Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya VI ya Pasaka: Upendo wa Yesu
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya neno la Mungu dominika ya sita ya Pasaka mwaka B. Mama Kanisa katika Dominika za kipindi hiki cha Pasaka, anatupa nafasi ya kutafakari zawadi za Fumbo la Pasaka. Dominika ya Pasaka tunatafakari juu ya uwepo wa Kristo mfufuka kati yetu; Dominika ya 2 zawadi ya Roho Mtakatifu inayotolewa na Kristo mfufuka akisema; “Amani iwe kwenu”; Dominika ya 3 Msamaha wa dhambi; Dominika ya 4 Kristo mchungaji mwema; Dominika ya 5 Kristo Mzabibu wa kweli nasi tu matawi na uzima wetu unategemea kushikamana naye na pasipo yeye hatuwezi kitu. Dominika ya 6 ya Kipindi cha Pasaka tunatafakari juu ya upendo ambao ni dira na ukumbusho wa wajibu wetu kama wakristo, kuishi kwa ukarimu na wema, huruma, amani na uaminifu, kupokeana, urafiki na umoja na kuonyana kidugu.
Somo la kwanza la matendo ya mitume (Mdo 10:25-27, 34-35, 44-48); lahusu kuongoka kwa Kornelio na watu wa nyumbani kwake walipohubiriwa na Petro na kumpokea Roho mtakatifu huko Jaffa baada ya Kornelio kutokewa na Malaika akimwagiza atume ujumbe kwa Mtume Petro aje kuwahubiria. Petro alipofika, Kornelio akatoka kumlaki akamwangukia miguu, kumsujudia. Lakini Petro akamwinua akisema; simama, mimi nami ni mwanadamu”. Anayestahili kuabudiwa ni Mungu peke yake na sio binadamu. Ili Mungu apewe sifa ni lazima sisi tunaomwamini tumshuhudie kwa maneno na matendo yetu. Ndiyo maana Yesu anasema; “Ni lazima mwanga wenu uangaze mbele ya watu, ili wayaone matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Mathayo 5:16). Na mtume Petro anatuasa akisema; “Anayesema kitu, maneno yake yawe kama maneno ya Mungu; anayetumikia anapaswa kutumikia kwa nguvu anayojaliwa na Mungu, ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristo ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele! Amina (1 Petro 4:11).
Katika somo hili tunaona ufunuo wa mpango wa Mungu juu ya wokovu kwa watu wote hata wapagani/watu wa Mataifa kinyume kabisa na mtazamo na fikra za taifa teule la Israeli/Wayahudi waliofikiri kuwa wokovu ni kwa ajili yao tu na wale walioongokea dini yao na kutahiriwa. Akiongozwa na mwanga wa Roho Mtakatifu, Mtume Petro alitambua kwamba wapagani haikuwapasa kutahiriwa ili waweze kuokoka kama Sheria ya Kiyahudi ilivyodai. Kwa upande wao imetakiwa tu wasadiki mafundisho ya Yesu na kupokea ubatizo. Jinsi Roho Mtakatifu alivyowashukia wote waliolisikia lile neno waliokuwepo katika nyumba ya Kornelio, Jemedari wa kijeshi mpagani, wale waliotahiriwa, walioamini/wayahudi walishangaa, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa maana walisikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Naye Petro kwa mshangao anauliza; Nani awezaye kukataza maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vilevile kama sisi? Akaamuru wabatizwe kwa jina lake Yesu Kristo.”
Somo la pili la Waraka wa kwanza wa Mtume Yohane kwa Watu Wote (1Yoh 4:9-17); linatueleza juu ya asili ya Mungu kuwa ni Mapendo. Mungu kwa asili ni upendo. Ingawa tulimkashifu kwa dhambi, Yeye hakuacha kutupenda. Alimtuma Mwanae wa pekee kama kipatanisho ili sisi tumrudie Yeye Mungu Baba. Kwa hiyo, kama vile Mungu asivyokoma kutupenda, nasi tusikome kupendana. Maneno ya mtume Yohane ni ya maana sana. Anasema: “Wapenzi, na tupendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu.”
Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yoh 15:9-15); inatueleza kuwa ili kuonyesha kuwa anatupenda, Yesu Kristo alitoa uhai wake kwa ajili ya wokovu wetu. Ili tuweze kudumu katika pendo hilo, Kristo anatuagiza tushike amri yake ya kupendana kindugu. Upendo ambao Bwana wetu Yesu Kristo anatuasa sisi wafuasi wake tuuishi na kudumu nao kwa kupendana kindugu ni upendo usiojitafuta wenyewe. Je, ni aina gani ya upendo ambao ni amri na usiojitafuta wenyewe? Wagiriki wanayo maneno matatu kuonesha itifaki ya upendo. Neno la kwanza ni eros. Hili linawakilisha upendo unaongozwa na vionjo vya mwili vinavyomfanya mwanaume ampende mwanamke na mwanamke ampende mwanaume na kuwafanya wakae pamoja kama mume na mke. Neno philia. Hili linawakilisha upendo wa kidugu au kirafiki na uelewano. Katika injili Yesu anasema “ninyi mmekuwa rafiki zangu, kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake, lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyosikia kwa baba nimewaarifu.”
Neno la tatu ni agape. Hili linawakilisha upendo wa Kimungu ambao ni fadhila ya kimungu ndani mwetu na ni msingi wa fadhila zingine zote ambazo kwayo zahuishwa na kuangazwa na Mungu mwenyewe ndani mwetu. Asili ya upendo huu ni Mungu mwenyewe, aliyeupenda ulimwengu hivi hata akamtoa mwanae wa pekee ili kila amwaminie asipotee bali awe na uzima wa milele” (Yoh 3:16). Huu ndio upendo ambao Kristo anatutaka tuuishi. Ndio upendo wa Kristo mwenyewe ndiyo maana anatuamuru akisema; “pendaneni kama nilivyowapenda ninyi.” (Yoh 13:34). Upendo huu ni amri na ni wajibu kila mkristo kutumikia na kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Mimi ni upendo, kaeni katika pendo langu, hakuna upendo wa kweli pasipo muungano na Kristo. Kama Baba alivyonipenda mimi, na mimi nilivyompenda, pendaneni ninyi kwa ninyi. Upendo una nafasi tatu. Upendo wa Baba kwa Mwana. Upendo wa Mwana kwetu. Upendo wetu kwa jirani/watu wote. Upendo wa Mungu ni kama chemchem inayotiririka kutoka kwa Baba kwenda kwa Mwana kuja kwetu sisi kwenda kwa Jirani na kurudi kwa Baba.
Yesu anatuambia kwamba tukizishika amri zake na kukaa katika pendo lake tutakuwa ndani ya Mungu na Mungu ndani yenu. Kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake vivyo hivyo nanyi mfanye. Yesu anaendelea kusisitiza; mimi niliwachagua ninyi, mwende mkazae matunda na matunda yenu yapate kudumu. Kumbe kwa upendo wake, Yesu kwa mateso, kifo na ufufuko wake ametushirikisha maisha ya familia ya Mungu na uzima wa Kimungu ndani yetu. Hivyo upendo umekuwa ni amri ndiyo maana Kristo anasema; “Nawaamuru mpendane (Yn 15:17). Ni lazima kupendana kwa sababu Mungu ni upendo na anatupenda sote pasipo ubaguzi, ananyeshea mvua (Baraka) wote wema na wadhambi. Upendo ni lazima ulete furaha: Furaha ya Kikristo ni furaha shirikishi. Tunafurahi kwa sababu sisi ni familia ya Mungu. Tunafurahi kwa sababu Mungu anakaa ndani yetu. Tunafurahi kwa sababu Mungu anatulisha kwa Neno lake na kwa Ekaristi Takatifu. Tunafurahi kwa sababu baada ya maisha haya tumealikwa katika karamu ya milele mbinguni. Upendo wetu sisi kwa Mungu unajidhihirisha katika kuvipenda vyote alivyoviumba mwenyezi Mungu na kutukabidhi ili tuvitiishe. Ndiyo kusema vyote vilivyoko duniani ni ishara ya upendo wa Mungu. Ndiyo maana tunapaswa kumpenda Mungu siyo tu katika jirani ila katika viumbe vyote.
Baba Mtakatifu Yohane wa pili katika barua yake kwa mapadre ya tarehe 06/04/1979 anasema; “kwa kuwa upendo katika nyanja zake zote si wito tu bali ni wajibu” kumbe leo hii mnakumbushwa kuwajibika, kuonesha upendo na kuudhihirisha, kwani mmewekwa kati ya waamini ili muwaongoze katika umoja wa upendo wa agape “kwa kupendana kindugu. Kila mmoja amfikirie kwanza mwenzake kwa hekima” (Rom 12:10). Na kuleta maelewano katika mawazo yanayokinzana msikimbie wala kuomba udhuru. Upendo wa agape unawezekana kuuishi tukitanguliza kuomba msaada wa Mungu na tukifanya jitihada kutawala tamaa za miili yetu zinazotupelekea kuharibu upendo wa Kristo.