Ijumaa Kuu: Mama Kanisa anaadhimisha Fumbo la Mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani kwa ajili ya wokovu wa walimwengu. Ijumaa Kuu: Mama Kanisa anaadhimisha Fumbo la Mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani kwa ajili ya wokovu wa walimwengu. 

Maadhimisho ya Juma Kuu: Ijumaa: Mateso na Kifo cha Kristo!

Ijumaa kuu ni siku ya kufunga, kusali na kulitafakari, ili kukumbuka mateso na kifo cha Kristo Yesu, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Waamini wanaalikwa kuuabudu Mti wa Msalaba, ambao wokovu wa dunia umetundikwa juu yake, yaani Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Siku ya Ijumaa Kuu. Siku ambapo Kanisa zima liko kimya likitafakari Mateso na kifo cha Msalaba cha Bwana wetu Yesu Kristo kilichotuletea wokovu kama anavyosali Padre kwa niaba ya jamii ya waamini katika sala ya mwanzo akisema; “Ee Mungu, kwa mateso ya Kristo Mwanao Bwana wetu, umetuondolea mauti tuliyorithi sisi binadamu wote kwa dhambi ya kale. Utujalie sisi tuliozaliwa na hali ya kibinadamu kwa maumbile, vivyo hivyo tuzaliwe na hali ya kimungu kwa kutakaswa na neema yake.”  Ibada ya Ijumaa Kuu ina sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ni Liturujia ya Neno kiini chake ni simulizi la mateso ya Yesu ambayo inamalizika kwa maombezi kwa watu wote. Sehemu ya pili ni Kuuabudu Wokovu wa dunia uliotundikwa Msalabani, ndiye Yesu Kristo.  Na sehemu ya tatu ni Ibada ya Komunyo Takatifu. Tukumbuke kuwa Ijumaa Kuu Kanisa haliadhimishi Sadaka ya Misa Takatifu kwa sababu ni siku ambapo Yesu mwenyewe alijitoa Sadaka msalabani. Jumamosi Kuu Kanisa linakaa kimya likiyawaza-waza Mateso na kifo cha Yesu, hivyo haliadhimishi Sadaka ya Misa Takatifu hali Meza Takatifu, Altare iko tupu, mpaka zitakapoanza sherehe za Pasaka baada ya Vijilia Takatifu au Kesha la ufufuko. Hapo tena sherehe zitaendelea muda wa siku hamsini.

Katika somo la kwanza la Nabii Isaya, tunatafakari wasifu wa mtumishi wa Bwana aliyetuokoa kutoka utumwa wa dhambi kwa njia ya mateso makali; uso wake uliharibiwa sana, hakuwa na umbo wala uzuri wa kumtamani, alidharauliwa na kukataliwa na watu, mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko, hakuhesabiwa kuwa kitu, lakini ndiye aliyeyachukua masikitiko yetu, akajitwika huzuni zetu, alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu, adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Bwana aliweka juu yake maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, hakufunua kinywa chake mbele ya watesi wake, kwa kuonewa na kuhukumiwa, akapigwa kwa sababu ya makosa ya watu, wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya. Ingawa hakutenda jeuri, wala hapakuwa na hila kinywani mwake; lakini Bwana aliridhika kumchukua amehuzunisha, akaifanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, na hivyo mapenzi yake yakafanyika mkononi mwake. Kwa haki yake akawafanya wengi kuwa wenye haki kwa kuyachukua maovu yao kwa kumwaga nafsi yake hata kufa ili kuwaombea wakosaji. Tumlipe nini basi huyu mtumishi wa Bwana aliyeteseka hivikwa dhambi zetu. Hatuna chochote cha kutoa kama fidia isipokuwa kujinyenyekesha kwake kwa moyo wa toba na majuto kumuomba msamaha na kuzitupilia mbali dhambi zetu.

Somo la pili la Waraka kwa Waebrania linatuasa tumwamini Yesu Kristo kuhani wetu mkuu aliyeonja na kuvumilia taabu na mateso mengi kwa ajili yetu, maana yeye anafahamu taabu na matatizo yetu, daima yupo tayari kutuombea kwa Baba. Sharti ni hili; kuyashike sana maungamo yetu tuliyofanya naye. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji yetu. Maana “Yeye aliyemtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti maombi na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.” Injili ilivyoandikwa na Yohane inasimulia jinsi Yuda alivyomsaliti Yesu kwa busu na hivyo kukamatwa na Askari wakiwa na taa mienge na silaha (Yn. 18:3) akiwa katika bustani ya mizeituni. Baada ya kukamatwa, Yesu alipelekwa katika baraza la wayahudi, “Sanhedri”, chombo chenye mamlaka ya juu ya kidini (Yn. 18:12-14); baraza likaamuru apelekwe kwa gavana wa Kirumi; Pontio Pilato naye akaamuru apelekwe kwa mkuu wa mkoa wa Galilaya; Herode Antipas kwa vile Yesu alikuwa mwenyeji wa Nazareti katika Galilaya (Yn.18:28ff).

Mahangaiko haya yote ni kwasababu kila kundi liliona kuwa Yesu hana hatia. Lakini mwisho anahukumiwa hukumu isiyo haki. Baada ya hukumu hii isiyo haki, Yesu alipigwa mijeledi, akavikwa taji ya miiba, akapigwa kwa mwanzi, akatemewa mate, akabebeshwa Msalaba mzito, akavuliwa nguo, akasulubiwa msalabani, akafa, nchi ikatetemeka, jua likafifia, kukawa na giza juu ya nchi, pazia la hekalu likapasuka mara mbili, naye askari mmoja wapo akamtoboa ubavu kwa mkuki na mara ikatoka damu na maji, chemchemi za Sakramenti za Kanisa. Yesu anatendewa haya yote kwa mashtaka ya uongo yakiwemo ya kisiasa na kidini. Mashitaka ya kidini yalikuwa; kuidhihaki nyumba ya Mungu kwa kudai hekalu livunjwe naye kulisimamisha kwa siku tatu (Yn. 2:19), na pia kujiita Masiha na mwana wa Mungu (Yn. 5:16). Mashtaka haya yote ni ya uongo, kwani kweli Yesu ni mwana wa Mungu hata akida aliyeshuhudia kifo chake anakiri wazi hakika mtu huyu alikuwa mwana wa Mungu, yeye ni masiha na hekalu walilolivunja alilisimamisha kwa siku tatu ndilo mwili wake (Yn. 2:21). Kwa makosa haya kadiri ya sheria ya Kiyahudi Yesu alistahili adhabu ya kifo lakini kwa kuwa wayahudi walikuwa chini ya utawala wa kirumi, hayakuwa makosa ya kutoa hukumu ya kifo. Ndiyo maana yakatungwa makosa ya kisiasa/uhaini ambayo ni; kujiita mfalme wa Wayahudi, kuwakataza watu kulipa kodi na kuchochea mgomo.

Tukumbuke kuwa nyakati hizi Wayahudi walitawaliwa na warumi na mfalme wao alikuwa Kaisari na walipaswa kulipa kodi kwake. Makosa haya yote ni ya uongo kwani Yesu alimwambia Petro aende ziwani, na samaki wa kwanza atakayemshika achukue humu shekeli akalipe kodi kwa ajili yake na yeye pia. Hata walipomuuliza swali kama ni halali kutoa kodi au la, jibu la Yesu lilikuwa wazi ya Kaisari mpeni Kaizari na ya Mungu mpeni Mungu. Kumbe Yesu hakuwa na hatia yoyote ndiyo maana Yuda anasema nimekosa kuisaliti damu isiyo na kosa. Anarudisha pesa kwa wakuu wa Makuhani. Pilato naye anasema; mimi sioni kosa la mtu huyu (Yn.18:38). Kwa woga anamtoa ateswe akisema, mimi sina hatia juu ya kifo cha mtu huyu ananawa mikono. Naye Yesu kwa upendo na hiari akayapokea hayo yote, akateswa na kufa msalabani kwa ajili ya wokovu wetu. Basi, sisi tunapaswa kuona fahari kwa Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo (Gal. 6:14). Ni kwa njia ya msalaba tumekombolewa. Je, ni mara ngapi tumeukana na kuutupilia mbali msalaba? Jogoo amekwisha wika mara ya tatu tunaalikwa kujirudi tujiweke chini ya msalaba kwani hatuna tumaini lingine, japo kwao wanaopotea msalaba ni kikwazo na upuuzi kwetu sisi ni nguvu ya Mungu, tuutazame sasa msalaba kwa imani kuu na moyo wa toba. Katika simulizi la mateso ya Yesu, Baraba anaachwa huru na Yesu kusulibiwa. Huku kuachwa huru kwa Baraba kuna maana kubwa sana. Baraba alikuwa mdhambi. Kuachwa kwake huru ili Yesu auawe ni kudhihirisha kuwa kifo cha Yesu kinawaweka huru wale wote walio katika vifungo vya dhambi watakaomwamini.

Sehemu ya pili ya Liturujia ya Ijumaa Kuu ni ibada ya “kuabudu Msalaba”, kuuabudu wokovu wetu ndiye Yesu Kristo aliyetundikwa juu yake. Msalaba ulitumiwa na Warumi tangu zamani kabla ya Yesu kwa kutoa adhabu ili kukomesha uhalifu, wizi, ujangili, ujambazi, uhaini au uasi. Mtu aliyefanya makosa haya aliteswa sana na baadae kusulibiwa msalabani na kuachwa hapo mpaka afe. Kwa wayahudi adhabu hii pia ilitumika kama tunavyosoma; “Ikiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, nawe ukamtundika juu ya mti, mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utauzika siku hiyohiyo. Kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu; asije akatia najisi katika nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako iwe urithi wako” (Kum.21:22-23). Kwetu sisi Msalaba ni bendera na bango la ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Msalaba ni alama ya ukombozi (Yn.12:13-33), ni alama ya upendo wa Kristo kwetu sisi wadhambi (Yn.3:14-18). Msalaba ni alama ya maisha ya kikristo (Mk.8:34). Msalaba ni alama ya umoja na Kristo. Msalaba ni alama ya ufuasi wa kweli wa Yesu Kristo (Mk 8: 34). Msalaba ni sadaka ya Yesu, ni zao la upendo (Yn 13:1; 15: 13).   

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema; “Msalaba siyo ishara ya kifo, bali uzima; siyo jambo la kutuvunja moyo, bali matumaini; siyo ishara ya kushindwa, bali ya ushindi”. Nasi hatuna shaka yoyote kuinama, kupiga magoti na kuubusu msalaba ambao juu yake ametundikwa Wokovu wetu, Yesu Kristo, Nafsi ya Pili ya Utatu Mtakatifu, Mungu halisi anayestahili kuabudiwa ndiyo maana mwaliko wa ibada hii unasema: “Huu ndio mti wa Msalaba ambao Wokovu wa dunia umetundikwa juu yake, njoni, njoni, njoni tuuabudu”. Mwenye macho ya kiimani anaukaribia msalaba, kwa unyenyekevu, kwa utulivu, kwa hekima na kwa moyo wa majuto na toba, na kwa moyo wa ibada na shukurani kwa makuu aliyotufanyia Yesu Kristo, kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Kumbe sasa msalaba si tena alama ya adhabu bali ya wokovu. Basi, kama mtume Paulo nasi tuone fahari kwa msalaba wa Yesu Kristo (Gal. 6:14). Kristo yupo anatuona hadi moyoni. Wakati wa kumwabudu, tujongea mbele zake tukimwomba atusamehe dhambi zetu na kumwahidi kwamba sasa tunaachana na dhambi na tupo tayari kumwamini yeye tu. tumwombe atuondolee udhaifu wetu ili tuwe kweli wafuasi wake waaminifu.

Ijumaa kuu 2021
02 April 2021, 07:53