Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Pasaka: Huruma ya Mungu: Waamini wanatafakari ushuhuda wa Fumbo la Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafua na Ufunuo wa huruma ya Mungu Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Pasaka: Huruma ya Mungu: Waamini wanatafakari ushuhuda wa Fumbo la Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafua na Ufunuo wa huruma ya Mungu 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 2 ya Pasaka: Imani na Huruma

Mwinjili Yohane anamtumia Mtume Tomaso kuwa ni mfano hai wa wale waamini ambao bado wanaona shaka kuhusu Fumbo la Uufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu na wanataka kuona na kugusa Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu. Kwa hakika Madonda Matakatifu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Hii ni Jumapili ya Huruma ya Mungu, yaani!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani ya Kristo Mfufuka! Dominika ya pili ya Pasaka pia inajulikana kuwa ni Dominika ya Huruma ya Mungu. Pasaka ni sherehe ya ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo, ni sherehe ya upendo na huruma ya Mungu kwetu, ni kwa mateso, kifo na ufufuko wake, sisi tumekombolewa, sisi tumejaliwa tena hadhi ya kuitwa wana wa Mungu, warithi pamoja na Mwana pekee wa Mungu, ni rafiki zake Mungu! Sehemu ya Injili Takatifu ya leo tunaweza kuigawa katika sehemu kuu mbili; Yohane 20:19-23 ambapo Yesu Kristo Mfufuka anawavuvia Roho Mtakatifu wanafunzi wake na kuwapa uwezo wa kuondolea watu dhambi zao na ya pili ni kuanzia aya ya 24-31 ambapo tunasikia zaidi juu ya simulizi maarufu la Tomaso asiyeamini mpaka amwone na kumgusa Yesu Kristo Mfufuka. Simulizi la Mtume Tomaso linatuchia maswali mengi kama ni kweli alikuwa Mtume pekee au mwanafunzi pekee aliyepata ugumu kuamini juu ya ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa hakika hapana, hakuwa mwanafunzi pekee aliyepata ugumu wa kuamini juu ya ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo, na ugumu huu si tu kwa nyakati zile za mitume bali pia hata katika nyakati zetu za leo. Hata leo wapo wengi wanaopata ugumu kuamini Ufufuko wake Yesu Kristo kutoka kwa wafu. Wapo wanaohoji na kuona ni suala la kufikirika tu na kusadikika kwa wale wanaopenda kuamini!

Mwinjili Marko 16:14 anaonesha jinsi Yesu Kristo Mfufuka anavyowaonya wanafunzi wake dhidi ya kutoamini kwao. Mwinjili Luka anaonesha pia jinsi Yesu Kristo Mfufuka alivyowatokea wanafunzi wake na kuwauliza kwa nini wanafadhaika mioyoni mwao. Luka 24:38. Mwinjili Mathayo naye anatuonesha kuwa Yesu Kristo Mfufuka anawatokea wanafunzi wake kwenye Mlima Galilaya na baadhi yao bado walikuwa na mashaka na wasiwasi. Mathayo 28:17. Hivyo, ni wengi walikuwa na mashaka na wasiwasi na sio tu Mtume Tomaso pekee. Mwinjili Yohane anamtumia Mtume Tomaso kama kielelezo cha wafuasi wengine wanaopata ugumu wa kuamini katika ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Wapo wengi pia wanaotaka uthibitisho wa kisayansi juu ya ukweli huu wa imani. Sayansi inataka uthibitisho wa kuonekana kwa macho ya nyama ili kukiri ukweli wa jambo. Ni lazima kuthibitishwa katika maabara. Wapo wengi hata leo wanaotaka kweli za kiimani pia ziweze kuthibitishwa kisayansi katika maabara, la sivyo wapo wanaokuwa na mashaka na kweli zisizoweza kuthibitishwa kisayansi katika maabara. Tomaso anawakilisha kundi hili, kwani kwake lazima aone na kugusa madonda ya Yesu Kristo Mfufuka ndipo aamini.

Na ndio wainjili Marko, Luka na Mathayo pia wanatuonesha kuwa hata wanafunzi wengine pia walikuwa na safari ndefu na ngumu ya kufikia kuamini juu ya Ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo.  Mwinjili Yohane anamtumia Tomaso kama mwakilishi na kielelezo cha wengi wanaohitaji kuona na kugusa ili waamini, mathalani baadhi ya wanasayansi wengi katika ulimwengu wa leo. Ni safari ya imani, ni safari isiyokuwa rahisi bila kuangaziwa au kurejelea Neno la Mungu mwenyewe kama tunavyosikia katika simulizi la wanafunzi wa Emau, ni katika adhimisho la Kuumega mkate, hapo nasi tunaweza kukutana na Kristo Mfufuka. Kwetu ni heri walioona ila kwa Yesu ni kinyume chake, ni heri kwa wale wasioona na wakaamini. Imani ya wale wasioona ni imani halisi, ni imani ya kweli. Imani ni kukutana na Yesu Kristo Mfufuka katika maisha yetu ya kila siku, ni tukio katika historia ya kila mmoja wetu. Ni kumwona Yesu Mfufuka sio kwa jicho la nyama au kwa mikono ya nyama, bali ni kukutana na Nafsi ya Yesu Kristo Mfufuka.

Ni kitendo cha kiimani. Ni katika Neno lake na katika Sakramenti za Kanisa na kwa namna ya pekee kabisa katika Adhimisho la Kuumega Mkate, ni Yesu Kristo Mwenyewe anayejitoa mwili na damu yake katika Ekaristi Takatifu. Mwenyeheri Carlo Acutis, kijana mwenye fadhila nyingi za Utakatifu anatuonesha kuwa tuna heri sisi tunaoishi katika ulimwengu wa leo kuliko wale walioishi na Yesu Kristo zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita, sisi leo alipenda kusema tunaweza tena kirahisi kabisa kukutana na Yesu Kristo Mfufuka katika makanisa yetu, kwani ni kweli Yesu Kristo Mfufuka anakuwepo katika uhalisia wake katika tabernakulo, katika maumbo yale duni ya mkate na divai, ni huko tunaweza kuongea na kukutana naye, kumuomba na kumshukuru, kumlilia na hata kumsifu! Mwinjili Yohane anamwonesha tena Mtume Tomaso katika Injili yake; Katika tukio la kufufuliwa kwake Lazaro. Yohane 11:16. Mtume Tomaso bado hajamuelewa Yesu Kristo kuwa ndiye Bwana wa uzima na hivyo anaongea ikiwapasa kufa naye basi hawana budi kufa naye. Ni Tomaso pia aliyemuuliza Bwana hatujui uendako nasi tutaijuaje njia. Yohane 14:5 Ni Tomaso anayeoneka mwenye mashaka bado juu ya utambulisho halisi wa Yesu Kristo.

Mwinjili Yohane pamoja na kutuonesha ugumu wa kuamini kwa Mtume Tomaso ila bado ndiye anayekuwa wa kwanza kumkiri kuwa ni Bwana na Mungu kweli. Yohane 20:28 Ameanza na mashaka mengi ila mwishoni ameweza kufikia ukweli wa imani. Katika safari hii ya Tomaso, tunabaki na maswali na hasa Yesu Mfufuka anayewatokea tena jioni ya siku ile ile badala ya kuwaonesha sura yake, tunaona anawaonesha mikono na ubavu wake. Sura ya Kristo Mfufuka ni katika madonda yake ya mikono na ubavu wake uliochomwa kwa mkuki, kumbe sura kweli ya Mungu ni katika mateso yake kwa ajili ya Upendo wake kwa mwanadamu. Sura ya Mungu ni Upendo wake. Ni mikono inayotumika kwa ajili ya wadogo, ndivyo mimi na wewe tunaalikwa kuhudumia wengine kama wafuasi wa ufufuko. Ni ubavu wake unaotoa maji na damu kama ishara za uzima ili kwake nasi tunapata uzima wa kweli na wa daima. Ni katika madonda yake hapo tunaonja Huruma ya Mungu kwa mwanadamu, upendo usio kifani wa Muumba wetu kwetu viumbe wake. Ni katika kujitoa kwake hapo nasi tunapata uzima wa kweli, ni katika kuutafakari Msalaba, tunauona utukufu wa ufufuko wake!

Ni upendo huu Yesu Kristo Mfufuka anawapulizia uwezo wa Roho Mtakatifu ila kwa nguvu hiyo waweze kuwapelekea wadhambi upendo wa Mungu, ndio Huruma ya Kimungu. Kwa kifo chake sisi tumepona, ni kwa madonda yake sisi tumepata wokovu. Anawapa uwezo wa kuwaondolea watu dhambi. Neno la Kigriki ni φιεμι (fiemi) likimaanisha kwa tafsiri sisisi ni kukatakata vipande vipande, kuondoa na kutokomeza kabisa dhambi. Na ndio Dominika ya leo Mtakatifu Yohane Paulo II ameitenga na kuiita Dominika ya Huruma ya Mungu. Kristo Mfufuka ni upatanisho kati yetu na Mungu Baba, ni Mkombozi na Mwokozi wetu. Tomaso anaitwa pia Pacha, Mwinjili Yohane anasisitiza juu ya jina hili ili kumaanisha ni pacha wa kila mmoja wetu, tunaokuwa pia katika safari ngumu ya kuweza kufikia imani na kumkiri Yesu Kristo Mfufuka kuwa ni Bwana na Mungu wetu. Tomaso Mtume ni baada ya kusikia mwaliko wa Yesu Kristo Mfufuka, ni kwa sauti ya Mfufuka anamtambua kuwa ni Bwana na Mungu; ni hakika aliyofikia sio kwa kumgusa bali kwa kumsikia na kumsikiliza.

Ni katika Neno lake tunakutana na Yesu Kristo Mfufuka, anayetualika nasi kushika madonda ya mkono wake na ubavu wake. Ni kupitia Neno lake nasi tunakutana na Kristo Mfufuka, na pia kwa njia ya masakramenti tunagusa na kumuona Yesu Kristo Mfufuka. Ni ishara za wazi zinazomtambulisha Mfufuka kwetu katika safari yetu ya kiroho. Mwinjili Yohane anaiita miujiza aliyotenda Yesu Kristo kuwa ni ishara. Ishara hizi Yesu alizifanya sio kwa ajili ya kuwafanya watu wamshangae ila kuwafunulia uwezo na nguvu za Kimungu ndani mwake. Ni ishara za kumtambulisha Yesu Kristo. Ni utambulisho wake ili kwa ishara hizo tuweze kukiri Umungu wake. Na Kristo Mfufuka anawatokea wanafunzi wake siku ya Dominika yaani Jumapili, na ndio siku ya Ufufuko wake, Siku ya Bwana, “Dies Domini”. Na ndio Dominika tunaisikia sauti ya Kristo Mfufuka katika Neno lake na pia tunamgusa Kristo Mfufuka katika Ekaristi Takatifu. Dominika ni Pasaka ya daima, ni adhimisho la upendo wa Kristo Mfufuka anayenena na kutujitoa Mwili na Damu yake kama chakula chetu cha kiroho. Dominika njema ya Huruma ya Mungu.

08 April 2021, 12:06