Tafakari Jumapili 3 Kwaresima: Yesu Ni Hekalu Jipya na la Milele
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya tatu ya Kwaresima mwaka B wa Kilitrujia, siku ya kumi na tisa ya kujitakatifu kama wimbo wa mwanzo kutoka kitabu cha Nabii Ezekieli unavyosema; Nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtatakasika na uchafu wenu wote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, asema Bwana. Ni utakaso wa kiroho tunaoupata kwa kufunga na kusali ndiyo maana katika sala ya Koleta Padre anasali kwa niaba ya Taifa la Mungu akisema; Ee Mungu, wewe ndiwe asili ya rehema zote na mema yote. Umeonyesha kuwa dawa ya dhambi ni kufunga, kusali na kuwapa maskini. Utusikilize kwa wema sisi tunaokiri unyonge wetu, ili tunaponyenyekea moyoni, utuinue daima kwa huruma yako. Somo la kwanza ni la kitabu cha Kutoka. Somo hili linatusimulia jinsi Mungu alivyowakomboa Waisraeli toka utumwani Misri. Kisha akafanya nao agano, akawapa amri kumi ziwe mwongozo katika maisha yao (Kut.20:1-17). Amri hizi ni mwongozo wa maisha yote ya mwanadamu na zinatusaidia kujenga uhusiano mwema na Mungu na jirani.
Kila azishikaye amri hizi anapata amani na heri katika maisha yake kama anavyoshuhudia mzaburi katika wimbo wa katikati akisema; Sheria ya Bwana ni kamilifu, huiburudisha nafsi, ushuhuda wa Bwana ni amini, humtia mjinga hekima. Maagizo ya Bwana ni ya adili, huufurahisha moyo na amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru (Zab. 19: 7-10). Kwa kufanya nao agano Mungu alionyesha mapendo makubwa kwa taifa hii na taratibu alifunua mpango wake wa kuwakomboa wanadamu wote kutoka katika utumwa wa dhambi. Lakini wana wa Israeli kila mara walivunja agano walilofanya na Mungu kwa kuabudu miungu ya uwongo. Mungu aliwaadhibu kwa njia ya vita; walivamiwa na mataifa ya jirani na kuwachukua mateka ili kuwafanya wamkumbuke na kumrudia. Hatimaye, akaamua kufanya nasi Agano jipya na la milele kwa njia ya Mwanae Bwana wetu Yesu Kristo. Somo la pili la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho linatueleza namna watu wa mataifa mbalimbali walivyopata ugumu katika kulielewa na kuliamini fumbo la ukombozi wetu kwa njia ya msalaba yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Wayahudi walidhani Kristo alilaaniwa na Mungu kwa kufa msalabani, na Wayunani wakitaka hoja za kiakili. Kwetu sisi ni bahati ya pekee kumsadiki Kristo, njia pekee ya wokovu wetu. Kwani Kristo kwetu ni nguvu na hekima ya Mungu. Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu. Katika Injili ilivyoandikwa na Yohane Yesu anawafukuza waliokuwa wanafanya biashara Hekaluni, ishara kuwa nyakati za kimasiya za kujenga hekalu mpya ambapo watu wote watamwabudu Mungu katika kweli na roho zimekaribia. Swali la kujiuliza; Ilikuwaje watu hawa wakafanya biashara hekaluni, hali wakijua wazi kuwa ni nyumba ya sala? Injili inasema wazi kuwa ilikuwa karibu na Pasaka ya Kiyahudi. Sikukuu hii ilisherehekewa siku ya 14 ya mwezi wa Nisani (Machi-Aprili) iliyofuatiwa na sherehe ya majuma iliyojulikana kama Azzimi ambapo walikula mikate isiyotiwa chachu (Kut. 34:23).
Kilikuwa ni kipindi cha kuhiji. Moja ya tendo muhimu la kuhiji lilikuwa kutoa sadaka za wanyama wa kuteketezwa kama kondoo, ng’ombe au njiwa kila mmoja kadiri ya uwezo wake. Wanaume wenu wote lazima wajitokeze mara tatu kwa mwaka mbele za Bwana Mungu wenu mahali atakapopachagua: kwa ajili ya Sikukuu ya Mikate isiyotiwa chachu, Sikukuu ya Majuma na Sikukuu ya Vibanda. Hakuna mtu atakayejitokeza mbele ya Bwana mikono mitupu: Kila mmoja wenu ni lazima alete zawadi kulingana na jinsi ambavyo Bwana Mungu wenu alivyowabariki (Kumb. 16:16) (Walawi 5:7), pia walipaswa kulipa kodi au zaka (Kut. 30:13). Kwa kuwa watu walitoka mbali hawakuweza kusafirisha wanyama kwa ajili ya kutolea sadaka. Kumbe kulikuwa na watu wanaouza wanyama wanaostahili kwa sadaka hekaluni na wengine walikuwa wakivunja au kubadilisha fedha kutoka sarafu ya kirumi kwenda sarafu ya kiyahudi kwani sarafu iliyoruhusiwa kutolea sadaka hekaluni ilikuwa sarafu ya Kiyahudi tu. Kadiri ya sheria ya sarafu ya kiruma ilikatazwa kutolewa kama sadaka kwa sababu ilikuwa na picha ya mtawala wa Roma. Lakini kwa vile walikuwa chini ya utawala wa kirumi, sarafu ya kiruma ilitumika katika biashara na maisha ya kawaida. Hivyo ilibidi kuibadilisha na kupata sarafu ya kiyahudi ili kutolea sadaka. Kwa hiyo baadhi ya wayahudi walifanya biashara hizi hekaluni.
Kumbe, kipindi hiki cha Pasaka ya Kiyahudi sehemu ya kwanza ya Hekalu ambayo ilikuwa kwa ajili ya watu wa mataifa ndiyo iliyotumika kwa biashara hizi zote. Ni katika hali hii Yesu anaingia Hekaluni ili apate kusali na anakutana na hali hii. Akatengeneza kikotoo cha Kamba, akawatoa wote nje, akapindua meza za wavunja fedha na kuwaambia; “Msiifanya nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya Biashara. Nyumba hii ni nyumba ya sala.” Ukatimia utabiri wa nabii Zakaria usemao; Katika siku hiyo hatakuwepo tena mfanyibiashara katika nyumba ya Bwana Mwenye Nguvu (Zak 14:21-22). Kumbe, kitendo cha Yesu kuwafukuza wafanya biashara hekaluni ni ishara ya kutimia kwa unabii na utabiri wa kimasiha. Ndiyo maana Wayahudi wanamuuliza kwa mamlaka gani na ni ishara ipi utakayotuonyesha kwamba unafanya haya? Wanataka kudhibitisha nguvu na uweza wake.
Yesu akawajibu; “Livunjeni hekalu hili na baada ya siku tatu nitalisimamisha (Yn 2:21). Jibu hili hawakulielewa hata mitume wake maana wao walifikiria Hekalu lililojengwa na Herode Mkuu. Hili ndilo Hekalu lilichukua nafasi ya sanduku la Agano liliashiria uwepo wa Mungu. Hivyo Wayahudi waliamini kuwa Mungu anapatikana katika Hekalu la Yerusalemu tu, ndiyo maana walipaswa kwenda huko kusali na kutolea dhabihu. Yesu anaongelea Hekalu jipya, ambapo dhabihu safi zitatolewa na kukubaliwa. Ndiyo maana Yesu alimwambia mwanamke msamaria; “Mama usadiki kuwa saa inakuja, ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu, ila wale waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli (Yn 4:21-24). Hekalu hili jipya ndio mwili wake. Maana ukamilifu wote wa uungu umo ndani ya Kristo katika umbile la mwili wa kibinadamu (Kol. 2:9). Yesu analilinganisha Hekalu la Yerusalemu na mwili wake, na hivyo anatufunulia fumbo la umwilisho la Mungu kuchukua mwili na kuja kukaa nasi na baada ya mateso, kifo, ufufuko na kupaa kwake mbingu, sasa Yesu yupo katikati yetu katiki Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.
Kwa Ubatizo sisi nasi tumekuwa hekalu la Roho Mtakatifu kama anavyotuambia Mtume Paulo; Je, hamjui kwamba Miili yenu ni Hekalu la Roho Mtakatifu? Na Yesu anasema; “Mtu akinipenda atalishika Neno langu na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao kwake (Yn 14:23). Kila mbatizwa ni sehemu ya Kanisa, ni sehemu ya Hekalu la Mungu. Miili yetu ni Hekalu la Mungu lililojengwa kwa thamani kubwa. Ndipo Mungu anapoabudiwa katika Roho na Kweli. Ubani, manemane na dhabihu ya kweli katika hekalu hili jipya ni matendo ya upendo kwa wahitaji, ukarimu kwa maskini, yatima, wajane, wafungwa, wagonjwa, walio uchi ambao utu wao unadhalilishwa kwa sababu ya dhambi na tamaa zetu. Hao ndio mwili wa Kristo. Kila tunapochukua hatua kumhudumia ndugu yetu mhitaji, harufu ya majitoleo yetu inaongezeka katika altare ya Mbinguni. Kumbe ndani ya Kristo, pamoja na Kristo na katika Kristo tunafanya Hekalu la Mungu kwani kwa ufufuko wake sisi sote tunafanywa kuwa na uhusiano mwema na Mungu.
Katika kipindi hiki cha Kwaresima Kanisa linatuhimiza kufanya bidii kubwa zaidi katika kusali, kufunga na kuwasaidia maskini na walio wahitaji. Ni kipindi maalum cha kufanya malipizi kwa dhambi zetu kwa kufanya toba. Tunaalikwa kusafisha mahekalu ya mioyo yetu kwa toba na kuondoa yale mambo ambayo tumefungamana nayo na kutufanya tukamsahau Mungu. Ni wakati wa kusafisha mahekalu ya roho zetu kwa toba na matendo ya huruma kwa wenzetu na kuyapamba kwa fadhila mbali mbali hasa fadhila kuu ya upendo. Mioyo yetu ni makao ya Mungu, ni mahali ambapo Mungu anaabudiwa. Kwa hiyo panapaswa kuwa safi. Tuanze kupindua meza za maovu kwa toba kwa kuwa maovu yanaharibu thamani ya makao ya Mungu. Ni wakati wa kufanya tathmini katika maisha yetu ya kiroho na kufanya malipizi ya dhambi zetu ili kuwa karibu zaidi na Mungu wakati tukijiandaa kuadhimisha mafumbo makuu ya wokovu wetu yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.