2019.05.29 L'Ascensione del Signore di Gesù - solennità - vangelo della domenica 2019.05.29 L'Ascensione del Signore di Gesù - solennità - vangelo della domenica 

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Hatima ya Binadamu!

Kwa muda wa siku arobaini, Kristo Yesu aliwatokea na kuzungumza na wafuasi wake, akala na kunywa nao akawaimarisha katika misingi ya imani, matumaini na mapendo thabiti. Wakati wote huo, utukufu wake ulikuwa bado umefunikwa na alama za ubinadamu wa kawaida. Kanisa linakiri na kufundisha kwamba, Kristo Yesu alipaa mbinguni, amekaa kuume kwa Baba. Utukufu wa Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican popote pale unapoendelea kututegea sikio lako wakati huu, tunapoadhimisha Kipindi cha Liturujia ya Neno la Mungu, Sherehe ya Kupaa Bwana Yesu Kristo Mbinguni. Leo pia Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni. Baba Mtakatifu Francisko amechagua sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mwinjili Yohane, Sura 1: 46: “Njoo Uone”: Mawasiliano Kwa Kukutana na Watu Jinsi na Mahali Walipo” kama kauli mbiu inayonogesha maadhimisho ya Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni inayoadhimishwa tarehe 16 Mei 2021 sanjari na Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni. Njoo uone ni maneno ya Mtume Filipo ambayo ni kiini cha Injili ya cha kama ilivyoandikwa na Yohane, kinachoonesha ushuhuda wa kikristo kabla hata ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa maneno. Huu ni ushuhuda unaodhihirisha mchakato wa watu kuangaliana machoni, shuhuda mbalimbali, uzoefu na mang’amuzi; kukutana pamoja na kukazia ujirani mwema.

Baba Mtakatifu anawataka waandishi wa habari kuzingatia mambo msingi katika maisha ya watu. Watambue kwamba, Injili ni habari inayoendelea kujipyaisha kila kukicha. Baba Mtakatifu anawashukuru wadau wote wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kwa huduma makini kwa watu wa Mungu. Watu wa Mungu watambue fursa na hatari zilizomo kwenye mitandao ya kijamii na kwamba, uzoefu na mang’amuzi ni mambo msingi yanayosiyokuwa na mbadala. Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni inabainisha hatima ya maisha ya mwanadamu, yaani kwenda mbinguni, ili kukaa na Kristo Yesu na watakatifu milele yote! Huu ni mwaliko wa kuendelea kujikita katika ushuhuda wa upendo, changamoto endelevu kama wafuasi wa Kristo Yesu. Kwa muda wa siku arobaini, Kristo Yesu aliwatokea na kuzungumza na wafuasi wake, akala na kunywa nao akawaimarisha katika misingi ya imani, matumaini na mapendo thabiti. Wakati wote huo, utukufu wake ulikuwa bado umefunikwa na alama za ubinadamu wa kawaida.

Kanisa linakiri na kufundisha kwamba, Kristo Yesu alipaa mbinguni, amekaa kuume kwa Baba. Atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu; nao ufalme wake hautakuwa na mwisho!Maana yake ni kwamba, Kristo Yesu anakamilisha mchakato wote wa uwepo wake wa kibinadamu na hivyo sasa anarudi katika utukufu wa Mungu unaojionesha katika sura ya wingu na mbingu. Lk 24:51 na tangu hapo ameketi kuume kwa Mwenyezi Mungu. Hakuna mtu aliyepaa mbinguni kwa Baba ila Yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani Mwana wa mtu. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, ubinadamu ukiachiwa katika nguvu zake za maumbile hauwezi kufika kwenye nyumba ya Baba, kwenye uzima na furaha ya milele pamoja na Mwenyezi Mungu. Kwa kupaa mbinguni, Kristo Yesu amemfungulia mwanadamu njia, ili akae na kuamini, kwamba, waamini ambao ni viungo vya mwili wake, amewatangulia huko aliko Yeye aliye kichwa chetu na shina letu. Rej. KKK 659-662. Huyu ndiye Kristo Yesu aliyeinuliwa juu ya Msalaba, ili kuwavuta wote kwake. Ni Kuhani wa Agano Jipya na la milele anayewaombea binadamu wote mbele za Mwenyezi.

Ni kiini na mtendaji mkuu wa Liturujia inayomheshimu na kumwadhimisha Baba wa mbinguni. Kristo Yesu ameketi kuume kwa Mungu Baba. Maana yake ni kwamba, Kristo Yesu yuko katika utukufu na heshima ya kimungu, ambamo Kristo Yesu kama Mwana wa Baba wa milele alikuwako kabla ya nyakati zote, kama Mungu, na mwenye uwamo mmoja na Baba, anaketi kimwili, baada ya kumwilishwa na baada ya mwili wake kutukuzwa na huo ni mwanzo wa utawala wake wa Kimasiha. Kristo Yesu, kichwa cha Kanisa, ametutangulia sisi waja wake katika ufalme mtukufu wa Baba wa milele, ili nasi, viungo vya Fumbo la huo mwili, tuishi katika tumaini kwamba siku moja tutaishi naye milele. Kristo Yesu akiwa ameingia mara moja kwa daima ndani ya hekalu la mbinguni, anasali daima kwa ajili yetu kama mshenga anayetuhakikishia kumiminwa kwa daima kwa Roho Mtakatifu. Rej. KKK 664-667.

Kwa nguvu tendaji na Mapaji ya Roho Mtakatifu, tunaitwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudi Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Hakuna sababu msingi ya kusimama na kukodoa macho juu mbinguni, bali mwaliko ni kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha ya kila siku kama mashuhuda wa upendo, imani na matumaini. Ujumbe wa leo unaotolewa na Kristo Yesu ni kwamba, “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya”. Mk 16: 15-18.

Kwa ufupi hapa, wafuasi wa Kristo Yesu wamepewa dhamana ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema; wanatakiwa kuwa ni mashuhuda wa Injili inayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani, na hasa zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamiii na mwishoni, wanapaswa kuganga na kuwaponya watu, kielelezo cha uwepo na nguvu tendaji za Roho Mtakatifu. Mtakatifu Paulo Mtume katika Somo la Pili, anawataka Wakristo wa Efeso kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu unaosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu na ukarimu, kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ee Mungu Baba Mwenyezi wa milele, wewe watujalia sisi tulio hapa duniani kushughulika na mambo ya mbinguni. Tunakuomba uelekeze moyo wetu wa Ibada huko aliko Bwana wetu Yesu Kristo, Mungu kweli na mtu mkweli.

Ushuhuda
14 May 2021, 16:35