Sherehe ya Pasaka ya Bwana: Mashuhuda wa Ufufuko wa Yesu
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma
Amani ya Kristo Mfufuka iwe nanyi nyote! Mwinjili Yohane, katika simulizi la ufufuko tulilolisikia leo anajaribu kutuonesha wahusika wakuu watatu, wafuasi wake Bwana wetu Yesu Kristo, ambao walisukumwa na upendo mkubwa kwa Bwana na Mwalimu wao. Si tu walikuwa wana mahusiano na Yesu kwa vile alikuwa akitenda miujiza ila walielewa utume wake na kuwa na mahusiano naye ya pekee, ndio ufuasi unaojengeka katika upendo wa dhati na wa kweli. Upendo hauwezi kuondolewa na kifo. Unayempenda bado hata akiwa amekufa si tu utamlilia bali anabaki moyoni mwako siku zote. Na ndicho tunachokishuhudia katika Injili ya leo. Neno kaburi kwa lugha ya Kigiriki ni μενεμειον (menemeion) likimaanisha KUMBUKUMBU. Kumbukumbu hii ni ile ya kubaki moyoni, hivyo si kifo kinachoweza kuondoa mapendo yale ya awali. Labda hata baadhi yetu tunaweza kuwa mashuhuda wa hili, hasa pale anapokufa mtu uliyempenda kwa dhati, basi daima anabaki moyoni mwako, katika mawazo yako na hata katika sala zako za kila siku, ndivyo tufanyavyo kwa watu wanaokuwa wapendwa wetu.
Maria Magdalene, ni muhusika wa kwanza, ambaye Mwinjili Yohane anatuonesha kuwa alibaki na kumbukumbu ya Bwana na Mwalimu wake, kiasi ingali mapema alfajiri, ikiwa giza bado anaenda kaburini kwa yule aliyempenda. Alfajiri ni mwanzo wa siku mpya, ni wakati mwanga wa jua unachomoza na matumaini mapya yanaanza, kwani siku mpya inaanza. Mwanamke huyu naye kwa hakika alikuwa na giza ndani mwake kuhusu kifo cha Bwana na Mwalimu wake. Na ndio Mwinjili anaeleza kuwa ni alfajiri, maana yake mwanga unaanza kuonekana ila pia bado giza. Ni hali waliyokuwa nao hata wale marafiki zake Yesu Kristo, hali ya ndani yenye matumaini kiasi na pia mashaka kiasi. Kwani bado walikuwa hawajaelewa Maandiko kama tutakavyosikia pia hapo mbeleni katika Injili ya leo. Maria Magdalene anaona kuwa jiwe limeondolewa. Kuona kama tulivyotafakari katika Dominika zilizopita lina maana zaidi ya moja katika lugha ya Kigiriki. Maria Magdalena aliona kwa jicho la nyama, jicho la kawaida, ndio βλεπω (blepo) ni kuona kwa kawaida.
Ni tukio la kawaida katika historia kuwa ameshuhudia jiwe limeondolewa kaburini, ni ukweli usio na mashaka yeyote. Maria Magdalene anawakilisha wafuasi wa Yesu Kristo wanaompenda kwa dhati Bwana wao, bila Kristo maisha hayana maana, Kristo ndiye Bwana na mtawala wa maisha yangu. Ingawa kwake bado hajaweza kuelewa kuwa Yesu Kristo ni mzima, ila kwa mapendo yake kwa Bwana anatoka na kwa haraka anaenda kuwajuza mitume hofu yake kuwa wamemwondoa Bwana na hajui walipomweka. Upendo kwa Kristo daima unatualika nasi kutoka katika ubinafsi wetu na kwenda kuwajuza wengine yale tuliyoyashuhudia na kuyaona katika maisha yetu. Maria Magdalena ni kielelezo kizuri cha yule aliyepata kushuhudia kuwa jiwe limetolewa pale kaburini, aliyepata mang’amuzi ya uzima wa milele hana budi kutoka na kwenda kuwashirikisha wengine kwa haraka. Ndio sifa ya kila rafiki wa kweli wa Kristo Mfufuka, ni kuwa muinjilishaji, ni kuwa mmsionari, anayekwenda sio kwa misheni nyingine bali ile ya Kristo Mfufuka, kuwa shuhuda wa Habari Njema ya furaha, kuwa Kristo Mfufuka kweli, ni mzima, ameyashinda mauti!
Mwinjili Yohane mara moja anatutajia wahusika wengine wawili nao ni Simon Petro na yule mwanafunzi mwingine aliyependwa na Bwana, huyu wa pili hamtaji jina lake. Yatosha katika tafakuri yetu kubaki pasipo kutaja jina la huyu mwanafunzi mwingine. Hawa wanafunzi wawili tunaambiwa kuwa nao walitoka kwa haraka kuelekea kule lilipo kaburi. Wanafunzi hawa yawezekana nao kama Maria Magdalena wameshtushwa na habari ya kaburi kuwa wazi, na hivyo wanakimbia kwenda kuona ni nini kimetokea juu ya Bwana na Mwalimu wao. Baada ya maziko yake ni kama dunia ilisimama, na kujawa na hofu na mashaka makubwa kiasi cha kujifungia, ila leo mapema asubuhi tunaona wote wapo katika haraka ya kwenda kaburini baada ya kupokea taarifa ya mtu aliyeona kuwa jiwe limeondolewa. Wanakimbia wote wawili kuelekea kaburini ila yule mwanafunzi mwingine anakimbia kwa haraka zaidi na kufika mapema pale kaburini. Ni lugha ya picha kuonesha si tu kwamba alikuwa kijana bali upendo wake kwa Bwana na Mwalimu ulikuwa mkubwa hivi hakuona kitu cha kumchelewesha na anafika mara moja kaburini, naye pia anainama na kuona kama alivyoona Maria Magdalene.
Huyu mwanafunzi ambaye alipendwa na Bwana, anaonekana mara kadhaa katika Maandiko Matakatifu bila kutajwa jina. Ndiye pamoja na Andrea wanamfuata Yesu, na kumuuliza wapi anaishi na kukaa naye siku nzima. Hivyo tangu mwanzo alikuwa na hamu na shauku isiyoelezeka ya kumuona na kukaa na Bwana. Yohane 1:35-40. Ndiye anayesikika pia katika karamu ile ya mwisho ambapo Simon Petro anampungia ili amuulize Bwana ni nani atakayemsaliti na tunaambiwa alikuwa kifuani mwa Bwana. Yohane 13:23-26. Ndiye yeye aliyemfuata Yesu bila woga wakati wa mateso na kuingia naye katika behewa la kuhani mkuu. Yohane 18:15-27. Ni yeye anakuwepo hata pale Kalvario na ndipo Yesu anamkabidhi Mama yake kwa mwanafunzi aliyempenda. Yohane 19:25-27. Ndiye yeye hata leo katika Injili ya ufufuko anakimbia kwa haraka na pia anakuwa wa kwanza baada ya kuona anaamini. Yohane 20:3-10. Ndiye mwanafunzi huyu huyu aliyependwa anayemtambua Bwana Mfufuka pembeni ya ziwa Galilaya. Yohane 21:7.
Hata walipoalikwa na Yesu Kristo mfufuka kumfuasa tunaona Simon Petro anakosa ujasiri na hivyo kuambatana na huyu mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda. Yohane 21:20-25 Kwa nini basi hatajwi kwa jina. Hakika ni mwakilishi au kielelezo kwa kila mwanafunzi anayempenda kwa dhati na moyo Bwana wetu Yesu Kristo. Hana jina kwani kila mmoja wetu anaalikwa kuweka jina lake. Anamfuata Yesu Kristo bila kuwa na mashaka au uwoga wowote, anabaki kuwa mfuasi hata nyakati zile hatarishi, anaweka kando usalama wake na hata mali zake au ndugu na jamaa zake kwa ajili ya kumfuasa Yesu Kristo. Yupo tayari hata kutoa maisha na uhai kwa ajili ya Yesu Kristo. Wanafunzi hawa wanafika kaburini na kuona kaburi ni tupu na kuona zile sanda pamoja na leso zikiwa kando sehemu ya kichwa chake wakati wa maziko. Hivi wanaona vitu vya kawaida kabisa na hakuna lolote la ajabu kati ya sanda na leso aliyofungwa nayo kichwani Bwana wao wakati wa maziko.
Yatosha kutafakari pamoja na Mtakatifu Yohane Krisostom najaribu kuweka tafsiri yangu kwa kutumia maneno yangu: “Yeyote ambaye angelichukua mwili wa Yesu, hakuwa na sababu kwanza ya kuondoa zile sanda na kile kitambaa cha leso, wala asingekuwa na sababu ya kujisumbua kuanza kuziviringisha na kuziweka pale pembeni, hivyo mwili wake haukuwa umeondolewa au kuibiwa.” Mtume Petro baada ya kuona haya, akili yake ni kama ilisimama na kubaki na mshangao mkubwa ila mwanafunzi yule mwingine hakuishia katika kushangaa tu bali aliona na kuamini. Mbele ya kaburi, sanda, leso, huyu mwanafunzi anaona ushindi wa kifo yaani ufufuko. Ni kilele cha safari ya imani, ni kilele ambacho mimi na wewe tunaalikwa kufikia katika adhimisho hili la Pasaka. Huyu mwanafunzi mwingine anaona si tu kwa jicho la nyama au kawaida bali anaona kwa jicho la imani, ndiye ile aina ya pili ya kuona kwa kigiriki ni οραω (orao), ni kuona kwa jicho la ndani, yaani, la imani.
Mwinjili Yohane anatuonesha kuwa walikuwa bado hawajaelewa Maandiko na ndivyo safari yetu ya imani haina budi kuongozwa na Neno la Mungu, sio tu kwa macho ya kibinadamu na ishara za nje zinazoweza kutufikisha katika kilele cha imani yetu, bali kwa Neno la Mungu. Mfuasi wa kweli hana haja na ishara za nje au miujiza bali yatosha Neno la Mungu kumuongoza katika maisha yake ya ufuasi. Ni kwa mwanga wa Pasaka haunabudi kutuongoza katika maisha yetu ya kila siku. Wale wanafunzi wanarudi nyumbani kwao sio tu kuendelea na maisha yao ya awali bali sasa maisha yao yakiwa na maana kwa mwanga wa Kristo Mfufuka. Ndio ujumbe wa Pasaka kuongozwa na Mwanga wa Kristo katika maisha ya kila mmoja wetu. Kuwa na muono mpya, muono unaoongozwa na kweli za Injili, baada ya kukutana na Kristo Mfufuka! Ni kukubali kuongozwa na mantiki mpya, ndiyo ya Kristo Mfufuka na kamwe tusibaki na ile ya ulimwengu huu, kifo hakileti tena uoga wala wasiwasi kwani tunaamini katika maisha ya utukufu na ya milele mara baada ya maisha yetu ya hapa duniani.
Ni mwaliko wa kutoka na kwa haraka kumtangaza Yesu Kristo Mfufuka kwa maisha yetu ya kila siku bila uwoga na hofu kwani Kristo Mfufuka anatujaza maisha mapya yenye amani, matumaini na furaha ya kweli, kwani sisi ni huru na wana wa Mungu kwani kwa ufufuko wake mauti hayana nguvu tena. Kwa ufufuko wake sisi tumekuwa wana wa Mungu na hivyo hatuna budi kuchuchumilia mambo ya juu Kristo aliko kama anavyotualika Mtume Paulo. Ufufuko ni uumbaji mpya, Dominika ya Pasaka ni sherehe ya kuadhimisha mwanzo mpya, uumbaji mpya, ni maisha mapya, maisha ya kuwa wana kweli na warithi pamoja na Mwana pekee wa Mungu, yaani, Kristo Mfufuka. Pasaka inatutaka nasi kuwa kweli watu wapya kama nilivyotangulia kuonesha hivi punde hapo juu. Pasaka haina maana ya kula na kunywa, haina maana ya kufanya sherehe bali kuruhusu kuvaa vazi jipya, vazi la uumbaji upya, ndilo vazi la maisha ya neema, maisha ya urafiki na muungano na Mungu.
Pasaka ni uumbaji wa jumuiya mpya ya Mungu, yaani Kanisa. Kwa Kiebrania, Kanisa ni “Qahal”, yaani kusanyiko na kwa Kigiriki tafsiri sisisi yake ni “Synagoga”, likiwa na maana ile ile. Lakini katika Kigiriki cha Agano Jipya, neno linalotumika ni “Ekklesia”, likiwa ni neno linalotokana na maneno mawili ya Kigiriki, nayo ndio ek na kalein, yakiwa na maana ya kuitwa kutoka nje, ndio Kanisa la Kristo linaloalikwa kutoka kaburini, kutoka katika hali ya kujifungua kwa hofu na uwoga na badala yake kwenda kwa haraka na kuinjilisha, kuwashirikisha wengine Habari Njema ya Wokovu. Kama Kanisa na kama mtu mmoja mmoja sote tunaalikwa kutoka katika giza la kaburi, kutoka katika giza la dhambi na kuwa watu wapya, tunaobeba furaha ya kukutana na upendo na huruma ya Kristo Mfufuka, na hivyo kuwafanya na wengine pia wakutana na Kristo Mfufuka, Mwanga wa kweli kwa maisha ya kila mwanadamu. Huu ndio ujumbe na maana ya Pasaka, ni sherehe ya Habari Njema, yaani mwanga wa Kristo Mfufuka unaotutoa kutoka katika giza la kaburi! Nawatakia Pasaka njema yenye kila amani na furaha yake Kristo Mfufuka.