Tafuta

Msalaba wa wokovu wetu Msalaba wa wokovu wetu 

Huu ndiyo mti wa msalaba ambao ni wokovu wa ulimwengu,njoni tuabudu

“Huu ndiyo mti wa msalaba ambao ni wokovu wa ulimwengu,njoni tuabudu”.Ni mwaliko wa kwenda kuheshima ukuu wa Kristo Bwana aliyetukomboa,kupitia msalaba wa Mateso siku ya Ijumaa Kuu.

Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican.

Wakati Mama Kanisa anajiandaa kufanya na kutimiza ishara muhimu ya kupendeza na ngumu ya kufunua na kuonesha Msalaba, katika Liturujia ya Ijumaa Kuu, unaimbwa wimbo wa kizamani sana na ambao labda ulianzia karne ya nane au ya tisa ya enzi yetu ya Ukristo. Lakini dhana ya kitaalimungu na ya imani iliyounganishwa na wimbo huo ni ya zamani zaidi, ikiwa badala ya kutafsiri ubao wa Msalaba, wanatumia neno la mti wa Msalaba. Wimbo huo kwa kilatino unasema "Ecce lignum crucis, in quo salus mundi pependit: venite, adoremus,yaani Huu ndiyo mti wa msalaba ambao ni wokovu wa ulimwengu, njoni tuabudu”.  Kiutamaduni huo wimbo unaimbwa mara tatu, wakifunua taratibu msalaba ambao kwa kawaida hufunikwa Kanisani hata picha zozote zinazoonekana na msalaba katika Dominika ya V ya kwaresima kabla ya Dominika ya Matawi katika baadhi ya makanisa. Katika barua ya Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti ya hati ya Paschalis sollemnitatis inayohusu maandalizi na maadhimisho ya Siku Kuu za Pasaka iliyoandikwa mnamo tarehe 16 Januari 1988 inatoa maelekezo kuhusiana na maadalizi ya kipindi chote siku hizp kuu ikiwemo hata suala la kufunika misalaba na picha Kanisani tangu Dominika ya V ya Kwaresima lakini hata kwa ushauri wa kuhifadhi  na kuendelezwa kwa sababu ya wema na kulingana na uamuzi wa maaskofu.

Msalaba kwa kawaida inabaki imefunikwa hadi mwisho wa sherehe ya Mateso ya Bwana na siku ya Ijumaa Kuu inafunuliwa na picha hizo mwanzo wa Mkesha wa Pasaka. Lakini hata hivyo kwa kuwa na mazoea mazuri, hiyo inaweza hata kushauriwa katika kila familia katoliki kufunika picha na misalaba muhimu ndani ya  familia zao ili iweze kusaidia hasa katika kuishi kipindi cha liturujia kuu hasa ikiwa mtu  hatuwezi kwenda kwenye Misa za kila siku katika juma hivyo siyo rahisi kugundua hili badala yake tukio la kufinikwa msalaba wanaliona kanisani labda mara moja au mbili kabla ya Pasaka na ndiyo maana linakuja swali la kuuliza nini maana yake ya kufunika msalaba. Pia zoezi hili linaaweza kuwa zuri na  utamaduni mzuri wa kupitisha kwa kizazi katoliki au kurithisha kizazi cha kujua vema ishara zifanyikazo Kanisa hasa katika ibada hii kuu ya msalaba wa wokovu.

Ndugu msomaji huu ndiyo mti wa msalaba ambao ni wokovu wa ulimwengu, njoni tuabudu. Mababa wa Kanisa tufikirie tu juu ya Mtakatifu Ambrose na Augostino ambao walikuwa wakilinganisha mti wa Msalaba na mti wa Edeni. Ulinganisho wao ulikuwa ukitofautisha kati ya mti wa Edeni ulioning’inzwa tunda lililosababisha hukumu yetu, wakati Mti wa msalaba ulining’inizwa tunda ambalo lilituongoza kufikia wokovu wetu. Asili ya mti wa Msalaba na kwa sababu hiyo tunda ambalo hutegemea kutoka kwake ni kiini tofauti kabisa na kile kilichoashiria mwanzoni mwa historia yetu ya kutotii na umbali wetu kutoka kwa Mungu. Kwa sababu hiyo, ikiwa kwa kutotii kwa Adamu wa kwanza, tunda la hukumu yetu lilinyang'anywa kutoka katika mti wa Edeni, na kwa utii wa Adamu mpya tunda la wokovu wetu liling'olewa kutoka mti wa Msalaba, ambalo katika hali ambayo hatuelewi zaidi lakini ya kupendeza na kushangaza inafanana na Adamu mpya huyo huyo, ambaye ni Kristo na ni ndilo tunda. Ni yule ambaye kwa kutii anachukua wokovu ambao unatoka kwa Mungu na kwa hali halisi ni mtu yule yule, yaani Bwana mmoja Yesu Kristu, mwana wa pekee wa Mungu. Aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bila kuumbwa, mwenye umungu mmoja na Baba,  tunasali katika (Kanuni ya Imani ya NICEA).

Huu ndiyo mti wa msalaba ambao ni wokovu wa ulimwengu, njoni tuabudu. Licha ya kujua wazo hilo la utofauti wa mti wa edeni na mti wa msalaba na matunda yake ndugu msomaji, tukumbuke jinsi ambavyo katika Agano la Kale, Bwana alimwambia Musa, “Tengeneza nyoka wa shaba, umtundike juu ya mlingoti. Mtu yeyote atakayeumwa na nyoka, akimtazama nyoka huyo wa shaba, atapona.” (Hes 21:8). Hii ni kutokana na dhambi za watu wa Israeli waliokuwa jangwani na kuanza kuendelea kuasi Mungu. Kwa mfano huo tayari unakupatia picha halisi ya wokovu wa Yesu msalabani kwa maana nyoka ya shaba katika Agano la kale ndiye  anakuwa mtu msalabani katika Agano jipya na kwa kila ainuaye kichwa na kikiri mwana wa Mungu anapata wokovu! Tukirudi katika tunda, ni kuwaza utamu wa kuonja na wakati huo hapa tuwaze tunda linazungumzia maisha si uchungu na kifo. Pamoja na hayo yote fumbo lilisiloeleweka kwa mwandamu la mapenzi ya Mungu hata mti wa msalaba unatoa tunda. Na zaidi ya utunda linatoa maisha tele au ya milele.

Tunajua kuwa haipendezi kula tunda la mti wa Msalaba, kwa sababu “halina uzuri wa kuvutia macho yetu, wala fahari ya kuweza kutupendeza, kama  wimbo wa nabii Isaya katika somo la kwanza lisomavyo siku ya mateso.  "lakini atafanya hivyo kuishi muda mrefu na uone uzao. Yeye ana uwezo wa kuzaa matunda ya mti wa Msalaba. Mwili wake ulisukumwa na kupigwa, kukatwakatwa na kuuawa na kuwa shahidi, alivuliwa kwa aibu na kufedheheshwa na vazi lake, uso wake ukafunikwa na mate na kuchafuliwa, kichwa chake kilivikwa na taji la miiba mikali, mikono na miguu yake ilichomwa misumari ya kutisha, inasema Zaburi 21,15. Tangu wayo wa mguu hata kichwani hamna uzima ndani yake; bali jeraha na machubuko na vidonda vitokavyo usaha; havikufungwa, wala havikulainishwa kwa mafuta (Is 1,6). Huyo ndiye kweli anaelezwa mtumishi wa Mungu ambaye anaelezwa na nabii  Isaya. Kwa hakika Isaya ni Nabii ambaye aliitwa  pia kama Injili ya tano, na ambaye anamwakilisha mtumishi wa Mungu katika wimbo huo, picha halisi ya Mateso ya mtumishi wa Mungu na hali halisi ambayo kweli baadaye inajionesha wazi kwa macho ya mwili na ya roho. Kwa maana hiyo mateso ya Kristo katika aya za Isaya zinagusa hisia zetu kama zile za wainjili wote na ndiyo kweli uwakilishi wa Mtu wa mateso ya kweli.

Ndugu Msomaji, hii inakupeleka kuona ishara ya wimbo wetu Huu ndiyo mti wa Msalaba ni wokovu wa ulimwengu, njoni tuabudu. Ni wito wa kukumbusha kile kilichotokea baada ya kusalitiwa na Yuda, walifika maaskari wakamkamata na mchakato mzima ambao unasikika katika Injili, hadi mauti msalabani (Yh 18:1-42).  Zaburi na Wimbo wa Isaya vyote viko wazi kuonesha ishara kuu zinafunuliwa kabla ya kuabudu msalabani na kukaribishwa mara tatu ili kufika na  kumwabudu mwokozi wetu aliyetukomboa akiwa msalabani. Mara tatu inatukumbusha ishara ya Utatu Mtakatifu kwa maana ni Mungu Baba, ni Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu ambaye anakamilika katika nafsi tatu. Ni mara tatu kwa kutukumbusha Yesu alivyosema wakati wa alipokuta hekalu linafanyiwa biashara: “Livunjeni Hekalu hili, nami nitalijenga tena kwa siku tatu!” (Yohana 2:19); kama hiyo haitoshi, Yesu mwenyewa alisema: “kama jinsi Yona alivyokaa siku tatu kutwa kucha tumboni mwa nyangumi, ndivyo naye Mwana wa Mtu atakavyokaa ndani ya ardhi siku tatu kutwa kucha (Mt 12,40). Ni ukamilifu wa Yesu ambaye ni Mungu mtu na ambaye tunaalikwa kumwabudu katika mti wa msalaba.

Ndugu  msomaji , “Huu ndiyo mti wa msalaba ambao ni wokovu wa ulimwengu, njoni tuabudu”, inaa maana kubwa kumwabudu huyo aliye tukomboa msalabani. Hii pia inamaanisha kwamba maisha yetu yamezungukwa na misalaba, ya kila saizi zote, sifa zote, uzito wowote na umbo lolote, wa aina yoyote ya muda na masaa na huwezi kukwepa labda kama siyo mwanadamu. Sisi sote tuna misalaba kwenye mabega yetu, kila mmoja wetu na kila mmoja tofauti na wakati mwingine zaidi ya mmoja lakini wote ambao wameumbwa na Mungu. Ni misalaba kweli, yote ni mizito, hakuna iliyo nyepesi au rahisi ya kubeba, kwa maana nyingine iliyo mingi tunaweza kusema kwamba ni kuvumilia tu. Watoto, vijana na wazee, wote hakuna mtu anayetengwa au kubaguliwa na msalaba, maskini na tajiri. Hakuna mtu anayeweza kulalamika zaidi ya mwingine, hakuna anayeweza kujifariji kuliko wengine, msalaba unagusa kila mtu, mapema au baadaye, lazima ukufikie. Na juu ya yote, hakuna mtu anayeweza kuitikisa kwa urahisi kwa kusema, haijalishi kwangu, siitaki. Sio lazima hata kuitafuta kwa maana misalaba yetu tayari ipo. Tunayo kwenye mabega yetu kabla hata hatujagundua na tunapoitambua tayari imechukua sura ya mwili wetu na maisha yetu! Ni sehemu ya historia maana umebatizwa katika maji na Roho Mtakatifu na kushiriki na Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka siku ya tatu kama ilivyo andikwa na manabii. Ndiyo taalimungu ya Msalaba.

Huu ndiyo mti wa msalaba ambao ni wokovu wa ulimwengu, njoni tuabudu, pamoja na hayo yote lazima kutambua wazi kuwa msalaba ni mti unaozaa matunda. Sio ya kupendeza sana kula, lakini hapo ndipo matunda huzaliwa. Na ubinadamu uliigundua tangu siku ile ya Ijumaa Kuu alasiri, siku  ya kila Ijumaa kuu kwa maaana ya mwaka huu 2021ambapo kutoka katika msalaba mmoja wa  bustani ya ubinadamu ulipandwa,  tunda lilining'inizwa ambalo ni wokovu wa ulimwengu na tangu wakati huo, hakuna msalaba ambao haukuzaa matunda, hakuna mateso ambayo yaliweza kudhuru mtu na wala hakuna ubaya ambao unakuja kudhuru, hakuna maumivu ambayo hayasafishwi, hakuna sadaka ambayo haitasikilizwa, hakuna chozi ambalo halitazaa matunda. Kwa sababu Mungu alichangua njia hiyo ya kumtundika mwanae kama tunda katika mti wa Msalaba. Na hivyo kweli hatuna budi kuimba Huu  ndiyo mti wa msalaba ambao ni wokovu wa ulimwengu, njoni tuabudu. Ni Mwana na Mungu kweli ambaye alishinda mauti kwa ajili yetu. Kifo hakina neno la mwisho kwa binadamu.

Ndugu Mpendwa ni wapeleke tena katika ushuhuda mwingine wa dhati wa uchungu na mateso ya msalaba, ambao aliuishi kwa dhati hadi kifo chake.  “Kanisa ambalo linazaliwa na Fumbo la wokovu wa Msalaba wa Kristo linatakiwa kujaribu kukutana na mwanadamu kwa namna ya pekee katika njia ya mateso”, anaandika Mtakatifu Yohane Paulo II katika Barua yake ya Kitume ya “Salvifici Doloris” yaani, “Mateso ya wokovu”, ya 1984” akiwalenga Maaskofu, makuhani, watawa Kike na kiume na waamini walei katoliki kuhusu maana ya Ukristo katika mateso ya mwanadamu. Yeye aliyeishi uzoefu wa mateso makali anasema “mateso ni kama hija ya safari ya huruma. Mateso pia ni jambo pana zaidi ya ugonjwa, ni ngumu kuelewa  kwa kina yanayoukumba   ubinadamu wenyewe. Na kwa haya mateso yanasababisha kujiuliza swali juu ya ubaya. Je nini  maana ubaya? Swali ni kuuliza Mungu katika moyo wake na akili ya mshango kwa maana Mungu anasubiri swali na anasikiliza.  Ni kwa sababu inaonesha  ufunuo wa jibu lake kupitia  Agano la Kale katika kitabu cha Ayubu”.  Vile vile Mtakatifu Yohane Paulo II anakumbusha maneno ambayo Kristo alimwambia Nikodemu wakati wanazungumza naye usiku kwamba: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yn 3:16-17), ikiwa na maana ya kutanguliza kitovu chenyewe cha mateso ya wokovu wa Mungu.

Ni maneno ambayo yanafafanua kwa mkristo taalimungu ya wokovu. Wokovu maana yake ni uhuru dhidi ya ubaya na kwa maana hiyo upo uhusiano mkubwa wa shida ya mateso.  Mtu hufa anapopoteza uzima wa milele. Kinyume cha wokovu kwa hivyo sio mateso ya muda tu, yaani mateso yoyote yale, bali mateso dhahiri: kupoteza uzima wa milele, kukataliwa na Mungu, na laana". Katika Waraka wa Kiitume wa Mtakatifu Yohane Paulo II anaendelea kuandika kuwa: "Wale wanaoshiriki katika mateso ya Kristo huwekwa katika mateso yao chembe maalum sana ya hazina isiyo na kikomo ya ukombozi wa ulimwengu, na wanaweza kushirikishana hazina hii na wengine. Kadiri mwanadamu anavyotishiwa na dhambi, ndivyo miundo ya dhambi ilivyo nzito ambayo ulimwengu wa leo umebeba ndani yake, na ndivyo unavyozidi kuwa ufasaha ambao mateso ya wanadamu wanayo wenyewe. Na ni kadri Kanisa linavyohisi zaidi hitaji la kukimbilia thamani ya mateso ya wanadamu kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu Na tunawaomba ninyi nyote mnaoteseka, kutuunga mkono. Na zaidi ninyi nyote  ambao  ni wadhaifu, muwe chanzo cha nguvu ya Kanisa na kwa ajili ya  wanadamu. Katika vita ya kutisha kati ya nguvu za mema na mabaya, ambayo ulimwengu wetu wa kisasa unatupatia, mateso yenu yashinde kwa muungano na Msalaba wa Kristo!”(Kutoka waraka wa Kitume wa Salvifici Doloris wa Mtakatifu Yohane Paulo II, 1984).

Ndugu msomaji, hadi hapo badi tuzungumze nafsini mwetu kwa uwazi je ni nini maana ya msalaba kwako? je unapofikiria msalaba wazo gani linakujia akilini?  hasa baada ya kusikiliza hayo yote? Sidhani kama unaweza kufikiria jambo zuri na chanya kwa haraka maana hupo katika shule ili uweze kuingia kwenye muktadha huu wa mateso ya msalaba na ambao ndiyo njia pekee ya kupta wokovu! Mara ngapi unajikuta unasema nina misalaba mingi ... ninayokutana nayo ni mingi na si kwa sababu ya kusifia, lakini ukiwa ni kwa masikitiko ya kibiandamu. Msalaba kwa hakika unatupelekea katika jambo gumu, mateso sadaka, ugumu wa magonjwa, uchungu hadi kufikia kifo, lakini kwa utambuzi kuwa ndiyo njia pekee ya wokovu na hakuna nyingine iliyochaguliwa kufika maisha ya milele. Mwaka 2020-2021, ulimwengu mzima huko unafanya uzoefu wa mateso, maombolezo na misalaba, shida nyingi za kiafya, kiuchumi na kijamii. Msalaba mzito na uchungu wa kufiwa na wapendwa kwa mfano halisi nchini Tanzania hivi karibuni tumepata msiba wa kuondokewa na rais wetu mpendwa Dk. John Pombe Magufuli. Siwezi kubisha binafsi hata kwa wale niliowasikia au kuona kwenye vyombo vya habari tulihisi uzito wa msalaba kundokewa na kiongozi wetu tuliye mpenda sana.

Ni kama vile hatukupendezwa na mapenzi ya Mungu na kama vile hatukuwa tofauti ya Petro baada ya Yesu kuwatangazia kifo na mateso yake, Petro alikataa kwamba jambo hilo halitatokea. (Mt 16, 21-23). Kumbe tunapaswa kulipokea kwa maana ni kama mbegu iliyopandwa, ambayo isipokufa haiwezi kutoa matunda na kila mmoja atakufa maana sisi sote ni mavumbi na mavumbi tutarudi. Ni mfano halisi ambao unaonesha mateso ya kiroho na kimwili. Ni wakati huu, ni kipindi muafaka cha siku hii ya Ijumaa kuu 2021 kutafakari zaidi kwa kuamini kuwa “Huu ndiyo mti wa msalaba ambao ni wokovu wa ulimwengu, njoni tuabudu”. Ni wito mbao kutokana na uzoefu wa vifo tilivyo viona nyakati hizi vinaweza kuwa fursa ya kujiandalia nasi kifo chema. Kila tuamkapo na kabla ya kulala tuutazame msalaba na kusema Huu ndiyo mti wa msalaba ambao ni wokovu wa ulimwengu, njoni tuabudu”.  Hakuna njia nyingine ya kufikia uzima wa Milele ni kupitia katika msalaba. Kuubeba pamoja naye , kufa pamoja naye lakini siku ya tatu kuna ufufuko. Ninawatakia Ijumaa Kuu njema, Jumamosi njema na Pasaka njema!

01 April 2021, 16:41