Tafakari Jumapili V Kwaresima: Yesu Kristo: Agano Jipya & Milele
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Tupo leo katika dominika ya 5 ya Kwaresima, dominika inayotangulia Juma Kuu. Ni dominika ambayo kadiri ya mapokeo Misalaba na sanamu zote hufunikwa. Hufunikwa sio tu kwa ajili ya kutupatia kiu ya kuziona ziking’ara wakati wa maadhimisho ya Pasaka bali pia ni kutukumbusha kuwa ni kutokana na dhambi zetu sisi Kristo aliingia katika mateso yake hayo, mateso ambayo ni dhamira kuu ya tafakari yetu katika kipindi hiki cha mwisho cha Kwaresima. Ufafanuzi wa Masomo ya Misa kwa ufupi: Somo la kwanza (Yer. 31:31-34) Katika somo hili la kwanza, Mwenyezi Mungu anatangaza kufanya Agano Jipya na watu wake. Anatangaza kufanya hivi kwa sababu anaona wazi kabisa kuwa lile agano la kwanza alilofanya nao mlimani Sinai wameshindwa kulishika. Na somo lenyewe linasema “agano langu hilo walilivunja ingawa nilikuwa mume kwao, asema Bwana”. Kinachothibitisha kuwa Waisraeli walilivunja agano hilo ni mazingira waliyopo katika kipindi hicho cha Yeremia. Wako utumwani Babeli, nje ya nchi yao ya ahadi. Kimsingi, kinachozungumzwa kama agano ni mahusiano ya pekee ambayo Mungu alikuwa ameyajenga na watu wake. Mahusiano yaliyoelezea ahadi yake kwa Abrahamu kuwa atakuwa Mungu wao na wao watakuwa watu wake. Ndiyo maana pia Biblia wakati mwingine inalielezea agano katika lugha ya ndoa ikimtaja Mungu kuwa mume.
Tunachokiona katika somo hili ni kuwa Mungu hapendi mahusiano hayo na watu wake yavunjike licha ya kuwa wao wameshindwa kushika Agano. Anatangaza kufanya agano jipya, yaani kufanya namna mpya atakavyoendelea kuhusiana na watu wake hao. Katika namna hii mpya anasema “nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika”. Hapa anarejea Agano la mlimani Sinai ambapo sheria yake aliaandika katika vipande vya mawe. Kumbe, Sheria ya Mungu ambayo katika Agano la Sinai iliandikwa kwenye mawe na Waisraeli wakapewa ni sheria hiyo hiyo ambayo sasa Mungu anaiandika katika mioyo ya watu. Maana yake ni kwamba Mungu anataka watu wahusiane naye – wamfuase si kwa msukumo kutoka nje bali kwa msukumo kutoka ndani yao wenyewe, ndani ya mioyo yao ambamo sheria ya Mungu sasa inaandikwa. Sisi ni watu wa Agano Jipya. Agano lililofungwa na Kristo Msalabani. Tunakumbushwa kuwa tunayo ndani ya mioyo yetu, katika dhamiri zetu nyofu sheria ya Mungu. Ile kiu ya kumtafuta Mungu (kumjua, kumpenda na kumtumikia) tunayo. Ile hofu ya Mungu imo ndani mwetu. Huenda tu ni pale ambapo tunaamua kwa utashi wetu wenyewe au kwa kuruhusu ukaidi utawale mioyo yetu ndipo hapo tunaigeuza mioyo yetu kutoka kuufata mkondo wake wa kawaida wa kumuelekea Mungu badala yake unafuata matakwa yetu sisi. Ni somo linalotupa mwaliko tuisikilize na tuifuate sauti ya Mungu inayozungumza ndani yetu, yaani dhamiri nyofu!
Somo la pili (Ebr. 5:7-9). Somo hili la pili kutoka Waraka kwa Waebrania linatupatia picha ya Yesu anayeteseka kwa mateso makali akiwa anayakabili mauti. Ni wakai mzito na mgumu kwa binanadamu yeyote. Katika wakati huo mgumu, somo linatuonesha kuwa Yesu alisali na aliendelea kuwa mtii kwa mpango wa Mwenyezi Mungu. Sala ya Yesu inaelezwa kuwa ilikuwsa ni maombi na dua pamoja kulia sana na machozi. Maneno haya yanaendana vizuri kabisa na mapokeo ya zamani sana ya kiyahudi kuhusu sala. Katika mapokeo hayo sala ilielezwa kuwa katika ngazi tatu. Ngazi ya kwanza ni ile sala ya kawaida, sala ambayo mtu anamtolea Mungu kimya kimya. Ngazi ya pili ni dua au sala ya kupaaza sauti. Ngazi ya tatu ni sala ya machozi. Hii ndiyo ilikuwa ni ngazi ya juu kabisa (Rej. V. Midr. Pesiq. R. 36). Sasa yote hayo matatu kuelezwa katika tukio moja tu la mateso ya Yesu, linalenga kutoa ujumbe kuwa Yesu aliyapokea mateso yake kwa njia ya sala. Alisali kikamilifu katika mateso yake kwa maana alipitia ngazi zote tatu za sala zilizofahamika. Ni mwaliko kwetu kuyapokea na kuyazamisha katika sala matukio magumu na mazito katika maisha.
Jambo la pili ni utii. Tunaonesha kabisa katika somo kuwa “ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo”. Yesu aliupokea wakati huo mgumu kama sehemu ya mapenzi ya Mungu na akaamua kujiweka pembeni, kujishusha ili Mungu huyo huyo achukue usukani na ampeleke pale anapotaka yeye kufika kwa njia ya mateso hayo. Ni fundisho kubwa la kujikabidhi ambalo somo hili linatupatia. Katika nyakati ngumu, sisi nasi tunaalikwa kujikabidhi kwa Mungu. Kuthubutu kumwambia Mungu, chukua wewe usukani wa maisha yangu na uyapeleke pale unapotaka wewe, najua utanipeleka mahala salama. Utii wa Kristo ni utii wa kuyapokea Mapenzi ya Mungu katika maisha.
Somo la Injili (Yoh. 12:20-33). Katika Injili ya leo, Kristo anatamka kuwa kuwa saa yake imefika, saa ya kutukuzwa kwake Mwana wa Adamu yaani saa yake ya kuingia katika mateso na kifo kwa ajili ya kuukomboa ulimwengu. Mara kadhaa katika injili hii ya Yohane Yesu mwenyewe amesikika akisema “saa yangu bado haijafika”. Na kwa sababu hiyo hakufanya baadhi ya vitu au hakuruhusu baadhi ya vitu vifanyike. Leo hapa anatamka kuwa saa hiyo sasa imefika. Yesu anatamka hilo mara tu baada ya kusikia kuwa kuna wayunani wanatafuta kumuona. Ni kana kwamba kitendo cha Wayunani, watu waliokuwa wanakaa nje ya Uyahudi, kuwa wameshasikia habari zake na kwamba wanamtafuta, kiliashiria tayari kusambaa kwa habari zake na pia kiliashiria utimilifu wa hiyo “saa yake”. Kisha akaanza kutoa mafundisho ya mwisho mwisho kabla ya kuingia katika hiyo saa. Katika mafundisho haya anaeleza kuwa kifo chake ni lazima ili ulimwengu ukombolewe. Ni kama vile mbegu inavyokufa ardhini ili baadaye kutoa mazao mengi. Kifo cha Kristo ni kifo kinachoanzia awamu mpya au agano jipya na kufungulia kuanza upya kwa mahusiano kati ya Mungu na watu wake kama alivyotabiri nabii Yeremia.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, maneno “nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika” ambayo yanasikika katika somo la kwanza leo, yananisukuma kutafakari pamoja nanyi fumbo la uwepo wa Mungu ndani ya nafsi zetu. Kuna swali katika ile Katekisimu Yetu linauliza Mungu yuko wapi? Au Mungu anapatikana wapi? Na jibu lake ni kuwa Mungu yuko mahali pote. Leo kupitia kinywa cha nabii Yeremia, Mungu mwenyewe anathibitisha kuwa yuko pote na zaidi anakumbusha kuwa yuko ndani ya mioyo yetu. Ameweka ndani yetu sheria yake, amepiga chapa ya uwepo wake katika mioyo yetu. Yupo na sisi. Yupo ndani ya dhamiri zetu njema. Tena wapo wanaoelezea hili kwa kusema kuwa kati ya vinasaba alivyonavyo mwanadamu kipo kimoja kinachomtambulisha Mungu na kumfanya mwanadamu kwa asili yake awe na hofu ya Mungu, awe na kiu ya kumtafuta Mungu na awe na msukumo wa asili wa kufanya yanayompendeza Mungu. Uwepo wa Mungu unaogopesha lakini pia uwepo wa Mungu unatuliza na kutupa nguvu.
Uhakika huu wa uwepo wa Mungu ndani yetu utupe kichocheo cha kutamani kumpendeza yeye katika mawazo yetu, katika maneno na katika matendo. Uwepo wake huu utupe pia uhakika kuwa Yeye anaona yote tunayopitia, anasikia yote tumuombayo na yupo ili kutusaidia. Uwepo wake huu utupe pia uhakika kuwa tunayo nguvu ndani yetu, nguvu inayotusaidia kupambana katika harakati mbalimbali ya safari ya maisha, uhakika wa kuvishinda vishawishi vinavyotusonga na uhakika wa kusonga mbele kwa matumaini. Naye Mungu aliyeamua kufanya makazi ndani yetu atujalie kufanana naye siku hadi siku.