Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu: Sherehe ya Pasaka ya Bwana: Ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Tafakari ya Neno la Mungu: Sherehe ya Pasaka ya Bwana: Ushindi dhidi ya dhambi na mauti. 

Pasaka ya Bwana: Matumaini, Imani na Uzima wa Milele!

Pasaka ya Bwana: Bila ufufuko wa Kristo, mwanadamu asingekuwa na tumaini la uzima wa milele. Ni kwa jinsi hiyo, Pasaka ndiyo imekuwa kiini cha habari njema ambayo tangu mwanzo Kanisa limetangaza na kuitolea ushuhuda. Mafundisho yale ya msingi (Kerygma) ambayo Mitume waliyatangaza, muhtasari wake ulikuwa ni Pasaka, yaani Kristo aliteswa, Kristo alikufa na Kristo alifufuka.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Jumapili hii ni Dominika ya Ufufuko wa Bwana, ni adhimisho la Sherehe ya Pasaka, sherehe ya ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi na giza la mauti. Ufafanuzi wa Masomo ya Misa kwa ufupi: Kabla hatujayangalia masomo ya sherehe hii ya Pasaka, ni muhimu tujikumbushe maana na uzito wa sherehe hii yenyewe kwa Wakristo. Pasaka ndiyo msingi wa imani ya kikristo. Kristo aliukamilisha ukombozi wetu pale Msalabani. Lakini kama asingefufuka, ulimwengu usingejua kama umekombolewa. Yesu mwenyewe angeonekana kama mwanadamu mwingine yeyote yule. Tena zaidi ya hapo, angeonekana tu kama mwanaharakati aliyeshindwa. Asingekuwa kipimo cha maisha ambayo watu wote wanaitwa kuyafuasa na wala asingekuwa yule ambaye watu wanaweka imani na maisha yao yote kwake. Kama anavyoandika Mtume Paulo “kama Kristo hakufufuka, basi kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure” (1Kor 15:14).  Kristo, ni kwa ufufuko wake ndio ameyapa maana mambo yote aliyoyafanya akiwa duniani: kuzaliwa kwake, mafundisho yake, miujiza aliyofanya, maisha yake yote na kifo chake msalabani.

Katika maisha ya Wakristo na maisha ya wanadamu wote kwa ujumla, ufufuko wa Kristo ndio umefungua mlango wa kuyaona maisha katika namna mpya. Na namna hii mpya ni kuwa maisha hayaanzi mtu anapozaliwa na kuisha pale anapokufa, maisha yanaendelea baada ya kifo. Baada ya maisha ya hapa duniani, mwanadamu anafunguliwa maisha ya umilele. Na wa kutufungulia maisha hayo ni Kristo kwa ufufuko wake. Hii ndiyo sababu Maandiko Matakatifu pamoja na taalilimungu yote ya maisha baada ya kifo hupata mfano wake katika ufufuko wa Kristo. Tunasikia mara kwa mara kiitikizano hiki “Kama vile Kristo alivyofufuka vivyo hivyo wote walio na imani watakavyofufuliwa”. Bila ufufuko wa Kristo, mwanadamu asingekuwa na tumaini la uzima wa milele. Ni kwa jinsi hiyo sasa, Pasaka ndiyo imekuwa kiini cha habari njema ambayo tangu mwanzo Kanisa limetangaza na kuitolea ushuhuda. Mafundisho yale ya msingi (Kerygma) ambayo Mitume waliyatangaza, muhtasari wake ulikuwa ni Pasaka, yaani Kristo aliteswa, Kristo alikufa na Kristo alifufuka.

Tukirudi sasa katika masomo ya Misa, somo la kwanza linatoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume (10:34a,37-43). Linatuletea hotuba ya Mtume Petro, hotuba ambayo aliitoa baada ya kuona wongofu wa askari asiye myahudi. Kiini cha hotuba anayoitoa ni fumbo la Pasaka. Anazungumzia maisha ambayo Yesu aliishi; anazungumzia mateso yake, kifo chake na hatimaye ufufuko. Petro anatafsiri anachokiona kutoka katika nguvu ya fumbo la Pasaka. Yaani kitendo cha mtu wa mataifa kuongoka na kuwa mkristo kwake ni alama kuwa nguvu ya Kristo mfufuka inatenda kazi. Na tukiiangalia vizuri hotuba hii anayoitoa Mtume Petro, inafafana kabisa na ile aliyoitoa mwanzoni siku ile ya Pentekoste. Hii yote inatupa picha ya namna ujumbe wa Pasaka ulivyopewa nguvu na kanisa la mwanzo. Haukuwa ujumbe tu bali ulikuwa ni nguvu yenyewe inayotenda kazi ndani ya Kanisa.

Somo la pili linatoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (3:1-4). Lenyewe linajikita kuonesha hali mpya ya maisha ambayo ufufuko wa Kristo umefungua. Haya ni maisha ya umilele tofauti na yale yanayokoma lakini pia ni maisha ambayo mwanadamu amepatanisha wa Mungu ikiwa ni tofauti na maisha mwanadamu aliyoishi kabla ya ufufuko wa Kristo. Kumbe hapa Paulo anawaasa Wakolosai waishi kwa kuyaelekea zaidi maisha yale ambayo Kristo amewafungulia. Wasiishi wakitaka kurudi katika hali ya mwanzo, hali ya kutokuwa na matumaini ya umilele wala ile hali ya kutokuwa karibu na Mungu. Anasema Paulo “yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketu mkono wa kuume wa Mungu”.

Somo la Injili ya dominika ni kadiri ya Mwinjili Yohane (20:1-9). Ni Injili inayoleta ushuhuda wa mwanzo kabisa waliokuwa nao wakristo juu ya ufufuko wa Yesu. Ushuhuda huu unajijenga juu ya tukio la kukuta wazi kaburi alimokuwa amezikwa Yesu. Maria Magdalena, Petro na yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda  hawakuweza kuelewa wala kueleza ni nani aliyeliondoa jiwe kubwa lililokuwa katika mlango wa kaburi. Na wala hawakuweza kuelewa na kueleza ni nani aliyetoa sanda na vitambaa vilivyoufunga mwili wa Yesu na akaviweka kando. Kukuta kaburi wazi kunakuwa ni hatua ya kwaza inayojenga hoja na imani kuwa Yesu amefufuka. Hoja hii inapochukuliwa pamoja na unabii uliokwisha tolewa juu ya Masiha, na tena hoja hii inapochukuliwa na kile ambacho Yesu mwenyewe alikuwa amekwisha kisema kuhusu kifo chake, imani juu ya ufufuko wa Yesu inazidi kupata uhakika. Tunaona “kweli Bwana amefufuka, amefufuka kama alivyosema”.

Katika simulizi hili la ufufuko wa Yesu, mwinjili Yohane alalenga pia kutoa fundisho kubwa kupitia mwanafunzi ambaye hamtaji kwa jina bali anasema tu ni “yule ambaye Yesu alimpenda”. Ni mwanafunzi huyu ambaye anakimbia upesi kuliko Petro lakini haingii kaburini hadi alipoingia Petro. Ni yeye alipoingia “akaona na kuamini”. Ni kana kwamba Petro na Maria Magdalena hawakuwa bado wamefumbuliwa macho ndiyo maana injili inapoendelea inasema “kwa maana hawajalifalifahamu bado andiko ya kwamba imempasa kufufuka. Mwanafunzi huyu ni nani? Katika Injili ya Yohane, mwanafunzi huyu ambaye Yesu alimpenda anadhaniwa kuwa ni Yohane mwenyewe aliyeandika Injili hii. Lakini pia inaonekana ni kiwakilishi cha wote wanaomwamini Kristo, wote ambao Kristo alikuja kwa ajili yao na ndio hao ambao Kristo anawapenda. Mara zote ambazo Yohane anamtaja mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda ana lengo la kutoa mwaliko wa pekee kwa wote wanaomwamini Kristo. Na mwaliko huo sio mwingine bali ni mwaliko wa imani.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Pasaka ni baragumu linalotangaza furaha kote ulimwenguni. Ni furaha ya ulimwengu kukombolewa, ni furaha ya ushindi wa maisha dhidi ya kifo, uzima dhidi ya dhambi; “hii ndiyo siku aliyoifanya Bwana, tuishangilie na tuifurahie”. Sherehe ya Pasaka inakuja kutangaza matumaini mapya katika maisha yetu. Matumaini kuwa Mungu hajatuacha katika taabu zetu, hajatuacha katika unyonge wetu wala katika mahangaiko ya maisha tuliyonayo. Kwa zaidi ya mwaka sasa, ulimwengu mzima umepita katika kipindi kigumu kwa sababu ya janga la ugonjwa wa korona. Na hata sasa bado dawa ya ugonjwa huu haijapatikana. Wahanga wa ugonjwa huu ni wengi na madhara yake katika nyanja zote za maisha bado yanaendelea. Ni kama sote tupo bado katika kwaresima isiyoona Pasaka. Na inafika wakati ni kama tunajiuliza “Mwenyezi Mungu haoni kuwa tunaangamia? Ziko wapi nguvu zake na upo wapi uwezo wake?

Pasaka hii iwe kwetu alama mpya ya matumaini kuwa Mungu wetu ambaye kwa njia ya Kristo amezishinda nguvu za dhambi na mauti atashinda pamoja nasi. Yeye mwenyewe azidi kubariki jitihada zetu za kupambana na janga hili na zaidi atufunulie Yeye mwenyewe njia ile ifaayo kupita ili tuwe salama. Kwa matumaini tuyarudie na tuyafanye sehemu ya sala yetu maneno haya ya Mbiu ya Pasaka “Basi ee Bwana utujalie nyakati za furaha na amani kwa sikukuu hii ya Pasaka. Amina”.

Pasaka ya Bwana

 

03 April 2021, 17:14