Jumapili ya Huruma ya Mungu: Picha na Rozari ya Huruma ya Mungu!
Na Padre Wojciech Adam Kościelniak, - Kiabakari, Musoma, Tanzania.
Madhabahu ni mahali muafaka pa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni mahali pa toba na wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kuchuchumilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha, kama chachu ya utimilifu na utakatifu wa maisha. Haya ni maeneo muhimu katika maisha na utume wa Kanisa. Kituo cha Hija Kitaifa cha Huruma ya Mungu, Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma kimeendelea kuwa kweli ni shule ya sala inayokita mizizi yake katika huruma ya Mungu, toba na wongofu wa ndani. Padre Wojciech Adam Kościelniak, Muasisi wa Kituo cha Hija Kitaifa cha Huruma ya Mungu, Kiabakari katika mkesha wa Jumapili ya Huruma ya Mungu, 10 Aprili 2021, amefafanua kuhusu: Umuhimu wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwamini; ahadi ya huruma ya Mungu inayosimikwa katika: toba na wongofu wa ndani; maadhimisho ya Ekaristi Takatifu kwa ibada na uchaji pamoja na wito wa kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Ametoa maelezo kuhusu Picha ya Huruma ya Mungu sanjari na Rozari ya Huruma ya Mungu kwa mahujaji wanaoendelea kumiminika Kituoni hapo kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Wapendwa Mahujaji, Katika Shajara ya Mtakatifu Maria Faustina Kowalska tunakuta kurasa kama kumi na nne hivi zenye maneno ya Bwana Yesu akimwelezea umuhimu wa "Sikukuu ya Huruma" kwa Kanisa. Yesu anasema: “Sikukuu hii ilichipuka kutoka kwenye kina cha Huruma yangu na imethibitika imara katika kina kirefu na kipana cha Moyo wangu wenye Huruma nyingi.” (420) “Natamani iadhimishwe Jumapili ya Pili ya Pasaka (…) Natamani sikukuu ya Huruma iwe kimbilio na kinga kwa roho zote - hasa wadhambi. Siku hiyo kina cha Huruma yangu ki wazi. Namwaga bahari nzima ya neema kwa roho zote zinazokaribia chemchemi ya Huruma yangu.” (699). Kutukuza Picha: Picha ya Yesu, Mfalme wa Huruma, haina budi kupewa heshima ya pekee siku hiyo na kutukuzwa; iwe ni ukumbusho unaoonekana kwa yale ambayo Bwana Yesu alitutendea kwa Mateso, Kifo na Ufufuko wake na itukumbushe wajibu wetu kwake - kumwamini na kumtumainia na kuwa na huruma kwa wengine. “Nataka picha hii ibarikiwe rasmi siku hiyo - Jumapili ya Pili ya Pasaka; nataka vilevile itukuzwe na kuheshimiwa hadharani ili kila roho iijue.” (341).
Ahadi Maalum ya Huruma: Ahadi ya Bwana wetu ya kutoa msamaha kamili wa dhambi na adhabu zake zote kwenye Sikukuu ya Huruma imeandikwa kwa namna tatu katika kitabu cha Mt. Sista Faustina - na kila moja inatofautiana na nyingine kidogo (kwa maneno): “Nataka kutoa msamaha kamili kwa roho zitakazoungama na kupokea Komunyo Takatifu kwenye Sikukuu ya Huruma yangu.” (1109). “Yeyote atakayekaribia chemchemi hii ya Uzima kwa siku hiyo atapata msamaha kamili wa dhambi na adhabu zake.” (300). “Roho itakayoungama na kupokea Komunyo Takatifu itapata msamaha kamili wa dhambi na adhabu zake.” (699). Kwa nini Bwana wetu alipenda kusisitiza jambo hili? Ni kwa sababu watu wengi hawaelewi. Wengi hawapokei Komunyo Takatifu na wengine huipokea vibaya. Kama asemavyo Mt. Paulo katika Waraka wake wa Kwanza kwa Wakorintho kuhusu Mkate na Kikombe cha Bwana - wanakula na kunywa "bila kujua na kutambua kuwa ni Mwili na Damu ya Bwana" (1 Kor 11:27-29). Bwana wetu alimdhihirishia Sista Faustina katika matokeo yake kile anachotupatia na kutujalia katika Komunyo Takatifu na jinsi anavyoumia tunapompokea bila kujali: “Furaha yangu kubwa ni kujiunganisha na roho za watu... Ninapoingia moyoni mwa mtu katika Komunyo Takatifu, mikononi mwangu mnakuwamo aina zote za neema nipendazo kutoa kwa roho hiyo. Lakini roho zenyewe hazionyeshi kunijali Mimi; zinaniacha mwenyewe, zinajishughulisha na mambo mengine. Inanisikitisha na kunihuzunisha sana kwamba roho hizi haziutambui Upendo!
Wananiona kama kitu, kisicho na uhai: dude…!" (1385). “Inaniumiza sana mtawa au Padre anapopokea Sakramenti ya Mapendo bila kujiandaa, kana kwamba ni chakula kama kinginecho. Ndani ya roho zao sioni imani wala mapendo. Naziendea roho hizo kwa ubaridi. Ingekuwa heri kama zisingenipokea kabisa.” (1258). “Ni maumivu yaliyoje kwangu kwamba mara chache sana watu huungana nami katika Komunyo Takatifu. Nawangoja, lakini hawanitaki. Nataka kuwamwagia neema zangu, lakini hawataki kuzipokea. Wananiona kama dude tu, wakati Roho yangu imejaa Mapendo na Huruma. Ili mweze kujua walau kidogo jinsi ninavyoumia, fikirini ni jinsi gani watoto wamekuwa wakidharau pendo la mama yao mwenye huruma na mpole jinsi anavyoumizwa nao. Hakuna aliye tayari kumfariji. Lakini huwezi kufananisha upendo wangu na huu.” (1447). Hivyo, ahadi ya Bwana wetu ya msamaha kamili ni ukumbusho na wito kwetu. Inatukumbusha kwamba Yu mzima kweli katika Ekaristi Takatifu, amejaa mapendo kwetu na anatungoja tumrudie kwa matumaini. Anatuita ili tuoshwe na kusafishwa katika Pendo lake tunapopokea KITUBIO na KOMUNYO TAKATIFU haidhuru tu wadhambi kiasi gani na KUANZA MAISHA MAPYA. Anatupatia mwanzo mpya, ukurasa mpya safi.
Tufanye nini ili tuweze kujipatia neema hizo? Wanataalimungu makini wanaendelea kujibu: "Kwa kuwa MATUMAINI ndiyo njia ya kuikaribia Huruma, hatuna budi kusema kuwa maana halisi ya ahadi zinazoambatana na Sikukuu ya Huruma ni hii ifuatayo: katika Sikukuu hii Yesu apenda kutujalia sote - hasa wadhambi - wingi usio wa kawaida wa neema zake. Na kwa sababu hii, anatungoja siku hiyo tuikaribie Huruma yake kwa matumaini yote tuwezayo". Jitayarishe Vizuri: Kwenda kuungama si njia pekee ya kujiandalia Sikukuu hii. Kama Mwadhama Kardinali Macharski aendeleavyo kueleza katika barua yake, hatuitwi ili kuomba Huruma ya Mungu kwa matumaini tu; tunaitwa pia kuwa na huruma: "Huruma iliyo mioyoni mwetu nayo vile vile ni matayarisho. Bila matendo ya huruma ibada yetu haitakuwa halisi; kwa kuwa Kristo hafunui tu Huruma ya Mungu, bali pia huwadai watu waonyeshe upendo na huruma katika maisha yao. Mt. Yohane Paulo II anatamka kwamba hitaji hili ni kiini cha Ujumbe wa Injili (Tajiri wa Huruma, 3) na ni amri ya Upendo na ahadi: 'Heri wenye huruma, kwa maana watapata huruma' (Mt 5:7). Basi, na iwe huruma ya kweli na inayosamehe, huruma kwa wote, kwa matendo na maneno mazuri na kwa kuwaombea wengine".
Maneno ya Bwana wetu kwa Mtakatifu Sista Faustina Kowalska kuhusu hitaji hili la kuwa na huruma ni mazito na hayawezi kutafsiriwa vinginevyo: “Ndiyo, Jumapili ya pili ya Pasaka ni Sikukuu ya Huruma, lakini vile vile lazima matendo ya Huruma yawepo (…) Nawadai matendo ya huruma yatokanayo na upendo wenu kwangu. Hamna budi kuonyesha huruma kwa jirani zenu kila wakati na kila mahali. Hamwezi kukwepa au kujitetea au kujitoa kwa visingizio vyovyote vile.” (742). Hivyo, ili kuishika na kuiadhimisha ipasavyo Sikukuu ya Huruma, hatuna budi:
1. Kuiadhimisha Dominika ya Pili ya Pasaka.
2. Kutubu dhambi zetu zote na kujibandua nafsi na mazoea yote ya dhambi.
3. Kumtumainia kabisa Bwana wetu.
4. Kuungama, ikiwezekana kabla ya Dominika yenyewe.
5. Kupokea Komunyo Takatifu siku yenyewe.
6. Kutukuza, kuheshimu Picha Takatifu ya Yesu, Mfalme wa Huruma.
7. Kuwa na huruma kwa wengine - kwa matendo, maneno na sala zetu kwa niaba yao. Sisi, katika ratiba nzima ya hija yetu, tutatimiza vipengele vyote hivi kama tufanyavyo wakati wa Sherehe ya Huruma ya Mungu. Aidha, kwa vile si wote wawezavyo kushiriki Sherehe ya Huruma ya Mungu kila mwaka hapa Kiabakari, ni vema katika kila Parokia wachungaji wahakikishe kwamba taratibu zote sahihi za maadhimisho haya zinaandaliwa na kufuatwa kikamilifu.
MAELEZO KUHUSU PICHA YA YESU WA HURUMA NA ROZARI YA HURUMA: PICHA TAKATIFU: Mnamo mwaka 1931, Bwana wetu alimtokea Mt. Sista Faustina katika maono. Sista Faustina alimwona Yesu akiwa amevaa vazi jeupe, mkono wake wa kuume umeinuliwa kubariki; mkono wake wa kushoto ulikuwa umegusa vazi lake kifuani kwenye sehemu ya Moyo ambamo miali miwili mikubwa ya mwanga ilitokea - mmoja mwekundu, mwingine kama maji. Alimwangalia Bwana kwa makini sana akiwa kimya na roho yake ilijawa mshangao, ukichanganyikana na furaha kubwa. Yesu akamwambia: “Chora picha kama unavyoiona hapa na chini yake uandike maneno haya: ‘Yesu, nakutumainia!’ Naahidi kwamba roho yoyote itakayotukuza picha hii haitaangamia kamwe. Naahidi pia ushindi kwa maadui wa roho hiyo walio duniani humu, hasa saa ya kifo chake. Mimi mwenyewe nitailinda kama utukufu wangu.” (47,48) “Nawapatia watu chombo watakachotumia kila mara wajapo kupata neema kwenye chemchemi ya Huruma yangu. Chombo hicho ni picha hii na maneno: ”Yesu, nakutumainia!” (327) “Napenda picha hii itukuzwe, kwanza kwenye kikanisa chenu na baadaye duniani kote.” (47).
Baba yake wa kiroho alimwomba Mt. Sista Faustina amuulize Bwana wetu maana ya miali hiyo kwenye picha. Sista Faustina alijibiwa kwa maneno haya: “Miali hiyo miwili humaanisha Damu na Maji. Miali ya maji ni kwa ajili ya Maji yale yatakasayo roho na kuzifanya zenye haki; miali myekundu humaanisha Damu ambayo ni uzima wa roho. Miali hii miwili ilichomoza toka kwenye Moyo wangu wenye Huruma siku ile nilipochomwa kwa mkuki Moyoni pale Msalabani... Heri atakayefunikwa na miali hiyo, mkono wa Mungu wenye haki hautamgusa.” (299) “Nitazipa roho neema nyingi kwa kutumia picha hii. Iwe ni ukumbusho wa madai ya Huruma yangu, kwani hata imani kali kiasi gani bila matendo haina maana.” (742). Picha hii imeishachorwa na mafundi wengi mbalimbali, lakini Bwana Yesu alisema wazi kuwa usanii au ufundi wa uchoraji si jambo muhimu. Mt. Sista Faustina alipoona kwa mara ya kwanza ile picha iliyochorwa kwa maelekezo yake alilia na kuduwaa huku akimlilia Yesu: "Ni nani awezaye kukuchora na kuonyesha uzuri ule ule ulionao?"(313). Baadaye alisikia maneno haya: "Ukuu wa picha hii hauko katika rangi wala kifaa kilichotumika kuichora, wala ufundi, bali katika Neema yangu" (313).
ROZARI YA HURUMA YA MUNGU: Chombo cha pili cha kutuunganisha na Huruma ya Mungu na zana maalum aliyotukabidhi Yesu mwenyewe kupitia kwa Mt. Sista Faustina - ni Rozari ya Huruma. Mnamo mwaka 1935, Mtakatifu Sista Faustina alipata maono ya Malaika wa Bwana aliyetumwa kuangamiza mji fulani. Sista Faustina akaanza kuomba HURUMA, lakini sala zake hazikuwa na nguvu yoyote. Ghafula, akaona Utatu Mtakatifu na nguvu ya neema ya Yesu ikamjia. Wakati huo huo alijikuta anamwomba Mungu Huruma yake kwa maneno aliyoyasikia ndani ya moyo wake: “Baba wa milele, ninakutolea Mwili na Damu, Roho na Umungu wa Mwanao Mpenzi, Bwana wetu Yesu Kristo, kwa kulipia dhambi zetu na dhambi za dunia nzima; kwa ajili ya Mateso makali ya Yesu, utuhurumie sisi na dunia nzima “ (476). Alipokuwa anaendelea kusali sala hii, Malaika alionekana kushindwa kutimiza adhabu hiyo (taz. Shajara, nn. 474 na 475).
Siku ya pili yake, alipokuwa anaingia kanisani alisikia tena moyoni mwake sauti ikimfundisha jinsi ya kusali sala hii ambayo Bwana wetu aliita "ROZARI YA HURUMA". Tangu siku hiyo, aliendelea kusali sala hiyo bila kukoma, akiitoa hasa kwa ajili ya wanaokufa. Katika mafunuo mengine, Yesu alimdhihirishia kuwa Rozari hiyo haikuwa yake hasa, bali ilikusudiwa kwa ajili ya dunia nzima. Alitoa pia ahadi zisizo za kawaida kwa wale watakaoisali: “Uwatie watu moyo ili wasali Rozari hii niliyokupatia.” (1541) “Yeyote atakayeisali atapata Huruma Kuu saa ya kufa.” (687) “Watakaposali Rozari hii mbele ya mtu anayekufa, nitasimama kati ya Baba yangu na mtu huyo, si kama HAKIMU mwenye haki, bali kama MWOKOZI mwenye Huruma.” (1541) “Mapadre wawatolee wadhambi sala hii kama matumaini yao ya mwisho na wawafundishe hivyo. Hata mtu angekuwa na dhambi nyingi au roho ngumu kiasi gani, asalipo Rozari hii hata mara moja tu, atapata neema zangu zisizo na mipaka.” (687) “Natamani kuzigawia neema nyingi sana, roho zote zinazoitumainia Huruma yangu.” (687) “Rozari hii itakupatia kila kitu, iwapo maombi yako hayatapingana na mapenzi yangu.” (1731).
Inaposaliwa kwa kutumia Rozari ya kawaida, ROZARI YA HURUMA YA MUNGU ni sala ya maombezi yenye nguvu ya kuongeza ukuu wa Sadaka ya Ekaristi, hivyo inafaa sana isaliwe baada ya kuwa mtu amepokea Komunyo Takatifu kwenye Misa Takatifu. Inaweza kusaliwa wakati wowote, lakini Bwana wetu alimwambia Mtakatifu Sista Faustina kuisali siku tisa kabla ya Sikukuu ya Huruma ya Mungu. Na alisema: "Kwa Novena Hii, Nitazipatia Roho Neema Zote Zinazowezekana" (796). Natumaini sote tunajua tayari kusali Rozari ya Huruma, sivyo? Thamani ya pekee ya Rozari ya Huruma ya Mungu: Katika mtazamo wa siku hizi wa watalaam wengi wa taalimungu na wa Ujumbe na Ibada ya Huruma ya Mungu, Rozari ya Huruma ya Mungu haina budi kuangaliwa upya na thamani yake ya pekee kugunduliwa kwa faida ya Kanisa zima.
Watalaam hao wanasema kwamba kila mwamini anayesali kwa uchaji Rozari ya Huruma anatimiza Ukuhani wa Mkristo utokanao na Ubatizo wake na kimsingi anatenda yale ayatendayo Kuhani altareni anapogeuza mkate na divai kuwa Mwili wa Bwana na Damu yake Azizi. Si kwamba, mkristo ana uwezo wa kutenda Mageuzo kama Padre wakati wa Misa, lakini kwa kusali Rozari ya Huruma anatimiza kikamilifu Ukuhani wake utokanao na Ubatizo wake na kumtolea Mungu mwenye Huruma sadaka ya Bwana wetu Yesu Kristo aliyoitoa Msalabani siku ya Ijumaa Kuu akiyatamka maneno haya: ‘Baba wa milele, ninakutolea Mwili na Damu, Roho na Umungu wa Mwanao Mpenzi, Bwana wetu Yesu Kristo, kwa kulipia dhambi zetu na dhambi za dunia nzima.” Hivyo, waamini wote wanapaswa kupokea upya zawadi hiyo ya Rozari ya Huruma ya Mungu kama chombo kinachowawezesha kutumiza Ukuhani wao wa Ubatizo Mtakatifu na kugeuza maisha yao kuwa sadaka safi kwa Mungu iliyounganishwa kikamilifu na Sadaka ya Yesu Mfalme wa Huruma.