Tafuta

Jumapili ya 4 ya Kipindi cha Pasaka: Jumapili ya Yesu Kristo Mchungaji Mwema: Siku ya 58 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa Jumapili ya 4 ya Kipindi cha Pasaka: Jumapili ya Yesu Kristo Mchungaji Mwema: Siku ya 58 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa 

Jumapili ya Kuombea Miito: Yesu Mchungaji Mwema na Mfano Bora!

Uzuri wa Yesu Kristo kama Mchungaji mzuri unajikita katika kujitoa sadaka; katika kila Adhimisho la Ekaristi Takatifu. Ni katika sadaka ya Misa Takatifu hapo kwa namna ya pekee kila tunapoiadhimisha Yesu Kristo anakuwa ndiye Kuhani, Kondoo na Altare. Na pia kutualika kuiga mfano wake, mfano wa kuwa wazuri, wa kumpenda Mungu na jirani kwa kujisadaka bila kujibakiza.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani ya Kristo Mfufuka iwe nanyi nyote! Sehemu ya Injili Takatifu ya Dominika ya leo naweza kusema ni moja kati ya Injili zinazofahamika na kukumbukwa na wengi wetu. Ni utambulisho wa Yesu Kristo kama MCHUNGAJI MWEMA/MZURI. Pia Dominika ya leo ya Mchungaji Mwema tunaalikwa na Mama Kanisa kuombea Miito Mitakatifu katika Kanisa. Wanawaisraeli hata baada ya kuwa katika nchi ile ya Kaanani na kuanza kujihusisha na kilimo, bado waliendelea pia na maisha ya ufugaji hasa wa kondoo na mbuzi.  Mifugo ilionekana kuwa na thamani kuliko hata utajiri wa vito vya thamani. Mithali 27:23-27 Mifugo ilithaminiwa sana na wafugaji wa nyakati zake Yesu Kristo kati ya Wanawaisraeli. Wafugaji wa nyakati zile, walikuwa wanachunga mifugo yao katika sehemu za maporini na hivyo walibaki na mifugo hiyo mbali na makazi ya kawaida kwa muda na hata miaka mingi. Ni katika muktadha huu mfugaji aliwajua mifugo yake kwa majina, na wanyama pia walimjua mchungaji wao kwa sauti yake. Ni huko machungani pia wachungaji walikutana na hatari hasa ya wanyama wakali wa mwituni.

Mchungaji kwa kuthamini mifugo yake alifanya kila awezalo katika kuilinda, kuilisha na kuitetea mifugo yake kiasi hata cha kuhatarisha maisha yake. Mfugaji alikuwa na mahusiano ya upendo wa dhati na mifugo yake, labda kwa baadhi yetu hasa tunaotoka katika jamii za wakulima yawezekana tunapata ugumu kufikiri juu ya hili, yatosha kuingia katika moyo wa mfugaji ili kuelewa muktadha wa Injili ya leo. Lakini hata katika jamii zetu nyingi za kifugaji wanaweza kuelewea kirahisi thamani anayopewa mnyama na mchungaji na hasa maisha ya kujisadaka katika kuwalisha na kuwalinda dhidi ya hatari mbali mbali. Katika Maandiko Matakatifu, taswira ya Mchungaji inatumika mara nyingi. Mathalani, mfalme Daudi anaitwa kuwa mfalme na kuwaongoza Wanawaisraeli akitokea kuchunga kundi la kondoo wake. Zaburi 78:70-72 na hata wafalme wengine wa Israeli walikuwa wanafananishwa na wachungaji wa kuwachunga watu. Tunasoma katika Kitabu cha Nabii Ezekieli pale ambapo wafalme wakaacha kuchunga watu na kuanza kujichunga wenyewe. Ezekieli 34. Katika Agano la Kale Mungu anatambulishwa kama mtunza mizabibu na mkulima. Isaya 27:3 na Zaburi 65 lakini zaidi sana kama mchungaji anayeongoza, kulilinda na kulisha kundi lake, yaani Taifa la Israeli. Zaburi 80:2 na 23 Zaburi mashuhuri ya Bwana ndiye Mchungaji wangu sitapungukiwa na kitu. Rejea pia Isaya 40:11 na Yeremia 23:3-5.

Injili yetu ya leo inaanza kwa maneno yafuatayo kwa Kigiriki, naomba niiweke katika lugha yake halafu nitajaribu kuelezea maana yake ili tuweze kuelewa vema ujumbe wa Injili ya leo. Εγω ειμι ο ποιμην ο καλος . (Ego eimi o poimen o kalos) Tafsiri yake sisisi inayotumika mara nyingi na kujulikana na wengi ni ‘’Mimi ndimi Mchungaji mwema’’. Pamoja na kuwa si mbali na ukweli ila yafaa kurudi haswa katika maana halisi ya sentensi hii. Nitajaribu bila kuwachosha sana na kuelezea baaadhi ya maneno ya Kigiriki na maana zake haswa. Yatosha kufuata kwa makini na inaweza kueleweka kirahisi kabisa bila kuhitaji uwe mtaalamu wa hali ya juu katika lugha hiyo ya Kiyunani. Maneno “Mimi ndimi” au kwa Kiyunani “Ego eimi” ni utambulisho wa Mungu mwenyewe katika Maandiko Matakatifu. Mungu ni uwepo wenyewe, ni uwepo wa lazima anayesababisha vingine vyote kuwepo. Mtakatifu Tomaso wa Akwino anamtambulisha Mungu kama “Ipsum Esse Subsistens” Yaani ni “Ule Uwepo wenyewe na ndio sababu ya uwepo wetu”; God is the Self-subsisting Act of Existing. He is the Creator-source of all that is… Sisi tupo kwa vile Mungu yupo. Mungu ndiye asili ya uwepo wetu.

Hivyo Yesu Kristo kwa kusema “Mimi ndimi” ni kujitambulisha kama Mungu anayesababisha ulimwengu na vyote vilivyomo kuwepo.  Tunasoma kutoka Kitabu cha Kutoka 3:14 pale Musa anapomuuliza Mungu jina lake ni nani. Na Mungu anajibu “MIMI NDIMI NILIYE”. Hivyo Yesu Kristo anajitambulisha kuwa ni Mungu aliyepo. Katika tafsiri nyingi zinasema kuwa Mimi ni mchungaji mwema. Kwa kweli kivumishi kilichotumika katika Injili ya leo sio mwema na badala yake ni mzuri. Neno mwema kwa Kigiriki ni αγαθος (agathos) ambalo halijatumika katika Injili ya leo na badala yake kimetumika kivumishi kingine cha καλος (kalos) likimaanisha mzuri. Hivyo yafaa haswa kuelewa kuwa Yesu Kristo anajitanabaisha kama Mchungaji mzuri. Ni katika uzuri wake pia tunakutana na wema wake. Neno καλος kwa maana mzuri ni kusema ni mzuri wa nje na ndani, kama tunavyomwona kwa nje ndivyo alivyo kwa ndani, uzuri wake tunauona hata kwa nje. Mara nyingi katika maisha ya kawaida hata utasikia kuwa fulani ni mzuri kwa mwonekano ila roho yake au moyo wake ni mbaya, ila haikuwa hivyo kwa Yesu Kristo Mchungaji mzuri, uzuri wake wa nje ni sawa na ndani, hakugawanyika(schizophrenic). Kila anayekutana na Yesu Kristo anabaki na mmoja asiyegawanyika, asiyekuwa na sura mbili bali daima tunakutana na kuuonja uzuri wake, na humo pia tunaona huruma na upendo wake wa daima.

Hivyo ni Yesu Kristo anatualika nasi kuuangalia uzuri wake na kuutafakari ili nasi tuweze kujifunza na kuwa kama yeye. Kutokuwa watu wa kugawanyika na badala yake kuwa na maisha mazuri, uzuri wetu wa nje uakisi uzuri wetu wa ndani. Ni Yesu Kristo anatufunulia uso wa Mungu, uso mzuri wa Mungu, uzuri wa Mungu ambao kwao nasi tunaitwa kuushiriki, ni kila mmoja wetu anaitwa kuwa mchungaji mzuri. Kuwa na uzuri wa Mungu mwenyewe katika maisha yetu. Yesu Kristo pia anatueleza ni kitu gani kinamfanya yeye kuwa mzuri, ni kuwa tayari kutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo zake. Tunaposoma mifano ile ya kondoo aliyepotea katika Injili za Matayo 18:12-14, na Luka 15:4-7, Mchungaji anayetoka na kumtafuta kondoo aliyepotea tunabaki kuguswa na mantiki ile ya Kimungu iliyo tofauti na ile ya mwanadamu. Mungu anayetoka kumtafuta kondoo mmoja aliyepotea na kuacha wale 99 zizini. Ni Upendo wa Mungu usioelezeka kwa akili na mantiki zetu za kibinadamu. Katika Injili ya leo tunaona Mchungaji anayehatarisha hata maisha yake kwa ajili ya kondoo wake. Ni kama mfalme Daudi aliyebaki porini na mifugo yake ili kuwalinda na kuwatetea katika nyakati hatarishi. Na ndivyo Yesu Kristo anavyoutambulisha uzuri wake katika Injili ya leo.  Rejea 1Samweli 17:34-35

Neno καλος linamaanisha kuwa mkweli, mwenye ujasiri na mwenye upendo wa dhati. Yesu Kristo anatumia picha ya mtu wa mshahara kumtofautisha na uzuri wake. Mtu wa mshahara hana mahusiano ya dhati ya upendo na kondoo bali aliajiriwa na kupewa ujira wake baada ya kuwachunga kwa siku nzima au wiki zima. Hivyo kwake kondoo sio kitu cha thamani zaidi ya ujira wake, cha kwanza kwake sio kondoo bali ujira wake anaoupata baada ya kutimiza wajibu wake. Na ndio maana hawezi kuhatarisha maisha na uhai wake katika nyakati za hatari dhidi ya wanyama wakali wa porini wanapovamia kundi. Mtu wa mshahara ataokoa maisha yake tu na kuwaacha kondoo katika hatari. Wanyama wakali wa mwituni ni hatari mbalimbali zinazotufanya kuwa mbali na Mungu, ni ukosefu wa uaminifu na upendo wa dhati kwa Mungu na jirani. Ni maisha mabaya yasiyofaa na kumpendeza Mungu. Yesu Kristo kwa Neno lake na Masakramenti yake katika Kanisa alizotuachia ili daima kutusaidia kubaki katika kundi moja chini ya uchungaji wake. Kanisa linachungwa daima na mchungaji mmoja aliye mzuri na ndiye Yesu Kristo mwenyewe. Kanisa ni mali ya Kristo ni la Yesu Kristo Mfufuka, aliye pia Mchungaji mzuri.

Mara nyingi katika Kanisa tunaposoma somo hili la Mchungaji mwema basi tunawaza kuwa linawahusu wachungaji wetu kwa maana ya makasisi na mashemasi na maaskofu, kwa kweli hapana ila kila mmoja wetu kama mbatizwa tunaalikwa kuwa na uzuri huu wa mchungaji mwema, kwa maana ya kuwa na moyo usiogawanyika kwa Mungu na kwa jirani. Na ndio kupenda katika kweli. Anayependa hajifikirii yeye mwenyewe tu. Uzuri wa Yesu Kristo kama Mchungaji mzuri unajikita katika kujitoa sadaka kwa daima, na ndio tunaona anaongea na kundi lake kila siku kwa njia ya Neno lake, lakini zaidi sana anajitoa Mwili na Damu yake katika kila Adhimisho la Ekaristi Takatifu. Ni katika sadaka ya Misa Takatifu hapo kwa namna ya pekee kila tunapoiadhimisha Yesu Kristo anakuwa ndiye Kuhani, Kondoo na Altare, ni hapo linakuwa sio tendo la zamani bali na sasa ya milele, kwani ni kweli anajitoa sadaka na pia kutualika nasi kuiga mfano wake, mfano wa kuwa wazuri, wa kumpenda Mungu na jirani kwa kujisadaka bila kujibakiza. Na ndio sala yetu katika Dominika ya leo, ili nasi iwe tu makasisi wa daraja au makasisi kwa ubatizo wetu, kila mmoja wetu tuweze kuiga mfano na kufananisha maisha yetu na Sadaka ya Misa Takatifu na pia Neno lake tunalolisikia.

Upendo wa kweli hauna mipaka na haujitafutii faida zake yenyewe bali unajitoa kwa ajili ya mwingine, hata katika mazingira ya kuhatarisha maisha yetu. Huu ndio uzuri halisi, yaani upendo usio na masharti, upendo wa Kimungu, kama asemavyo Mtume Yohana kwa kuwa Mungu ni Upendo. 1 Yohane 4:16. Sifa ya pili ya uzuri wa Yesu Kristo Mchungaji ni kuwajua kondoo zake. Kujua kunakozungumziwa hapa sio tu kitendo cha akili bali ni mahusiano ya ndani haswa kama yale ya watu wa ndoa kati ya mume na mke.  Ni mahusiano yanayohusisha zaidi moyo kuliko akili. Ni kujua kunakoamsha mapendo ya ndani na ya kweli. Ni hali ya kutaka kuingia katika mahusiano ya ndani na ya kweli. Yesu Kristo aliyemchungaji mzuri anamjua kila mmoja wetu, kwa maana anampenda kwa dhati kila mmoja wetu na anatupenda upeo bila masharti yeyote na daima yupo kutuongoza, kutulinda na kutulisha ila anatualika nasi kumpenda kwa kuisikia sauti yake na ndio Neno lake na kumfuata.

Yesu Kristo mchungaji mzuri anayetoa maisha yake kwa ajili ya kondoo wake na ndio anasema anao uweza wa kuuchukua tena uhai wake. Ni katika kuutoa uhai wetu kwa upendo ndipo tunapopata maisha ya kweli ni kama mbegu isipoanguka na kuoza haiwezi kutoa matunda mengi. Ni mwaliko wa kuwa wazuri kama Yesu Kristo kwa maana ya kuwa watu wenye upendo kwa Mungu na kwa jirani. Yohana 12:24-25 Niwasihi pia katika Dominika ya leo kuombea miito mitakatifu lakini pia tuwaombee wale wote walioitikia katika miito hiyo ili daima neema za Mungu ziwategemeze na kuwafikisha katika ukamilifu wa wito maana, yaani wito wa kuwa watakatifu, wa kufanana zaidi na zaidi na Yeye anayetuita iwe katika maisha ya Ukasisi, Utawa, Wakfu, na Ndoa Takatifu. Tumuombee Baba Mtakatifu, Maaskofu wetu, mapadre wetu, mashemasi wetu, watawa wa kike na kiume, wenye maisha ya wakfu na wale wanaoishi maisha ya ndoa, na pia tuwaombee vijana popote ulimwenguni wanaojiandaa kuitikia na kuishi miito yao mbali mbali. Nawatakia tafakari njema na tuzidi kusali kwa ajili ya Miito Mitakatifu katika Kanisa.

21 April 2021, 15:46