Pentekoste: Ujio wa Roho Mt. na Mwanzo wa Utume wa Kanisa!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, katika sherehe ya Pentekoste, siku ya hamsini baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni siku ya ujio wa Roho Mtakatifu, ishara ya umoja wetu na Mungu kama wimbo wa mwanzo unavyoimba; “Roho ya Bwana imeujaza ulimwengu, nayo inayoviunganisha viumbe vyote, hujua maana ya kila sauti, aleluya” (Hek.1:7). Roho Mtakatifu akaaye ndani mwetu, hutuunganisha na Mungu na pia hutuunganisha sisi kwa sisi tuishi kwa upendo kama anavyotuambia Mtume Paulo; Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu, na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi Aleluya” (Rum.5:5). Kumbe basi, Pentekoste ni adhimisho la mwanzo wa Agano Jipya, ni mwanzo wa taifa jipya la Mungu, ni siku ya kukumbuka ujio wa Roho Mtakatifu na vitu “kuumbwa” upya. Ni siku ya kukumbuka kuzaliwa kwa Kanisa na mwanzo wa utume wa Kanisa la mwanzo la mitume. Ni sherehe ya waamini walei wote. Sherehe hii inakamilisha fumbo la Pasaka kwa kuhitimisha kipindi cha Pasaka na hivyo Mshumaa wa Pasaka unatunzwa kwa heshima karibu na kisima cha ubatizo na unawashwa wakati wa ubatizo, ili mishumaa ya wabatizwa iwashwe kutokea mshumaa huu. Katika mazishi mshumaa wa Pasaka unawekwa kando ya jeneza kuwa ishara ya kifo cha mkristo ni Pasaka halisi. Nje ya kipindi cha Pasaka Mshumaa wa Pasaka hauwekwi patakatifuni na wala hauwashwi. Kuanzia Jumatatu baada ya Jumapili ya Pentekoste, tunaacha kusali sala ya Malkia wa Mbingu na tunaanza kusali sala ya Malaika wa Bwana.
Somo la kwanza la matendo ya Mitume (Mdo. 2:1-11), linasimulia jinsi tukio la ujio wa Roho Mtakatifu lilivyotukia siku ile ya Pentekoste kuwa; upepo wa nguvu na ndimi za moto ambazo ni alama ya uwepo wa Roho Mtakatifu viliwashukia Mitume. Kwa nguvu ya Roho Mitume walipata ujasiri wa kuhubiri Injili. Pia umoja na uelewano uliopotea sababu ya dhambi uliletwa tena kati ya mataifa kwa maana watu wote walisikia mitume wakisema kwa lugha zao matendo makuu ya Mungu ndiyo maana utanguliza wa sherehe hii ya Pentekoste unasema; “Hapo mwanzo wa Kanisa huyo Roho Mtakatifu aliyafundisha mataifa yote kumjua Mungu, akawaunganisha watu wa lugha mbalimbali katika kuungama imani moja. Somo la pili la Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorinto (1Kor.12:3b-7,12-13), linatueleza kuwa Roho Mtakatifu ni msingi wa karama na huduma mbalimbali katika Kanisa. Yeye ndiye anayefanya karama hizo zilete faida na umoja katika jumuiya nzima kama viungo mbalimbali vya mwili vinavyosaidiana kwa faida ya mwili ndiyo maana katika sala baada ya komunio Padre anasali akisema; “Ee Mungu, umelijalia Kanisa lako mapaji yako ya mbinguni. Uilinde neema hiyo uliyotujalia, ili mapaji ya Roho Mtakatifu tuliyoyapokea yasitawi daima, nacho chakula cha roho kituongezee ukombozi wa milele.
Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yn.20:19-23); inatufundisha kuwa Roho Mtakatifu aliyefanya kazi ya kuwaunganisha Mitume na Yesu mfufuka na sasa anawaunganisha watu na Mungu kwa kuwaondolea dhambi zao. Pato la kazi hii ya Roho Mtakatifu ni amani kati ya Mungu na watu ndiyo maana katika sala ya kuombea dhabihu Padre kwa niaba ya jamii ya waamini anasali; “Ee Bwana, tunakuomba Roho Mtakatifu atufumbulie zaidi siri ya sadaka hii, kama alivyotuahidia Mwanao. Atujulishe pia ukweli wote kwa rehema yake.” Kihistoria katika Agano la Kale, Pentekoste ilikuwa ni sikukuu ya wakulima wakaanani ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya mazao mapya waliyovuna na kumwomba awajalie tena mavuno mengi na mazuri msimu ufuatao. Hivyo iliitwa sikukuu ya mavuno (Kut. 23:16), au “Sikukuu ya Mavuno ya kwanza” (Hes 23:26) au “Sikukuu ya Majuma,” kwa sababu iliadhimishwa majuma saba baada ya Pasaka (Kut 34:22). Sikukuu hii ya shukrani ni agizo la Mungu kwa Waisraeli baada ya kutolewa utumwani Misri: Na itakuwa, ukiisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi, na kuimiliki, na kukaa ndani yake; twaa malimbuko ya ardhi, utakayoyavuna katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako mbele ya madhabahu katika mikono ya kuhani (Kumb 26:1–13).
Sikukuu hii ilikuwa ni kwa ajili ya kukumbuka Agano la Sinai, jinsi Mungu alivyowapa amri kumi na kuzaliwa kwa Taifa lao. Iliadhimishwa siku ya 50 baada ya Pasaka, kwa sababu tangu kutoka Misri (Pasaka) mpaka kufika Mlima wa Sinai zilipita siku 50 (Kut 19:1). Hivyo sherehe hii ikapewa jina la sikukuu ya majuma kwa vile ilisherehekewa majuma saba baada ya pasaka ya Wayahudi ambayo yanafanya siku hamsini ndiyo maana ikaitwa Pentekoste neno la kigiriki likimaanisha siku ya hamsini baada ya pasaka (2Mak 12:31ff; Tob 2:1). Nanyi mtatoa katika makao yenu mikate miwili ya kutikiswa, itakayookwa na chachu, iwe malimbuko kwa Bwana...” Ni katika siku hii walikula mikate iliyotiwa chachu. Katika sikukuu kubwa za kuhiji Yerusalemu katika mwaka kwa Wayahudi ni katika sikukuu ya Pentekoste/sikukuu ya shukrani kwa Mungu watu walipaswa kubeba zawadi mbalimbali. “Hakuna mtu atakayejitokeza mbele ya Bwana mikono mitupu: Kila mmoja wenu ni lazima alete zawadi kulingana na jinsi ambavyo Bwana Mungu wenu alivyowabariki” (Kumb. 16:16-17). Desturi hii ya kutoa shukrani ya mazao ilienea katika nchi nyingi kuzunguka bahari ya kati, na watu kutoka nchi mbalimbali pande zote za dunia, walikuja Yerusalemu kutoa shukrani kwa Mungu kwa neema na baraka za mavuno mapya.
Siku ya Pentekoste ya Kiyahudi, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume na kuwajaza nguvu na ujasiri wakatoka nje, wakaenda hekaluni ambapo walikuwapo watu wa kila lugha, kila jamaa na kila taifa waliokuja kuhiji na kumtolea Mungu shukrani za mazao yao mapya ambao majina yao yanatajwa katika somo la kwanza la kitabu cha Matendo ya Mitume (2:1-11). Mitume wakaanza kuwahubiria kwa nguvu habari za Yesu mfufuka na wote wakasikia na kuelewa kila mmoja kwa lugha yake ya kuzaliwa na wakabatizwa. Kama vile Wayahudi walivyomshukuru Mungu kwa baraka za mavuno mapya huku wakikumbuka kuzaliwa upya kwa taifa lao la Israeli na kupewa amri kumi za Mungu, katika sherehe hii ya Pentekoste Kanisa linamshukuru Mungu kwa zawadi ya wakristo wapya waliobatizwa katika mkesha wa Pasaka ambapo mbiu ilipigwa tukisherekea usiku ule Mtakatifu tulipokombolewa kutoka utumwa wa dhambi. Tunasherehekea ujio wa Mungu Roho Mtakatifu, nafsi ya tatu ya Utatu Mtakatifu, asiye na mwanzo wala mwisho, yeye ndiye mfariji, mtakatifuzaji, kiongozi na mwalimu wetu. Ndiye anayewajalia watu anaowashukia vipaji mbalimbali kama; hekima, akili, shauri, nguvu, elimu, ibada na uchaji kwa Mungu na karama mbalimbali kama; unabii, Uponyaji, ualimu na kunena kwa lugha, kila mmoja kadiri atakavyo yeye kusudi tuvitumie kwa kufaana. Hivyo basi, yatupasa kutambua karama hizo zote kuwa ni zawadi kutoka kwa Mungu zinazotufikia kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Kumbe, hatuna budi kumshukuru Mungu kwa zaidi ya Roho Mtakatifu kwa kuzitumie vyema karama anazotujalia kwa manufaa ya wote maana tusipozitumia vyema tutadaiwa siku ya mwisho kama anavyouambia Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wa Kwanza kwa Wakorintho (1kor.12:3b-7,12-13). Tutambue kuwa vipaji hivi ni zawadi kwa ajili ya kuhudumiana, kujengana na kufaidiana sisi kwa sisi tukiongozwa na karama iliyo kubwa kuliko zote yaani upendo. Tujihadhari na dhambi ya kumkufuru roho mtakatifu kwa kujifanya kila tulichonacho ni chetu kwani Yesu anasema; “kwa sababu hiyo nawaambieni, watu watasamehewa dhambi na kufuru zao zote, lakini hawatasamehewa dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu” (Mt.12:31). Kwa Ubatizo wetu na Kipaimara sote tumejazwa Roho Mtakatifu, yatupasa kuongea lugha moja tu, lugha ya upendo kwa wote, lugha ambayo hakuna asiyeielewa. Upendo daima huvumilia, ni mpole, hauna wivu, haujidai, haujivuni, una adabu, tena hautafuti faida yake binafsi, haufurahii maovu, bali ukweli (1Kor.4-6). Tumruhusu Roho Mtakatifu aingie ndani ya mioyo yetu, ndani ya nafsi zetu, akae nasi, akae ndani ya familia zetu na jumuiya zetu atufundishe kuishi kwa upendo, achome mioyo yetu atufanye tuwe safi, aondoe tabia zote ambazo zinaendana na hila za shetani, achome uovu wetu, achome roho ya kisasi.
Roho Mtakatifu awashe ndani mwetu moto wa mapendo, atupe Roho ya hekima na elimu, atufundishe kusali vizuri, atushushie kipaji cha ukweli na mapendo ya kweli. Aondoe vilema vyote ambavyo vinatuvuruga na kutuletea maafa, atutie nguvu ya kuweza kufahamu madhaifu yetu, ili sote tuungane na kuwa mwili mmoja katika Kristo na tuione sura ya Mungu katika wenzetu kwa kuwapenda kama Kristo alivyoagiza.