Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 3 ya Kipindi cha Pasaka! Waamini wanahamasishwa kujenga utamaduni wa kukutana na Kristo Yesu katika: Neno, Sakramenti, Historia na Huduma kwa maskini. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 3 ya Kipindi cha Pasaka! Waamini wanahamasishwa kujenga utamaduni wa kukutana na Kristo Yesu katika: Neno, Sakramenti, Historia na Huduma kwa maskini. 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 3 ya Pasaka: Kutana na Yesu!

Masomo ya Dominika hii yanatualika kukutana na kumtambua Kristo Yesu Mfufuka katika adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu kwa kusikiliza neno lake na katika kuumega mkate. Lakini ili tustahili kukutana na Yesu sharti tujiandae kwa kujitakasa, kwa kuziungama na kuzikiri dhambi zetu ili tuweze kusamehewa. Kila mwamini anahamasishwa kuwa ni shuhuda wa ufufuko wa Yesu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya tatu ya Pasaka mwaka B. Masomo ya Dominika hii yanatualika kukutana na kumtambua Kristo Yesu Mfufuka katika adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu kwa kusikiliza neno lake na katika kuumega mkate. Lakini ili tustahili kukutana na Yesu sharti tujiandae kwa kujitakasa, kwa kuziungama na kuzikiri dhambi zetu ili tuweze kusamehewa. Zawadi hii ya kusamehe dhambi ni matokeo ya mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Damu yake Azizi ndiyo bei ya wokovu wetu na kutufanya wana wa Mungu ndiyo maana katika sala ya mwanzo Padre kwa niaba ya jamii ya waamini anasali; “Ee Mungu, watu wako na waone furaha sikuzote kwa ajili ya kutiwa nguvu mpya roho zao. Kwa vile sasa wanafunzi kwa kurudishiwa ile heshima ya kuwa wana wako, waitazamie ile siku ya kufufuka kwao, wakitumaini kupewa pongezi.”

Somo la kwanza la kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo.3:3-15,17-19), ni mawaidha ya Mtume Petro kwa Wayahudi baada ya kumponya mtu kiwete nje ya mlango wa Hekalu alipokwea na Yohane kwenda kusali. Katika mawaidha yake, mtume Petro anawaasa wayahudi kuwa; wakitubu dhambi zao, wanaweza kuokoka ingawa walimwua Yesu Mkombozi wetu. Yeye alikufa kwa kadiri ya mapenzi ya Mungu; na sasa yu Mkuu wa Uzima. Hivyo kwa kifo na ufufuko wake, Yesu ametufungulia mlango wa mbingu. Mtume Petro kwa ujasiri mkubwa anawambia waziwazi akisema; “Yesu ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe. Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; Mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake.” Kwa maneno haya, mioyo yao ilichomwa. Wakajiona kuwa wakosaji. Petro kwa kuwafariji na kuwapa matumaini mapya anawaambia; “Basi sasa, ndugu, najua ya kuwa mliyatenda haya kwa kutokujua kwenu, kama na wakuu wenu walivyotenda. Basi, tubuni, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe.” Ni mwaliko kwetu sote wa kujirudi kila tunapotenda dhambi, kutubu, na kurejea kwa Kristo, kwa kufanya toba ya kweli, naye atazifuta dhambi zetu na kutusamehe.

Somo la pili la waraka wa kwanza wa Mtume Yohane kwa watu wote (1Yoh. 2:1-5), latufundisha kuwa kumjua Mungu ndio kushika amri zake na katika kuzishika amri za Mungu, upendo wake unakamilika ndani mwetu. Sisi tulio wafuasi wa Kristo tupaswa kuenende katika nuru ya Mungu kwa tujitenge na dhambi. Na kama tumetenda dhambi, basi, tumkimbilie mara moja Yesu aliye Mwokozi na Mpatanishi wetu kwa Baba kama anavyosisitiza mtume Yohane akisema; “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwokozi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu…na za ulimwengu wote.” Injili zote nne zinaeleza kuwa Yesu baada ya kufufuka na kabla ya kupaa kwake mbinguni, aliwatokea wanafunzi na wafuasi wake mpaka mara nane ili kuwaimarisha katika imani na kuwadhibitishia kuwa ni kweli amefufuka kama alivyosema: Maria Magdalena (Mk 16:9ff; Yn 20:1ff), Wanawake wawili kwenye kaburi (Mt 28:9-10), Wanafunzi wa Emau (Lk 24:13ff; Mk 16:12-13), Mitume bila Thomaso (Yn 20:19-24), Mitume pamoja na Thomaso (Yn 20:26-29), Wafuasi kwenye ziwa Tiberia (Yn 21:1-14), Wafuasi katika mlima wa mizeituni (Mt 28:16-20; Lk24:36-49; Mk 16:14-18) na Simoni Petro (Lk 24:34).

Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk. 24:35-48), ya dominika hii ya tatu ya pasaka mwaka B, inaanzia pale Wanafunzi wa Emau waliporejea Yerusalemu na kutoa taarifa juu ya kile walichokiona na kusikia juu ya Kristo mfufuka na jinsi walivyomtambua katika kuumega mkate. Injili hii inashuhudia kuwa; Yesu mfufuka ni Mungu na mtu. Kudhihirisha hali yake ya kibinadamu Yesu anawaambia Mitume wake; “Mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikeni shikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo…Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia, Mna chakula cho chote? Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakitwaa, akabariki, akala mbele yao.” Akawakumbusha torati na maandiko ya manabii yanasema Kristo atateswa lakini atafufuka, Mataifa yatahubiriwa habari zake nao watamwamini. Kwa jina la Kristo, toba na ondoleo la dhambi ni kwa wote watakaomwamini yeye. Hili ndilo tunda la fumbo la Pasaka; Msamaha wa dhambi kwa wote. Haijalishi ukubwa wa dhambi. Tubuni mkaokoke. Upendo wa fumbo la pasaka unadhihirishwa katika Sakramenti ya Upatatanisho. Hapa watu wote wanaonja upendo, huruma na msamaha wa dhambi, kupatanishwa na Mungu na wanadamu.

Kwa kifo cha Kristo tumekombolewa, sote ni wana na warithi wa uzima wa milele mbinguni. Lakini inafaa tukumbuke maneno ya Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa kwamba; “Mungu aliyetuumba pasipo sisi kupenda, hawezi kutukomboa pasipo sisi kupenda.” Tunaalikwa kupokea zawadi ya wokovu, kwa kuishi ndani ya Kristo kwa kulisoma Neno lake kwa moyo wa sala na ibada, kwa kupokea vyema Sakramenti, kwa kushika Amri na maagizo ya Mungu, kwa kushika maagano na viapo vyetu vya ubatizo, ndoa, nadhiri na daraja takatifu kwa upendo, uaminifu, uvumilivu, msamaha, uwazi na kusali. Kila mmoja atambue nafasi yake katika mpango wa Mungu; wazazi, watoto, vijana na hata wazee. Upendo wa Kristo ukitubidisha ili siku moja nasi tuweze kustahilishwa kuupokea uzima wa milele mbinguni.

Uzima wa milele ndilo tumaini letu kama linavyojidhihirisha katika mfululizo wa sala anazosali Padre kwa niaba ya jamii ya waamini. Katika sala ya mwanzo anasali akisema; “Ee Mungu, watu wako na waone furaha sikuzote kwa ajili ya kutiwa nguvu mpya roho zao. Kwa vile sasa wanafunzi kwa kurudishiwa ile heshima ya kuwa wana wako, waitazamie ile siku ya kufufuka kwao, wakitumaini kupewa pongezi. Na katika sala ya kuombea dhabihu anasali; “Ee Bwana tunakuomba uzipokee dhabihu za Kanisa lako linalofanya shangwe. Na kama ulivyolifanya lifurahi sana sasa, ulijalie pia furaha ya milele. Na kuhitimisha katika sala baada ya komunyo akisali; “Ee Bwana, tunakuomba utuangalie kwa wema sisi taifa lako. Utujalie tufufuke na miili mitukufu, sisi ambao umependa kutufanya wapya kwa mafumbo haya ya milele.” Tujiweka basi chini ya Kristo Mfufuko ili siku moja tukashiriki naye uzima wa milele mbinguni.

Jumapili 3 Pasaka

 

14 April 2021, 16:27