

Tafakari Neno la Mungu Jumapili V ya Kwaresima: Msalaba wa Yesu

Yesu anajibu ombi la Wayunani kutaka kumwona kwa kuwaeleza kiini cha fumbo la Umwilisho kuwa ni fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wake. Yesu anaweka wazi kuwa saa imefika ya mwana wa Adamu kutukuzwa, atateseka na kufa, ambapo kwa mateso yake, watu wataokoka na Baba yake aliye mbinguni atatukuzwa, naye ataingia katika utukufu, chemchemi ya wokovu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya tano ya Kwaresima mwaka B wa Kiliturujia siku ya 33 ya kujitakatifuza.  Siku arobaini za kipindi cha Kwaresima zinatuhimiza kwa kurudia tena na tena mwaliko wa kufunga, kufanya toba, kusali zaidi, kutenda matendo ya huruma na upendo na kusoma na kutafakari neno la Mungu zaidi. Zimebaki siku 7 tuingie Juma Kuu. Pasaka imekaribia. Hivi karibuni tutaadhimisha mateso, kifo na ufufuko wa Yesu, ushindi wake dhidi ya dhambi na mauti. Ni kipindi cha kujihoji na kujiuliza ndani ya mioyo yetu kama tumeyaishi tunayopaswa katika kipindi hiki: Je, dhambi ile ninayoipenda sana nimeiacha, tendo gani la huruma nimetenda tangu kwaresma ianze, nimejinyima nini kwa ajili ya wengine, nimeweza kuwasaidia wahitaji kwaresma hii? Kama bado zimebakisha siku 7, chukua hatua haraka hujachelewe.

Katika somo la kwanza la Kitabu cha Nabii Yeremia, Mungu anaahidi kufanya Agano Jipya na la milele, Agano ambalo kwalo Mungu anaahidi kuwasamehe watu uovu wao, wala hataikumbuka tena dhambi yao. Kwa Agano hili jamii yote ya wanadamu inajazwa Roho Mtakatifu na kuwezeshwa kumjua Mungu kama Baba yetu mwema na hivyo tunapata ujasiri wa kusali na kuomba kama mzaburi katika wimbo wa katikati tukisema; Ee Mungu, unirehemu, sawasawa na fadhili zako, kiasi cha wingi wa rehema zako, uyafute makosa yangu, unioshe kabisa na uovu wangu, unitakase dhambi zangu, uniumbie moyo safi, uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu. Usinitenge na uso wako, wala roho wako mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako, unitegemeze kwa roho ya wepesi nami nitawafundisha wakosaji njia zako, na wenye dhambi watarejea kwako.

Somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waebrania linatufafanulia fumbo hili la Agano Jipya na la milele lililosimikwa juu ya msalaba. Mateso, uchungu na kifo cha Yesu vinaonyesha kuwa Yeye alikuwa kweli wakili na kuhani wetu. Utii wake ulimpendeza Mungu, hata ukaleta wokovu kwetu. Yesu alitolea maisha yake, dua na maombi na kulia sana na machozi, akawa mtii, akavumilia mateso hata kufa msalabani, kifo ambacho yeye mwenyewe anakitabiri katika Injili (Yn.12:20-33) baada ya kuambiwa kuwa kuna wayunani wanataka kumwona. Ilikuwaje Wayunani kuomba kumwona Yesu? Ilikuwa hivi: wakati wa Yesu wayahudi wengi waliishi uhamishoni, nje ya Palestina, nao walijulikana kama Wayahudi wa Diaspora. Popote walipokuwa walijenga masinagogi kwa ajili ya kusali na kusoma neno la Mungu. Watu wa mataifa yaani wapagani walivutiwa na namna ya ibada zao walizozifanya katika Masinagogi yao kwani jinsi ilivyojaa uchaji kwa Mungu, tofauti kabisa na ibada za kipagani.

Hivyo wengi walijiunga na dini ya kiyahudi, wakajifunza maandiko matakatifu, namna yao ya kusali na wakawa wanashika mila na tamaduni za Kiyahudi kama vile kwenda kuhiji Yerusalemu wakati wa sherehe kubwa za kiyahudi. Wapagani walioingokea dini ya Kiyahudi waliitwa Waproseliti (Proselytes) yaani Wacha Mungu au Watu waliokuja Karibu na Mungu (mdo.2:10), mfano ni Nikolaus wa Antiokia, mmoja kati ya Mashemasi Saba (Mdo 6:5) na Kornelio afisa Jeshi wa Kirumi (Mdo 10:11-12). Kundi hilo la wacha Mungu ndilo lililokuja kuhiji Yerusalemu. Watu hawa Yohane anawaita Wayunani au Wagiriki, waliomwendea Filipo mtu wa Bethsaida ya Galilaya, na kumweleza shauku yao ya kumwona Yesu. Filipo akamwambia Andrea, kisha wakamwambia Yesu. Yesu anajibu ombi la Wayunani kutaka kumwona kwa kuwaeleza kiini cha fumbo la Umwilisho kuwa ni fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wake. Yesu anaweka wazi kuwa saa imefika ya mwana wa Adamu kutukuzwa, atateseka na kufa, ambapo kwa mateso yake, watu wataokoka na Baba yake aliye mbinguni atatukuzwa, naye ataingia katika utukufu.

Hivyo kama wao nao wanataka kuwa wafuasi wake, wanapaswa kuwa tayari kukishiriki kikombe chake ambacho ni kukataliwa, kuteswa na kuuawa, lakini hatima ya yote ni kushiriki taji ya utukufu pamoja naye. Katika kutabiri kifo chake Yesu anasema; “chembe ya ngano isipoanguka chini ikafa, hubaki hivyo hivyo ilivyo peke yake, bali ikifa hutoa mazao mengi.” Sisi ndio mazao na matunda ya mateso, kifo na ufufuko wake Yesu Kristo, aliyekubali kuteseka na kufa kifo cha aibu msalabani kwa wokovu wetu. Tukitaka kufaidi wokovu huu yaani uzima wa milele, yatupaswa kumtumikia Kristo kati ya ndugu zetu. Maana yeye mwenyewe anasema; Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu. Sisi kwa Ubatizo, kwa njia ya maji na Roho Mtakatifu tumefanya Agano na Mungu wetu, tumezaliwa upya, tumekuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa. Agano hili limeandikwa ndani kabisa mwa Roho zetu, tumetiwa mhuri usiofutika milele kwa kumkataa shetani na mambo yake yote na fahari zake zote na tukajiweka katika himaya ya mwenyezi Mungu.

Lakini wakati mwingine tunakuwa na mioyo migumu na kushindwa kuisikiliza sauti ya Mungu na kuvunja ahadi za Agano letu na Mungu, kwa kujishikamanisha na shetani na kuishi katika hali ya dhambi. Hali hii wakati mwingine inasababishwa na mateso na mahangaiko katika maisha na kushindwa kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Tutambue kuwa hata Yesu mwana wa Mungu aliyakabili mateso kwa huzuni kubwa moyoni hata akasali na kuomba: “Baba chochote chawezekana kwako, ikibidi niondolee kikombe hiki, lakini mapenzi yako yatimizwe. Mateso yalipoongezeka alilia kwa sauti kuu: “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha” (Mk 15:34), mwisho akayakubali mateso na kusema: “Baba, Mikononi mwako naiweka Roho yangu” (Lk 23:46). Nasi pia katika mateso na mahangaiko ya kila siku tujikabidhi kwa Mungu, tumwombe atupe nguvu na ujasiri wa kuyakabili majukumu na mahangaiko ya maisha yetu kwa uvumilivu, huku tukitafuta kuyatimiza mapenzi ya Mungu.

Zimebaki siku saba tu tuingie katika juma kuu. Ni juma la kuadhimisha Fumbo Kuu la ukombozi wetu yaani mateso kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo ambalo linaanzia na Dominika ijayo, Dominika ya matawi, Dominika ya mateso. Tuchunguze dhamiri zetu, kila mmoja ndani ya nafsi yake na kwa nafasi yake aangalie mahusiano yake na Mungu, na jirani zake, na familia yake pia yeye mwenyewe na nafsi yake. Je kipindi hiki cha kwaresima kimekuletea matunda mema ya kiroho. Umebadili mwenendo wako au bado umezama katika kilindi cha dhambi. Usiogope bado hujachelewa, Mungu Baba yetu ni mwenye huruma, bado anakusubiri umrudie. Ijongee kwa ujasiri Sakramenti ya kitubio, Sakramenti ya utakaso, Sakramenti ya upatanisho, Sakramenti ya ungamo la dhambi, ujipatanishe na Baba kwani siku si nyingi Yesu ametuambia kuwa “sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo, sasa mkuu wa ulimwengu huu (Ibilisi) atatupwa nje, naye akiinuliwa juu ya nchi atawavutia watu wote kwake, tuwe na utii kwake. Mungu kupitia Nabii Yeremia 31:34 ametuambia kuwa tukiyakiri makosa yetu na kuyatubu yeye atatusamehe uovu wetu wote wala dhambi yetu hataikumbuka tena kamwe. Tujiweke tayari siku yaja ili itukute tu tayari tufufuke naye tusije tukabaki ndani ya kaburi naye akatuacha huko kamwe hatutatoka.

Jumapili 5 Kwaresima
19 March 2021, 15:59