Utatu Mtakatifu: Kiri ya Imani ya Kanisa: Baba, Mwana na Roho Mt.
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na salama! Kwa Jina la Baba na la Mwana na Roho Mtakatifu Amina. Imani yetu imejengwa katika msingi huu: Tunaamini katika Mungu mmoja aliye katika nafsi tatu, yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Kanisa linatufundisha kwamba mgawayiko huu wa Nafsi hujidhihirisha katika kazi zao: Baba ndiye muumbaji, Mwana ni mkombozi na Roho Mtakatifu ni mfariji. Utangulizi wa Ekaristi wa Sherehe ya Utatu Mtakatifu unaelezea kwa kifupi imani hiyo ukisema: “Wewe (Baba) pamoja na Mwanao wa pekee na Roho Mtakatifu u Mungu mmoja na Bwana mmoja, siyo katika umoja wa nafsi, ila katika utatu wa Mungu mmoja”. Nafsi hizi tatu katika Umungu mmoja zina utukufu ulio sawa na kamwe hazigawanyiki. Tukiwa na imani kwa Mungu mmoja, bado tunakiri kuwa katika Uungu kuna Ubaba, Umwana na Upendo wa Kimungu. Ndilo fumbo la Utatu Mtakatifu. Kwa maneno marahisi kabisa au kutumia lugha ya Mtakatifu Augustino, fumbo la upendo wa Mungu, yaani Mungu Baba anayependa milele yote, Mungu Mwana anayependwa na Baba milele yote, na Mungu Roho Mtakatifu ambaye ni upendo wa milele kati ya Baba na Mwana. Ni Mungu Mwana anayetoka kwa Baba milele yote, na Mungu Mwana anayekuwa nakala kamilifu na Mungu Baba, na Upendo unaozaliwa milele yote kati ya Baba na Mwana ndiye Roho Mtakatifu, ni Mungu mmoja katika nafsi tatu. Tunaliita ni fumbo si kwa sababu hasi, ya kuwa ni jambo lisiloeleweka au kinyume au linapingana na mantiki za kiakili, bali ni utajiri wa ukuu wa Mungu unaopita mipaka ya akili zetu za kibinadamu.
Ni fumbo kwa kuwa linazidi akili zetu za kibinadamu, uwezo wetu wa kulielewa na ndio maana msaada pekee wa kuweza kulielewa ni kwa msaada wa Mungu mwenyewe kadiri anavyojifunua. Hakuna hata mmoja wetu anayeweza kumuelezea Mungu katika ukamilifu wake, kwani Mungu sio mmoja mwenye mipaka na ukomo, ni mmoja anayezidi mipaka na ukomo wa aina yeyote ile. Kusema kwa hakika Mungu ni nani ni kumdogosha Mungu, ni kumfanya Mungu awe sawa na sisi tulio viumbe. Mungu ni uwepo wenyewe. Aquinas wrote that God is “ipsum esse subsistens," translated as "the shear act of 'to be' itself." So the idea of God not simply as a noun but as an action (i.e., verb). On St. Thomas Aquinas’s analogical interpretation, God is not one item, however impressive, even in the genus of existing things. Indeed, St. Thomas insists that God is not an individual and is not to be categorized in any genus, even that most generic of genera, the genus of being. God is not so much ens summum (highest being) as ipsum esse subsistens (subsistent being itself). Na hata inakuwa ni rahisi kwetu wanadamu kusema kwa njia hasi, kusema kile ambacho hakipo katika asili ya Mungu kuliko kumzungumzia kwa njia chanya, yaani sifa za Mungu, hakika hatuwezi kupata sifa moja inayojitosheleza katika kumzungumzia Mungu. Mungu hatuwezi kumzungumzia kwani hana mipaka ya aina yeyote ile, hawezi kuingia katika mipaka na uelewa wetu wa kibinadamu.
Ni fumbo au kwa lugha ya Kigiriki “Mysterion”, na lina mzizi wake katika neno lingine la Kigiriki “muein”, likimaanisha “kufunga mdomo, kuwa kimya”. Ni ukimya kwani Mungu si mmoja baina yetu, hana mfanano wowote ule nasi viumbe, haingii wala hatuwezi kumuelewa kwa upeo wa akili zetu za kibinadamu. Hivyo kweli za Mungu tunazipata kwa njia ya Ufunuo. Ni pale Mungu anapoona inafaa kujifunua na kujidhihirisha kwetu. It is a mystery simply because, there is just too much to understand, the truth is so vast, the light of such intensity, that the mind is dazzled and amazed! It is not a deficiency but an excess of intelligibility.Mwanafalsafa mwenye asili ya Kiyahudi Martin Buber aliwahi kusema; “Kama tunazungumzia Mungu ambaye tunaweza kusema juu yake au kumzungumzia, basi itakuwa rahisi kwangu kutokumuamini; lakini kwa kuwa tunamzungumzia Mungu anayeweza kunena nasi, ni kwa sababu hiyo basi nami ninamuamini” NiMungu anayekubali kujifunua mwenyewe kwa mwanadamu na kamwe hawezi kuwa Mungu kutokana na ugunduzi wa akili na uwezo wetu wa kibinadamu.
Ni Mungu anayejifunua kwa mwanadamu, na ndio maana tafakuri yetu ya leo inajikita katika Maandiko Matakatifu, ni fumbo linajaribu kumfunua Mungu mwenyewe kwa mwanadamu kwa njia ya Neno lake. Waislamu wana majina tisini na tisa ya Mungu ila la mia moja hawalifahamu, ndio kukiri pia ukuu upitao mipaka yote ya Mungu huyu mmoja. Wayahudi nao wanamtambua Mungu katika matukio ya historia yao ya wokovu. Ila kwa Wakristo kitabu pekee kinachomfunua Mungu ni Yesu Kristo, ndio sura halisi iliyokuja kutufumbulia ukuu na Upendo wa Mungu kwa watu wote. Ni kwa njia ya fumbo la Umwilisho tunapata kufunuliwa nafsi ile ya pili ya Mungu, ni siku ya Pentekoste nasi tunapata kumfahamu Mungu Roho Mtakatifu. Mtakatifu Yohane anapoandika utangulizi wa Injili anasema kwa mshangao mkubwa; Hapo mwanzo palikuwepo Neno! Sio mwanzo wa nyakati, bali ni leo isiyogawanyika, ni sasa ya milele yote, ni Mungu wa milele anayekuja kwetu katika historia lakini yupo milele yote.
Hakika sio kusudi langu na sitegemei kuwa ni lengo la muhubiri yeyote yule duniani kujaribu kuelezea kwa ufasaha kwa akili ya kibinadamu juu ya ukuu wa Mungu maana hata kujaribu tu ni sawa na kufanya kufuru. Mungu ni mkuu na ukuu wake hauna mipaka na hivyo hatuwezi kumwelezea wala kumwekea mipaka ndani ya akili zetu. Mungu ni yule apitaye mipaka yote. Kujaribu kumwelewa kwa asilimia mia ni sawa na kazi ya kujaza au kujaribu kuyakamata maji kwa chujio, lazima tu yatatuchomoka au kujaza kashimo kale kadogo maji ya bahari yote. Yatosha kwanza kukiri ukuu wake usio na mipaka wala kipimo. Katika jumuiya zile za kwanza za waamini, watu walibatizwa kwa Jina la Yesu Kristo Mfufuka. Rejea Matendo 2:38. Ni katika nusu ya karne ya kwanza ndio waamini wakaanza kubatizwa kwa Jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu kadiri ya Mwinjili Matayo. Hivyo hata fundisho na imani kwa Utatu Mtakatifu haikuwa rahisi sana katika Kanisa la Mwanzo, ni kwa msaada wa Roho Mtakatifu, Kanisa linapata kuelewa fumbo hili taratibu na kwa wakati. Wale wanafunzi kumi na mmoja leo wapo katika mlima Galilaya.
Mlimani katika lugha ya Kibiblia ni mahali ambapo Mungu anajifunua. Ni pale mlimani Kristo mfufuka anawatokea na baadhi yao bila shaka wanamsujudia na baadhi wakiwa bado na mashaka juu ya ukuu ya Umungu wake. Kristo Mfufuka ili kumtambua kunatutaka kuwa na si macho ya nyama bali ya moyoni, yaani imani. Imani ni safari, na ndio maana wengine wakaona shaka, na hata leo bado wapo wengi wanaoona shaka katika fundisho hili la imani. Kumkiri Mungu mmoja katika Nafsi tatu, inahitajika imani na sio akili zetu au mantiki zetu za kibinadamu. Ni katika tukio la Kristo mfufuka kujifunua kwake pale juu mlimani pia anawapa utume au misheni wanafunzi wake wa kwenda na kubatiza watu wa mataifa yote na kuwafundisha kuyashika yale yote waliyofundishwa na Yesu Kristo wakati wa maisha yake. Ni Mungu anajifunua baada ya fumbo la ufufuko, lakini zaidi sana anawapa misheni ya wanafunzi wake, na ndio sisi kwenda ulimwenguni kote na kuwabatiza, na kuwabatiza ni kuwaalika kushiriki maisha ya Kimungu, kushiriki fumbo la Mungu mmoja katika nafsi tatu. Ni kukubali kuteseka, kufa na kufufuka pamoja na Kristo, ni kuingia katika mahusiano na nafsi zile tatu za Mungu mmoja. Ni Mungu mmoja katika nafsi tatu, nafsi zinaonesha mahusiano yanayokuwepo katika Mungu mmoja, na pili kutualika nasi kuingia katika mahusiano hayo.
Ni wazi tayari walishapokea utume huo hata kabla ya tukio la leo, ila walitumwa bado wafanye utume wao kwa mipaka, yaani kwa Wanawaisraeli waliopotea. Rejea Mt. 10:6-6 Ni baada ya Pasaka sasa tunaona utume wao unakuwa mkubwa, unagusa sasa watu wa mataifa yote ulimwenguni. Ni baada ya Pasaka mwanga ule uliokuwa umeangaza katika Nazareti na Galilaya, sasa unaangaza ulimwengu mzima. Isaya 42:6 Ni wakati wa neema sasa baada ya ufufuko wake anapoufunua ukuu wake wa Kimungu, kama vile Baba alivyompeleka, naye Kristo Mfufuka anatupeleka nasi, kuwa wajumbe wa Habari Njema kwa kila kiumbe. Kwani amepewa kila uwezo juu mbinguni na duniani, maana yake ukuu wake ni kwa kila kiumbe iwe cha mbinguni na kile cha duniani. Ukuu na uweza wake sio kama ule wa ulimwengu huu, bali ni katika kumtumikia mwanadamu kwa upendo na kumkomboa kwa kutuweka sote karibu na Upendo wa Mungu na ndio Roho Mtakatifu anayebaki nasi siku zote za maisha yetu mpaka ukamilifu wa dahari. Fumbo la ukuu na uweza wa Mungu liliimbwa hata na jumuiya zile za waamini wa mwanzo, na ndio Mama Kanisa leo anatualika kusherehekea ukuu wa Mungu upitao akili zetu za kibinadamu kwa imani na unyenyekevu mkuu. 1Yohane 3:1-3 Ni furaha ya upendo wa Mungu kuweza nasi kufanyika wana wa Mungu kwa njia ya Mwana pekee wa Mungu yaani Yesu Kristo Mfufuka. Ni kukiri kuwa Mungu amejifunua kwetu kwa msaada wa Roho wake Mtakatifu. 1Wakorintho 2:9-10
Mungu anapenda kukamilisha mpango wake wa wokovu kwa njia ya Kanisa lake. Hivyo Yesu Kristo kwa vile alivyotupenda hakutaka kubaki na uwezo huo peke yake bali anawapa pia wanafunzi wake uwezo na mamlaka ya kufundisha na kubatiza, ndio kuwapa uwezo nao wa kushirikisha watu wote maisha yasiyo na mwisho. Ni kwa njia ya Kanisa sasa kazi ile ya Kristo Mwenyewe inapata kuenea kwa kila kiumbe ulimwenguni, na ndio misheni ya kila mbatizwa kuwa mashahidi wa upendo wa Mungu kwa kila kiumbe ulimwenguni, ndio jukumu na utume wetu wa kuwafanya wengine waingie katika mahusiano ya milele na Mungu mmoja katika nafsi tatu. Na ndio pia Paulo Mtume anatufundisha juu ya mpango wake Mungu wa kuukomboa ulimwengu mzima. 1 Timoteo 2:4 Ni huruma yake kwa watu wote, kwa kila kiumbe ili asipotee hata mmoja wetu bali sote tupate uzima wa milele. Ni mpango na mwaliko wa upendo wa Mungu kwa kila mmoja wetu kuufikia ule uzima wa milele. Warumi 11:32. Ni kwa njia ya Habari Njema yaani Injili na Ubatizo nasi pia tunashirikishwa uzima wa milele. Ni wajibu wetu nasi kuwashirikisha wengine ukuu na upendo wake Mungu kwa kila kiumbe.
Utatu Mtakatifu ni familia kamilifu ya umoja na upendo wa Kimungu. Na ndio mapenzi yake kwetu sisi wanadamu, kuwa kundi moja lenye mchungaji mmoja yaani Mungu mwenyewe anayejifunua katika Ubaba, Uwana na Upendo mkamilifu. Ni Mungu anayependa milele yote, ni Mungu Mwana anayependwa na Baba milele yote na Mungu Roho Mtakatifu ambaye ndio ule upendo wa milele baina ya Mungu Baba na Mungu Mwana. Hakika wito wa kushiriki ukuu na uweza wa Mungu sio jambo la kibinadamu, hivyo kila mmoja wetu anahitaji neema za Kimungu kuweza kushiriki utume wake wa kupelekea kwa kila kiumbe upendo na ukuu wake. Na ndio ahadi ya Kristo Mfufuka ya kubaki nasi siku zote, hivyo tusiogope kutoka na kwenda kushuhudia ukuu wa Mungu kwa ulimwengu mzima. Ni kwa njia ya Mungu Roho Mtakatifu nasi tunaweza kutoka na kushuhudia makuu ya Mungu, ya kumpeleka Mungu kwa njia ya Neno na masakramenti yake kwa wengine. Ni kwa njia ya Ubatizo kila mmoja wetu anafanyika kuwa mwana wa Mungu, kuwa mrithi wa ufalme wa mbinguni pamoja na Mwana pekee wa Mungu. Tunapotafari ukuu wa Mungu katika Fumbo hili la Utatu Mtakatifu tuzidi kumwomba Mungu neema ya kubaki daima wenye imani thabiti kwake inayoakisiwa si tu kwa maneno yetu bali hasa kwa maisha yetu, ya kuwa wajumbe na wapelekaji wa Habari njema kwa kila kiumbe. Tafakuri njema na Dominika njema ya kusherehekea fumbo la Utatu Mtakatifu.