Tafuta

Maadhimisho ya Juma Kuu: Jumamosi Kuu: Mkesha wa Pasaka. Waamini wanahimizwa kutafakari Neno la Mungu, kumbukumbu endelevu ya historia ya wokovu: Mwanga, Ubatizo na Ekaristi Takatifu Maadhimisho ya Juma Kuu: Jumamosi Kuu: Mkesha wa Pasaka. Waamini wanahimizwa kutafakari Neno la Mungu, kumbukumbu endelevu ya historia ya wokovu: Mwanga, Ubatizo na Ekaristi Takatifu 

Maadhimisho ya Juma Kuu: Kesha la Pasaka: Historia ya Wokovu!

Sisi tuliokufa katika dhambi, tumefufuka katika Kristo pamoja naye. Ishara ya ushindi ni mshumaa wa Pasaka, mwanga wa Kristo, uondoao giza la usiku huu, lililo ishara ya dhambi na mauti. Kanisa linausalimu na kuuheshimu mwanga wa Kristo Mfufuka katika alama na ishara ya Mshumaa wa Pasaka. Kristo ndiye mleta uzima. Kwa furaha kubwa tunausimamisha mwanga huu katikati yetu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu mkesha wa Pasaka. Ni mkesha mtakatifu tunapoadhimisha kilele cha fumbo la ukombozi wetu; ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Ni usiku mtakatifu inapopigwa mbiu ya Pasaka, kutujulisha ushindi umepatikana, Bwana wetu Yesu Kristo ametoka mautini, ni mzima. Hivyo, Kanisa linawaalika wanawe wote popote duniani, kukesha na kusali pamoja, ili kuadhimisha Pasaka ya Bwana kwa kusikiliza neno lake na kuyatukuza mafumbo yake, kwa tumaini la kushiriki naye shangwe ya kushinda mauti, na kuishi pamoja naye milele yote mbinguni kwa Mungu. Kristo amefufuka kweli kweli, aleluya. Kesha hili la usiku wa Pasaka limegawanyika katika sehemu kuu nne. Sehemu ya kwanza ya ni Liturujia ya Mwanga. Katika Liturjia hii, Kanisa linatafakari maajabu aliyofanya Bwana Mungu taifa lake tangu mwanzo kwa kubariki moto na kuutayarisha mshumaa wa Pasaka, tukimwomba Mungu atutie moto wa upendo wake kwa njia ya Mwanae, atujalie tuwake tamaa ya mbinguni kwa sikukuu ya Pasaka, ili tuweze kuzifikia raha za heri yake ya milele kwa mioyo iliyotakata.

Katika matayarisho ya Mshumaa wa Pasaka, Padre anauchora ishara ya msalaba kwa kalamu ya chuma. Kisha anauchora herufi za Kigiriki: Alfa juu ya Msalaba, Omega chini yake Kati ya mikono ya msalaba anachora tarakimu nne za mwaka husika akisema: Kristo jana na leo, Mwanzo na Mwisho, Alfa na Omega, nyakati ni zake na karne pia, utukufu ni wake na enzi pia daima na milele. Baada ya kuuchora mshumaa ishara ya msalaba na ishara nyingine, padre anachomeka katika mshumaa chembe tano za ubani kwa kuzipanga mfano wa msalaba, akisema: Kwa majeraha yake matakatifu, na matukufu, Kristo Bwana wetu atulinde na atuweke salama. Hii ni kuonyesha na kukiri ukuu na utakatifu wa msalaba ambao kwao wokovu wetu, Yesu Kristo alitundikwa juu yake, akafa, akazikwa na sasa amefufuka yu mzima ameshinda dhambi na mauti, ametuweka huru kutoka utumwa wa shetani, utumwa wa dhambi. “Huu ndio usiku mtakatifu, ambapo Kristo alikata minyororo ya mauti, akatoka kuzimu ameshinda.

Kanisa halichoki kutueleza maana ya usiku huu kwamba ni usiku wa kutoka katika hali ya upotevu na kuingia katika hali ya uzima wa Kimungu. Sisi tuliokufa katika dhambi, tumefufuka katika Kristo pamoja naye. Ishara ya ushindi wetu, ni mshumaa wa Pasaka, mwanga wa Kristo, uondoao giza la usiku huu, lililo ishara ya dhambi na mauti. Kwa hiyo katika adhimisho hili, Kanisa linausalimu na kuuheshimu mwanga wa Kristo katika alama na ishara ya mshumaa ndiye Kristo mfufuka, mleta uzima. Kwa furaha kubwa tunausimamisha mwanga huu katikati yetu. Sehemu ya pili ni Liturujia ya Neno. Katika mkesha huu, ambao ni mama ya mikesha yote, yanatolewa masomo kenda; saba ya Agano la Kale na mawili ya Agano Jipya (Waraka na Injili). Baada ya kupigwa mbiu takatifu, Padre anawaalika waamini kulisikiliza Neno la Mungu kwa makini ili kulijua vyema fumbo la ukombozi wetu tangu matayarisho yake katika Agano la kale na utimilifu wake katika Agano jipya na la milele akisema; “Tumeingia katika mkesha wa Pasaka, sasa tusikilize neno la Mungu kwa moyo mtulivu. Tuwaze jinsi Mungu alivyolikomboa taifa lake wakati ulipowadia, na mwishowe akamtuma kwetu Mwanawe awe Mkombozi. Tumwombe Mungu wetu aifanikishe hii kazi ya wokovu wakati huu wa Pasaka, ili nasi tupate ukombozi kamili. Masomo haya ni ya kusikiliza kwa makini sana, ili kulitambua na kuliishi vyema fumbo la ukombozi wetu, yaani Pasaka.

Sehemu ya tatu ni Liturujia ya Ubatizo ambapo wakatekumeni walioandaliwa vyema wakati wa kwaresima wanapokea Sakramenti ya Ubatizo, wanazaliwa upya kwa maji na Roho Makatifu, wanakufa kuhusu dhambi na kufufuka pamoja na Kristo ndiyo maana kabla ya adhimisho la Sakramenti hii Padre anawaalika waamini akisema; “Ndugu zangu, tuwasaidie kwa sala zetu hawa ndugu zetu wawe na matumaini ya wokovu. Na hapo watakapoijongea chemchemi ya uzima mpya, Baba Mwenyezi azidi kuwasaidia kwa huruma yake.” Kumbe ufufuko wetu huonekana na kudhihirishwa katika sherehe ya ubatizo. Wanaobatizwa huzaliwa upya katika Kristo, lakini hata tuliokwisha batizwa, tunashirikishwa huko kuzaliwa kupya, kwa kuweka tena ahadi za ubatizo. Kwa tendo hilo, umoja wetu na Kristo mfufuka huimarishwa. Sehemu ya nne ni Liturujia ya Ekaristi Takatifu ndiyo kilele na kiini cha adhimisho la fumbo la ukombozi wetu ndiyo maana Padre kwa niaba ya jamii ya waamini anasali akisema; “Ee Bwana, tunakuomba uzipokee sala na dhabihu za taifa lako, ili hayo tuliyoanza kutenda katika mafumbo tupate uzima wa milele.

Sala ya utangulizi inatupa muhutasari kamili wa fumbo hili kuwa; Kristo ametolewa Pasaka yetu. Yeye ndiye Mwana kondoo wa kweli aliyeondoa dhambi za dunia, alishinda mauti yetu kwa kufa kwake, akaturudishia uzima wetu kwa kufufuka kwake. Na kwa sababu hiyo, watu wote wanaitukuza sikukuu ya Pasaka kwa furaha kubwa popote duniani. Nao Malaika wote wa mbinguni wanaimba wimbo wa kukutukuza, wakisema bila mwisho. Ni furaha kweli kweli kwani Kristo Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani Kristo; basi na tuifanye karamu kwa yasiyo chachika, ndio weupe wa moyo na kweli. Turudi sasa katika sehemu ya pili ibada Mkesha wa Pasaka ambayo ni Liturujia ya Neno. Masomo kenda yanayosomwa katika liturujia ya neno katika vijilia vya mkesha wa pasaka, yote kwa pamoja yanatupa simulizi kamili la historia ya wokovu wa mwanadamu tangu alipoanguka katika dhambi baada ya kuubwa. Simulizi la uumbaji katika kitabu cha mwanzo linatufundisha kuwa asili na chanzo cha mwanadamu ni Mungu katika Utatu Mtakatifu.

Katika viumbe vyote vilivyoumbwa (Mw.1-2), ni binadamu tu peke yake ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mw.1:26-27) ili amjue, ampende, amtumikie na mwisho afike kwake mbinguni. Mungu kabla ya kumuumba mwanadamu aliviumba vitu vingine vyote (Mw1:1-25) kama maandalizi ya mazingira ya kuishi mwanadamu. Baada ya kumwumba mwanadamu alimkabidhi vyote ili avitiishe na kuvitawala (Mw. 1:28), akampa na ruhusa ya kuvitumia vyote (Mw.1:29-30) na kula matunda ya miti yote (Mw. 2:16), lakini kwa sharti moja tu, asile matunda ya mti wa katikati (Mw. 2:17). Maana yake jukumu la lipi ni jema na lipi ni baya sio jukumu lake mwanadamu bali la Mungu. Lakini ikawa ni kinyume chake, kwani mwanadamu akakaidi maagizo ya Mungu, akataka kuwa sawa na Mungu, akaamua lipi liwe jema na lipi liwe baya, akala alichokatazwa (Mw.3:6-7). Kwa kosa la kutotii amri na maagizo ya Mungu dhambi iliingia duniani. Mungu akawaadhibu kwa kosa lao la kuttotii maagizo yake (Mw. 3:14-19).

Baada ya kosa la wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva la kukaidi maagizo na amri za Mungu, walipoteza neema ya utakaso, sura na mfano wa Mungu ndani mwao na mahusiano mazuri na Mungu yakatoweka kwa sababu ya kiburi na ukaidi, ndipo taabu, mahangaiko na mateso yakamwandama mwanadamu kwa kujitenga kwake na Muumba wake. Hivyo walichokipoteza Adamu na Eva ndicho tulipokipoteza nasi kwani ubinadamu wetu ulikuwa tayari kwao. Hata hivyo Mungu kwa upendo wake na kwa huruma yake hakumwacha mwanadamu apotee na kuangamia kabisa. “Kwa nyakati mbalimbali na tofauti, mara nyingi na kwa namna nyingi na njia mbalimbali, Mungu nyakati zote amefanya juu kubwa kumrudisha kwake mwanadamu aliyejitenga kwa ukaidi wake (Waeb.1:1-4). Kwanza aliwaangamiza kwa gharika wakati wa Nuhu (Mw. 6:1-9:29), akafanya agano na Ibrahimu Baba wa imani (Mwa.22:1-18). Akaliteua taifa la Israeli, si kwasababu ya ubora wake bali kwa mpango na makusudi yake akalifanya kuwa taifa teule litakalo mpokea mwokozi. Kila walipokosea, Mungu aliwaadhibu kwa kupelekwa utumwani na walipotubu makosa yao, aliwasamehe na kuwarudisha katika nchi yao. Kwanza aliwapeleka utumwa wa Misri, akawatoa kwa mkono wa Musa akawavusha bahari ya shamu (Kut. 14:15 –15:1). Akafanya nao Agano na kuwapa Amri kumi ziwe mwongozo wa maisha yao (Kut. 19:3-24:8).

Ukaidi wa mwanadamu uliendelea. Mungu akawatuma waamuzi, wakaja pia wafalme na manabii wakati wa utumwa wa Babeli. Walipotubu na kumrudia, Mungu aliwasamehe na kuwarudisha katika nchi yao ya ahadi kwa mkono wa mfalme Koreshi wa uajemi. Lakini hata hivyo, Taifa la Israeli liliendelea kuwa na moyo mgumu kama binadamu wengine, kwa ukaidi wao, waliwatenda jeuri waliotumwa na Mungu na wengine kuwaua kabisa. Nabii Isaya akatabiri ujio wa masiha, mtumishi wa Mungu, mwana wa pekee wa Mungu, mpatanishi wetu na Mungu Baba. Aliyezaliwa na Bikira Maria muda ulipotimia. Mungu akamtambulisha siku ya ubatizo wake mtoni Yordani (Mk.1:9-10) na alipogeuka sura mlimani Tabor kuwa ndiye mwanaye mpendwa tumsikilize yeye (Mk.9:2-10). Huyu ndiye Kristo tuliyemtesa mateso mengi, tukampiga mijeledi (Yn. 19:1), tukamvika taji ya miiba kichwani (Yn.19:2,5), tukampiga makofi usoni (Yn. 19:3), tukamtemea mate, akiwa amechoka kabisa yuko hoi tukambebesha msalaba mzito kwenda kumsulibisha (Yn. 19:17), alipoanguka kwa udhaifu wa kimwili tulimpiga bila huruma, hatimaye tukamtundika juu ya Msalaba kwa kumpigilia misumari kama mhalifu katikati ya wahalifu (Yn. 19:18), alipoona kiu tukampa siki badala ya maji (Yn. 19: 28-30), alipokufa hatukuamini, tukaona haitoshi tukamtoboa ubavu wake kwa mkuki ikatoka damu na maji (Yn.19:34), ndizo chemchemi ya Sakramenti za Kanisa.

Watu wema wakamzika (Yn 19:38-40), siku ya tatu akafufuka ili arudishe tena uhusiano wetu Mungu Baba na kuwatokea wengi katika wanafunzi wake (Yn. 20). Usiku mtakatifu wa Pasaka tunaimba na kushangilia kuwa Kristo amefufuka kweli kweli Aleluya. Tumekombolewa kutoka utumwa wa dhambi. Ni usiku Mtakatifu, ni usiku wa wokovu. Ni usiku wa kuutangazia ulimwengu kuwa Kristo amefufuka yu hai. Ni usiku wa kuepuka nafasi za dhambi. Ni usiku wa amani, ni usiku wa kwenda mbio kuutangazia ulimwengu habari za ufufuko wa Bwana. Ni usiku wa kutanga habari za kaburi kuwa wazi, Kristo amefufuka, yu mzima nasi tunamtambua katika kuumega mkate. Kristo amefufuka kweli kweli, Aleluya.

Kesha la Pasaka

 

03 April 2021, 07:58