Jumapili ya Kuombea Miito Duniani: Sifa za Mchungaji Mwema!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika kipindi hiki cha Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Kristo Yesu, Mchungaji mwema. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Miito Ulimwenguni, tarehe 25 Aprili 2021, unanogeshwa na kauli mbiu “Mtakatifu Yosefu Ndoto ya Wito”. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa: Ndoto, huduma na uaminifu; mambo msingi katika kukuza na kudumisha miito mbalimbali ndani ya Kanisa. Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Miito Duniani yanakwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu uliozinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na yanatarajiwa kufungwa kwa kudemka hapo tarehe 8 Desemba 2021. Yote haya yamo kwenye Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu.
Kristo Yesu tangu mwanzo wa maisha na utume wake, aliwaita, akawachagua na kuwatuma Mitume kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote wa Mataifa. Rej. Mk. 3:14. Aliwataka wawe ni wasaidizi wake wa karibu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: haki, amani, upendo na mshikamano na kwamba, angekuwa pamoja nao hadi utimilifu wa dahali. Dhamana na utume huu wa Kanisa unaendelezwa na Wabatizwa wote, lakini kwa namna ya pekee kabisa na wakleri pamoja na watawa, miito ambayo inapata chimbuko lake katika maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Miito Duniani, anamweka Mtakatifu Yosefu mbele ya macho ya wakleri na watawa kama mfano bora wa kuigwa katika: ndoto, huduma na uaminifu. Haya ni mambo yanayoweza kumpatia mwamini furaha na upendo wa kweli unaotoa maana ya maisha na kumwilishwa katika huduma.
Ndoto za Mtakatifu Yosefu ziligeuka na kuwa ni zawadi ya maisha. Akabahatika kuwa ni Baba Mlishi wa Mtoto Yesu. Wakati wa madhulumu ya Mfalme Herode, akakimbilia nchini Misri ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Baada ya kuishi uhamishoni, waliweza kurejea tena na hivyo kwenda kuishi mjini Nazareti الناصرة kwa Kiarabu, נצרת na kwa Kiebrania. Huu ni mwaliko wa kukubali na kupokea mpango wa Mungu katika maisha na hivyo kuunafsisha. Mtakatifu Yosefu alikuwa ni mtu mwenye upendo uliomwilishwa katika huduma makini kwa Mungu na jirani. Akabahatika kuwa ni Baba mlishi wa Kristo Yesu, Mlinzi wa Kanisa la Kiulimwengu na Mwombezi wa kifo chema. Hiki ni kielelezo cha huduma na sadaka ya maisha iliyopambwa kwa upendo mkuu unaoonesha utashi wa kuishi na kuhudumia na hivyo akawa tayari kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto mamboleo katika maisha.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Ndoto za Mtakatifu Yosefu zilinafsishwa katika huduma na kushuhudiwa katika uaminifu. Kumbe, hofu, matatizo na magumu ya maisha ni hali ya kawaida katika historia, maisha na utume wa Kanisa. Kumbe wakleri na watawa wanapaswa kuwa ni ni mashuhuda wa uaminifu wa Mungu. Mama Kanisa anaadhimisha Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema. Hii inaonesha kwamba, kulikuwepo na wachungaji dhalimu, wakatili waliowanyonya na kuwatesa kondoo wao. Kristo Yesu anajipambanua bila shaka hata kidogo kwamba, ni Mchungaji mwema; ni Mwanakondoo wa Mungu anayezichukua dhambi za Ulimwengu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake Msalabani. Ni Mhudumu mwaminifu na mnyenyekevu.
Ninapenda sasa kuchukua fursa hii, kudadavua kidogo dhana ya “Mchungaji katika Agano la Kale na Agano Jipya” kama inavyofafanuliwa na Kristo Yesu mwenyewe katika Maandiko Matakatifu, lakini zaidi katika Agano Jipya. Wachungaji katika Agano la Kale ni cheo walichopewa viongozi wa kisiasa, wafalme na makuhani. Nabii Ezekieli anasema, hawa hawakuwa na sifa za kuitwa wachungaji wema ndiyo maana wanatabiriwa: “Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; Je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo? Mnawala walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona; lakini hamwalishi kondoo. Wagonjwa hamkuwatia nguvu, wala hamkuwaponya wenye maradhi, wala hamkuwafunga waliovunjika, wala hamkuwarudisha waliofukuzwa, wala hamkuwatafuta waliopotea; bali kwa nguvu na kwa ukali mmewatawala”. Eze. 34: 1-4.
Kristo Yesu katika Agano Jipya anaonya kuhusu tabia hii na kuwaambia Mitume, ikiwa kama kati yao kuna mtu anataka kuwa “Mchungaji” au Kiongozi lazima awe mnyenyekevu na mtumishi wa wote. Rej. Lk. 22:25. Katika Injili kama ilivyoandikwa na Yohane, 10: 1-19 anataja na kupembua sifa za Mchungaji mwema kuwa ni mlango wa kondoo na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje. Anawaonesha dira na njia ya kufuata kwa maana waijua sauti yake. Kristo Yesu alikuja ulimwenguni ili watu wawe na uzima, kisha wawe nao tele! Kristo Yesu ni mchungaji mwema na anafahamiana na kondoo wake. Anakazia umoja miongoni mwa wanakondoo wake. Baba yake wa mbinguni anampenda, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, amefunua huruma na upendo wa Baba yake wa milele kwa binadamu.
Kristo Yesu ni utimilifu wa ahadi ya Baba wa milele kwa waja wake kuhusu Mchungaji mwema, anayesadaka maisha yake kwa ajili ya upendo unaomwilishwa katika huduma kwa kuwaondolea dhambi zao, kuwatakasa, kuwaponya magonjwa na kuwalisha wenyewe njaa. Muhtasari wa huduma ya upendo ni Siku ile ya Alhamisi kuu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma ya upendo na mshikamano wa kidugu. Huyu ndiye Kristo Yesu mchungaji mwema, aliyekuja kutoa huduma na wala si kuhudumiwa. Kristo Yesu ni “Mwanakondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!” Yn. 1:29. “Kwa maana huyu Mwanakondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mingu atayafuta machozi yote katika macho yao.” Ufu. 7:17. Kristo Yesu ni mchungaji mwema, tujibidiishe kumpenda, kumtangaza na kumshuhudia katika ndoto za maisha yetu; katika huduma makini kwa Mungu na jirani, kila mmoja wetu akiwa mwaminifu kwa maisha, wito na utume wake ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.