Tafuta

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kiini cha imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Kanisa. Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kiini cha imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Kanisa. 

Fumbo la Utatu Mtakatifu: Kiini cha Imani, Matumaini na Mapendo

Utatu Mtakatifu ni fumbo la imani kuwa katika Mungu mmoja kuna Nafsi Tatu yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho. MtakatifuHizi nafsi tatu za Mungu mmoja, zote ni sawa katika uasili. Tunasadiki siyo kwa sababu ya utambuzi wetu bali kwa kuwa Mungu mwenyewe ametufunulia hivyo. Imani hii ni Fumbo ambalo malaika na wanadamu hawawezi kulielewa kwa ukamilifu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, katika Sherehe ya Utatu Mtakatifu. Utatu Mtakatifu ni fumbo la imani kuwa katika Mungu mmoja kuna Nafsi Tatu yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho. Hizi nafsi tatu za Mungu mmoja, zote ni sawa katika uasili. Hii ni imani yetu. Tunasadiki siyo kwa sababu ya utambuzi wetu bali kwa kuwa Mungu mwenyewe ametufunulia hivyo. Imani hii ni Fumbo ambalo malaika na wanadamu hawawezi kulielewa kwa ukamilifu. Na kwa kuwa ni fumbo la imani, imani tu, imani tu, yaelewa. Kumbe lengo la tafakari hii katika sherehe hii ya Utatu Mtakatifu siyo kuwaelewesha namna ambavyo nafsi tatu katika Utatu Mtakatifu zilivyoungana na kufanya Mungu mmoja. Hii ni kwasababu akili zetu za kibinadamu haziwezi kulielewa kikamilifu fumbo hili. Ndiyo maana hata masomo tunayosoma katika liturujia ya sherehe hii hayalengi kutufafanulia waziwazi juu ya fumbo hili.

Kwa kifupi, somo la Kwanza la Kitabu cha Kumbukumbu la Torati (4:32-34, 39-40); Musa anataja matendo makuu ya Mungu aliyowatendea Waisraeli kwa kuwateua kuwa taifa lake teule, uteule ambao ni wa pekee kabisa. Hivyo anawakumbusha wawe waaminifu kwa Mungu, kwani ndiye Mungu pekee aliye juu na chini ya nchi hakuna mwingine. Yeyé ndiye aliyewatoa utumwani Misri na kuwaongoza katika nchi ya Ahadi Kanaani. Anawakumbusha kuwa Mungu aliwatoa katika utumwa/tope la dhambi nakuwatakasa, hivyo wasirudie tena matapishi ya dhambi nakuabudu sanamu. Anawaasa wazishike amri zake ili wapate kufanikiwa wao na watoto wao. Sisi tumetendewa maajabu makubwa zaidi. Kama Mwenyezi Mungu kamtuma kwetu Mwanae wa pekee na katuletea Roho Mtakatifu. Tukiwa waaminifu kwa Mungu siku zetu zitaongezeka na wingi wa neema zake zitakuwa nasi

Somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (8:14-17); linatueleza kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu Baba kwa namna ya pekee. Sisi tunaweza kuwa na haki ya kumwita Mungu “Aba” yaani, Baba yetu tukikubali kuongozwa na Roho Mtakatifu anayekamilisha siri ya wokovu wetu. Hivi wokovu wetu ni mapato ya kazi ya Nafsi zote Tatu za Mungu mmoja. Injili ilivyoandikwa na Mathayo (28:16-20); inatusimulia jinsi Yesu, mwenye mamlaka yote juu ya wokovu wa binadamu alivyowaagiza wanafunzi wake wakaihubiri Injili kwa mataifa yote, na wale watakaowapokea kwa njia ya ubatizo katika Jina lake Yeye Kristo wawaimarishe zaidi kwa kuwafundisha kushika mafundisho yake kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Na anatoa mwongozo wa namna ubatizo unavyopaswa kuwa, ni katika Utatu Mtakatifu akisema kuwa; “Mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Na kwamba yeye yupo pamoja na Kanisa lake siku zote, hata ukamilifu wa dahari. Masomo haya yote hayataji neno “Utatu Mtakatifu”, lakini yanadhihirisha uwepo wa wake.

Yesu ndiye anayetujulisha juu ya nafsi tatu za Mungu. Yeye alimtambulisha Baba kwetu; “Hakuna amjuaye Baba ila Mwana” (Mt 11:27). “Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu pia, kwa Mungu wangu na Mungu wenu” (Yn 20:17). Na msalipo semeni Baba yetu uliye mbinguni (Mt 6:10). Yesu anasisitiza; “Baba yangu anawapenda” (Yn 16:27), na uthibitisho kwamba Mungu Baba anatupenda alimtuma yeye ulimwenguni ili kila amwaminiye asipotee bali awe na uzima (Yn 3:16). Yesu pia alimtambulisha Roho Mtakatifu kwetu na kumkabidhi kwetu, ili atufundishe na kutukumbusha yote juu ya Baba na Mwana. Katika Roho Mtakatifu tumeshirikishwa uzima wa kimungu ndani mwetu. Roho Mtakatifu anatuhakikishia kuwa sisi ni wana wa Mungu, akituwezesha sisi kumwita Mungu Abba-Baba (Rum 8:15). Yesu alitumia neno “Abba” kuonesha mahusiano ya karibu na kufungamana kwetu na Baba yake (Mk 14:36).

Kumbe sasa, shabaha ya sherehe ya Utatu Mtakatifu ni kutafakari jinsi Mungu mmoja katika Nafsi zake tatu yaani Utatu Mtakatifu unavyofanya kazi katika maisha yetu na hivyo sisi nasi tuweze kuutukuza huu Utatu Mtakatifu katika Mungu mmoja. Kila Sadaka ya Misa Takatifu huanza kwa kufanya ishara ya msalaba tukitamka maneno; “Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho mtakatifu”. Maneno hutamkwa wakati wa ubatizo anapomiminiwa maji katika paji la uso anayembatiza, wakati wa Kipaimara. Padre anapomwondolea mtu dhambi zake wakati wa Sakramenti ya upatanisho anasema: “Nami nakuondolea dhambi zako, kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho mtakatifu.” Hutumika pia wakati wawili wanapofunga ndoa ambapo baada ya ahadi za mwanandoa kwa kumvika mwenzi wake pete anahitimisha kwa maneno; “Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho mtakatifu.”

Hata mtu anapokaribia kufa tunasali tukimuombea tukisema: “Ee, Mkristo, uondoke sasa duniani, katika jina la Baba aliyekuumba, kwa Jina la Kristo aliyekukomboa, na katika Jina la Mungu Roho Mtakatifu aliyekutakasa.” Na siku ya mazishi maneno haya yanatumika kwa namna moja au nyingine tunaposema; “Uandikwe ishara ya Msalaba Mkombozi wetu”. Huku ndiko kukiri na kuliishi fumbo la Utatu Mtakatifu unaoundwa katika umoja wa Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.  Hii ni imani juu ya Mungu Mmoja katika Nafsi Tatu: Baba aliye Muumba, Mwana aliye Mkombozi, Roho Mtakatifu aliye Mfariji. Wataalamu wa mambo ya dini wanatuambia kwamba watu hutaka kufanana na Mungu wanayemwabudu. Watu wanaomwabudu Mungu ambaye ni shujaa na jemedari, hupenda kuwa watu wa vita, utawala na mamlaka. Watu wanaomwabudu Mungu wa starehe, huwa ni watu wanaopenda sana kujistarehesha kwa gharama yeyote. Watu wanaomwabudu Mungu aliye mwingi wa hasira wana tabia ya kulipa kisasi, watu wanaomwabudu Mungu anayependa, huwa ni wakarimu na watu wanaopenda.

Utatu Mtakatifu unatueleza uhalisia wa Mungu tunayemwabudu. Mungu ni mmoja katika nafsi tatu zisizogawanyika, zilizoungana kwa umoja na upendo kwani Mungu kwa asili ni Upendo. Mungu wetu haishi katika ubinafsi ila katika Jumuiya ya upendo na ushirikiano. Mungu si mpweke. Nasi tunayemwabudu hatupaswi kuwa na ubinafsi, kujitenga na kukaa katika upweke (Mt 5:48). Maisha ya kiroho ya Kikristo yanatudai siyo kuukimbia ulimwengu ili kuutafuta utakatifu, bali tuutafute utakatifu katika jumuiya na katika jamii. Utatu Mtakatifu unatuonesha kwamba watatu ni Jumuiya. Tatu ni upendo katika ukamilifu wake. Tatu ni namba kamilifu. Tuchukue mfano katika hali ya wanadamu. Mtu-Mume anapokuwa katika mahusiano ya upendo na Mtu-Mwanamke, muungano huo wa upendo huzaa tunda la furaha ambalo ni Mtu-Mtoto. Upendo wa Baba, Mama na Mtoto unapokamilika tunaongelea mambo ya Utatu Mtakatifu. Tumeumbwa kwa Sura na Mfano wa Mungu.

Kama Mungu alivyo katika Utatu Mtakatifu, basi tunaweza kuwa wakamilifu katika ubinadamu wetu tunapohusiana vyema na Nafsi Tatu za Utatu Mtakatifu. Nafsi zetu sharti zijenge utamaduni wa mahusiano na Jirani zetu, lakini zaidi mno mahusiano na Mungu katika Utatu. Kwa namna hiyo maisha yetu yanakuwa Utatu kama yalivyo maisha ya Mungu. Ndipo tunapogundua kwamba kile kinachoitwa “mimi” kinakuwa “mimi” tu katika mahusiano na wengine, kinyume na utaratibu wa ulimwengu wa sasa unaoendekeza ubinafsi na umimi. Fundisho la Utatu Mtakatifu linatupatia changamoto ya mahusiano kati ya Mimi, Mungu na Jirani. Mimi ni Mkristo kwa kuwa ninaishi katika mfungamano na mahusiano baina yangu na Mungu na Jirani yangu. Neema ya Utatu Mtakatifu na Baraka zitokanazo na maadhimisho haya zitusaidie tubandukane na kila aina ya ubinafsi, tukinuia kuishi maisha ya umoja na Upendo kwa Mungu na kwa Jirani.

Vipindi mbalimbali vya Kiliturujia katika mwaka wa Kanisa vinatupa nafasi ya kulitafakari fumbo hili la Utatu Mtakatifu. Majilio: Tunajifunza juu ya upendo wa Mungu katika kuwaandaa wanadamu ili wampokee Masiha – Kristo mwokozi wa dunia. Noeli: Tunaonja wema wa Mungu kwa kukubali kuwa kati yetu katika hali zote isipokuwa dhambi, upendo wake kwa miaka 30 alionesha akiwa mtoto wa mseremala na seremala kule Nazareti. Amekuwa mtu ili amrudishie mwanadamu hali ya umungu. Sisi tumepewa hadhi ya wana na warithi pamoja na Kristo katika uzima wa milele. Kipindi cha kawaida cha mwaka, tunajifunza Kristo aliyejimwilisha, akienda huko na huko akitangaza Habari Njema za Ufalme wa Mungu, akiponya wagonjwa, akiwajali na kuwahurumia wadhambi akiwarudisha kwa Baba (Lk 4:16 ff).

Kwaresima: Kristo anatutafakarisha juu ya ubaya wa dhambi. Anatiwa majaribuni, anateswa na kufa kama fidia kwa dhambi zetu. Pasaka: ni juu ya Ufufuko wa Bwana. Katika pasaka tumepewa uzima wa kimungu ndani yetu. Msamaha unapatikana kwa wote, mlango wa mbingu uko wazi kwa wote na mwisho kabisa Kristo anakaa kati yetu kama ndugu. Pentekoste: Kristo anahitimisha ahadi ya kumpeleka Roho Mtakatifu na katika yeye tunapata maisha mapya ndani ya Mungu. Kanisa linatualika tutafakari matendo haya ya wokovu ya utatu mtakatifu siyo kama historia bali katika kuyahuisha na kuyaishi katika nyakati zetu kama mtu binafsi na kama jumuiya. Kwa maneno mengine; Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wanafanya mchana na usiku katika ulimwengu wetu kama walivyofanya zamani wakitupa hekima, nguvu na upendo kila mmoja katika mwaka wote wa liturujia. Basi na tuifungue mioyo yetu tuuruhusu Utatu Mtakatifu uendelee kujidhihirisha katika maisha yetu ya kila siku, ili siku moja tukashirikishwe katika utukufu wao huko mbinguni.

Utatu Mtakatifu
27 May 2021, 15:51