Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Pasaka; Jumapili ya Huruma ya Mungu: Ushuhuda wa Wakristo wa Kanisa la Mwanzo katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Pasaka; Jumapili ya Huruma ya Mungu: Ushuhuda wa Wakristo wa Kanisa la Mwanzo katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu. 

Jumapili 2 Kipindi cha Pasaka: Jumuiya ya Wakristo! Imani!

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya huruma ya Mungu, Mama Kanisa analeta ushuhuda wa wakristo wa Kanisa la mwanzo katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Imani katika Kristo Yesu ilipaswa kutangazwa kwa maneno lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda! Imani na Amani ni zawadi ya Kristo Mfufuka!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya neno la Mungu Dominika ya pili ya Pasaka mwaka B. Masomo ya Dominika hii ya pili yanatualika kuihifadhi furaha ya Pasaka kama zawadi ya thamani kubwa na ya kudumu. Katika masomo ya dominika hii kuna wahusika wakuu ambao ni; jumuiya ya kwanza ya Wakristo iliyojengwa na Mitume kabla na baada ya Pentekoste, jumuiya ya Wakristo miaka 60 baada ya ufufuko wa Yesu, na Jumuiya ya mitume na Yesu kabla ya kupaa kwake mbinguni. Katika somo la kwanza la Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo 4:32-35), tunapata simulizi la maisha ya Jumuiya ya kwanza ya Wakristo iliyojengwa na mitume kabla na baada ya Pentekoste. Ni jumuiya changa kiimani ndiyo maana Mtume Petro anawaambia katika maneno ya wimbo wa mwanzo akisema; “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu, aleluya” (1Pet.2:2). Somo hili linatupa picha halisi ya uzuri wa Kanisa la mwanzo, jumuiya ya kwanza ya Wakristo jinsi waliovyoishi kwa pamoja na upendo, na umoja wao ulivyojidhihirisha wakiishi kwa furaha kubwa, furaha waliyoipata katika Kristo Mfufuka hivyo wakawa na moyo mmoja na roho moja, wakiishi kwa kupendana.

Kwa upendo, waliweka mali yao pamoja wakagawana kadiri ya uhitaji wa kila mmoja, wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika. Uchoyo na mkono wa "birika" kwao ulikuwa ni mwiko, ulafi na wizi haukuwa na nafasi. Kupendana kati yao ndiko kulikuwa msingi wa kuhubiri Injili. Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote. Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa jamii ya jumuiya ya kikristo, kuishi kwa pamoja na umoja na kwa kupendana. Upendo ni utambulisho wetu. Ni mwaliko kwetu sisi sote tuliobatizwa na kukiri kuwa Yesu ndiye Bwana na mwokozi wa maisha yetu, katika kipindi hiki cha pasaka kudumisha maisha ya kijumuiya kuishi pamoja tukisaidiana katika kumjua, kumpenda na kumtumikia Mungu katikati yetu, hasa kwa walio wadogo na dhaifu. Tuuvue utu wa kale uliojengeka katika ubinafsi, wivu, ulafi, ufisadi na wizi kwa maana vitu vyote vilivyopo Mungu aliviweka vitufaa kwa pamoja.

Somo la pili la Waraka wa Kwanza wa Mtume Yohane (1Yn 5:1-6), ni mashauri ya Yohane kwa jumuiya ya Wakristo walioishi baada ya miaka ya 60 hivi baada ya Ufufuko wa Kristo. Wakristo hao walikuwa chini ya madhulumu na mateso makali, na wengi walikuwa wameanza kulegea katika imani yao. Yohane aliwatia moyo akiwaambia kuwa watakuwa watoto wa Mungu wakisadiki kuwa Yesu ni “Kristo”, Mkombozi wao. Na ya kuwa watazishinda nguvu zimpingazo Mungu wakisadiki kuwa Yesu ni kweli Mwana wa Mungu. Hivyo wadumu katika upendo, wakipendana kidugu. Ndivyo tunavyopaswa kuwa hata sisi katika nyakati zetu, kuwa na ujasiri wa kuishuhudia Imani yetu bila kuogopa, huku tukiishi kwa kupendana. Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yn 20:19-31), inaeleza habari za Mitume na Yesu kabla ya kupaa kwake mbinguni. Kwa kuwa Yesu alifufuka siku ya kwanza ya Juma, wakristo wa kwanza waliitukuza siku hiyo wakaifanya siku rasmi ya sala na kuadhimisha Ekaristi Takatifu wakiwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi. Katika hali hii Yesu anawatokea na kusimama katikati yao.

Maneno ya kwanza ya Yesu ni; “Amani iwe kwenu” nao wakajaa furaha walipomwona. Naye “akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.” Ni habari njema ya kuwekwa kwa Sakramenti ya upatanisho, sakramenti ya ondoleo la dhambi. Nasi hatuna budi kuipokea kwa moyo wa shukrani ili tupate Amani na furaha ya kweli ndani mwetu. Roho Mtakatifu aliyewavuvia Yesu baada ya ufufuko wake ndiye anayeliongoza Kanisa tangu wakati wa mitume, ndiye Kiongozi wetu hata leo. Ni kwa njia ya Roho Mtakatifu Kristo Yesu aliyewahakikishia mitume wake kwamba yuko katikati yao mpaka ukamilifu wa dahari anaendelea kuwa kati yetu kwa njia ya viongozi wa Kanisa ambao wanatiririka katika mti ule ule na wanatumia mafundisho yale yale ya mitume, na Yesu tunakutana naye katika neno lake na katika sakramenti zake hasa ya Ekaristi Takatifu tunapoumega mkate. Kila Dominika tunakutana na Kristo Mfufuka anayekuja kati yetu kama alivyowajia mitume jioni ile ya kwanza ya ufufuko wake. Kristo anakuwepo kila wanapokutana waamini kwa sala, kila linaposomwa Neno la Mungu na kuhubiriwa, kila zinapoadhimisha sakramenti zake alizozikabidhi kanisa hasa Ekaristi Takatifu ambayo Yeye mwenyewe yupo mzima kabisa katika maumbo ya mkate na divai.

Ni katika jumuiya, ndipo tunakutana na Yesu. Katika Injili ya dominika hii tunaona jinsi, Tomaso baada ya kutoka nje ya jumuiya alivyokosa bahati ya kumwona Yesu Mfufuka. Hiki ni kitu ambacho hatupaswi kusahau hata mara moja, kila tunapojitenga na jumuiya ya kikristo, kila tunapokosa kushiriki katika sala za jumuiya na katika maadhimisho ya Sadaka ya misa takatifu siku za dominika, tunakosa nafasi ya kukutana na Kristo Mfufuka, na tunakosa zile zawadi ambazo Kristo Mfufuka anazikabidhi kwa Jumuiya inayosali hususani, amani, furaha, msamaha na haki ya kuwa wana wa Mungu. Kristo anawapa wale wote wanaoshiriki kwa moyo mmoja Ibada pamoja na jumuiya, zawadi zile zile ambazo aliwapa mitume katika ile siku ya ufufuko wake. Yesu aliwapa mitume wake amani. Alianza kuwapatia kile ambacho walikihitaji zaidi. “Amani”, “shalom” ndiyo zawadi ya kwanza ya Yesu mfufuka kwa mitume wake: “Amani kwenu” (Jn. 20, 19). Kwa kusikia maneno haya woga na wasi wasi ukawatoka, wakajawa na furaha kubwa na amani (Jn. 20, 20). Kinyume chake ni kweli, amani na furaha hutokomea tunapomfukuza Kristo mioyoni mwetu kutokana na dhambi hasa pale tunapojitenga na jumuiya zetu.

Mtume Thomaso alipata kumwona Yesu mfufuka pale tu aliporudi na kuamua kukaa ndani ya jumuiya. Injili inasema wazi kuwa: “Baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu. Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako, uitazama mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.” Yeye ambaye hakuwaamini wenzake walipomjuza habari za kufufuka kwake Kristo, alikiri kiri kuu na kusema; “Bwana wangu na Mungu wangu!” Ni katika jumuiya ni ndani ya jumuiya tunakutana na kumwonaYesu Mfufuka na kujaza furaha na amani ya kweli. Wito mliojitenga na jumuiya zenu; Rudini katika jumuiya zenu hata kama zina mapungufu ni jumuiya zenu ni mahali pa kukutana na Yesu mfufuka.

Ili amani na furaha itawale mioyoni mwetu yatupasa kuiishi Amri ya mapendo (Mt.22:34-40). Kuharakisha kumsaidia kila mmoja anayehitaji msaada wetu. Kuishi katika umoja na mshikamano. Katika siku za mwisho wa maisha yake hapa duniani Yesu alitoa wosia; “Pendaneni kama nilivyowapenda ninyi” (Jn.13:34). Kumbe umoja na mshikamano wa mapendo vitahuisha amani na furaha ya kweli katika Jumuiya ya Kikristo. Tutambue kuwa Jumuiya zetu za Kikristo, hasa jumuiya ndogondogo za Kikristo ni mwendelezo wa Jumuiya za kwanza ya wakristo baada ya ufufuko wa Yesu Kristo. Tuzidhamini na kuzienzi kwani kila tunapokuna, tunakukutana na Kristo mfufuka. Yeye yuko anatusubiri kila siku tumjie ili akatubariki na kutujaza Neema na kutupatia amani ili tubaki tumeunganika naye, mfalme wa amani. Hizi ndizo zawadi ambazo hatupaswi kuzificha bali kuwashirikisha wengine. Kule kuwajali majirani zetu ni ishara kwamba tumeelewa wajibu tunaokabidhiwa na Kristo mfufuka baada ya maisha yake hapa duniani.

Jumapili 2 Pasaka

 

 

 

08 April 2021, 15:51