Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Seherehe ya Pentekoste: Zawadi ya Mungu Baba na Mungu Mwana kwa Kanisa tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho yote ya dunia. Tafakari ya Neno la Mungu Seherehe ya Pentekoste: Zawadi ya Mungu Baba na Mungu Mwana kwa Kanisa tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho yote ya dunia. 

Sherehe ya Pentekoste: Zawadi ya Baba na Mwana Kwa Kanisa!

Pentekoste ni sherehe ya kuzaliwa kwa Kanisa, jumuiya ya waamini inapompokea Roho wa Mungu na kutumwa kuwa mashahuda wa Habari Njema ya wokovu kwa watu wote. wa Mataifa. Roho wa Mungu ambaye ni Bwana na mleta uzima! Roho Mtakatifu ni zawadi kutoka kwa Mungu Baba Mwenyezi na kwa Kristo Yesu, Mwanae wa pekee. Ni Sherehe ya Waamini Walei kutangaza Injili!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama ya Kristo Mfufuka iwe nanyi nyote! Yesu wakati wa karamu ile ya mwisho, anawaahidia wanafunzi wake kutokuwaacha peke yao kwa kuwapelekea Roho Mtakatifu, Yohane 14:16,26. Na ndio leo Mama Kanisa anatualika kuadhimisha Sherehe ya Pentekoste. Ni sherehe ya kuzaliwa kwa Kanisa, jumuiya ya waamini inapompokea Roho wa Mungu na kutumwa kuwa mashahidi wa Habari Njema ya wokovu kwa watu wote. Roho wa Mungu ambaye ni Bwana na mleta uzima! Mwinjili Luka anatuonesha ujio wa Roho Mtakatifu katika siku ya Pentekoste, yaani siku ya hamsini baada ya Ufufuko wa Kristo, ni Pentekoste inayogongana na ile ya Kiyahudi, ya siku hamsini baada ya Pasaka ya zamani. Injili ya Yohane ambayo ndiyo tunayoitafakari leo, tukio la ujio wa Roho Mtakatifu linatokea jioni ya siku ile ile ya Ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo, yaani jioni ya siku ya kwanza ya juma. Yohana 20:22.

Yafaa tangu mwanzo kutambua kuwa Fumbo la wokovu wetu ni moja. Kwa maana mateso, kifo, ufufuko, kupaa na zawadi ya Roho Mtakatifu ni tukio moja la wokovu wetu wanadamu, lililotokea katika saa ile ile ya wokovu wetu pale juu Msalabani Kalvario. Hivyo Mwinjili Luka ili tuweze kulielewa vema fumbo hili la Wokovu wetu anatuonesha kujiri katika nafasi mbali mbali. Mwinjili Yohane kwa upande mwingine, anatuonesha leo ujio wa Roho Mtakatifu siku ile ile ya ufufuko ili kutuonesha kuwa ndio zawadi pekee ya Kristo Mfufuka kwa Kanisa lake. Pentekoste ya Mwinjili Yohane inatuonesha kuwa Roho Mtakatifu au Roho wa Mungu ni kama alimiminika moja kwa moja kutoka ubavu wake pale juu msalabani, ambaye anaonekana katika ishara ya maji yaliyotoka ubavuni mwake, na huo ndio upendo wa Kimungu, upendo wa Mungu Baba na Mwana, na tunda la upendo huo ndio Roho Mtakatifu. Yohane 19:34 na 7:37-39. Na ndio tunaona pia Yesu Kristo Mfufuka mara baada ya ufufuko wake alipowatokea Mitume wake akiwaonesha mikono na ubavu wake.

Pentekoste kama Sikukuu ya Wayahudi iliadhimishwa siku hamsini baada ya Pasaka ile ya Wayahudi. Ilikuwa ni kusherehekea kumbukumbu ya wao kufika Mlima Sinai, mahali pale ambapo Musa alipanda juu mlimani na kupokea amri za Mungu, ni kumbukumbu ya maagano waliyofanya kati yao na Mungu aliye Mkombozi wao. Mwinjili Luka kwa kuonesha ujio wa Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste ni kutualika nasi kuona mwanzo wa maagano ya amri ile kuu na mpya, ndio Roho wa Upendo. Roho Mtakatifu daima ni ishara ya upendo wa Mungu Baba kwa Mungu Mwana, anakuja na kutuunganisha nasi na Mungu na jirani kwa njia ya upendo. Kila anayempokea Roho wa Mungu anaanza mwanzo mpya, maisha mapya, maisha kama ya Mungu, maisha ya kumpenda Mungu na jirani, maisha ya upendo. Zawadi ya Kristo Mfufuka kwa kila mmoja wetu ni Roho wake anayetuwezesha nasi kupenda kama Yeye iwe kwa Mungu na pia kwa jirani zetu. Pentekoste kama Pasaka ni sherehe ya uuumbaji mpya, ni mwanzo mpya. Imani yetu inatualika kila siku kufanya mapinduzi katika maisha yetu si tu kwa bidii zetu bali kwa msaada wa Roho Mtakatifu, aliye Bwana mleta uzima na anayetutatifuza.

Pentekoste ya Yohane, kwa maana tukio la Pentekoste kadiri ya Injili ya Yohane kama nilivyotangulia kusema hapo juu ni tukio linalojiri siku ile ile ya Pasaka, siku ya nane au siku ya kwanza ya juma, ndio siku ya ufufuko, ni siku ya uumbaji mpya, mwanzo mpya wa maisha ya kila mfuasi wa Kristo Mfufuka. Kristo Mfufuka anawatokea wanafunzi wake wakiwa ndani wamejifungia kwa hofu ya wayahudi. Kitendo cha Yesu kuwatokea wanafunzi wake ndio kinaitwa kwa Kigiriki “ofte”, likiwa na maana ya kujidhihirisha na kujifunua, ni kukutana na wanafunzi wake. Pamoja na kwamba Yesu anajifunua kwao tunamwona Maria Magdalena na hata Mitume wanashindwa kumtambua mara moja, kujifunua na kujionesha kunakozungumziwa hapa sio tu katika umbo lake la nyama bali kwa kadiri ya uelewa wa watu wa Mashariki ya kati, ilimaanisha hasa kujidhihirisha “nafsi yake”. Hivyo ili kumtambua haikutosha kuwa na macho ya nyama bali yale ya imani, sio kuona kwa kawaida bali kwa kuongozwa na jicho lile la imani.

Mitume na hata nasi leo tunaalikwa sio kumuona Kristo Mfufuka kwa macho ya nyama, bali kwa macho ya imani, ndio kuona kule kunakutambulishwa kwa kitenzi cha kigiriki οραω (orao), kuona kwa ndani kabisa kwa jicho la imani, tofauti na aina ya pili ya kuona nayo ni βλεπω (Blepo), kuona kwa macho ya nyama, kuona kwa nje na juujuu tu bila kuwa na imani. Nasi leo tunaalikwa kukutana na Kristo Mfufuka kwa jicho la imani na daima anajidhihirisha na kujifunua kwetu. Kwa Wakristo wale wa mwanzo kama ilivyo kwetu leo siku muhimu kabisa ni Dominika, siku ambapo Mwili wa Kristo yaani Kanisa linakusanyika na kuadhimisha fumbo la wokovu wetu. Matendo 20:7 na 1Wakorintho 16:2.  Ilikuwa jioni ya siku ile ya ufufufuko mitume wakiwa wamejifungia kwa hofu ya wayahudi. Ilikuwa jioni ndio kusema saa ile ambapo wote waliweza kuwa pamoja baada ya shughuli zao za siku nzima, ila ni muda ule ambao mashaka na wasiwasi na uoga wao ulikuwa ni mwingi zaidi, ni saa ile ya kuisha kwa siku, saa ya giza na hofu kuu Yesu anakuja na kujifunua kwao. Na ndivyo Yesu kila mara anafika na kujifunua kwetu saa ile yetu ya mashaka na wasiwasi na uoga mkubwa katika maisha yetu.

Kristo Mfufuka anajifunua si tu saa ya jioni bali hasa pale tunapokusanyika na wengine, na ndio kusema kusanyiko la waamini, iwe katika familia zetu tunapokutana kwa sala au jumuiya zetu ndogo ndogo, vigangoni, maparokiani na popote pale tunapokutanishwa na Roho huyo huyo ili tuweze kuingia katika mahusiano ya ndani na Mungu. Ilikuwa ni asubuhi ya siku ile ya Ufufuko Maria Magdalena na wanawake wengine wanafika na kuwapa habari mitume kuwa Kristo ni mzima, amefufuka na amejifunua kwao. Mitume wanajawa na mashaka na hata kupondeka mioyoni mwao hasa wakijiuliza pia kwa nini hajawatokea wao kwa nafasi ya kwanza kama mitume na rafiki zake wa karibu? Na ndio tunaona Yesu hawaachi kumaliza siku wakiwa na mawazo yale, anajifunua pia kwao, anajionesha kwao na hasa saa ile ya jioni, saa ile ya mashaka na hofu kubwa, saa ile wanapokuwa wote pamoja. Milango ikiwa imefungwa si tu kwa kuwa walikuwa na hofu ila zaidi sana kutuonesha kuwa Kristo Mfufuka sasa yupo na mwili wa utukufu, mwili ule ulio tofauti kabisa na mwili ule wa nyama kwa asili kwani hauzuiliwi tena na kuta wala milango. Ufufuko sio kuipa uzima tena miili ile ya nyama kama alivyofanya Yesu kwa Lazaro, bali ni kuanza na kuingia katika maisha mapya kabisa, maisha ya utukufu. Kuvaa mwili usioharibika. 1Wakorintho 15:42-44 Mtakatifu Augostino anatuambia kama vile kuzaliwa kwake hakukuharibu ubikra wa Mama yake, hivyo hivyo baada ya ufufuko milango na kuta hazikumzuia kufika na kujionesha kwa wanafunzi wake.

Pale ambapo akili zetu zinafika ukomo wa uelewa basi hapo imani haina budi kuchukua hatamu. Fumbo sio kile kilicho kinyume na akili bali kinachopita akili na uelewa wetu wa kibinadamu, hivyo sio upuuzi au ujinga bali ni kile kinachopita uwezo wa akili zetu. Amani kwenu, hii si tu salamu ya kawaida kwa maana ya “Shalom”, bali Kristo Mfufuka anawapa zawadi ya amani, zawadi hiyo ni Yeye mwenyewe kwa wanafunzi wake, kwani anatambua mashaka na wasiwasi wanaokuwa nao, mahangaiko ya ndani kabisa wanayokuwa nayo, hivyo Kristo Mfufuka anatambua hali yao ya kimwili na kiroho na hivyo kujitoa mwenyewe kama zawadi kwao. Ndio zawadi ambaye kila mara Kristo Mfufuka anatupatia kwa nafasi ya kwanza katika saa ile ya jioni, saa ya giza na mashaka na hofu katika maisha ya kila muumini. Anawapa pia zawadi ya Roho wake, Roho Mtakatifu si tu atokaye kwa Baba bali pia atokaye kwa Mwana, Kristo Mfufuka. Kwa uwezo wa Roho huyo anawapa tena mamlaka ya kusamehe dhambi. Kama Kristo alivyotumwa na Baba ulimwenguni ili sisi tuweze kupatanishwa na Mungu Baba, vivyo hivyo tunaona Kristo Mfufuka anatupa wanafunzi wake Roho Mtakatifu ili tuweze kusamehe wengine dhambi, si tu mamlaka ya kikasisi kwa wadarajiwa bali kwa Kanisa zima tunapokea utume wa kusamehe.

Msamaha ni Mungu mwenyewe anayejitoa zawadi kwa kila atubuye, hivyo kwa kila mwamini kufanya toba maana yake ni kumpokea Mungu mwenyewe, ni kukubali kuongozwa na kuunganika naye. Na ndio leo tuna neno la Kiingereza na hata lugha nyingine zenye asili ya Kilatini neno “to perdon”, ni muunganiko wa maneno mawili, “per” na “donare”, ni Mungu anayejitoa zawadi mwenyewe, hivyo kutubu ni kukubali Mungu aingie na kuongoza maisha yangu, ni kumpokea Yeye kama zawadi. Ni uumbaji mpya, na ndio maana tunasikia pia aliwavuvia, ni ishara ile ilyotumika katika uumbaji na ndio pia siku ya Pentekoste, Mungu anamvuvia kila mmoja wetu, Mungu anajitoa zawadi kwa kila mmoja wetu, ni sherehe ya kupokea uzima wa Kimungu, ni kupokea msamaha wa Mungu kwetu ili tuweze kufanyika viumbe wapya. Kristo Mfufuka anaendelea kubaki na Kanisa lake kwa njia ya Roho Mtakatifu, na ndio kwa njia ya Roho huyu wa Mungu tunaalikwa kuwa wajumbe na mashahidi wa msamaha, si kingine bali msamaha kwa upendo na hasa msamaha wa dhambi. Ni Roho anayekuja na kukaa nasi ili tuweze kumshinda yule muovu na uovu. Kristo Mfufuka haliachi Kanisa lake ukiwa au wafuasi wake yatima bali anabaki nasi daima kwa njia ya Roho Mtakatifu, hivyo Kanisa linabaki na amani na furaha kwani daima tunasafiri na kutembea na Kristo Mfufuka, sio tena katika umbo na namna ile ya nyama bali kwa njia isiyoonekana, ndio uwepo wa Roho Mtakatifu.

Roho Mtakatifu anakuja kuufanya upya uso wa dunia, Pentekoste ni Sherehe ya uumbwaji mpya wa sura ya nchi. Yesu anawavuvia mitume wake na kuwaambia pokeeni Roho Mtakatifu, analivuvia Kanisa lake kwani ni kwa njia ya Roho Mtakatifu Kanisa linapata uzima na uhai wa kimungu na hivyo kuweza kutimiza utume na misheni yake. Ni kwa njia ya Roho huyo dhambi na uovu na yule muovu wanashindwa, na badala yake anatawala Roho wa upendo na msamaha.  Sote tuliompokea Roho Mtakatifu siku ile ya Ubatizo na Kipaimara hatuna budi kuwa mashahidi wa Roho huyo kwa kuwa watu wa upendo na msamaha. Roho anakuja ili sote tuweze kuwa na umoja na ndio maana anawatokea wakiwa wote wamekusanyika pamoja, ni huyo anayetuunganisha sisi kama wanakanisa, umoja kati yetu lakini zaidi sana umoja wetu na Mungu aliye muumbaji wetu. Uwezo anaotupa Kristo Mfufuka kwa njia ya Roho wake ni kusamehe, ni kuwa watu wa msamaha, huu ni utume sio wa hiari bali wa lazima kwa kila aliye mfuasi na shahidi wa Kristo mfufuka. Ni utume kwa kila mmoja wetu na hilo litawezekana sio kwa nguvu na akili zetu bali kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Lugha ya Roho Mtakatifu sio lugha ya kutugawa bali inayotuunganisha na inayoeleweka na watu wa kila rangi, kabila na taifa, ni lugha ya upendo. Na ndio tumesikia katika somo la kwanza kuwa watu wa lugha mbali mbali waliweza kuwasikia mitume, kwani mitume wanatoka na kuwa mashahidi wa lugha ya Roho Mtakatifu na si nyingine bali ni lugha ya upendo. Upendo ndio ujumbe wa Kipasaka, ndio ujumbe wa Pentekoste na ndio ujumbe wa wanafunzi na rafiki zake Kristo Mfufuka! Niwatakie Dominika na tafakari njema.

19 May 2021, 08:18