Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 3 ya Kipindi cha Pasaka: Mashuhuda wa Kristo Yesu Mfufuka, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 3 ya Kipindi cha Pasaka: Mashuhuda wa Kristo Yesu Mfufuka, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 3 ya Pasaka: Mashuhuda wa Yesu

Mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake Habari Njema ya Wokovu, toba na maondoleo ya dhambi kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashuhuda wa mambo hayo! Huu ni utimilifu wa Torati na Unabii unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani. Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha ya waamini. Kila mwamini kadiri ya wito wake anapaswa kuwa shuhuda wa ufufuko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ilimpasa Kristo Yesu ateswe, afe na kufufuka kwa wafu siku ya tatu kama ilivyoandikwa! Na kwamba, Mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake Habari Njema ya Wokovu, toba na maondoleo ya dhambi kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashuhuda wa mambo hayo! Huu ni utimilifu wa Torati na Unabii unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani. Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha ya waamini. Kwa utangulizi huu, ninapenda kuchukua fursa hii, kukukaribisha ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Pasaka, Mwaka B wa Kanisa. Naye Kristo Yesu “akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya.” Lk. 24:46-49. Huu ni wosia tete sana ambao Kristo Mfufuka aliwaachia Mitume wake kama sehemu ya mchakato wa kutangaza na kushuhudia: mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu!

Katika kutoa ushuhuda huo, Mitume wa Yesu walikamatwa na kuanza kushughulikiwa mmoja mmoja, kwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, kupigwa na kuambiwa kunyamaza na wala wasithubutu tena kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka. Lakini ikumbukwe kwamba, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ni kiini cha imani ya Kanisa. Ndiyo maana Mitume wakasema, “maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Mdo. 4:20. Mitume ni tofauti sana na wale Askari walioamua kuchukua “vigunia vya fedha” ili kuficha ukweli kuhusu Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Mitume wa Yesu walipewa ujumbe wa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka, wakati bado wakiwa na hofu kuu na woga dhidi ya “mkong’oto wa Wayahudi” Bado akilini mwao, Kashfa ya Msalaba ilikuwa inaendelea kuwapekenya pole pole! Kumbe, wosia wa Kristo Yesu, uliwasukuma kutoka kifua mbele, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, toba, msamaha na maondoleo ya dhambi huku wakianzia Yerusalemu.

Siku ile ya Pentekoste, baada ya Roho Mtakatifu kuwashuhudia Mitume, Petro mtume, kwa ujasiri mkubwa alisimama na kuwaambia “Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake.” Mdo. 13:14-15. Katika kipindi hiki, Mitume na wafuasi wa Kristo Yesu walikuwa ni wachache sana, kuweza kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka hadi miisho ya dunia. Tangu wakati ule, Mitume pia walitambulikana kama “Mashuhuda wa Fumbo la Pasaka”. Ushuhuda huu ulisimikwa katika maisha na utume wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Na Mitume ni mashuhuda wa tukio hili muhimu sana katika historia ya ukombozi wa mwanadamu. Ushuhuda wa Fumbo la Pasaka, umewagharimu sana Mitume wa Yesu na Wakristo katika ujumla wao. Wengi walikamatwa na kuuwawa, lakini mchakato wa Uinjilishaji ulizidi kusonga mbele, kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyekuwa akitenda kazi ndani mwao. Rej. Mdo. 5: 32 na Yn. 15:2.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu ni kati ya majukumu mazito waliokabidhiwa Maaskofu pamoja na wasaidizi wao. Kimsingi Maaskofu ni watangazaji na mashuhuda wa imani, ni walimu wanaofundisha kwa Mamlaka ya Kristo Yesu. Ni viongozi wanaopaswa kuhubiri si tu kwa maneno bali kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka katika maisha yao adili na matakatifu. Maaskofu wanaofundisha wakiwa na ushirika na Khalifa wa Mtakatifu Petro ni mashuhuda wa ukweli wa Kimungu. Rej. LG. 25. Kristo Yesu kwa njia ya huduma ya Maaskofu huyatangazia Mataifa yote Neno la Mungu na kuwapatia waamini Sakramenti za imani na viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu yaani, Kanisa ni mawakili wa siri za Mungu. Maaskofu kwa namna iliyo bora na dhahiri wanashika nafasi ya Kristo Yesu aliye: Mwalimu, Mchungaji na Kuhani mkuu na kutenda katika Nafsi yake “In Eius Persona”. Rej. LG. 21. Waamini walei nao ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka.

Kila mwamini mlei anapaswa kuwa mbele ya ulimwengu chombo na shuhuda wa mateso na ufufuko wa Kristo Yesu na Ishara ya Mungu aliye hai. Walei wanapaswa kuwalisha walimwengu matunda ya kiroho. (Tazama. Gal 5: 32) na kueneza ndani yake ile roho iwahuishayo maskini, wapole na wapatanishi ambao Kristo Yesu aliwaita wenye heri. Rej. Mt. 5:3-9. Kama vile roho ilivyo mwilini, ndivyo Wakristo wawe ulimwengeni. Rej. LG. 38. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia kuna changamoto kubwa zinazoendelea kujitokeza mintarafu kanuni msingi za maisha ya imani, maadili, utu wema na hata mambo ya kisiasa na kijamii. Kumbe, waamini wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, huku wakiendelea kuipyaisha kwa kutumia kipaji cha ugunduzi sanjari na kusoma alama za nyakati. Ni muda muafaka kwa watu wa Mungu kujifunza kwa bidii zaidi: Maandiko Matakatifu, familia na jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zisaidie kutekeleza wajibu huu msingi, ili kweli Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha ya waamini. Waamini wajifunze Katekesimu ya Kanisa Katoliki: muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Maisha ya sala.

Waamini wajiendeleze zaidi katika kuyafahamu na kuyaishi Mafundisho Jamii ya Kanisa. Mambo yote haya ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu wao wa: Kikuhani, Kinabii na Kifalme waliojitwalia wakati walipokuwa wanapokea Sakramenti ya Ubatizo. Watu wa Mungu katika ujumla wa, wawe waaminifu kwa viapo vyao vya Ubatizo, Ndoa, Maisha ya wakfu na Daraja Takatifu. Wazazi na walezi watekeleze vyema dhamana na wajibu wao, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Yosefu sanjari na Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani. Kilele cha maadhimisho haya mjini Roma ni tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”.

Liturujia j3 Pasaka

 

 

 

 

16 April 2021, 16:31