Sherehe ya Kupaa Bwana: Kutukuka Kwa Yesu Mbinguni!
Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu katika sherehe ya kupaa Bwana, mwaka B wa kiliturujia. Ujumbe mahususi katika sherehe hii ni kuwa; Yesu amepaa mbinguni mwili na roho, ukamilifu wa umasiha wake, ushindi dhidi ya dhambi na mauti/kifo, silaha za shetani. Kupaa kwa Bwana Mbinguni ni adhimisho la tendo la ukombozi ambapo Kristo baada ya kufufuka kutoka wafu na kuingia katika utukufu wake na kuendelea kuwatokea wafuasi wake kwa siku arobaini/muda wa kutosha akiwaimarisha kiimani, alitoweka rasmi katika upeo wa macho yao wasimuone tena, zaidi ya kumtokea Saulo katika barabara ya Dameski (Mdo.9:1-9). Katika somo la kwanza la matendo ya Mitume (Mdo. 1:1-11); ni wosia wa Yesu kwa Mitume kabla hajapaa kwenda kwa Mungu Baba. Katika wosia huu Yesu anawaambia Mitume kuwa wanapaswa kuhubiri habari njema duniani kote pia anawaahidi zawadi ya Roho Mtakatifu atakayewakumbusha yote aliyowafundisha na kuwaongoza siku zote katika kuitangaza habari njema ya wokovu. Baada ya maagizo haya yesu “aliyochukuliwa/akainuliwa juu na wingu likampokea wasimwone tena. Na walipokuwa wakitazama mbinguni watu wawili wakawaambia; “mbona mmesimama, mkitazama mbinguni? Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja vivyo hivyo mlivyomuona akienda zake mbinguni”. Nacho kiitikiko cha wimbo wa katikati kutoka (Zab. 47:5) kinaimba; “Mungu amepaa kwa kelele za shangwe na Bwana kwa sauti ya baragumu.”
Somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (Ef.1:17-23); ni sala ya Mitume inayotupa fundisho juu ya uweza na utajiri wa Mungu uliofunuliwa katika Yesu Kristo. Mungu alimfufua Yesu Kristo toka wafu akamweka kuwa Kichwa cha Kanisa na ulimwengu. Yesu akiwa kichwa cha Kanisa yu pamoja na Kanisa daima. Yeye yuko juu ya vyote vilivyoumbwa na Mungu. Injili ilivyoandikwa na Marko (16:15-20); inatuhabarisha majukumu ya mitume waliyoachiwa na Yesu ambayo ni; kuihubiri Injili ulimwenguni kote na kuwabatiza watakaowaamini. Matunda ya kubatizwa na kuamini katika jina la Yesu ni kutolewa pepo wachafu, kunena kwa lugha, kukingwa na mabaya yote na kuponywa magonjwa. Baada ya kutoa haya maagizo, Yesu akachukuliwa juu mbinguni. Katika masomo haya yote ya Liturujia ya sherehe hii ya kupaa Bwana, tunaona maneno yanayotawala ni kuchukuliwa, kwenda au kupaa juu mbinguni. Nini hasa maana ya kupaa, kwenda au kuchukuliwa juu mbinguni? Katika lugha ya kawaida ya Kiswahili neno kupaa ni kitenzi kikimaanisha kwenda juu, kutoka katika mzizi paa yaani sehemu ya juu.
Katika lugha ya Kibiblia neno kupaa ni kuhama kwa mwili wa utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo mfufuka, kutoka duniani na kuingia Mbinguni. Ni hali ya kutukuzwa kwa Yesu, kuwa mkuu na mmiliki wa vitu vyote mbinguni na duniani kama somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso linavyotuambia. Ni kuwa juu ya vitu vyote. Ni kurudia utukufu aliokuwa nao kabla ya umwilisho, yaani kuchukua mwili kwa mama Bikira Maria. Ni kuvikwa taji ya ushindi. Kristo ni mshindi ameshinda dhambi na mauti (Mk 16:19). Je, ni lini hasa Kristo mfufuka alipaa mbinguni? Tunakiri katika kanuni ya Imani kuwa; “Akafa, Akazikwa, Akashukia kuzimu na siku ya tatu Akafufuka katika wafu na akapaa mbinguni ameketi kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi”. Injili ya Luka inatuarifu kuwa; “Mmojawapo wa wale wahalifu waliosulibiwa pamoja na Yesu alimwambia; “Ee Bwana unikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.” Naye Yesu akamwambia; “Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami mahali pema peponi” (Lk 23:42-43). Kwa maneno haya ni dhahiri kuwa hakukuwa na wakati fulani uliopita kutoka ufufuko mpaka kupaa katika maana ya kuwa na hali ya utukufu.
Kwa ufufuko Yesu alitoka kaburini akiwa na mwili wa utukufu, usiofungwa na nguvu za maumbile, ndiyo maana aliweza kuingia katika chumba walimokuwamo Mitume hata milango ilipokuwa imefungwa kwa kuwa alikuwa na mwili wa utukufu. Kumbe tunaposema Yesu mfufuka alipaa mbinguni siku ya arobaini, tunamaanisha siku ambapo alionana ana kwa ana, uso kwa uso, macho kwa macho na wanafunzi wake kwa mara ya mwisho na kuwapa maagizo ya kuihubiri injili ulimwenguni mwote mpaka ukamilifu wa dahari na baada ya hapo hakuonekana tena. Na siku arobaini hapa zina maana ya muda wa kutosha, ambao Yesu mfufuka aliwatokea wanafunzi wake akiwaimarisha ili waweze kushuhudia ufufuko wake kwa watu wote. Katika simulizi la tukio la kupaa Bwana wetu Yesu Kristo mbinguni, tunaambiwa kwamba, “Wingu likampokea wasimwone tena.” Wingu katika Maandiko Matakatifu ni alama ya uwepo wa utukufu wa Mungu. Musa alikutana na Mungu katika wingu (Kut. 20:21), Wingu lilitanda juu ya hema ya kukutana na Mungu na wana wa Israeli (Kut. 40:34). Ni katika mnara wa wingu kama kivuli wakati wa mchana na moto wakati wa usiku, Mungu aliwaongoza Waisraeli ili waweze kusafiri mchana na usiku (Kut. 13:20–22).
Ni katika wingu ilitoka sauti ya Mungu Baba baada ya ubatizo wa Yesu mtoni Yordani na baada ya Yesu kugeuka sura mlimani Tabor ikisema; Huyu ni mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye. Kumbe kupaa kwa Yesu mbinguni ni kwenda kwa Mungu Baba, kurudi katika makao ya Mungu ambayo yanawakilishwa katika ishara ya wingu. Kupaa juu mbinguni kwa Yesu mfufuka haimaanishi kuwa Yesu alisafiri kwenda juu angani. Kwenda juu mbinguni ni lugha ya picha inayoashiria ukuu na utukufu wake. Ni namna ya kusema kuwa Yesu amerudi katika makao yake ya milele katika hali ya utukufu wa kimungu. Wayahudi waliamini kuwa makao ya Mungu yako juu angani ndiyo maana kilele cha mlima ilichukuliwa kuwa ni sehemu ya karibu zaidi na Mungu na ni sehemu ya kukutana, kumuabudu na kumsikiliza Mungu. Mungu alimtokea Musa katika kichaka kilichowaka moto katika mlima Horebu/Sinai (Kut.3:1-6), mahali alipopokea Amri kumi za Mungu/Torah (Kut.24:12-18) na Mfalme Sulemani alijenga hekalu la Mungu juu ya mlima Sayuni, mlima huo ukawa mahali pa pekee pa kukutana na Mungu. Baadaye Sayuni ukawa mji wa mfalme/Masiha kama walivyotabiri manabii (Isa.2:1-3, Zek.14:16–19; Ebr.12:22; Uf.14:1).
Kwa Wayahudi neno Juu au mbinguni pia ni jina mbadala la Mungu. Malaika Gabrieli alipompasha habari Bikira Maria alimwambia usihofu, kwa maana “Roho Mtakatifu atakujia juu yako na nguvu zake Aliye Juu zitakufunika kama kivuli (Lk. 1:35). Zakaria katika wimbo wa kinabii anasema “naye mtoto ataitwa nabii wake Aliye Juu” (Lk. 1: 76). Yesu katika kuhubiri anasema, tubuni kwa maana ufalmwe wa Mbinguni umekaribia. Na kabla ya kupaa, Yesu aliwaambia wanafunzi wake wasitoke Yerusalemu mpaka watakapovikwa uweza na nguvu kutoka Juu naye alichukuliwa kwenda Juu mbinguni (yaani kwa Mungu). Kupaa mbinguni kwa Yesu ni uthibitisho kwamba maisha ya hapa duniani siyo ya umilele. Maisha ya umilele yako mbinguni Kristo aliko, ndiyo maana katika sala ya koleta Padre kwa niaba ya jamii ya waamini anasali; “Ee Mungu Mwenyezi, utufanye tuwe na furaha takatifu na shukrani; kwa maana kupaa kwake Kristo Mwanao ni mfano wetu; na huko alikotangulia yeye kichwa chetu, ndiko tunakotumaini kufika sisi tulio mwili wake.”
Ili tuweze kufika Mbinguni aliko Kristo, yatupasa tufuate agizo lake; “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu (Mt. 28: 19). Hili ni jukumu la kila mbatizwa. Kmbe kuihubiri injili kwa maneno na matendo yetu, kusali, kulisoma, kulitafakari na kuliishi neno la Mungu, kupokea sakramenti kwa kustahili na kutenda matendo mema ndiyo masurufu yetu ya njiani kuelekea juu mbinguni. Tuombe neema ya kuyafanya haya ili mwisho nasi tupae twende juu mbinguni aliko Yesu Kristo Bwana na Mkombozi wa maisha yetu, tukaishi naye milele yote.