Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 3 ya Kipindi cha Pasaka: Kristo Yesu amefufuka kweli kweli na walioshuhudia kufufuka kwake ni: wanawake, Simon Petro na mwanafunzi yule mwingine pamoja na wafuasi wa Emau. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 3 ya Kipindi cha Pasaka: Kristo Yesu amefufuka kweli kweli na walioshuhudia kufufuka kwake ni: wanawake, Simon Petro na mwanafunzi yule mwingine pamoja na wafuasi wa Emau. 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 3 ya Pasaka: Yesu Kristo Mfufuka!

Muktadha wa Injili ya leo bado ni jioni ya ile siku ya Pasaka, hivyo pia ni tukio lililojiri katika mji wa Yerusalemu. Ni baada ya wanawake kufika kaburini na kukuta kaburi tupu na kutokewa na watu wawili wenye mavazi meupe yanayong’aa. Luka 24:1-8. Walikusanyika pamoja, na hapa wanazungumza na kujadili juu ya ufufuko wa Bwana na Mwalimu wao baada ya shuhuda mbalimbali! Imani

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani ya Kristo Mfufuka iwe daima nanyi! Muktadha wa Injili ya leo bado ni jioni ya ile siku ya Pasaka, hivyo pia ni tukio lililojiri katika mji wa Yerusalemu.  Ni baada ya wanawake kufika kaburini na kukuta kaburi tupu na kutokewa na watu wawili wenye mavazi meupe yanayong’aa. Luka 24:1-8. Walikusanyika pamoja, na hapa wanazungumza na kujadili juu ya ufufuko wa Bwana na Mwalimu wao baada ya ushahidi wa wanawake, Simon Petro na yule mwanafunzi mwingine aliyependwa na Bwana na sasa wale wafuasi wawili wa Emau. Katika mazingira haya tunashawishika kuona mitume walijawa na furaha kusikia ufufuko wa Bwana na Mwalimu wao. Wakati Mwinjili Yohane 20:20 anatuonesha kuwa Mitume walijawa na furaha, hapa kinyume chake Mwinjili Luka anatuonesha hata baada ya kutokewa na Yesu Kristo Mfufuka, Mitume walijawa na mshangao na woga na mahangaiko wakiamini kuwa wameona mzimu. Safari ya imani katika ufufuko bado ilikuwa ni ndefu na ngumu kwao!

Mwinjili Luka anakazia sana juu ya mwili wa Kristo Mfufuka. Mwinjili Luka anawaandikia wakristo wenye asili ya Kiyunani au Kigiriki. Kadiri ya falsafa ya Wagiriki waliamini kuwa mwili ni gereza la roho na hivyo wakati wa kifo, roho inapata uhuru wake kwa kujitenganisha na mwili. Ni katika mazingira haya Mwinjili Luka leo anakazia kuwa Yesu Kristo Mfufuka, anafufuka na mwili wake halisi ila unaokuwa katika hali ya kutokuharibika tofauti na mwili ule wa nyama kabla ya kifo. Ni mwili wa utukufu. Sio mwili wa nyama kama tulio nao sasa, bali ni mwili wa utukufu, uliogeuzwa na hivyo kuwa na hali ya kutokuharibika kama asemavyo Mtume Paolo, 1Wakorintho 15:35-43. Ni mwili uwezao kuingia ndani hata pale ambapo milango imefungwa Yohane 20:26, kama hivi ndivyo basi mwili huo hahuitaji chakula wala kinywaji.

Mwili wa ufufuko unatoka nje ya mipaka ya muda na mahali, ni mwili usiokuwa na mipaka ya aina yeyote ile, ni mwili unaoingia katika maisha ya umilele, ni mwili unaokuwa nje ya nyakati na nafasi za kijiografia. Na ndio mwaliko kwetu tunaoamini katika ufufuko, kuachana na yale yote yanayotufanya kuwa watumwa wa ubinafsi na umimi, imani katika ufufuko, inatutaka tutoke ndani mwetu na kumsogelea mwingine kwa upendo usio na masharti. Kila anayeamini katika Kristo mfufuka, hana budi kuachana na maisha ya kuwa watumwa wa umimi na ubinafsi. Yesu Kristo Mfufuka anaona wanafunzi wake bado wamejawa na mashaka na wasiwasi na hofu, anawaalika watazame na kushika mikono na miguu yake. Yesu Kristo Mfufuka anatambulika sio kwa sura bali kwa makovu ya mikono yake na miguu yake. Ni kwa upendo wake wa kujisadaka pale Msalabani ndio utambulisho wa Yesu Kristo Mfufuka. Ni kwa mateso na kifo chake sisi tunakombolewa. Ni pale Msalabani anajifunua kuwa Yeye kwa hakika ni Upendo wenyewe. Ni upendo kamili hiyo ndiyo sura ya Mungu tunayokutana nayo katika maadhimisho ya Pasaka.

Mwinjili Luka bado anakazia kuwa kutokana na mashaka na wasiwasi wa wanafunzi ndipo pia anaomba wampe chakula. Hapo tunabaki na maswali kwani mwili wa ufufuko usiobanwa na muda wala nafasi, hauna hitaji la chakula wala kinywaji. Na labda tunaona Yerusalemu ni mbali na bahari, hivyo upatikanaji wa samaki si rahisi sana nyakati zile. Kwa hakika lengo na shabaha la Mwinjili Luka ni kuonesha kuwa hakika Yesu Kristo amefufuka na sasa ana mwili wa utukufu na sio mzimu kama walivyokuwa wanadhani wanafunzi wa Yesu Kristo. Ni muktadha wa hadhira yake Mwinjili Luka tunaona anazidiki kukazia juu ya mwili wa Kristo Mfufuka. Ni kukazia kwa wasikilizaji wake kuwa KWELI KWELI YESU KRISTO AMEFUFUKA na mzimu bali ni yeye Kristo mwenyewe amefufuka na kuwatokea baaadhi ya wafuasi wake.

Wanafunzi wanajawa na woga; katika Maandiko Matakatifu tunaona katika tukio lolote la uwezo au uwepo wa Mungu, hapo pia kunakuwa na woga na hofu.  Nabii Isaya wakati wa wito wake tunaona anaogopa na kujitambua kuwa ni mdhambi na mwenye midomo michafu. Isaya 6:5. Katika Agano Jipya pale Malaika anapotumwa kwa Zakaria na Mama yetu Bikira Maria tunaona wote wawili wanajawa na hofu. Luka 1:12,29 na Marko 9:6 pale mitume walijawa na hofu katika tukio la kugeuka sura Yesu Kristo pale juu mlimani Tabor. Uwepo wa Mungu daima huleta hofu. Yesu Kristo Mfufuka anapotutokea daima tunaingiwa na hofu na mashaka mengi kwani ni mwaliko wa kubadili maisha yetu na hata namna zetu za kufikiri. Ni kututaka tuishi maisha ya kimungu na kuachana na maisha ya kidunia. Mashaka na hofu bado yanatawala katika maisha yetu ya safari ya kiimani kwani ni kuacha ya kale na kuanza maisha mapya, na huu ni mwito wa kila siku katika maisha ya mfuasi wake Kristo Mfufuka.

Safari ya imani ya Mitume tunaona haikuwa rahisi hata baada ya kutokewa mara kadhaa na Kristo Mfufuka. Imani sio tunda la ushahidi bali ni moyo unaofunguka na kupokea tusiyoweza kuyaona kwa macho ya nyama. Ni kutaniko la nafsi zetu na ile ya Muumba wetu, ni mwitikio wa upendo wa Mungu kwetu wanadamu tulio wadhambi na wakosefu. Ni neema, hivyo ni zawadi kutoka kwa Mungu na sio mastahili yetu. Na ndicho anachosema Mwinjili Luka leo kuwa aliwaangazia akili zao ili waweze kuelewa Maandiko. Bila mwanga wa Kristo Mfufuka akili zetu zinabaki zimefungwa kuelewa ukweli huu wa imani. Kristo Mfufuka haishi tena kama awali na hivyo inakuwa ngumu kumtambua si tu kwa sisi leo bali hata wale aliokula na kunywa nao!  Pamoja na kuwa ngumu kumtambua maana sasa la muhimu ni kumkiri na kumtambua sio kwa sura au mwili wenye kuharibika bali katika makovu yake, na ndio anatualika nasi leo kuangalia na kumtambua katika makovu ya upendo wake katika mikono, miguu na kifuani.

Ufufuko haukuondoa alama zile za makovu ya mateso yake, ukweli wa ufufuko kumbe ni kutafakari upendo wa Mungu kwetu wanadamu. Na ndio anawaalika wanafunzi wake kumgusa na kuyaangalia, ndio mwaliko wa maisha ya kila mfuasi wa Kristo Mfufuka, maisha yetu daima yaakisi upendo wa Kristo, yaakisi makovu yaliyopo miguuni, mikononi na ubavuni mwake Kristo Mfufuka. Ndio kusema alama ya mkristo au mfuasi wa Mfufuka ni upendo usio na masharti, ni upendo wa kujisadaka daima. Ni Mwinjili Luka pekee yake anayekazia sana juu ya mwili wa Kristo Mfufuka. Hivyo anasema kuwa wafuasi waliweza kumshika mfufuka na hata kula naye na pia kuona mwili na mifupa yake. Ni katika mazingira yale ya wayunani kama nilivyotangulia kusema anakazia kuwa Kristo Mfufuka siyo mzimu bali kweli ni yeye na ana mwili kweli tofauti na mzimu. Ila yafaa ieleweke mwili wa Kristo Mfufuka ni ule wa utukufu na sio tena wenye kuharibika kama miili yetu ya sasa. Na ndivyo tutakavyokuwa nasi tutakapofufuliwa ile siku ya mwisho. Miili yetu itageuzwa na kuvaa kutokuharibika. 1Wakorintho 15:44.

Mwili wa Kristo Mfufuka bado una alama za upendo wake kwetu wanadamu. Na ndio anawaalika waangalie mikono na miguu yake. Ni mwaliko nasi leo kutafakari upendo wa Mungu kwa kuangalia mikono na miguu yake Mfufuka. Nasi hatuna budi kutumia mikono na miguu yetu kwa upendo kwa Mungu na kwa jirani. Mtume Paolo anatukumbusha kuwa nasi hatuna budi kubeba madonda ya Kristo Msulubiwa katika miili yetu, na ndio moyo wa upendo kwa Mungu na jirani. Wagalatia 6:7. Mwinjili Luka anamalizia Injili ya leo kwa mwaliko wa kimisionari wa kuhubiri wongofu na msamaha wa dhambi. Hakika huu ndio ujumbe wa Pasaka unaotutaka sote kubadili maisha yetu na kuanza maisha mapya katika Kristo Mfufuka. Kila mmoja wetu awe mjumbe wa Habari Njema si tu kwa maneno bali hasa kwa maisha yetu, na ndio maisha ya kishahidi. Ni Injili inayopaswa kuishi katika nafsi na maisha ya kila mmoja wetu. Mimi na wewe tunaalikwa kuwa Habari Njema iwe katika familia zetu, sehemu zetu za kazi na popote tulipo. Mikono na miguu yetu haina budi kutumika kwa upendo kwa Mungu na jirani.

Na ndio katika kusanyiko letu la kila Dominika tunakutana na Yesu Kristo Mfufuka, kwanza katika Neno lake wakati wa Liturujia ya Neno na pia mwili wake halisi katika Liturujia ya Ekaristi. Tunaposikia Neno lake hatuna badi kuliweka katika maisha yetu kwa nguvu tuipatayo kwa kushiriki Meza ile ya upendo wake, yaani Mwili na Damu yake Azizi. Ni Kristo Mfufuka anayebaki pamoja nasi kila siku katika maisha ya Kanisa. Si tu anatutokea na kupotea bali anabaki daima nasi katika Neno lake na Sakramenti yake katika Kanisa lililo Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume. Zaidi sana “Mwili wa Kristo Mfufuka”, tunakutana nao na akitualika kumsogelea kwa kumgusa na kumwangalia katika Neno lake na zaidi sana na kwa namna ya pekee kabisa katika Ekaristi Takatifu. Ni katika Sakramenti ya altare tunaendelea kubaki na Mwili wa Kristo Mfufuka, tunaendelea kuona na kugusa makovu ya upendo wake kwetu, na ndio maana tunaalikwa kumpokea Kristo katika maumbo yale duni kabisa ya mkate na divai. Na ndio kama asemavyo Mtakatifu Tomaso wa Akwino, ni katika Sakramenti ya Altare hapo tunakutana na Kristo mzima, Nawatakia tafakari njema ya Neno la Mungu na Dominika yenye kila neema na baraka zake Yesu Kristo Mfufuka.

13 April 2021, 11:34