Tafuta

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni msingi wa mafumbo yote yanayoadhimishwa na Mama Kanisa. Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni msingi wa mafumbo yote yanayoadhimishwa na Mama Kanisa. 

Fumbo la Utatu Mtakatifu: Msingi wa Mafumbo Yote ya Mama Kanisa

Leo tunasherekea Fumbo la Utatu Mtakatifu moja ya mafumbo msingi sana ya imani yetu kwa sababu tunaliadhimisha na kulitukuza Fumbo la Mungu mwenyewe ambaye amejifunua kwetu kuwa ni Mungu mmoja katika Nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Mafumbo mengine ya imani yetu yanachipuka na kuchanua kutoka katika fumbo hili msingi la Mungu mwenyewe!

Na Padre Andrew Mlele, - Vatican.

Tunaongozwa na Maandiko Matakatifu kama ifuatavyo: Somo I: Kum. 4:32-34, 39-40: Somo II: Rum 8:14-17 Somo la Injili: Mt 28:16-20 Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican karibu katika tafakari ya Neno la Mungu tupoadhimisha Dominika ya Utatu Mtakatifu. Leo tunasherekea moja ya mafumbo msingi sana ya imani yetu kwa sababu tunaliadhimisha na kulitukuza fumbo la Mungu mwenyewe ambaye amejifunua kwetu kuwa ni Mungu mmoja katika Nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Mafumbo mengine ya imani yetu yanachipuka na kuchanua kutoka katika fumbo hili msingi la Mungu mwenyewe. Wazo msingi linalojitokeza katika masomo ya Dominika hii ni kwamba Mungu amejifunua kwetu kwa njia ya matendo yake ya Upendo. Hakuna sehemu yoyote katika Maandiko Matakatifu ambapo jina “Utatu Mtakatifu” linatajwa. Biblia haitaji jina hilo hata kidogo. Basi sisi tunapata wapi fundisho hili kubwa namna hii ambalo ni msingi hata katika kuamini kwetu? Hatuwezi kwenda mbali kutafuta jibu la swali hili bali tunarudi tena katika Maandiko Matakatifu na humo kwa tafakari ya kina tunagundua kuwa Fumbo hili la Utatu Mtakatifu limejulishwa na kutambulishwa na Mungu mwenyewe kwa watu wake hatua kwa hatua. Ingawa Utatu Mtakatifu ni fumbo, tunajaliwa mwanga wa kuweza kulizungumzia na kulieleza ingawa si katika ukamilifu wake.

Mafumbo yote yanaweza kuzungumziwa lakini fumbo linalomuhusu Mungu mwenyewe linadai tulizungumzie kwa umakini na unyenyekevu mkubwa. Na zaidi ya hayo, fumbo hubaki kuwa fumbo. Fumbo hili kubwa halikuja kwetu kwa njia ya kanuni na nadharia bora za kisayansi bali kwa matendo halisi ya Mungu mwenyewe anayefanya kazi kati ya wanadamu. Katika somo la kwanza, kutoka katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati, Musa ambaye alijua wazi kwamba hataingia nchi ya ahadi anatoa hotuba yake ya kuwaaga watu wa taifa teule la Mungu akiwakumbusha juu ya thibitisho la upendo wa Mungu kwao. Anawakumbusha ya kwamba Mungu amejifunua na kujitambulisha kwao kwa matendo halisi ya upendo kwao. Kwa maneno mengine anawakumbusha ya kuwa Mungu kwao si nadharia au jambo la kufikirika bali ni Nafsi halisi ambaye amehusiana nao kwa matendo yanayothibitika. Wao wamemtambua Mungu kama Bwana wa historia yao kwa matendo yake ya huruma na upendo. Aidha, kwa tafakari ya kina wamemtambua kama Muumbaji aliye chanzo cha ubinadamu na kila mtu. Kwa sababu hiyo, Musa anawaasa kwamba watakapoingia nchi ya ahadi wasimsahau Mungu ambaye amekuwa nao tangu mwanzo. Somo hili linatupa ujumbe kwamba ukweli kumhusu Mungu ambaye ni Mmoja katika Nafsi tatu, si ukweli tunaoufahamu kwa njia ya nadharia za kisayansi bali ni ukweli tunaoutambua kwa njia ya ufunuo wa Mungu mwenyewe kupitia matendo yake halisi ya wema, huruma na upendo kwetu ambayo tunayaonja kwa namna mbalimbali katika maisha yetu ya kila siku.

Katika somo la pili kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi tunaendelea kupata mwanga zaidi juu ya fumbo la Utatu Mtakatifu. Mkazo mkubwa bado unawekwa katika Mungu anayejifunua kwetu kwa matendo ya upendo. Ni kwa njia ya upendo huo wa Mungu hata sisi tulio wadhambi tumekwezwa na kupewa hadhi ya kuwa wana wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu katika Roho Mtakatifu. Kwa kufanyika wana wa Mungu tumekuwa na uhusiano na Mungu mwenyewe. Mtume Paulo anaonesha namna nafsi tatu za Mungu mmoja zinavyofanya kazi katika kujenga uhusiano huo. Tuna amani na Mungu Baba kwa njia ya mateso ya Mwanaye Yesu Kristo, na kwa njia ya ya Roho Mtakatifu tumejifunza kumuita Mungu Abba! Baba!. Tuko hivi tulivyo kwa sababu Mungu katika Utatu wake anatutunza. Katika Injili Mwinjili Mathayo anaonesha jinsi ambavyo Kristo Mfufuka anafunua kwa wanafunzi wake ukweli juu ya ufalme ambao amekabidhiwa, analitambulisha jina la Mungu kama Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, na kuwatuma wanafunzi wake kwenye utume wa kuyafanya mataifa yote kuwa wafuasi wake. Na zaidi ya hayo anawahakikishia kuwa nao katika utume huo hata mwisho wa dahari.

Katika agizo analolitoa kwa wanafunzi wake Yesu analitaja jina la Mungu kuwa ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Na ni kwa jina hilo wote walio wafuasi wake wanabatizwa. Jina hili linaonesha ushirika wa Utatu Mtakatifu ambao ni msingi wa maisha ya ufuasi. Hivyo basi ubatizo ni sakramenti ya mkutano na Nafsi Tatu za Mungu. Na kwa kuwa upendo ndio kiini cha Utatu Mtakatifu, basi kwa njia ya Ubatizo kwa jina la Utatu Mtakatifu tunazamishwa katika uzima na upendo wa Mungu mwenyewe. Ndugu zangu wapendwa katika Kristo, fundisho juu ya Utatu Mtakatifu ni fumbo la msingi la imani yetu. Tulisifu na kulitukuza fumbo hili la Utatu Mtakatifu, kwani kwa njia yake tumeshirikishwa katika mpango wake wa ukombozi yaani, Baba si tu ametuumba sisi bali ametukweza hata kutufanya tuwe tena watoto wake kwa njia ya Mwanaye mpendwa aliyemtoa kwetu sisi apate kutukomboa kutoka katika utumwa wa shetani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, na Roho Mtakatifu aliye tunda la upendo la Baba na Mwana amekuja kukaa katika kanisa na katika kila nafsi ya mwamini ili apate kuijaza mioyo yetu mapendo ya kweli ya Mungu.

Kwa hiyo wapendwa, pendo hili tulilolipokea kutoka kwa Utatu Mtakatifu tulitunze, tulidumishe, tuliendeleze na kuliishi katika maisha yetu ya kila siku pasipo kubaguana. Tuoneshe mapendo hayo kwa watu wote: matajiri kwa maskini, wachamungu kwa wasio wachamungu, wagonjwa kwa wenye afya, kwa wema na kwa wasio wema n.k. Tukifanya hivyo, hakika tutawafanya watu wengi wayapokee mapendo hayo ya Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu na mara baada ya maisha haya waweze kuunganika na Utatu Mtakatifu katika furaha ya milele mbinguni. Tukumbuke ya kuwa tumepewa wajibu wa kumshuhudia Kristo na kuwafanya watu wote kuwa wanafunzi wake. Tutafanikiwa katika wajibu huo ikiwa tunaongozwa na upendo wa Mungu. Mungu hatotambulika kwa watu kwa njia tu ya nadharia ambazo tutazieleza kwa hekima ya kibinaadamu bali atajulikana na kuwagusa watu kwa njia ya matendo ya upendo kutoka kwetu sisi tuliomtambua na kumuamini. Kama ambavyo watu wa taifa lake teule walivyomtambua kwa matendo yake halisi ya wema na upendo kwao, ndivyo ambavyo watu watamtambua kwa njia ya matendo yetu mema na ya upendo.

Leo tunapoadhimisha sherehe hii ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni vema tukaomba neema ya Mungu ili tuweze kudumisha upendo na umoja katika maisha yetu tukianzia katika familia maana familia inatupa picha nzuri sana juu ya Utatu Mtakatifu. Hii ni namna bora ya kulifundisha na kuliishi fumbo la Utatu Mtakatifu. Ni katika familia tunajifunza kujitoa kwa ajili ya wengine na kwa namna hiyo tunaushuhudia ukweli wa Utatu Mtakatifu uliojitoa kabisa kwa ajili yetu sisi. Pia ndugu zangu, kama vile tofauti za nafsi za Utatu Mtakatifu haziuvunji umoja wake yaani Mungu mmoja tu katika nafsi tatu; vivyo hivyo nasi tulio wafuasi wake Kristo, yatupasa kuudumisha umoja wetu katika kanisa. Tofauti zetu zisiwe sababu ya sisi kutengana na kuubomoa huu umoja wetu, bali ziutajirishe na kuudumisha umoja huo. Kwa hiyo ndugu, leo tunapoiadhimisha sherehe hii ya Utatu Mtakatifu, tutoe shukrani zetu za dhati kwake kwa mema yote uliotutendea na unayoendelea kututendea katika maisha yetu ya kila siku. Shukrani zetu kwake inaweza ikawa ni katika kuyatii, kuyafuata na kuyazingatia mambo yote yaliyo mema tunayoamiriwa ili mara baada ya maisha haya sisi nasi tupate kuunganika na mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu katika ufalme wake huko mbinguni.

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu…!

Fumbo Upendo
28 May 2021, 15:30