Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 3 ya Kipindi cha Kwaresima: Hekalu ni nyumba ya sala na ibada. Kristo Yesu ni kielelezo cha sadaka ya hali ya juu kabisa iliyotolewa kwa ajili ya wokovu wa walimwengu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 3 ya Kipindi cha Kwaresima: Hekalu ni nyumba ya sala na ibada. Kristo Yesu ni kielelezo cha sadaka ya hali ya juu kabisa iliyotolewa kwa ajili ya wokovu wa walimwengu. 

Tafakari Jumapili 3 Kwaresima: Hekalu Ni Nyumba ya Sala na Ibada

Mwinjili Yohane anaonesha kuwa Yesu Kristo aliwafukuza sio tu wauzaji, bali hata wanyama waliokuwa wanauzwa katika sehemu ile ya hekalu. Hii ni ishara wazi kutoka kwa Yesu Kristo mwisho wa sadaka za wanyama. Sadaka pekee inayompendeza Mungu Baba ni ile ya upendo wa Mwanaye anayejitoa sadaka Msalabani kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Rejea Isaya1:11 na 1Yohane 3:16.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na salama! Tukio la Injili ya Dominika ya leo kutoka kwa Mwinjili Yohana inaelezwa pia katika zile Injili pacha! Hivyo kuonesha umuhimu wa tukio hilo na hasa ujumbe nyuma yake.  Wakati wa Sikukuu ya Pasaka ya wayahudi, Yerusalemu ilikuwa inajaa mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za ulimwengu wa wayahudi. Jiji la Yerusalemu kwa kawaida lilikuwa na wakazi wapatao 50,000 ila wakati wa Pasaka waliweza kufika mpaka idadi ya watu takribani 180,000. Mahujaji hawa wengi wao walikuwa wanatoka mbali na pia walijikatalia mengi ili waweze nao kufanya hija hii takatifu walau mara moja katika maisha yao. Rejea Zaburi 84:6 Mahujaji walifika Hekaluni Yerusalemu kwa ajili ya kusali, kupata ushauri wa kiroho kutoka kwa makuhani, kutolea sadaka za wanyama, kutoa zaka zao kwa kutumia pesa isiyokuwa najisi hivyo walipaswa kubadili pesa wanapofika hekaluni, ili wapate pesa iliyo safi yaani isiyo na taswira wala picha ya miungu. Mfano wasingeweza kutumia pesa ya kirumi kwani ilikuwa ni sawa na kuabudu miungu ya kirumi iliyoonekana katika pesa hiyo. Na ndio maana tunasikia uwepo wa wabadilishaji wa fedha katika tukio la Injili ya leo.

Kwa wafanyabiashara wa nyakati zile, Sikukuu ya Pasaka ilikuwa ni wakati muafaka wa kufanya biashara zao, na hivyo kutopoteza fursa hii adimu iliyopatikana mara moja kwa mwaka, na ilidumu kwa muda wa majuma matatu. Pamoja na kuwa vitu vilipanda sana bei wakati wa sikukuu hizi, ila bado mahujaji walikuwa wanajaa madukani kuanzia mapema asubuhi mpaka saa za jioni. Ni katika mazingira haya ya biashara na kujenga uchumi tunaona hata makuhani nao walinaswa katika mtego huu wa fedha. makuhani walihusika na uuzwaji wa kondoo na wanyama wa kutolewa sadaka. Inasemekana nyakati za Yesu waliweza kuuza mpaka kondoo na wanyama wengine wapatao 18,000 kwa sikukuu ya Pasaka kwa mwaka mmoja. Na wasimamizi wakuu wa biashara hii walikuwa ni Masudukayo chini ya uongozi wa familia ya kuhani mkuu Anna na Kayafa. Hivyo Nyumba ya Sala au hekalu ikageuzwa na hawa makuhani kuwa soko la biashara. Hivyo nimeona ni vyema kuanza kuonesha mazingira na hali halisi ilivyokuwa ili kuweza kuelewa vyema ujumbe wa Injili ya Dominika ya leo.

Ni katika muktadha na mazingira haya tunaona Yesu Kristo naye anafika hekaluni na kuonesha hasira yake wazi wazi kwa wanafunzi wake na wote waliokuwepo pale hekaluni wakifanya biashara aidha ya wanyama au ya kubadili pesa. Hekalu la Yerusalemu ni vyema pia tukaelewa lilikuwa ni kubwa sawa karibu na viwanja takribani 20 vya mpira wa miguu, na hivyo liligawanywa katika sehemu mbali mbali kadiri ya hali ya usafi wa mahujaji. Kimsingi kulikuwa na sehemu iliyotengwa na kuweza kufikiwa na wayahudi tu tena walio safi, wasio najisi kwa maana wakoma, walemavu na wengine walioonekana kuwa ni wadhambi. Na hata katika patakatifu pia wanawake walitengwa na wanaume, na wanaume pia kulikuwa na makuhani waliokuwa na sehemu yao na kati ya makuhani aliyeweza kuingia ndani kabisa kutolea sadaka katika patakatifu pa patakatifu alikuwa ni kuhani mkuu wa zamu peke yake. Hivyo unaweza kupata picha ni ibada ya dini iliyowaweka watu katika matabaka na makundi mbali mbali. Kwa nini nasema haya yote naomba kurudia ili kutusaidia kuelewa kile ambacho Yesu Kristo alichokiona na hata kumpelekea kukasirika kwa jinsi alivyoumizwa na ubaguzi ule hekaluni.

Mwinjili Yohane anaonesha kuwa Yesu Kristo, aliwafukuza sio tu wauzaji, bali hata wanyama waliokuwa wanauzwa katika sehemu ile ya hekalu. Hii ni ishara wazi kutoka kwa Yesu Kristo mwisho wa sadaka za wanyama. Sadaka pekee inayompendeza Mungu Baba ni ile ya upendo wa Mwanaye anayejitoa sadaka pale Msalabani kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Rejea Isaya1:11 na 1Yohane 3:16. Yesu Kristo anayeoneshwa na wainjili kuwa ni mnyenyekevu na mpole, ila leo tunastushwa na jinsi alivyokuwa kinyume na makundi haya ya watu pale hekaluni. Jibu la swala na mshangao wetu linapatikana katika maneno ya Yesu mwenyewe katika Injili ya leo. Yesu anatumia maneno ya Nabii Zakaria, kuwa nyumba ya Baba yake ni nyumba ya sala.  Rejea Zakaria 14:21 Yesu Kristo anapinga ibada zinazogeuzwa kuwa biashara, au sababu za kiuchumi. Kutoka kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu anategemea upendo na sio mali au vitu au fedha au wanyama.

Na ndio maana hata mahali pengine katika Injili ya Mathayo, Yesu Kristo anawakumbusha wanafunzi wake kuwa mmepewa bure basi mtoe bure. Rejea Mathayo 10:9-10 Inasikitisha leo kuona utitiri wa makanisa yanayojikita katika miujiza na kulaghai waamini ili watoe sadaka na mali zao. Ni makanisa biashara hatuna budi kuepukana nayo. Hatupaswi kuingia katika kishawishi na majaribu ya kugeuza nia na misheni ya Kanisa kama chombo cha kuwaonesha watu upendo na huruma ya Mungu kwa mwanadamu. Ni vema leo kama Kanisa, kukumbuka na kuzingatia utume wake, ndio kuwa wajumbe na mashuhuda wa Habari Njema ya upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote. Uinjilishaji mpya unatuhitaji sote kuzingatia ni nini misheni ya Kanisa, na hapo tubadili vichwa au namna zetu za kufikiri ili tuenende kadiri ya Injili ya Yesu Kristo. Ni kwa kukubali kuongozwa na Injili pekee hapo tutakuwa na Kanisa linaloakisi kweli sura ya Mungu, Kanisa litakaloweza kubadili na kugusa maisha ya watu wote, maana ulimwengu leo unahitaji maisha ya ushahidi zaidi kutoka kwetu Wanakanisa.

Pili, Yesu Kristo anazungumzia juu ya kulibomoa hekalu na kulijenga kwa siku tatu. Hekalu analozungumzia hapa, kama alivyoweka bayana mwinjili ni mwili wake. Wayahudi walijua kuwa Utukufu wa Mungu au kwa kiyahudi “Shekinah”, ulikuwepo hekaluni tu pale Yerusalemu, ila Yesu Kristo anaanzisha mahusiano mapya na kutupa Mwili wake kuwa sadaka safi na takatifu.  Kupasuka pia kwa pazia la hekalu ni mwanzo mpya, maana Mwenyezi Mungu anaondoa kila aina ya matabaka au utengano kwa watu wake. Ikumbukwe kama nilivyosema hapo awali kuwa hata Wayahudi walitengwa kulingana na makundi mbali mbali walipoingia katika hekalu. Kanisa kama jumuiya ya waamini wa Mungu haina budi kuwa katoliki, kwa maana iliyo wazi kwa watu wote bila ubaguzi wa aina yeyote ile. Rejea Mathayo 27:51 Kukutana na Mungu sio tu pale hekaluni bali mwanzo mpya wa kukutana na Mungu katika roho na kweli. Rejea Yohane 4:21-24 Katika Agano Jipya kuna sehemu kadha wa kadha tunapooneshwa juu ya ibada ya kweli katika roho. Rejea Warumi 12:1; Waebrania 13:16; Yakobo 1:27. Hekalu jipya ni Yesu Kristo mwenyewe ambaye anatualika nasi kuwa mawe hai katika kuujenga mwili wake yaani Kanisa kama jumuiya ya wana wa Mungu. Rejea 1Petro 2:4-5.

Sadaka iliyo safi na inayompendeza Mungu ni kujitoa mwenyewe sadaka kwa Mungu kwa kumpenda mwingine, hasa walio maskini, wagonjwa, waliosetwa, wenye njaa na kiu, walio uchi, walio gerezani na kadhalika na kadhalika. Pamoja na sala na ibada mbali mbali tunazokuwa nao au kuzifanya kila mara, hatuna budi kukumbuka kuwa maisha yetu sasa ni mwaliko wa kuishi yale tunayoyaadhimisha. Neno la Mungu na Sakramenti ni kutujalia neema na kuchota mwanga na nguvu za Kimungu ili kuweza kuishi katika maisha yetu ya siku kwa siku. Injili ya leo inaishia kwa kuonesha kuwa Yesu Kristo alifanya miujiza mingi na watu wakamwamini ila Yesu Kristo alijua mioyo yao kuwa walikuwa mbali na Neno lake. Tumwombe nasi Mungu katika Dominika ya leo, kuwa na mahusiano mapya na Mungu, siyo yale yanayojikita katika mali au vitu au miujiza bali iwe ya Upendo wa kweli kwake. Nawatakia Dominika njema na mfungo mwema wa Kwaresma.

06 March 2021, 17:13